Kuna njaa inanukia nchini tanzania--JK

Rais Kikwete usiku wa kuamkia leo alizungumza na wananchi kwa ufupi aliwaasa kuhusu hali ya chakula na ukame nchini na pia juhudi za serikal...

Rais Kikwete usiku wa kuamkia leo alizungumza na wananchi kwa ufupi aliwaasa kuhusu hali ya chakula na ukame nchini na pia juhudi za serikali kuwaptia tena mbegu wananchi waliochanganyikiwa kwa ukame ili wajaribu tena.
Pia alizungumzia haja ya kuwa waangalifu katika matumizi ya chakula kutokana na ukweli kuwa hata kama una fedha hali ya upatikanaji wa chakula duniani ni tete.
tatu aliwataka wenye mvua angalau kidogo kupanda mazao ya muda mfupi na yanayohimili ukame.
Lakini kubwa alisema kuna ziada kidogo sana ya chakula.
katika mahusiano ya jkidplomasia alizungumzia ujio wa wageni mbalimbali na jinsi ya kuwakarimu na kuwatumia.
Wanaojifanya wanajua biashara ya albino sasa wangoje kuumbuliwa tu kikaango kiko tayari na wale wanaofanya mazabe na fedha za watumishi wa umma haki ya nani watakoma.
sasa soma hotuba yenyewe


HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI
TAREHE 28 FEBRUARI, 2009


Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Naomba tuendelee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia tena fursa nyingine ya kuzungumza kuhusu masuala muhimu ya nchi yetu katika siku hii ya mwisho ya mwezi Februari 2009. Leo nakusudia kuzungumzia mambo manne, nayo ni:
(a) Mapokezi ya wageni wetu kutoka nchi za nje;
(b) Hali ya chakula nchini;
(c) Ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi (Albino); na
(d) Malimbikizo ya madai ya Watumishi wa umma.




Mapokezi ya Wageni Wetu Kutoka Nchi za Nje
Ndugu Wananchi;
Mwezi huu tunaoumaliza leo ulikuwa na baraka tele kwa nchi yetu. Tumepata bahati ya kutembelewa na wageni mashuhuri watano kutoka nchi za nje. Wa kwanza alikuwa Rais Rupia Banda wa Zambia aliyetutembelea tarehe 9 mpaka 10 Februari, 2009. Wa pili alikuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Hu Jintao aliyetutembelea tarehe 14 mpaka 16 Februari. Akafuatiwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Mhe. Kamalesh Sharma tarehe 20, Februari. Tarehe 22 hadi 23 Februari, tulikuwa na ugeni wa Rais wa Uturuki Mheshimiwa Abdullah Gül. Hatimaye tarehe 26 Februari, tukawa na ugeni wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki-moon ambaye ameondoka nchini leo.
Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru sana wananchi wenzangu hasa wa hapa Dar es Salaam na maeneo mengine walikotembelea wageni wetu kwa mapokezi mazuri. Tumewapokea kwa upendo mkubwa na wote wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri za nchi yetu na ukarimu wa watu wake. Mmeturahisishia sana kazi yetu ya kujenga mahusiano mema na nchi hizo na mashirika hayo muhimu ya kimataifa.
Viongozi hao tumefanya nao mazungumzo mazuri ambayo yamelenga kukuza ushirikiano baina ya nchi yetu na nchi zao pamoja na mashirika wanayoyaongoza. Mazungumzo yetu yalikuwa ya mafanikio tuliyoyatarajia. Kilichobaki kwa upande wetu na wao ni kufuatilia utekelezaji wa yale tuliyokubaliana. Kwa upande wetu tumejipanga vizuri kufanya hivyo na wenzetu pia wamenihakikishia kufanya hivyo. Baadhi wamekwishaanza utekelezaji. Kwa mfano, Gavana wa Benki ya Maendeleo ya China anakuja nchini mwishoni mwa wiki kwa mazungumzo na Gavana wa Benki Kuu kuhusu maombi yangu kwa Rais Hu Jintao ya kutaka serikali zetu zishirikiane kuongeza mtaji wa Benki ya Rasilimali (TIB) na kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo.
Ndugu Wananchi;
Mwezi ujao wa Machi, nchi yetu imepewa heshima nyingine kubwa ya kimataifa. Kwa makubaliano baina yangu na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa yaani IMF, Bw. Dominique Strauss-Khan, Tanzania tutakuwa mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu wa nchi za Afrika na IMF. Mkutano huo tunaouitisha kwa pamoja utafanyika hapa Dar es Salaam tarehe 10 na 11 Machi, 2009.
Agenda kuu ya mkutano ni Hali ya Uchumi wa Dunia ilivyo sasa na athari zake kwa nchi za Afrika. Lengo ni kutafakari hali ya machafuko ya mfumo wa fedha wa kimataifa na kudhoofika kwa uchumi wa mataifa makubwa kiuchumi duniani na jinsi matatizo hayo yanavyoathiri na kutishia ustawi wa uchumi wa watu katika bara la Afrika. Jambo la msingi katika mkutano huo ni kuelewana kwa pamoja kuhusu mikakati na mbinu za kukabiliana na tishio hili kubwa kuliko yote kutokea duniani tangu miaka ya 1930. Nawaomba Watanzania wenzangu kama ilivyo kawaida tuwapokee wageni wetu hao nao kwa mujibu wa takrima na upendo wa asili wa wananchi wa nchi yetu. Mambo ambayo yametuletea sifa na heshima kubwa duniani na kutufanya tuwe na marafiki wengi.
Ndugu Wananchi;
Wakati sisi tukiwa wenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa Afrika na IMF, mjini London, Uingereza kutakuwa na mkutano wa uwekezaji wa Afrika Mashariki. Nchi zote tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zitashiriki. Rais wa Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume ataongoza ujumbe wa Tanzania. Mkutano huu unaoandaliwa na marafiki zetu wa jiji la London ni fursa nzuri ya kutangaza vivutio vya uwekezaji vya nchi yetu. Tumejiandaa vya kutosha. Naamini wenzetu wanaotuwakilisha watashiriki vizuri.
Hali ya Chakula Nchini
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwaka 2008 nilieleza kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini imekuwa nzuri kwa miaka miwili mfululizo, yaani 2007 na 2008, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2006. Nilieleza pia hofu yangu kuwa kutokana na kukosekana kwa mvua za vuli katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, hali ya upatikanaji wa chakula katika mikoa hiyo inaweza kuwa ya matatizo siku za usoni. Na, inaweza kuwa mbaya zaidi kama mvua za masika nazo hazitanyesha vizuri.
Baadae katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Januari, 2009 nilielezea mashaka yangu kuwa katika baadhi ya mikoa inayopata mvua moja kwa mwaka, nako kumejitokeza uhaba mkubwa wa mvua. Nilieleza pia wakati ule kuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inafanya tathmini ya hali ya chakula nchini na watatoa taarifa yao ipasavyo baada ya kazi hiyo kukamilika. Kazi hiyo imekamilika na taarifa imetolewa na inaendelea kufanyiwa kazi.
Ndugu Wananchi;
Mvua za msimu katika mikoa inayopata mvua mara moja kwa mwaka (Mikoa ya Kati, Magharibi, Nyanda za Juu Kusini Magharibi na Kusini) zinaendelea kunyesha kwa viwango vya wastani na chini ya wastani katika maeneo mengi. Mikoa ya Lindi na Mtwara kati ya mwezi Desemba, 2008 na Januari, 2009 ilikabiliwa na vipindi virefu vya ukame uliosababisha karibu asilimia 90 ya mazao ya chakula yaliyopandwa mwanzoni mwa msimu kunyauka. Hata hivyo, mvua sasa zinaendelea kunyesha. Serikali imetoa msaada wa mbegu na wakulima ambao wamelazimika kupanda tena. Tuendelee kumuomba Mungu mvua ziendelee kunyesha ili jaribio hili la kupanda mara ya pili liwe na matokeo tunayoyatarajia.

Ndugu Wananchi;
Kwa jinsi hali ya mvua ilivyo nchini, ni dhahiri kuwa mavuno ya msimu ujao huenda yakawa pungufu. Labda mvua za masika ziwe nzuri sana na mvua zinazoendelea sasa katika mikoa iliyoathirika ziendelee kunyesha vizuri mpaka mwisho wa msimu.

Upatikanaji wa Chakula
Ndugu Wananchi;
Tathmini ya hali ya chakula nchini iliyofanywa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inaonesha kuwa hadi kufikia mwezi Desemba, 2008 mavuno ya mazao ya chakula yalifikia jumla ya tani milioni 10.872 wakati makadirio ya mahitaji nchini ni tani milioni 10.337. Kuna ziada ndogo ya tani 535,000. Ziada hii ni ndogo mno. Haiweze kuleta utulivu wa kutosha kwa upande wa upatikanaji wa chakula kwa msimu unaoishia Juni, 2009. Hivyo, kuhitajika tahadhari na uangalifu mkubwa katika hifadhi na matumizi ya chakula. Hili ni muhimu sana hasa ikizingatiwa kwamba ziada hii inatokana na mazao ya chakula yasiyo ya nafaka kama vile muhogo, ndizi, viazi na mazao ya jamii ya kunde.
Tathmini hiyo imebainisha kuwepo kwa upungufu wa chakula katika wilaya 19 nchini. Tani 7,128 zimetengwa kusaidia watu katika wilaya hizo. Mpaka Februari 25, 2009 tani 3,265 zilikuwa zimeshagawiwa kwa watu katika wilaya hizo. Kati ya hizo tani 359 zilitolewa bure kwa watu 12,027 wasiokuwa na uwezo wa kununua.

Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini
Ndugu Wananchi;
Tathmini ya hali ya chakula nchini, pia, imeonesha kuwa bei za vyakula nchini zimeendelea kupanda. Zipo sababu kadhaa na mojawapo kubwa ni ile ya kutokuwepo ziada kwa mazao ya mahindi na mchele ambavyo ndivyo vyakula vikuu. Pia, hali ya upungufu mkubwa wa chakula katika nchi jirani ambazo zimetokea kutegemea Tanzania kupata mahitaji yao ya chakula, imekuwa kichocheo kikubwa cha kupanda kwa bei za ndani za chakula hapa nchini. Wenzetu wako tayari kununua chakula chetu kwa bei yoyote ile jambo ambalo limetumika na wauzaji nchini kama kigezo kwa bei wanazouzia mahindi na mchele hapa ndani.
Wakati mwingine matatizo ya miundombinu nayo yamechangia kupanda kwa bei za vyakula katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Kwa mfano, katika mwezi Januari 2009, soko la Lindi liliongoza kwa kuwa na bei ya juu zaidi ya mahindi iliyofikia Shs.45,000/= kwa gunia wakati soko la Sumbawanga lilikuwa na bei ya chini zaidi ya Shs.26,455/= . Kama kungekuwa na njia rahisi ya kufikisha mahindi ya Rukwa mkoani Lindi bei isingekuwa juu kiasi hicho.



Hali ya Hifadhi ya Chakula Nchini na Hatua za Serikali

Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kwa mara nyingine tena kuwa, Serikali yetu inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa hayupo mwananchi yeyote atakayekufa kwa njaa. Tunayo akiba ya kutosha ya chakula katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). Hadi tarehe 25 Februari 2009, akiba ya chakula iliyohifadhiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ilikuwa tani 125,673 za nafaka. Wakati huohuo, hadi tarehe 31 Januari, 2009 wafanyabiashara wakubwa wa mazao ya chakula nchini walikuwa na akiba ya jumla ya tani 149,200 za mazao ya nafaka zikiwemo tani 38,608 za mahindi, tani 1,637 za mchele, tani 107,870 za ngano na tani 1,090 za mtama.
Tuko tayari wakati wowote kuitumia akiba yetu hiyo kuokoa maisha ya Watanzania pale itakapohitajika kufanya hivyo. Tunafanya hivyo hivi sasa katika baadhi ya maeneo kama nilivyokwishaeleza. Aidha, tuko tayari kutumia akiba hiyo kupunguza makali ya bei za vyakula nchini. Tunajiandaa kufanya hivyo baada ya muda mrefu kwa upande wa mchele.

Wito wa Serikali kwa Wananchi
Ndugu Wananchi;
Tishio la upungufu wa chakula ni jambo la hatari ambalo sote, Serikali na wananchi, hatuna budi kulichukulia kwa uzito unaostahili. Nimeeleza jinsi Serikali tulivyojipanga kutimiza wajibu wetu. Napenda kuitumia nafasi hii kusisitiza au kutoa wito kwa wananchi nao kutimiza wajibu wao.
Tunawategemea kuzingatia mambo matatu yafuatayo: Kwanza, tutumie vizuri akiba ya chakula tuliyonayo. Tulitambue tishio lililopo na kuwa waangalifu, hali siyo nzuri sana, inaweza kuwa mbaya mbele ya safari. Tuwe na tahadhari kubwa. Kwa sababu, hali ya upungufu wa chakula ilivyo duniani hivi sasa, tunaweza kuwa na fedha lakini tukakosa chakula cha kununua.
Pili, maeneo yaliyopata tatizo la upungufu wa mvua wazitumie mvua zinazonesha sasa kupanda mazao yanayostahimili ukame na hasa yale yenye kukomaa kwa muda mfupi. Tatu, tuongeze bidii kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula ili tujitosheleze kwa chakula na kuuza akiba nje ya nchi. Tuzingatie kanuni za kilimo bora na tutumie pembejeo za kisasa.
Tunawasihi wanaopata mvua za masika wahakikishe kuwa wanazitumia vizuri ili kufidia pengo la upungufu. Serikali kupitia Mfuko wa Maafa ilitoa tani 1,091 zenye thamani ya shilingi bilioni 1.76 kwa ajili ya wakulima waliolazimika kupanda tena baada ya mazao yao kunyauka. Tuko tayari kutoa ziada kama hapana budi.


Mauaji ya Albino
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwaka jana tarehe 31 Desemba 2008, nilitamka juu ya uamuzi wangu wa kuitisha na kuendesha zoezi la Kura ya Maoni nchi nzima kuhusu mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, yaani Albino. Dhamira yangu ni kuwapa nafasi wananchi ya kuwataja watu wanaowafahamu kuwa wanajihusisha na mauaji ya albino au kukata viungo vyao. Pia wawataje watu wanaojihusisha na biashara ya viungo vya albino na watumiaji wa viungo hivyo. Kadhalika, wananchi wasaidie kuwataja waganga wa jadi wanaojihusisha na upigaji ramli au uganga unaohitaji matumizi ya viungo vya albino. Aidha, watu wawataje wanaojihusisha kwa namna yoyote ile na jambo lolote linalosababisha mauaji ya Albino.
Ndugu Wananchi;
Maandalizi ya kutekeleza uamuzi wangu huo yanaelekea kukamilika. Mheshimiwa Waziri Mkuu atafanya uzinduzi rasmi wa zoezi hilo mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2009 na zoezi lenyewe la kupiga kura kufanyika kuanzia wiki ya pili ya Machi, 2009. Katika zoezi hilo pia wauaji wa vikongwe, majambazi wa kutumia silaha na wauzaji wa madawa ya kulevya nao watahusishwa.
Katika kuendesha zoezi hili, Mikoa imegawanywa katika Kanda saba zifuatazo: Kanda ya Ziwa inayojumuisha Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, na Shinyanga; Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye Mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma; Kanda ya Kati ya Mikoa ya Dodoma, na Singida; Kanda ya Kusini yenye Mikoa ya Lindi na Mtwara; Kanda ya Magharibi yenye Mikoa ya Kigoma na Tabora; Kanda ya Kaskazini yenye kujumuisha Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara; na Kanda ya Mashariki itakayokuwa na Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Wakuu wa Mikoa yote Nchini wameshapewa Mwongozo wa jinsi ya kutekeleza zoezi hili. Miongoni mwa mambo ya kuzingatia ni haya yafuatayo:
(a) Kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushriki katika zoezi hili. Kazi hiyo inaendelea.
(b) Kwamba Upigaji Kura ufanyike mwezi Machi, 2009 kwa tarehe zitakazopangwa kwa kuzingatia Kanda nilizokwisha kuzitaja. Kila Kanda itachagua siku yake maalum ya kuendesha kura hizo. Kanda ya Ziwa itakuwa ya kwanza.
(c) Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa zikiongozwa na Wakuu wa Mikoa zisimamie zoezi hili kwa makini. Kadhalika, Kamati za Ulinzi na Usalama za wilaya zikiongozwa na Wakuu wa Wilaya zitaongoza utekelezaji katika Wilaya zao na kushirikisha serikali za vijiji na mitaa.

Aidha, Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa kuzingatia mazingira ya kila Kanda ili waweze kutumia utaratibu wowote utakaoonekana kufaa kuleta ufanisi wa hali ya juu katika kutimiza dhamira ya Kura hizi za Maoni.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuitumia fursa hii kuwasihi Watanzania, wake kwa waume, vijana na wazee tujitokeze kwa wingi kuwataja watu wanaojihusisha na maovu hayo katika jamii. Kura ni siri, hakuna atakayejua umemtaja nani. Hata msimamizi wa kituo hawezi kujua. Naomba tusaidiane tukomeshe ukatili huu na aibu hii katika taifa letu. Jina la nchi yetu limechafuliwa sana kwa vitendo vya watu wachache waovu waliotawaliwa na tama ya utajiri iliyopita mipaka. Inawezekana, timiza Wajibu Wako!!




Malimbikizo ya Madai ya Watumishi Serikalini

Ndugu Wananchi;
Hivi karibuni nilipokutana na viongozi wa kisiasa na kiutendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nilizungumzia malimbikizo ya madai ya malipo ya stahili mbalimbali za walimu. Jambo hilo limekuwa chanzo cha mivutano kati ya Serikali na walimu. Katika mazungumzo yangu nao, nilisisitiza kuwa mivutano hiyo haina lazima wala sababu ya kuwepo. Kama wahusika katika idara za utawala na fedha katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Utumishi na Wizara ya Fedha na Uchumi wangetimiza ipasavyo wajibu wao hakuna tatizo. Napenda kusema kuwa matatizo wayapatayo walimu ndiyo wayapatayo watumishi wengine wa umma katika Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali.
Sehemu kubwa ya madai ya malimbikizo ya walimu yanahusu stahili zao za uhamisho, kupandishwa madaraja, likizo n.k. Nilielekeza kuwa kama Halmashauri haina pesa za uhamisho wasiwahamishe watumishi wao. Wamekuwa wanafanya hivyo na kulimbikiza madeni makubwa ambayo yamekuwa yanalipwa na Serikali Kuu mara nyingi baada ya walimu kuchachamaa. Serikali Kuu imekuwa inafanya hivyo kuepusha shari, bahati mbaya hiyo imegeuka kuwa mazoea. Sasa inaonekana kana kwamba kumhamisha mtumishi kutoka kituo kimoja kwenda kingine Wilayani ni wajibu wa Serikali Kuu kugharamia. Matokeo yake ni malimbikizo na madai yasiyokwisha yanayozua migogoro ya mara kwa mara. Baya zaidi panapotokea migogoro hiyo wale waliosababisha malimbikizo hayo hawaonekani kuwa ndiyo wakosaji bali inaonekana Serikali Kuu ambayo huingilia kati kuokoa jahazi. Hali hii haiwezi kuachwa iendelee.

Ndugu Wananchi;
Niliagiza mtindo wa kuhamisha walimu bila ya kuwa na fedha za uhamisho ukomeshwe mara moja. Ni marufuku kufanya hivyo. Na, agizo langu hilo haliwahusu walimu tu, bali watumishi wote wa umma. Kiongozi au mhusika yeyote atakayekiuka agizo hili alipishwe yeye gharama za kumhamisha mtumishi huyo.
Madai ya likizo nayo yako kama ya uhamisho. Ninachosema kama hazikutengwa fedha za kugharamia likizo za watumishi, usilimbikize madeni. Uzuri wa likizo ni kuwa hazipotei. Wakati wa kustaafu siku za likizo ambazo mtumishi hakuchukua hulipwa. Hata hivyo, napenda kusisitiza kutengwa fedha za kutosha za likizo kwani mapumziko ni muhimu kwa wafanyakazi.
Ndugu wananchi;
Tulikubaliana pia kwamba suala la kuwapandisha watumishi vyeo bila kuwarekebishia mishahara yao ni upungufu wa kiutendaji ambao ni lazima ukomeshwe mara moja. Nimeagiza viongozi wa Wizara zote na Halmashauri kuhakikisha kuwa watumishi wote wanaopandishwa vyeo wanalipwa stahili zao kwa wakati. Napata ugumu kuelewa kwanini kuwepo tatizo hili. Hivi inatokeaje mtumishi wa umma apandishwe ngazi au cheo na kuwa na tatizo la kumlipa mshahara wa ngazi mpya kwa mwaka au miaka? Nina ushahidi wa mwalimu kupandishwa madaraja mara tatu lakini bado analipwa mshahara ule ule wa kabla hajapandishwa daraja la mwanzo. Hii si sawa hata kidogo na siyo haki.
Kwa mujibu wa utaratibu wa Serikali, mtumishi hupandishwa cheo kwa misingi miwili. Kwanza, kutimiza masharti ya muundo wake wa utumishi, na pili, kuwepo kwa fedha kwenye bajeti ya Wizara au Idara husika kwa madhumuni hayo. Je, iweje leo mtu apandishwe madaraja bila kulipwa mashahara stahiki? Hili halikubaliki. Nimewataka wahusika warekebishe kasoro hii ambayo haina sababu ya kuwepo. Ni migogoro ya kujitakia. Kwa nini tuwe watawala wa aina hii kwa watumishi tunaowaongoza?
Ndugu Wananchi;
Mlundikano wa malimbikizo ya madai ya watumishi husababishwa na wakuu wa kazi wazembe na wasiojali maslahi ya walio chini yao. Aghalabu, unasababishwa na watumishi wa Idara ya Fedha na Utumishi wasio waaminifu ambao wamekuwa wakijinufaisha kupitia mlundikano wa madai ya watumishi. Nimeagiza Viongozi wa Wizara ya Elimu kuwashughulikia ipasavyo watumishi wa aina hiyo wasichelee kuwaondoka kwenye nafasi zao. Wakati mwingine watu kukaa kituo kimoja kwa muda mrefu huzaa tabia za namna hii. Nimeagiza watu walioko kituo kimoja kwa muda mrefu wahamishwe. Kuwahamisha mara kwa mara kutasaidia kuondoa usultani.
Ndugu Wananchi,
Naomba nimalize kwa kuwashukuru kwa kunisikiliza. Tuendelee kushikamana kujenga nchi yetu. Lakini pia kwa pamoja tuwapongeze wachezaji wetu wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa ushindi walioupata majuzi na tuzidi kuwahamasisha washinde pia mchezo wao wa leo na mingine inayofuata. Tuelekeze dua zetu kwao.

Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Asanteni Sana

COMMENTS

Name

Anga,11,Arusha,27,Burudani,302,burundani,1,come rain,1,come sun,1,Crazy in Love kama wimbo kama wao wenyewe,1,dahh sijui kweli mbona shida,1,Dar utakuja je tumejiandaa,1,daraja sahau nini,1,demokrasia ya upanga,1,Dodoma,77,Dole tupu vijana wa zamani,1,Duhh bibie endeleza libeneke,1,Duhh kaisikie Walibana,1,duhh kwa mbagala mama lazima awe supa,1,Fedha za maiti haziliwi bure,1,Fedha za watu kwa maendeleo ya watu,1,Fikira,14,filamu,238,Filamu ndio kielelezo cha ukuzi wa taifa,1,flamu,7,Gandamiza Kibara baba ake,1,Habari,4816,habari. dodoma,24,hadithi,19,hakika tumeweka historia,1,hakuna noma jongwe,1,hapa kwetu inakuwaje vile,1,hasira hasara,1,hata maji,1,hataki masikhara na maisha yake,1,hatubonyezi kizenji,1,haya ndiyo mambo ya Ulaya,1,haya si yangu ni ya mdau mwenye hasira,1,haya wabongo na mambo kutoka nje,1,He he he wananikumbusha upishi wa shaba,1,Headline,1,Hii hurejesha uhai,1,Hii iko sawa kweli?,1,Hii imekaa vizuri,1,Hii inakaaje vile,1,Hii kweli noma,1,Hii maana yake Moro kuna uhaba wa chakula,1,Hii mexico,1,Hii mihasira mingine bwana,1,Hii ndio moro sio mpaka dar,1,hii ni hatari,1,Hii ni kiboko anayetaka kubisha ajibishie tu,1,Hii ni moja ya staili za kunyoa nywele,1,Hii si lukwangule,1,hii staili mpya,1,hili ni jengo pacha la malaysia ghorofa 88,1,Hivi ni ngoma tu,1,hivi nini siri za serikali,1,hivi sisi tunajua kama kuna vitu vya aina hii,1,hivi vitu bwana,1,Hiyo ndiyo gharama ya demokrasia,1,Hizi imani nyingine ni hatari,1,Hizi takwimu hizi mhh,1,Hongera bibie,1,Hongera dada etu kwa kutuletea kaka etu (shemeji) kwani mwenye dada hakosi shemeji,1,Hongera sana,1,huhitaji mifedha kuwa msafi,1,Huko Ulaya,1,Huu ndio ustaarabu,1,huu ujiko utakuwa mkubwa,1,imetosha,1,Inahitaji nidhamu fulani,1,inakuuma au...,1,Inakuwaje kama filamu yenyewe itahitaji busu la nguvu,1,Inaonekana watanzania hatukuwepo,1,Ipo kazi Maximo,1,Iringa,22,Isiwe mijineno tu manake mihela hubadili watu kweli,1,Itakuwa laki moja ya halali,1,jamani huu kama si ushamba kumbe nini,1,Jamani mbona Mungu anatupigania,1,Jamani watoto wanatakiwa kupendwa,1,jamani.. jamani ukiikosa Diamond usijutie,1,Je nyumbani hakuna vitu vya aina hii?Tuambie,1,je walikuwepo watu wa huduma ya kwanza,1,Je watanzania wanalipa kodi,1,jela kwa raha,1,Jolie,1,juhudi za lazima kuinua filamu,1,kama si kiwanda cha chumvi nani atawajua hawa,1,Kama kweli ndio kweli basi kila heri,1,Kama Mkristo naamini hilo hiyo si sahihi,1,kama unajua kuyarudi nenda Malta,1,kama wao wanaweza sisi je,1,Kamua baba waache wakanyagane,1,karibu nyumbani dada yote maisha tu,1,karibu Tatiii,1,KARIBUNI,1,Katavi,5,kaza buti hakuna kukata tamaa inalipa,1,kazi kwako mheshimiwa waziri wa madini,1,kazi na burudani,1,keep it up bloggers,1,kero ya usafiri sasa kwisha,1,Kila chenye roho na mwili kitaonja umauti,1,kila kitu kina vitu,1,Kila la Heri jamila,1,kila la heri kwani ni changamoto,1,Kipya,51,Kiuno bila mfupa,1,Kolelo mzimu ambao bado hai,1,KUBWA,1,Kudumisha urafiki wa dunia,1,Kuna dalili za wasomi kukubali Uafrika,1,kuna makala humu humu ndani ya blogu sijui mnasemaje,1,Kuu,113,kwa mara nyingine tena Tigo imewezesha,1,Kwa mchanganyiko huu muungano lazima udumu,1,Kwa mihasira hajambo,1,kweli,1,Kweli ina mkono mrefu tuone,1,Kweli duniani tunatofautiana,1,la maana ni kuwa na jiko au vipi,1,labda halitabadilika tena,1,lakini mwafaka lazima,1,lengo ni kutafakari,1,leteni vitu tuvione,1,lets us,1,Lucy wanakuelewa hawa...,1,Lukwangule nyumbani kwetu,2,M ungu bariki mikono ya madaktari wafanikiwe,1,MAARUFU,1,maendeleo ya soka siku zote yanahitaji fedha ili yapatikane,1,maisha ni vyema kuyaangalia,1,MAJIBU,1,makala,51,mama ni mama tu anapendeza,1,mambo mengine we angalia tu,1,mambo msimamo,1,mambo sasa mchanganyiko,1,Mara nyingine huona tunakotoka kwa kuona wenzetu,1,Mashabiki wa rhumba mpooooooooo,1,Masitaa,12,Maskani,1,MASOKO,3,Masupa staa mnaoinukia mpoo,1,Matamasha,6,mavazi ya kuogelea yanaposhindaniwa,1,Mbeya,11,Mchakamchaka anti Asmah,1,Mchanganyiko,81,MCHANYATO,1,mchezo,5,mengi wanayoyaita siri ni public information,1,mfumuko wa bei mpaka noma,1,Mhh sijui watu wa Sua ambao wako huko wanasemaje,1,Mhh ugua pole dada watu wanataka burudani,1,Michezo,501,Michezo maalum inatakiwa kupigiwa debe,1,miguu,1,miguu babu,1,Mikataba mingine ama hakika tuiangalie hata wakopeshaji nao wanatugeuza sakala,1,MIMI NI KISURA NAJITAMBUA,1,Mimi sijajua hasa kumetokea nini kwani ninavyojua hawa huwa na ungalizi wa hali ya juu,1,Mimi simo,1,mimi sisemi,1,mkiwa chumvi basi mkoze,1,Mkiwa taa mulikeni,1,Mnaonaje je hii imekaa vyema,1,Mnaweza wakwetu hapa,1,Morogoro,51,mrithi wa mwanadada Whitney Houston,1,Mtwara,4,Mungu aiweke mahali pema roho yake,4,Mungu amrehemu,1,Mungu amweke pema peponi,1,Mungu awabariki sana,1,Mungu awe nao,1,Mungu ibariki Tanzania,1,Mungu tuepushe na imani hizi za kishirikina,1,mungu tufanye tuwe na upendo,1,Mungu twaomba utuhurumie,1,Muziki,350,muziki na fasheni,5,Mwanahabari,33,Mwanza,6,Mwendo mdundo dada,1,Mwenge huo utakimbizwa duniani kwa siku 130,1,Mwenge wa olimpiki ni ishara ya urafiki,1,Mzee wa Farasi nakupa saluti,1,Mzimbabwe huyu kutoka kwa mama mkali,1,N i dar mpaka Moro au bao tatu bila,1,Na sisi je,1,Naam kama haiwezekani hapa,1,Nairobi waanzisha tena utalii,1,namna bora ya kusaidia jamii,1,nani abebe hukumu na lawama,1,nani asiyejua utamu wa pipi,1,Nani kama baba,1,naona inafaa kuchangia mimi sitoi hoja,1,ndoa za mastaa huwa na mgogoro,1,nenda mwaya nenda,1,New Zanzibar Modern Taarab na wapenzi big up,1,news,5,Ni bikini kwa kwenda mbele,1,Ni Dar mpaka Moro au.. tatu bila,1,ni furaha za muungano,1,Ni kazi ngumu yenye kuhifadhi utamaduni,1,Ni kuchakarika kuonyesha urafiki na biashara pia,1,ni mfumuko wa bei au mfumuko wa nchi,1,Ni muhimu kutazama afya yako,1,ni muziki kwa kwenda mbele,1,Ni muziki mpaka China,1,Ni raha tupu,1,Ni Serengeti Premium Lager,1,Ni Tigo na mawasiliano ya kisasa,1,Ni wakati wa kuujadili utamaduni,1,Ni zaidi ya jazz,1,Nitasubiri and welcome home,1,nje je?,1,NUKUU YA LEO,1,nyie mnasemaje kuhusu hili,1,Ona Kolelo na sindikizwa na Wazee wa Gwasuma,1,ona vya dunia,1,One step ahead,1,patna mwingine mjamzito,1,Pengine anamuogopa Jada Pinkett manake kwa wivu..,1,picha,494,Pole Jamila hayo ndiyo mashindano,1,poleni sana,1,poleni sana wanyalukolo,1,Powa sana,1,Profesa jamaa wanakumaindi,1,Roho za marehemu zipate pumziko la milele,1,Ruvuma,9,sakata dansi mpaka kwenye kilele cha dunia,1,sasa kumebakia ugonjwa mmoja polisi kuendesha mashtaka,1,sasa mifedha kila mahali hongereni,1,Sasa ni mavuno,1,Sasa ni wakati wa kutafuta upenyo ndani ya IDOLS,1,SAYANSI,1,SAYANSI ANGA,1,See Uluguru Montains,1,serikali inataka kujihami kwanini,1,Show of support Big Up Madame,1,Si kitu kidogo hata kidogo,1,si unajua tena namie naimwaga hivyo hivyo,1,Siasa,346,siasa habari,2,Sijui kama City wanajua Mbagala noma,1,Sijui tunaishi karne gani yailahi,1,Sinema,9,sio advencha....kaaa ...niko kibaruani,1,Sisi ndio tunaanza vitongoji,1,Sisi yetu macho na masikio,1,Slow slow jamani,1,sto,1,tabasamu kali la mwenge wa olimpiki,1,Tabora,1,Tazama Waziri Mkuu Pinda wasije wakapindisha maamuzi yako,1,TEKNOLOJIA,1,Thats big man game,1,This is crazy Africa,1,This is Mgeta,1,Tibet wamegeuza Olimpiki jukwaa la siasa,1,Titbits collection,1,Tubadili tamaduni,1,Tuchangie mambo yaive,1,tuendeleze sanaa,1,tuienzi na sisi mbona wizara haituambii,1,Tuipeleke kaskazini,1,Tuisaidie serikali shida ya Mererani,1,tujue namna ya kupumzika,1,Tulienda kustarehe au kufanya fujo,1,Tumsaidie mtototo huyu kurejea katika hali ya kawaida,1,tunahitaji haya,1,Tunajifunza kweli kutoka kwao,1,Tunapandisha chati tu,1,Tunasubiri,1,tunazidi kuhesabu siku,1,TUNAZISUBIRI ZA VINARA ADAR,1,Tuombe nafuu kwa wagonjwa,1,Tuombe rehema kwa mungu,1,Tuone yatufae,1,Tusingoje wengine watusemee,1,tutampa tafu kubwa Prof,1,tuuenzi utamaduni au vipi,1,Tuukuze na kuulinda,1,tuvipende,1,tuwalinde maalbino,1,Tuwe kweli wakweli,1,ubunifu siku zote hulipa,1,uchumi huzunguka kwa kuwawezesha wasukaji,1,udumu muungano,1,Ugonjwa huu wa sasa ni kitendawili,1,Ukiiona kolelo utaipenda,1,Ukirejea salama kila mtu anafurahi,1,Umelenga Mkuchika utamaduni unakufa,1,unaposaka uwakilishi wa dunia,1,urafiki,1,Usisahau wazee wa Ngwasuma,1,UTAMADUNI,1,Video,2,Vionjo vipya ndani ya Gwasuma,1,Vita dhidi ya ufisadi,1,vitongoji Miss Tanzania navyo vimeanza,1,Vitu vikali vyazidi kuingia Dar,1,Vituko,77,Vituo vya polisi Tanga vyatelekezwa,1,VIVALO,1,Wacha tujifue,2,Wadau ilitolewa kiingereza,1,wakali wa ubunifu,1,wala usibabaike mwakwetu hii noma,1,wanadamu wanapotaka kujua zaidi,1,wanasema mpaka kieleweke,1,Wanataka kujua mali za JK na wengine,1,Wanawake wenye mvuto: Monroe,1,Wapo mabinti wa matawi ya juu,1,watu wanapofanya weli kwenye sanaa,1,waweza kurejea enzi ya Moro jazz na Cuban malimba,1,Wazee tupo kusindikiza,1,waziri,1,welcome dar baby,1,Wenzetu wameona sisi tunangoja nini kuangalia,1,wewe unasemaje,1,wigo mpana wa utamaduni,1,wilaya ya 'Mbagala' mlie tu,1,Yaaani sijui itawezekana,1,Yaani wakati mwingine hata huelewi prioty over priority,1,yeye mbele sisi nyuma,1,Yote maisha dada,1,ZA MOTOMOTO,1,Zanzibar,79,zawadi zinatakiwa ziende shule,1,ZILIZOTIA FORA,1,zitachangia kupunguza makali ya bei za umeme,1,
ltr
item
Lukwangule Entertainment: Kuna njaa inanukia nchini tanzania--JK
Kuna njaa inanukia nchini tanzania--JK
Lukwangule Entertainment
https://lukwangule.blogspot.com/2009/03/kuna-njaa-inanukia-nchini-tanzania-jk.html
https://lukwangule.blogspot.com/
http://lukwangule.blogspot.com/
http://lukwangule.blogspot.com/2009/03/kuna-njaa-inanukia-nchini-tanzania-jk.html
true
934549962738256429
UTF-8
Loaded All Posts Not found any posts VIEW ALL Readmore Reply Cancel reply Delete By Home PAGES POSTS View All RECOMMENDED FOR YOU LABEL ARCHIVE SEARCH ALL POSTS Not found any post match with your request Back Home Sunday Monday Tuesday Wednesday Thursday Friday Saturday Sun Mon Tue Wed Thu Fri Sat January February March April May June July August September October November December Jan Feb Mar Apr May Jun Jul Aug Sep Oct Nov Dec just now 1 minute ago $$1$$ minutes ago 1 hour ago $$1$$ hours ago Yesterday $$1$$ days ago $$1$$ weeks ago more than 5 weeks ago Followers Follow THIS CONTENT IS PREMIUM Please share to unlock Copy All Code Select All Code All codes were copied to your clipboard Can not copy the codes / texts, please press [CTRL]+[C] (or CMD+C with Mac) to copy