HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO W...
HOTUBA
YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA KUMI WA BUNGE LA
MUUNGANO, DODOMA TAREHE 08 FEBRUARI, 2013
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, tumekuwepo hapa Bungeni, Dodoma kwa takriban siku
11 ambapo leo tunahitimisha shughuli zilizopangwa katika Mkutano wa Kumi wa
Bunge lako Tukufu. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa
Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
2.
Mheshimiwa
Spika, awali ya yote naomba nitumie nafasi hii kutoa pole
kwa Ndugu, Jamaa na Marafiki waliopoteza Wapendwa wao katika ajali mbalimbali
zilizotokea hapa Nchini, ikiwemo ajali ya Jahazi la Sunrise iliyotokea Wangwi katika Bahari ya Hindi na Ajali ya Lori
kule Mbarali ambapo Watu wamepoteza maisha na kupata majeraha. Aidha, tunawapa
pole Majeruhi wote na Abiria waliopoteza mali katika ajali hizo. Kwa kipekee
kabisa napenda kutoa pole kwa Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Askofu Thomas Laiser
wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati - Arusha ambaye amefariki jana Mchana na
Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Moshi ambaye amefariki Usiku wa kuamkia leo huko Nairobi
alikokuwa anapata matibabu. Wote
tunawapa pole sana!
SHUGHULI ZA BUNGE
a)
Maswali
3.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu jumla ya Maswali 116 ya Msingi na 286 ya nyongeza yalipatiwa majibu. Vilevile, Maswali 6 yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu
wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
b) Miswada
4.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu, Miswada ifuatayo ilisomwa kwa mara
ya Kwanza:
i)
Muswada wa Sheria ya Vyama vya Ushirika wa Mwaka
2013 [The Cooperative Societies Bill,
2013]; na
ii)
Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa
Mwaka 2013 [The Written Laws
Miscellaneous Amendments, Bill 2013].
5.
Mheshimiwa
Spika, Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa
Mwaka 2012 [The Written Laws
Miscellaneous Ammendments (No. 3) Act, 2012] ulisomwa kwa mara ya Pili na
kupitia ngazi zake zote;
c) Hoja Binafsi za Wabunge
6.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu, pia Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya
kuwasilisha Hoja Binafsi kama ifuatavyo:
i)
Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba,
Mbunge wa Iramba Magharibi ya kuitaka Serikali iwasilishe Bungeni Muswada wa
Sheria ya Uanzishwaji wa Mfuko wa Elimu ya Juu (The Higher Education Fund Act);
ii)
Hoja Binafsi ya Mheshimiwa James Francis Mbatia,
Mbunge wa Kuteuliwa kuhusu udhaifu ulioko katika Sekta ya Elimu Nchini;
iii)
Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea
Kigwangalla, Mbunge wa Nzega ya kuitaka Serikali ianzishe Mpango Maalum wa
Kukuza Ajira kwa Vijana na kuanzisha Mfuko wa Mikopo ya Vyama Wanaowekeza
kwenye Kilimo na Viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja na Kilimo; na
iv)
Hoja Binafsi ya Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa
Ubungo juu ya Kuboresha Upatikanaji wa Maji Safi na ushughulikiaji wa Maji Taka
katika Jiji la Dar es Salaam.
d) Maazimio
7.
Mheshimiwa
Spika, vilevile, katika
Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kujadili na kupitisha Maazimio Mawili
yafuatayo:
i)
Azimio la Bunge la Kujiunga na Mkataba wa Kuzuia na
Kuadhibu Uhalifu Dhidi ya Watu wenye Kinga ya Kimataifa pamoja na Wakala wa Ki-Diplomasia
(Convention on The Prevention and
Punishment of Crimes Against Internationally Protected Persons Including
Diplomatic Agents 1973); na
ii)
Azimio la Bunge la Kujiunga na Mkataba wa Kimataifa
wa Kuzuia Vitendo vya Ugaidi wa Kutumia Nyuklia (International Convention for Suppression of Act of Neuclear Terrorism, 2009).
Ninawashukuru
Waheshimiwa Wabunge kwa kukamilisha Mijadala hiyo.
UJENZI WA UMOJA WA KITAIFA
8.
Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya pekee Taifa letu limejaliwa na
Mwenyezi Mungu kutimiza miaka zaidi ya
51 sasa ya Uhuru likiwa bado
linaendelea kudumisha Umoja wa Kitaifa. Umoja huu
wa Kitaifa umejengwa kwenye nguzo na misingi imara ya Amani, Utulivu na Mshikamano.
Mimi naamini sote tunapaswa kujivunia Umoja huu wa Kitaifa ambao ni Tunu kubwa
na nguzo muhimu ya maendeleo yetu. Msingi mkubwa wa Umoja wa Kitaifa
tunaoshuhudia leo uliwekwa na malezi mazuri ya Waasisi wa Taifa hili
wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Amani
Karume. Aidha, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza, pamoja na
mambo mengine, kujenga Jamii inayozingatia misingi ya Uhuru, Haki, Udugu na
Amani. Ni jukumu la kila Mwananchi kulinda Umoja huu ambao hauna mbadala.
9.
Mheshimiwa
Spika, Nchi yetu ina Makabila zaidi ya 120 ambayo kwa Mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya
Mwaka 2012 yamefikisha Idadi ya Watu Milioni
44.929. Aidha, hivi sasa tuna Madhehebu ya Dini yaliyoandikishwa takriban 885 na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
zaidi ya 6,675 na tumejenga
Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa ambapo hadi sasa tuna Vyama vya Siasa 19 ambavyo vimepata Usajili wa Kudumu.
Licha ya kuwepo kwa Idadi kubwa ya Watu wa Makabila tofauti yenye desturi
mbalimbali na makundi mbalimbali ya Madhehebu ya Dini, Itikadi za Kisiasa na
Watu wenye Rangi mbalimbali, bado tunajivunia kwamba tunaheshimiana na
hatubaguani kwa namna yoyote ile. Hali hii ya amani imeipatia Nchi yetu sifa
Kitaifa na Kimataifa na mfano wa kuigwa.
10.
Kutokana na Demokrasi pana iliyopo, Wananchi wetu
wana Uhuru mkubwa wa kutoa maoni, kuanzisha na kujiunga na Vyama vya Siasa
pamoja na kushiriki katika kuchagua Viongozi wa Chama chochote wanachokipenda
kwa kuzingatia Misingi ya Katiba na Sheria za Nchi. Vilevile, Serikali imetoa
uhuru mkubwa wa kupata na kutoa habari kwa uwazi bila vikwazo vyovyote kwa
kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni mbalimbali na Maadili ya Vyombo vya Habari.
Kutokana na Uhuru huo, Idadi ya Vyombo vya Habari imeongezeka sana ambapo hadi
sasa Idadi ya Vituo 86 vya Redio vilivyopewa
Leseni na vinafanyakazi, Vituo vya Televisheni 26 na Magazeti 768
yaliyoandikishwa na yanayotolewa na Taasisi mbalimbali.
11.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na mafanikio hayo yanayodhihirika wazi, hivi
karibuni kumekuwepo na dalili za kupoteza sifa yetu nzuri ya Umoja wa Kitaifa
na Amani ambayo imedumu kwa miaka mingi. Tumeshuhudia Wananchi mmoja mmoja
wakishindwa kuvumiliana, japo kwa tatizo dogo tu miongoni mwao. Aidha,
tumeshuhudia Vyama vya Siasa vikionesha dalili ya kuhamasisha Wanachama wao
kuingia kwenye malumbano ya
Siasa baina yao
wenyewe kwa wenyewe au baina ya Chama kimoja cha Siasa na
Chama kingine. Baadhi ya Wanachama wameshikana mashati na kujeruhiana.
12.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa hii kuwaasa Viongozi wa Vyama
vya Siasa kuepuka kutumia majukwaa ya Siasa kuvuruga Amani yetu na Utulivu
uliopo. Waepuke matamko ya vitisho na kuhamasisha Wanachama wao kuendeleza
vitendo vya uvunjifu wa amani na kujenga chuki na uhasama miongoni mwa Jamii na
kwa Serikali halali iliyopo madarakani.
Pamoja na kutofautiana kwa mawazo na Sera za Vyama vya Siasa, ni muhimu
tujenge mazingira ya kuvumiliana kwa hali ya juu katika kujenga Demokrasia ya
kweli hapa Nchini. Viongozi wa Vyama wanatakiwa kueleza Sera zao badala ya
kutukanana, kubezana, kushutumiana na kuzomeana. Tujenge Nchi yetu kwa Amani na
Utulivu ndipo tutapata maendeleo endelevu.
13.
Mheshimiwa
Spika, tumeshuhudia pia kuibuka kwa choko choko za Kidini.
Baadhi ya Waumini wa Dini wamekuwa wakikashifu Dini nyingine kwa kejeli na
vitendo vingine visivyostahili. Aidha, baadhi ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini wamekuwa
wakiwaingiza Waumini wao katika Migogoro isiyoisha, ikiwa ni pamoja na
kufungiana milango na kuzuia Waumini Wasiabudu siku za Ibada. Napenda kusisitiza
kuwa Madhehebu ya Dini yana nafasi kubwa ya kujenga Umoja wa Kitaifa, Amani na
mshikamano. Nawaomba Viongozi wa Madhehebu ya Dini kutatua kwa amani migogoro
iliyopo na kuelimisha Waumini wao kuthamini, kujenga na kuenzi Amani na Utulivu
uliopo Nchini. Serikali imetoa uhuru wa Wananchi wake Kuabudu, kila mtu kwa
Dini anayoitaka. Hivyo, hakuna sababu ya Dini moja kukashifu Dini nyingine. Aidha,
tupinge kwa nguvu zetu zote choko choko za Kidini ambazo zimeanza kujitokeza
katika sehemu mbalimbali Nchini.
14.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali baadhi
yao yamekuwa yakihusishwa kuwa mstari wa mbele katika kuwarubuni Wananchi
kufanya vurugu zinazolenga kuleta uvunjifu wa Amani. Napenda kusisitiza kuwa
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yana jukumu kubwa la kuelimisha Wananchi kuhusu
umuhimu wa kujenga Umoja wa Kitaifa. Viongozi wa Mashirika haya waepuke
kutumiwa na baadhi ya Viongozi kujenga mbegu mbaya kwa Wananchi kuvuruga Amani.
15.
Mheshimiwa
Spika, nigusie pia Vyombo vya Habari, ambapo kumekuwa na
kutiliana mashaka kwa baadhi ya Vyombo hivyo kuandika habari za Uchochezi,
hivyo kuashiria Uvunjifu wa Amani na Mshikamano wa Kitaifa tuliojijengea.
Vyombo vya Habari vina wajibu mkubwa wa kuelimisha Umma na kuhabarisha kuhusu masuala
mbalimbali ya maendeleo, kama wafanyavyo wenzetu jirani, husan Vyombo vya
Habari vya Nchi ya Rwanda. Aidha, Vyombo hivi vina fursa nzuri ya kutumia uhuru
uliopo kudumisha Amani na Utulivu Nchini.
Tufanye
Nini
16.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na changamoto zilizopo za baadhi ya Watu
waotaka kubomoa Umoja wa Taifa letu na kuhatarisha Amani na Utulivu Nchini, sisi
kama Taifa hatuna budi kufanya yafuatayo:
i)
Serikali, Wananchi na Wadau wote ikiwemo Vyama vya
Siasa, Madhehebu ya Dini, Vyombo vya Habari, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali,
n.k. tunapaswa tukae chini tuzungumze na kutafakari kuhusu hali hii;
ii)
Tunapaswa kwa namna zote tuvumiliane na
kuheshimiana kwa kuzingatia Utamaduni wa Kitanzania na Misingi ya Amani na
Utulivu tuliojijengea kwa muda mrefu; na
iii)
Wananchi wote tuzingatie na kuheshimu Utawala Bora
wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
17.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa hii kuwaomba sana Wananchi na
Watanzania wenzangu kuendeleza umoja na mshikamano
wa Kitaifa ili kudumisha Amani na
Utulivu uliopo Nchini. Ni vyema kutambua
kuwa Amani na Utulivu uliopo Nchini ni mazingira wezeshi
ya kusaidia kila mmoja wetu kufanya
shughuli zake za kijamii na kiuchumi na kujiletea maendeleo. Bila Amani na Utulivu hakuna maendeleo ya
Watu. Kwa upande wa Serikali itahakikisha kwamba, Umoja tuliojijengea
unadumishwa. Taasisi mbalimbali za Serikali, zikiwemo Vyombo vya Dola ni lazima
zihakikishe kwamba, Wananchi wanaishi kwa Amani na Utulivu. Vilevile,
kuhakikisha kuwa, Umoja wa Kitaifa tulioujenga kwa miaka mingi haupotei. Naziomba
Taasisi zote zinazohusika na kusimamia Amani na Usalama kuhakikisha kuwa,
pamoja na Changamoto zilizopo, Umoja wa Kitaifa unadumishwa.
HALI YA CHAKULA NCHINI
i)
Hali
ya Mazao na Mvua
18.
Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika
hivi karibuni juu ya upatikanaji wa chakula Nchini na athari za mvua
zinazoendelea kunyesha, inaonesha kuwa maeneo mengi hasa, yale yanayopata mvua
za msimu kama vile Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Iringa, Tabora, na Mtwara mazao mengi
yapo katika hatua mbalimbali za ukuaji. Inatarajiwa kwamba, endapo mvua hizi
zitaendelea vema, upatikanaji wa chakula katika maeneo hayo utakuwa mzuri.
19.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na hali hiyo ya hewa, tathmini ya kina ya
hali ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi Januari 2013 inaonesha upungufu wa
chakula katika Wilaya 47 zilizoko
katika Mikoa 15 ambazo zitahitaji
msaada wa chakula katika vipindi tofauti. Inakadiriwa kuwa jumla ya Watu 1,615,445 watahitaji jumla ya Tani 32,870 za chakula.
ii) Hatua Zinazochukuliwa na Serikali
20.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na matarajio hayo ya uhaba wa Chakula,
Serikali itahakikisha kuwa Kitengo cha Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA)
kinaendelea kusambaza mahindi katika maeneo yenye uhaba wa chakula. Hadi sasa
jumla ya Tani 20,000 zilishatolewa
kwa Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Morogoro, Lindi,
Tanga, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na Tabora.
Aidha, Kitengo hicho (NFRA) kitaendelea kununua nafaka mapema baada ya mavuno
ili kuhakikisha kuwa Serikali ina hifadhi ya kutosha ya chakula kwa ajili ya
kusambaza katika maeneo yatakayokuwa na uhaba wa chakula. Hadi tarehe 6
Februari 2013 Ghala la Taifa la Chakula lilikuwa na jumla ya Tani 68,712.9 za mahindi pamoja na Tani 3,335.989 za Mtama.
21.
Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya
upatikanaji wa chakula Nchini na kuhakikisha kuwa hakuna Mwananchi
atakayepoteza maisha kutokana na njaa. Nitoe wito kwa Wananchi kuendelea kuweka
utaratibu wa kuhifadhi sehemu ya mavuno yao baada ya kuvuna kwa ajili ya akiba
ya baadaye badala ya kuuza mavuno yao yote.
MAPAMBANO
DHIDI YA UGONJWA WA MALARIA NCHINI
i)
Hali
Halisi ya Ugonjwa wa Malaria Nchini
22.
Mheshimiwa
Spika, Nchi yetu inayo changamoto kubwa ya kukabiliana na
Magonjwa makubwa Duniani, yakiwemo Malaria, Kifua Kikuu, UKIMWI, Saratani, n.k.
Niruhusu leo katika Hotuba yangu nizungumzie kidogo kuhusu Ugonjwa wa Malaria. Ugonjwa
wa Malaria bado unaongoza kuwa sababu kubwa za Wagonjwa wengi wanaohudhuria
katika Vituo vya huduma za Afya Nchini. Aidha, ugonjwa huu unaongoza kwa
kusababisha vifo, hasa kwa Watoto walio chini ya umri wa miaka Mitano. Takwimu
kutoka Vituo vya kutolea huduma ya Afya Nchini zinaonesha kuwa, takriban
Wagonjwa Milioni 11 hadi 12 huhudhuria katika Vituo vya huduma
za Afya kwa sababu ya ugonjwa wa Malaria. Vilevile, tafiti zilizofanyika katika
Jamii [Tanzania HIV/Malaria Indicator
Survey (THMIS) 2011/2012] zinaonesha kuwa Asilimia 10 ya Watoto katika Kaya wana maambukizi ya vimelea vya
ugonjwa wa Malaria.
ii) Jitihada za Serikali katika kumaliza
tatizo la Malaria Nchini
23.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na tatizo hili
katika kuhakikisha Wananchi wanaendelea kujikinga na maambukizi dhidi ya
ugonjwa wa Malaria, Serikali imefanya mambo muhimu yafuatayo:
Moja: Kutekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa
Mapambano Dhidi ya Ugonjwa wa Malaria wa Miaka Mitano (2008-2013) ambao una
lengo la kupunguza vifo kwa Asilimia 80 ifikapo mwaka 2013 mwishoni.
Utekelezaji wa Mpango huu unafanyika kwa kushirikiana na Mikoa, Wilaya na Wadau
mbalimbali hadi katika ngazi ya Jamii;
Pili: Kusambaza
na kuongeza matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu katika Kaya.
Hadi sasa zaidi ya vyandarua Milioni 26 vimesambazwa kupitia Kampeni
iliyolenga Watoto wenye umri chini ya miaka Mitano;
Tatu: Kutekeleza
Mpango wa Hati Punguzo unaolenga kuhakikisha Akina Mama Wajawazito na Watoto
wanaozaliwa wanaendelea kupata vyandarua hivyo na kujikinga dhidi ya ugonjwa wa
Malaria;
Nne: Kuendeleza
Mpango wa kunyunyizia dawa ya ukoko majumbani ili kutokomeza mazalia ya Mbu.
Mpango huo unaendelea kutekelezwa katika Mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara ambapo
zaidi ya Kaya 1,440,000 sawa na Asilimia 90 katika Wilaya za Mikoa
hiyo zitanyunyiziwa viuatilifu. Kutokana na Mpango huo, zaidi ya Watu 6,500,000
wameendelea kukingwa dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Malaria;
Tano: Kuendeleza
Mpango wa kuangamiza viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia njia za Kibaiolojia. Mpango
huu ambao unafanywa na Serikali kwa ushirikiano na Serikali ya Nchi ya Cuba
unatekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam kuanzia mwaka 2011;
Sita: Kutumia
Mwongozo wa kutibu ugonjwa wa Malaria isiyo kali kwa kutumia Dawa ya Mseto ya Artemether/Lumefantrine (ALu). Mwongozo
huu unaendelea kutumika katika Vituo vyote vya Umma vya kutolea huduma za Afya;
na
Saba: Kusambaza
kipimo cha haraka cha kutambua na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya Malaria
kwenye damu katika Vituo vyote vya Umma vya kutoa huduma za afya Nchini.
iii) Changamoto
24.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo makubwa yaliyopatikana,
bado kuna changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi. Changamoto hizo ni
pamoja na:
Moja: Kujitokeza
kwa usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu vya aina ya “pyrethroids” vinavyotumika katika vyandarua na unyuziaji dawa ya
ukoko majumbani;
Pili: Kupata
vyanzo zaidi vya fedha za ndani za kuendeleza mkakati wa unyunyiziaji dawa ya
ukoko majumbani;
Tatu: Uwezo
mdogo wa uzalishaji wa dawa za kuangamiza viluwiluwi vya Mbu na kuanza
kuangamiza Viluwiluwi hivyo katika Jiji la Dar es Salaam; na
Nne: Kuendeleza
uhamasishaji Wananchi kutumia nyenzo na kushiriki katika mikakati iliyopo, hasa
inayohitaji ushiriki wao wa moja kwa moja, kama kuharibu mazalia ya Mbu.
iv) Matarajio ya Mkutano wa United Against Malaria – Afrika Kusini
25.
Mheshimiwa
Spika, katika juhudi za kupambana na Malaria Duniani,
Shirika la Roll Back Malaria Partnership
wakishirikiana na Wizara ya Afya ya Afrika Kusini wanatarajia kufanya Mkutano
mkubwa unaohusu mapambano dhidi ya Malaria kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) kuanzia tarehe 9 - 11 Februari, 2013. Mkutano huo
unatarajia kukutanisha Viongozi wa ngazi ya juu kutoka Nchi za SADC ikiwa ni
pamoja na baadhi ya Marais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri wa Afya na
Mawaziri wa Michezo katika Nchi hizo.
Mkutano huo pia utajumuisha Viongozi wa juu wa Makampuni mbalimbali ya Sekta
Binafsi.
26.
Mheshimiwa
Spika, lengo la Mkutano huo ni kukutanisha Viongozi
mbalimbali kwa lengo la kuendesha mjadala kuhusu janga la Malaria katika Nchi
za Afrika; ikizingatiwa kuwa ufadhili wa utekelezaji wa mikakati mbalimbali
unazidi kupungua. Mkutano huo unategemewa kuwa chachu kwa Viongozi kuongeza
Bajeti za udhibiti wa Malaria Nchini mwao na kuongeza ushirikiano na Sekta
Binafsi pamoja na Sekta ya Michezo, hususan katika Mpira wa Miguu katika dhana nzima ya Mpango wa “Safe Companies”. Aidha, Mkutano huo unatarajiwa kuongeza kasi ya Kupambana dhidi ya
ugonjwa wa Malaria katika Nchi hizo.
27.
Ni matumaini yangu kuwa, Mkutano huo utakuwa wa
mafanikio makubwa kwa Nchi za Kusini mwa Afrika katika vita dhidi ya ugonjwa wa
Malaria. Vilevile, utatupatia uzoefu kwa Nchi yetu katika kupambana na Ugonjwa
huu wa Malaria.
v) Jitihada za Chama cha Wabunge cha
Kupambana na Malaria
28.
Mheshimiwa
Spika, katika jitihada za kupambana na Malaria Nchini, Muungano wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania walianzisha Asasi inayojulikana kama Tanzania Parliamentary Against Malaria
(TAPAMA). Lengo la kuanzishwa kwa Asasi hii ni kuongeza utashi wa Kisiasa
katika kushiriki na kutekeleza Mpango na
Sera ya Taifa ya kutokomeza Ugonjwa wa Malaria Nchini. Asasi hii ilisajiliwa
mwaka 2008 na hadi sasa imetekeleza masuala mbalimbali katika jitihada zake za
kupambana na Malaria Nchini kama ifuatavyo:
Moja: Ugawaji wa Vyandarua kwa Watoto
wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa Mikoa ya Ruvuma, Kilimanjaro
na Mwanza ambapo zaidi ya Watoto 2,500
walifaidika na huduma hii;
Pili: Kufanya mazungumzo na Wawakilishi wa
Bunge la Jumuiya ya Ulaya mwaka 2009 waliotembelea Tanzania na kuona uwezekano
wa Jumuiya ya Ulaya kusaidia zaidi Mapambano dhidi ya Malaria Tanzania. Aidha,
walifanya mazungumzo na Viongozi na Wawakilishi wa Asasi ya Malaria
No More ya Marekani, ambao waliongozwa na Balozi Mark Green na kuwezesha kuanza kwa Mradi wa Zinduka, Malaria Haikubaliki;
Tatu: Kushiriki Kikao cha Nchi za Jumuiya ya Ulaya Nchini
Ufaransa mwaka 2009 ili kujadili juhudi za Viongozi wa Kisiasa katika
Kupamabana na Malaria Nchini;
Nne: Kushiriki kutayarisha Mwongozo (Advocacy Guideline) utakaotumiwa na
Wabunge, Madiwani na Viongozi wengine wa Kisiasa na Kijamii katika Utekelezaji
na ushawishi wao katika kutokomeza Malaria Tanzania.
29.
Mheshimiwa
Spika, nachukua fursa hii kuwapongeza Wajumbe wote wa
TAPAMA chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Riziki Said Lulida, Mbunge wa Viti Maalum
kwa juhudi zao za kuhakikisha kuwa wanaungana na Wadau wengine Nchini na
Duniani katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria. Nazipongeza pia Taasisi Zisizo za
Kiserikali kwa ujumla wao ambazo zimejitokeza katika Mapambano dhidi ya
Magonjwa mbalimbali, yakiwemo UKIMWI, Kifua Kikuu, Saratani, n.k. Tunawaomba
Waheshimiwa Wabunge zaidi wazidi kujiunga na Asasi hizi na hasa za Magonwa ili
kuweka hamasa kwa Wananchi katika Kupambana na Maradhi hayo. Aidha, natoa wito
kwa Wananchi wote kwa ujumla kuunganisha nguvu za Kupambana na Ugonjwa huu wa
Malaria ili kunusuru nguvukazi ya Watanzania. Suala kubwa ni kuzingatia
masharti ya Wataalam kuanzia katika kutunza mazingira yetu na kutumia Vyandarua
kama kinga iliyo ya uhakika.
LISHE
30.
Mheshimiwa
Spika, wakati nikitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge, mwezi Novemba, 2012 nilieleza
kwa kifupi utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa
Lishe wa Mwaka 2011/2012 – 2015/2016. Pamoja na mambo mengine nilionesha hatua
ambazo Serikali inachukua kuondokana na tatizo
la Lishe Nchini. Jambo kubwa na la msingi katika kupambana na
tatizo la Lishe ni kutoa elimu kwa Jamii ili kula vyakula vyenye Virutubisho
muhimu hasa kwa Mama Wajawazito na Watoto Wachanga. Jitihada za Serikali za
kuwashirikisha Wadau mbalimbali katika kutoa Elimu ya Lishe Nchini zimeleta
mwamko mzuri ambapo Wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa,
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Wadau wa Maendeleo sasa wanashiriki kikamilifu
katika utoaji elimu na kukuza kilimo cha mazao yenye virutubisho muhimu ili
kuongeza vyakula vyenye virutubisho.
31.
Mheshimiwa Spika, katika kuunga mkono
jitihada za Serikali za kupambana na tatizo la Lishe Nchini, hivi karibuni
Waheshimiwa Wabunge chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Lediana Mafuru Mng’ong’o
Mbunge wa Viti Maalum wameunda Kikundi cha kuongeza hamasa na kuzidisha chachu
ya kutoa elimu kuhusu Lishe Bora hapa Nchini. Nimearifiwa kwamba, Kikundi hicho
cha Wabunge kimekutana tarehe 10 hadi 12 Januari, 2013 na kukubaliana kuhusu
kazi ambazo watafanya ili kuongeza sauti yao kwenye jamii juu ya umuhimu wa
Lishe Bora. Kikundi pia kimeandaa Mpango
Mkakati wa Miaka Mitatu (2013-2015) wenye malengo ya kukuza uelewa wa Umma juu
ya Lishe, Chakula na Haki za Watoto. Aidha, kikundi hicho kiliazimia kushawishi
uwekaji wa vipaumbele vya Lishe katika Mipango ya Maendeleo na Bajeti za
Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuingiza masuala ya Lishe,
Chakula na Haki za Watoto katika Sera na Mikakati mbalimbali ya Serikali.
Azimio lingine ni kuimarisha usimamizi wa kazi za Bunge kuhusu Lishe, Chakula
na Haki za Watoto.
32.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua
fursa hii kukishukuru kwa dhati kikundi hiki ambacho kimeona umuhimu wa kuunga
mkono juhudi za Serikali za kupambana na tatizo la Lishe, ikiwemo Utapiamlo. Nitumie
fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuanzisha kikundi hiki.
Niwashukuru kwa kuona umuhimu wa kusimamia tatizo hilo ili kupata suluhu ya
kudumu. Ninatambua pia umuhimu wa Waheshimiwa Wabunge kuhamasisha masuala ya
Lishe kwa Wananchi wa Majimbo yao. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wengine wote
kushiriki kutoa msukumo wa pekee kwa Wananchi wa Majimbo yenu katika Mapambano
dhidi ya Utapiamlo ili kwa pamoja tujenge Taifa lenye Watu walio na Lishe Bora.
Lengo ni kuwawezesha kuchangia zaidi katika uzalishaji mali na ukuaji wa uchumi
wa Nchi kwa ujumla.
MCHAKATO KUELEKEA
KATIBA MPYA
33.
Mheshimiwa
Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba imetangaza kumaliza kazi ya kukusanya maoni binafsi ya
Wananchi mmoja mmoja kama mchango wao kwa ajili ya kuandika Katiba Mpya. Aidha,
imekamilisha kazi ya kukutana na Makundi Maalum, Viongozi wa Kitaifa Wastaafu
na Viongozi wa Kitaifa waliopo Madarakani. Kwa maana hiyo, Tume sasa
imekamilisha kazi ya ukusanyaji maoni kama ilivyopangwa. Hivi sasa Tume
inaendelea na kazi za uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na Wananchi na yale yaliyotolewa
na Makundi Maalum ili baadaye kutayarisha Rasimu ya Katiba ambayo itawasilishwa katika Mabaraza ya Katiba yatakayoitishwa na
Tume Nchini kote.
34.
Kulingana na Ratiba, Mikutano ya Mabaraza ya Katiba
itafanyika kuanzia mwezi Juni, 2013 na itajumuisha Wajumbe watakaochaguliwa na
Wananchi wenyewe kuanzia ngazi ya Kijiji. Wajumbe hao ndio watapaswa kuwasilisha
maoni ya Wananchi katika Mikutano ya Mabaraza.
35.
Mheshimiwa
Spika, nimearifiwa kuwa Tume imeandaa Rasimu ya Mwongozo
wa namna bora na ya Kidemokrasia ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
ambao unaendelea kusambazwa Nchi nzima. Mwogozo huo tayari umetangazwa katika
Vyombo vya Habari ili Wananchi waufahamu na kutoa maoni kuhusu namna ya
kuuboresha.
36.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Rasimu hiyo ya Mwongozo, katika Mikoa
ya Tanzania Bara ukiondoa Mkoa wa Dar es Salaam, kila Kata itawakilishwa na
Wajumbe wanne (4) watakaochaguliwa kutoka miongoni mwa Wakazi wa Vijiji
vilivyopo kwenye Kata ambao wataungana na Madiwani wa Kata na Madiwani wa Viti
Maalum kuunda Baraza la Katiba la Wilaya. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Tume
imeandaa utaratibu tofauti wa kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
ambapo kila Kata watatoka Wajumbe wanane (8) ambao wataungana na Madiwani wa
Kata na Madiwani wa Viti Maalum. Kwa
msingi huo, kutakuwa na jumla ya Wajumbe 18,169
watakaohudhuria Mabaraza ya Katiba ya Wilaya Kwa Tanzania Bara.
37.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa Zanzibar, kutakuwa na Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa 13. Kila Shehia itawakilishwa na Wajumbe watatu
(3), ambao wataungana na Madiwani wa Wadi, Madiwani wa Viti Maalum na Madiwani
wa kuteuliwa waliopo kazini kwa sasa. Kwa msingi huo, Wajumbe wote wa Mabaraza
ya Katiba kwa Zanzibar watakuwa 1,198.
38.
Wananchi wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya watatakiwa kuwasilisha majina
yao kwa Maafisa Watendaji wa
Vijiji na Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Tanzania Zanzibar watawasilisha
kwa Sheha kwa tarehe itakayoelekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba hapo
baadaye.
39.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutoa wito kwa Viongozi wote katika ngazi
za Wilaya na Serikali za Mitaa kusimamia kikamilifu utaratibu ambao umewekwa na
Tume. Kwa kufanya hivyo, Wajumbe ambao watashiriki katika Mabaraza ya Katiba watapatikana kwa njia
za Kidemokrasia na hivyo, kufanikisha
Vikao vya Mabaraza ya Katiba. Ni matumaini yangu kuwa Wananchi watausoma
Mwongozo huo, na baadaye kuwasilisha mapendekezo na maoni yao kwa Tume kabla ya
kazi ya uchaguzi wa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanza rasmi.
40.
Nitumie fursa hii kuwaomba Wananchi wote kushiriki
kikamilifu kutoa maoni kuhusu Mwongozo huo na pia katika kuwapata Wajumbe
watakaoshiriki katika Mabaraza ya Katiba kwa mujibu wa Sheria, na vilevile
Wajumbe hao washiriki kikamilifu katika Vikao vya Mabaraza ya Katiba na kutoa
maoni kwenye Rasimu ya Katiba.
RIPOTI
YA TATHMINI YA UTAWALA BORA AFRIKA (APRM)
41.
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza
dhamira ya uwazi na ujenzi wa pamoja wa utawala bora nchini kwa kuwashirikisha
Wananchi, Nchi yetu imekuwa miongoni mwa Nchi 33 za Umoja wa Afrika zilizoamua
kwa hiari yake kujiunga na Mpango wa Bara la Afrika wa Kujitathmini Kiutawala
Bora (The African Peer Review Mechanism -
APRM). Tanzania ilijiunga na mchakato huo mwaka 2004, na Bunge liliuridhia mwaka 2005.
42.
Mheshimiwa Spika, Mpango huu wa
kujithamini Kiutawala Bora ni muhimu kwetu na unaakisi Sera zetu na za Waasisi
wa Taifa hili juu ya Kujikosoa na Kujisahihisha. Aidha, unahusisha Viongozi wa
Afrika na unatoa fursa kwa Wananchi kutathmini hali ya Utawala Bora katika Nchi
zao na kuainisha kwa pamoja mambo mazuri yanayopaswa kuendelezwa na yale yenye
changamoto za kufanyiwa kazi. Miongoni mwa sababu za Nchi yetu kujiunga na
Mpango huu ni kutokana na ukweli kwamba Watanzania tuna mengi ya kuifundisha
Afrika na Watu wake kuhusu Utawala Bora na sisi pia kujifunza kutoka kwa
wenzetu.
43.
Mheshimiwa
Spika, ninayo furaha kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa
baada ya zoezi la muda mrefu la kukusanya maoni Nchi nzima kuhusu Mpango huu
ambapo Waheshimiwa Wabunge nao walishiriki kutoa maoni yao kuhusu Utawala Bora,
sasa hivi Nchi yetu, imefikia hatua muhimu katika Mchakato huo wa kujitathmini
kiutawala bora.
44.
Tarehe 26 Januari 2013, Ripoti ya Hali ya Utawala
Bora hapa nchini iliwasilishwa mbele ya Wakuu wa Nchi za APRM Addis Ababa,
Ethiopia ambapo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wetu alipata fursa
ya kuzungumzia mwelekeo wa Nchi yetu katika kujenga Taifa imara zaidi katika
kipindi cha miaka 50 ijayo.
45.
Mheshimiwa
Spika, katika Ripoti hiyo ambayo itatumika kama rejea,
zimeainishwa juhudi zetu kubwa za kulinda amani Nchini. Pamoja na kuimarisha
Utawala Bora wa Sheria na Haki za Binadamu. Aidha, kupitia Ripoti hiyo, wenzetu
katika masuala ya kuendesha Utawala Bora, Barani Afrika na Duniani kwa ujumla
wametambua jitihada zetu pamoja na mambo mengine katika kuulinda Muungano,
kuimarishwa kwa mapambano dhidi ya Rushwa na zaidi ya yote wamejua sura ya
Tanzania katika ukombozi na utetezi wa amani Afrika ambao Nchi yetu imepongezwa
sana kwa juhudi zake.
46.
Ripoti hiyo
pia imeainisha changamoto ambazo wenzetu wa Afrika wanadhani tunapaswa
kuzifanyia kazi zaidi. Changamoto hizo ni pamoja na suala la kushughulikia Kero
za Muungano, kuimarisha zaidi juhudi za kuondoa umaskini na kuilinda amani ya
Nchi yetu hasa kutokana na chokochoko za Kidini zilizoanza kujitokeza. Tumeaswa
kuutumia vyema mchakato wa sasa wa Mabadiliko ya Katiba kuijenga Tanzania bora
zaidi katika miaka 50 ijayo.
47.
Mheshimiwa
Spika, kuwasilishwa kwa Ripoti hiyo ya APRM kwa Wakuu wa
Nchi wa Mpango huu ndio mwanzo sasa wa Serikali yetu ya kuimarisha maeneo
yaliyoonekana kuwa tunafanya vyema. Pia hatua hiyo inatoa fursa ya kuanza
kutekeleza Mpangokazi wa Miaka Mitano ambao umeainisha namna gani ya kuyafanyia
kazi maeneo ambayo wananchi waliyaona kuwa yanapaswa kufanyiwa kazi zaidi.
Suala hili liliwekewa msisitizo na Mheshimiwa Rais katika Hotuba yake ya Mwisho
wa Mwezi Januari 2013 aliyoitoa kwa Taifa.
48.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na manufaa ya APRM kama daraja kati ya
Serikali na Wananchi wa kutatua matatizo yetu kwa pamoja, Serikali itaendelea
kuiimarisha Taasisi ya APRM hapa Nchini ili iweze kuwa kitovu chetu cha fikra (think tank) katika kushauri kuhusu
masuala ya Utawala Bora Nchini. Vilevile, kuiwezesha Taasisi hii kuendelea kuwa
kiungo kati ya Serikali yetu na Wananchi wake katika kutathmini na kutupatia
mrejesho juu ya mipango na Sera zetu za maendeleo.
49.
Aidha, Serikali itaendelea kufadhili shughuli za
APRM, kuiimarisha Taasisi kwa raslimali watu na fedha kwa ajili ya kazi pana
zaidi za kutoa ushauri, kuunganisha Wadau mbalimbali na kuendelea kuratibu
tathmini nyingine katika siku zijazo kwa lengo la kujipa nafasi ya kujikosoa
ili kujisahihisha. Napenda kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje,
Ulinzi na Usalama wakishirikiana na Sekretariati ya APRM Tanzania kwa kazi
nzuri waliyoifanya ambayo imetuwezesha kufikia mafanikio hayo.
UANZISHAJI
WA MAENEO MAPYA YA UTAWALA
i)
Uanzishaji
wa Mikoa na Wilaya
50.
Mheshimiwa
Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa, mwezi Machi
2012, Mheshimiwa Rais aliridhia kuanzisha Mikoa Mipya Minne (4) na Wilaya 19. Napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali sasa imekamilisha mchakato wa
kuanzisha maeneo hayo Mapya ya Utawala, kwa kuanzisha Mikoa Minne ya Geita,
Simiyu, Njombe na Katavi. Aidha, imekamilisha uanzishwaji wa Wilaya 19 za
Buhigwe, Busega, Butiama, Chemba, Gairo, Ikungi, Itilima, Kakonko, Kalambo,
Kaliua, Kyerwa, Mbogwe, Mkalama, Mlele, Momba, Nyang’wale, Nyasa, Uvinza na
Wanging’ombe. Mikoa na Wilaya hizo tayari zimeshaanza kufanya kazi na kutoa
huduma mbalimbali kwa Wananchi. Vilevile, Mheshimiwa Rais alishafanya Uteuzi wa
Viongozi Wakuu wa Mikoa na Wilaya Mpya. Serikali imeendelea kupeleka Watumishi
na kuanza kujenga miundombinu muhimu katika maeneo husika. Hata hivyo, pamoja
na dhamira njema ya Serikali ya kuanzisha maeneo hayo, bado zipo changamoto nyingi,
ikiwemo kupata Watumishi wa kutosha ambazo Serikali inaendelea kuzitatua.
ii)
Uanzishaji
wa Halmashauri
51.
Mheshimiwa
Spika, ili kupeleka huduma karibu zaidi kwa Wananchi,
Serikali pia iliazimia kuanzisha Halmashauri Mpya 37. Uanzishaji wa Halmashauri
hizo unaendelea na upo katika hatua mbalimbali kwa kuzingatia makundi
yafuatayo:
Kundi la Kwanza, linahusu Halmashauri Mpya 8 za
Manispaa, Miji na Jiji pamoja na Halmashauri Moja (1) ya Wilaya ambazo mchakato
wa uanzishaji wake tayari umekamilika Kisheria na zimeanza kufanya kazi. Kundi
hili linajumuisha Halmashauri za Jiji la Arusha, Manispaa ya Ilemela, Manispaa
ya Lindi, Halmashauri ya Mji wa Kahama, Halmashauri ya Mji wa Masasi,
Halmashauri ya Mji wa Makambako, Halmashauri ya Mji wa Geita, Halmashauri ya
Mji wa Bariadi na Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Halmashauri hizo tayari zimepata Hati na kupangiwa Wakurugenzi.
Kundi
la Pili, linajumuisha Halmashauri Kumi (10) ambazo mchakato
wa kuzianzisha umekamilika na tayari zimetangazwa katika Gazeti la Serikali la
tarehe 23 Novemba 2012. Halmashauri hizo ni Kalambo, Nsimbo, Mlele, Bumbuli,
Ushetu, Msalala, Mbogwe, Busega, Momba na Kyerwa. Halmashauri hizo kwa sasa
zinaandaliwa Hati ili zianze.
Kundi la Tatu, ni Halmashauri za Wilaya Kumi (10) ambazo mchakato
wa uhakiki wake umekamilika na Amri za Uanzishaji zimeshasainiwa na wakati
wowote zitatangazwa katika Gazeti la Serikali. Kundi hili linajumuisha
Halmashauri za Wilaya za Buhigwe, Kaliua, Nyang’hwale, Wanging’ombe, Chemba, Mkalama, Gairo, Nyasa, Itilima na Kakonko.
Aidha, zipo Halmashauri nyingine Nne (4) katika kundi hili ambazo Amri zake
zinakamilishwa na hatimaye zitasainiwa hivi karibuni. Halmashauri hizo ni Butiama,
Tarime, Uvinza na Ikungi.
Kundi la Nne, linajumuisha Halmashauri Nne ambazo Mchakato wa
uanzishaji wake umekamilika isipokuwa taratibu za Kisheria haziwezi kuanza kwa sababu
baadhi ya Kata katika Halmashauri hizo ni mpya, hivyo hakuna Madiwani.
Halmashauri hizo Nne (4) ni za Miji ya Kasulu, Handeni, Tunduma na Nzega. Mathalani, katika Halmashauri ya Mji wa
Kasulu kuna Kata 14, na kati ya hizo, Kata 6 ni mpya na hazina Madiwani. Kwa
upande wa Halmashauri ya Mji wa Handeni ina jumla
ya Kata 12, kati ya hizo 9 ni mpya na hazina Madiwani. Aidha, Halmashauri ya
Mji wa Tunduma ina Kata 5 mpya na zote hazina Madiwani na Halmashauri ya Mji wa
Nzega ina Kata 10, na kati ya hizo Kata 3 ni mpya na hazina Madiwani.
52.
Mheshimiwa
Spika, lengo la kuanzisha maeneo hayo mapya ni kuwawezesha
Wananchi kupata huduma karibu zaidi kwa Wananchi. Nitoe wito kwa Wakuu wa
Mikoa, Wilaya na Watendaji wote kuwaongoza Wananchi kutumia fursa hiyo ya
kuanzishwa kwa maeneo hayo katika kujiletea maendeleo. Serikali itaendelea
kupeleka huduma zaidi karibu na Wananchi ili kuongeza kasi ya maendeleo katika
maeneo hayo. Aidha, Serikali itaweka utaratibu wa kuzipatia Halmashauri
zinazoanzishwa Watumishi hatua kwa hatua.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI
DHIDI YA WATANZANIA WALIOFICHA FEDHA HARAMU NJE YA NCHI
53.
Mheshimiwa
Spika, tarehe 9 Novemba, 2012, Bunge lilipitisha Azimio
Na. 9/2012 kuhusu kuitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania
walioficha fedha haramu nje ya Nchi kufuatia Hoja Binafsi iliyowasilishwa na
Mheshimiwa Zitto Kabwe (Mb). Azimio hilo linahitaji, pamoja na mambo mengine,
Serikali iwasiliane na Benki ya Dunia kupitia Kitengo cha Asset Recovery Unit ili mabilioni yanayomilikiwa na Watanzania
katika Mabenki nje ya Nchi ambapo hufichwa kwa kukwepa kulipa kodi yarudishwe
na kwamba Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya Nchi waeleze
wamezipataje ili TAKUKURU wachukue hatua za Kisheria dhidi ya watu wote wenye
kumiliki fedha na mali kinyume na mapato yao halali. Aidha, iliazimiwa na Bunge
na Serikali ikakubali kwamba, katika Mkutano wa Bunge wa 11 italeta Taarifa ya
hatua iliyochukuliwa ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya Nchi.
54.
Mheshimiwa
Spika, tarehe 31 Desemba, 2012, Mheshimiwa Rais aliridhia
kuundwa kwa Kamati Maalum ya Kitaifa kushughulia hoja hiyo ya kuitaka Serikali
kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje ya Nchi. Kamati
hiyo inaundwa na Wajumbe wanane wanaotoka katika Taasisi za Kitengo cha
Kudhibiti Fedha Haramu; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa; Jeshi la
Polisi; Benki Kuu ya Tanzania; Usalama wa Taifa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali. Kazi za Kamati hiyo ni:
(i)
Kuchunguza na kubaini majina ya Watanzania
wanaodaiwa kuficha fedha nje ya Nchi kinyume na Sheria na Kanuni za Nchi;
(ii)
Kuchunguza iwapo fedha hizo ni haramu au la;
(iii)
Kutambua Mabenki na Nchi zilizofichwa fedha hizo;
(iv)
Kuandaa mashtaka dhidi ya Watanzania watakaobainika
kuficha fedha haramu nje ya Nchi; na
(v)
Kuishauri Serikali jinsi ya kuzuia uhalifu wa
makosa ya fedha.
55.
Mheshimiwa
Spika, Kamati hii imeanza kazi zake rasmi tarehe 9 Januari
2013 kwa kupanga namna ya kutekeleza kazi zake ikiwemo kukusanya taarifa kuhusu
Watanzania wanaodaiwa kutorosha fedha haramu nje ya Nchi na kuangalia namna ya
kupata taarifa muhimu nje ya Nchi. Kamati hiyo inaratibiwa na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali.
56.
Ili kuiwezesha Kamati hii kufanya kazi yake kwa
ufanisi ni wazi kwamba itahitaji kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Wananchi
kwa kutoa taarifa mbalimbali kuhusu suala hili. Hivyo, natoa wito kwa Wananchi
wote wenye taarifa sahihi na za ukweli zinazoweza kuisadia Kamati kutekeleza
kazi hii wanahimizwa wajitokeze kutoa maoni yao kupitia Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali na kushirikiana kwa karibu na Kamati iliyoundwa na Serikali.
Aidha, nawaomba Waheshimiwa Wabunge nao kutoa ushirikiano wa kufanikisha kazi
za Kamati hii.
HITIMISHO
57.
Mheshimiwa
Spika, kwa kumalizia napenda niwashukuru wote
waliofanikisha Mkutano huu wa Kumi wa Bunge. Kipekee nikushukuru wewe binafsi Mheshimiwa
Spika kwa kutuongoza vizuri ndani ya Bunge lako Tukufu. Nimshukuru vilevile,
Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha Vikao vya Bunge kwa ufanisi.
Aidha, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. Nimshukuru Katibu wa
Bunge na Wasaidizi wake kwa huduma nzuri walizozitoa wakati wote tukiwa hapa.
Niwashukuru Watendaji wa Serikali na
Taasisi mbalimbali kwa kutekeleza majukumu yao vizuri ili kufanikisha shughuli
za Bunge zilizopangwa. Niwashukuru Waandishi wa Vyombo vya Habari kwa kutufikishia
habari kwa Wananchi yale yaliyojiri hapa Bungeni na kwa wakati. Vilevile,
navishukuru Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kazi yao nzuri na Madereva wote
kwa huduma zao kwa Washiriki wa Bunge hili.
58.
Mheshimiwa
Spika, baada ya kusema hayo, naomba niwatakie Safari
Njema na sasa natoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi Siku ya
Jumanne tarehe 9 Aprili, 2013 Saa 3:00
Asubuhi kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
59.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
COMMENTS