Msanii Helen John akicheza na nyoka HAKUNA simulizi linalogusa nyoka katika jamii lilililojema. Na kawaida nyoka akionekana hutafu...
![]() |
|
Msanii Helen John akicheza na nyoka
|
Kulingana na hofu iliyotawala ndani ya simulizi za kitamaduni
za makabila mbalimbali hapa nchini, watu
wanapokutana na nyoka wanaona wamekutana na mkosi na balaa kubwa na wakati
mwingine hudhani kuwa ni uchuro.
Kwa wanasayansi nyoka ni kiumbe mwenye damu baridi
atambaaye na hupatikana sehemu
mbalimbali duniani ambapo katika bara la Afrika kuna aina 450 za nyoka na wengi
ni wale wenye sumu ya wastani na wengine kali zenye uwezo wa kuua sawia.
Pamoja na nyoka kutambulika kuwa ni viumbe hatari
kutokana na sumu walizonazo ingawa wapo ambao hawana sumu, nyoka ni sehemu ya
utunzaji wa ikolojia na adui mkubwa wa panya.
Ingawa simulizi katika jamii nyingi kuhusu nyoka ni zile
za kutisha zipo jamii mbalimbali duniani ambazo hutumia nyoka kama chakula na
wengine huwatumia kama sehemu ya ngoma za asili.
Ndio kusema kwa watu wengine nyoka wamekuwa ni sehemu ya
maisha.
Nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma kwenye njia ya kuelekea
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuna Kata ya Dodoma inayojulikana kama Makulu.
Eneo hili ndilo ambalo linalobeba historia nzito ya Mji
wa Dodoma kutokana na kuwa makazi ya Machifu kwa miaka ya nyuma japo wajukuu wa
machifu hao wengine wapo mpaka leo.
Eneo hili ndipo anapoishio Mzee Lazaro Masuma Chihoma
(63), Miongoni mwa wazee wanaojua vyema nyoka, maisha yake,shida zake na hata
umuhimu wake kwa jamii.
Pamoja na kuwa mtu anayefahamu nyoka vizuri yeye pia ni
mganga wa tiba za asili mwenye tabia ya kula nyoka tena bila hata ya kupika.
Pia mzee huyu ambaye hujihusisha na masuala ya uganga wa
tiba za asili na kufanya matambiko toka mwaka 1969 baada ya kuoteshwa na mizimu
ingawa alianza rasmi kazi za uganga 1974,anawafahamu nyoka kwa kiasi cha
kusisimua.
Kulingana na maelezo yake, alianza kuongozana na mizimu
kwenda kuonyeshwa dawa tangu akisoma shule ya msingi Ihumwa . Ingawa anatibu
magonjwa yote ya binadamu , mwaka 1976 alianza kupewa elimu na mizimu ya
kukamata nyoka na kukaa nao na dawa za sumu zote za nyoka.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida Chihoma amekuwa akiishi
na baadhi ya nyoka kwenye ofisi yake iliyopo eneo la Dodoma Makulu na pindi
anapowahitaji kwa shughuli zake huwaita.
Miongoni mwa nyoka ambao anakaa nao na wengine wako
kwenye Mlima wa Bwibwi na wengine huwafahamu kwa majina ya kabila la Kigogo ni swila, koboko, swaga,
moma, nyamhando, nzokalu, gwagu, sansavumea (chatu), hato na Fira (kobra).
“Wakati wowote ukitaka kuwaona nakuletea kwani nina uwezo
wa kwenda kuwaita na kuwabeba na kuja nao nyumbani.Hapa nyumbani ninaishi na
aina saba za nyoka akiwemo kobra, swaga koboko, nyamhando, mlalu, moma ambao nimewachimbia mashimo na wale nyoka wakubwa
wanakaa kwenye mapango ya milima ya Bwibwi na huwezi kuwaleta hapa
nyumbani itakuwa ni fujo” anasema.
Moja ya vitu ambavyo vinaonesha utaalamu wa mzee huyu
katika kuwa rafiki na nyoka ni namna anavyowaita nyoka hao.
Anasema nyoka wana muziki ambayo hupenda kuisikiliza na
wanapopigiwa muziki hiyo hata awe kwenye shimo la urefu kiasi gani hutoka na
kwenda kwa anayepiga muziki huo na kama akigundua kuwa mtu huo ni rafiki basi
huanza kumtambaa mwilini taratibu.Raha hiyo ya muziki anayoisikia nyoka
hupelekea kuwa rafiki wa binadamu kwa kufurahi na kwa kucheza pamoja.
Pamoja na kutumia muziki kuwaita pia huwa anatumia mizizi
ambayo hufanya nyoka wamzoee na hata anapowaita huja bila kuwa na wasiwasi.
“Mimi napiga vifaa vya utamaduni kama malimba, zeze,
ndonondo, sinjila na ipango hivi ni vifaa vinasababisha hadi nyoka akusogelee ili muwe pamoja hata unapoenda
porini unatafuta kichaka kizuri unaanza kupiga na nyoka wengine wanaanza kuja pembezoni mwako na wakikuona una wasiwasi
wanaanza kutambaa na wakikuta hushtuki wanajua kuwa ni rafiki yao” anasema.
Pia anasema kuna nyimbo ambazo unatakiwa kuimba wakati wa
kupiga vifaa hivyo nyimbo ambazo zinaendana na mizimu ili nyoka wakikusogelea na hata akija mgonjwa kagongwa
na nyoka lazima uzitumie nyimbo hizo wakati unamtibu.
“Nyoka ni muhimu
sana kaika kazi zangu na pia hunipatia nyama kama unavyoona ninaikausha na
ninakuwa nakula taratibu mpaka itakapoisha” anasema.
Pamoja na kuelezea mlo wake wa nyoka, mzee huyu ana
mashaka makubwa na maendeleo yanayofanyika kwamba yatafuta kizazi cha nyoka na
kuleta mkosi.
Katika moja ya utafiti uliowahi
kufanyika mkoani Dodoma, eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM) imeelezwa kuwa kuna aina 16 za nyoka walio
katika familia saba.
Tanzania ambayo inajulikana
kimataifa kama sehemu ya hifadhi ya bayoanui katika bara la Afrika kwa Dodoma
suala la ujenzi bila kuzingatia masuala ya asili na umuhimu wake kunatishia
kuondoa nyoka katika sehemu pia.
Ipoa haja ya kuhakikisha kwamba
nyoka wanahifadhiwa kwa kuwa ndio wanaotunza mfumo wa ekolojia na kukosekana
kwao kutaleta shida kama mzee huyu anavyosema.
Kuna mradi wa ujenzi unaotarajiwa kufanyika eneo la
Ndejengwa ambalo ndilo hukaliwa na nyoka hao ambao wengi ni wa matambiko.Pamoja
na hofu yake anaamini kwamba nyoka
hawatakimbia bali wataishi katika nyumba hizo kwa maana wameingiliwa kwenye mji
wao.
“Wameingia kwa fujo kuanza ujenzi eneo hili walitakiwa
kuonana na wenyeji wa milima hii tunaishi kwa kimila pale kuna matambiko”
alisema
Alisema kuwa nyoka hao wamekuwa wakitumika kwa kazi za
matambiko na nyoka wa namna hiyo hawaondoki kirahisi.
Anasema nyoka ingawa anatumika kama dawa kuna wakati hutumika kama chakula kama
anavyofanya yeye na huliwa akiwa mbichi bila hata ya kupikwa huku wengine
wakichomwa na unga wake kulambwa na kuwa tiba ya sumu mbalimbali zinazoingia
mwilini.
Chakula cha nyoka kinatajwa kuwa ni unga na panya na kama
unga ukikosekana hata majivu hutumika.
Chihoma anasema nyoka mdogo anapomeza panya wawili huweza
kukaa hata miezi miwili hadi mitatu na hapo huwa anakwenda haja ndogo tu hadi
panya aliyemmeza aoze na hatimaye kupata haja kubwa.
Pia nyoka ni moja ya wanyama wanaotajwa kuwa hawasumbuki
katika suala la njaa kwani anapomeza panya unyevunyevu wa kuoza kwa panya ule
humfanya hata asisikie kiu ya maji kwani akila mara moja tu anapumzika kwani
atakaa muda mrefu bila kutafuta chakula.
Kitendo cha
kuwaua nyoka kila wanapokutana nao kwa sababu mbalimbali wananchi wanaondoa ekolojia katika hali yake
huku nyoka wakiendelea kupungua.Nyoka wanasaidia sana kudhibiti panya ambao ni wadudu waharibifu wa mahindi na kama wakiendelea kuwapo ni dhahiri panya hawawezi kuwapo.
Akizungumzia dawa ya nyoka alisema:“Nyoka wadogo
ukishawachoma na kugeuka majivu unachangana na dawa ya mti unaoitwa mpande na
mti wa mwaliganza na ngwenyangale hizo dawa ukizichanganya na nyoka na tayari
unaondoa simu ya nyoka katika mwili wa binadamu, unachanja,
unachua na nyingine unampa kwenye maji anakunywa.”
Pia anasema kuwa, mtu anapogongwa na nyoka
anapocheleweshwa na sumu kuanza kusambaa lazima umchanje na kuvuta sumu kwa
kutumia pembe kubwa ya mbuzi au pembe ya ng’ombe iliyochongwa na kuwa ndogo
ambayo huwa maalum kwa ajili ya kunyonya sumu ya nyoka.
“Ukishanyonya sumu na kutoka unampa mgonjwa dawa na hapo
anakuwa amepona,” anasema Chihoma.
Source: Sifa Lubasi,Habarileo

COMMENTS