Na Mwandishi wetu, BSKY Media Aliyekuwa ananogesha Tamthilia ya Huba, Grace Mapunda, akicheza kama Tessa mama anayependa vibenteni amefa...
Na Mwandishi wetu, BSKY Media
Aliyekuwa ananogesha Tamthilia ya Huba, Grace Mapunda, akicheza kama Tessa mama anayependa vibenteni amefariki dunia saa tano usiku wa kuamkia leo akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Mwananyamala, Dar es salaam.
Huba yenye upenzi wa asilimia 88 kwa mujibu wa mitandao inazungumzia familia mbili zenye mambo shoo zikiwa zinaabudu fedha huku nadharia ikisema kwamba ni mapenzi pekee yanayoweza kuwaondoa katika udhalilishaji ndani ya kuabudu fedha kwao.
Ndani humo katika tamthilia hii inayorushwa na DSTV kwenye Magic Bongo Grace Mapunda akiwa ameuvaa uhusika wa Tessa ameonesha kwamba yeye ni wa misimu yote na maigizo ya aina yote.
Ikiwa imeanza kuoneshwa Agosti 29, 2017 nchini Tanzania, kifo cha Grace ambacho kimekuja ghafla kimetokea wakati ameanza kupiga picha sehemu zake nyingine zinazomhusu katika hoteli ya Travertine siku tano zilizopita.
Imeelezwa kuwa Grace anayetarajiwa kusitiriwa Jumatatu katika makaburi ya Kinondoni majira ya saa kumi alikuwa anaigiza huku akisema kwamba hajasikii vizuri japo halik yake ilionekana ya kawaida.
Aliyekuwa naye katika scene hiyo Abdul Kingo akielezea kusikitishwa na kifo hicho alisema hakutarajia mambo yaende mrama japo kwenye kazi alisema kwamba anajisikia hayuko fiti ingawa aliifanyakazi kazi uadilifu mkubwa.
Kwa mujibu wa rafiki wa karibu na familia hiyo Hashim Kambi Grace alipata tatizo la nyumonia akakimbizwa hospitali Mwananyamala ambapo alifariki akiwa katika matibabu.
Darekta wa Huba, Aziz Ahmed alisema Grace hakuumwa muda mrefu, ila alipelekwa Hospitali juzi na usiku wa kuamkia Novemba 2, 2024 akapoteza uhai.
Msiba upo nyumbani kwake Sinza Vatcan.
Kwa bahati mbaya, hakuna habari za kutosha za umma kuhusu maisha ya kibinafsi ya Marehemu Grace Mapunda, ikiwemo mahali alipozaliwa, mwaka, na shule alizopitia, lakini pia katika mahojiano yake mengi alionekana kutopendelea kuzungumza sana maisha yake binafsi, ingawa siku zote alikuwa akisema kwamba yeye ni Single Mother.
Ingawa mitandao haina maelezo kamili kuhusu maisha yake ya awali, tunajua kwamba Grace Mapunda alikuwa mwigizaji maarufu sana Tanzania, hasa kwa jukumu lake la sasa kama Tesa katika tamthilia ya Huba.
Akiigiza katika Huba akiwa na JB
Katika hili ameacha alama kubwa katika tasnia ya burudani nchini.
Kwa uhakika Grace Mapunda ni mwigizaji wa filamu za Tanzania anayesifika kwa uwezo wake mkubwa wa kuigiza filamu za hisia na hii ni kutokana na kuwa makini katika kuwakilisha uhusika halisi akionekana dhahiri kuzipatia filamu za aina hiyo.
Akihojiwa na Global TV hivi karibuni alikiri kwamba anapovaa uhusika anakuwa Mhusika hasa kwani hana mchezo na kazi yake.
Grace Mapunda ambaye amebarikiwa kuwa na watoto wawili,Happiness pamoja na Ritha, aliingia katika uigizaji kwa hila ya binti yake wa kwanza kwani pamoja na kipaji kinachoonekana sasa yeye hakuwa na hamu wala haja ya kuigiza.
Alisema katika mahojiano na Global kwamba mtoto wake alimtaka kwenda kuigiza Splendid kwani wakati huo binti huyo alikuwa humo na akamwambia kwamba waajiri wake wanataka kumuona mama yake, kumbe yalikuwa makubaliano ya binti yake na babu yake jinsi ya jumfanya awe muigizaji.
Akiwa na watoto wake
Mtoto wake huyo Happiness ambaye pia huimba na alishawahi kuigiza na mama yake katika filamu ya Fake Smile. Mtoto wake mwingine Ritha naye ni mwanamuziki wa muziki wa kizazi kipya.
Pamoja na Huba kazi zake zilizotia fora ni pamoja na House of death, hard price, nilindiwe, Kichupa, Majuto, Mwaka wa Hasara, chloroquine love, Chungu ya Nafsi, poor Minds, Jibu la ndoto na Back to life .
Muigizaji huyu pia alipata tuzo ya muigizaji bora wa kike mwaka 2015.
Mmoja wa mashabiki wake kutoka Kenya ambaye amedai kuwa amekuwa akiangalia Huba kutoka mwaka 2021 alisema alikuwa anampenda Grace Mapunda kwa jinsi alivyomudu character ya Tessa na kifo chake kimemuuma.
Jiffy Pictures ambao ndio wazalishaji wa Huba waliandika katika mtandao wao kuhusiana na kifo hicho.
“Tumeondokewa Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na Kwake ni marejeo,Kwaniaba ya Familia ya Grace Mapunda tunawajulisha kua Mama yetu Mpendwa Grace Mapunda (TESA) hutupo nae tena Duniani,Bwana ametoa,Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,”
Grace Mapunda atakumbukwa kwa mchango wake kwenye sekta ya maigizo, akicheza kama Mama mzazi wa mastaa wengi.
Aziz akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu alisema Mwili wa Grace utarejeshwa nyumbani kutoka hospitali ya Mwananyamala Jumapili Novemba tatu saa kumi na mwili wake kulala nyumbani hadi Jumatatu Novemba 4 utakapopelekwa viwanja vya Leaders kwa heshima ya mwisho kabla ya kupelekwa makaburi ya Kinondoni kwa maziko.
COMMENTS