Na Mwandishi Wetu, BSKY Media Mfuko wa Kimataifa wa Kusaidia Mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) umemuomba Rais ...
Na Mwandishi Wetu, BSKY Media
Mfuko wa Kimataifa wa Kusaidia Mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) umemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuongoza timu itakayofanya kampeni ya kutafuta fedha ili kunusuru mfuko huo kutokana na changamoto kubwa za kifedha.
Ombi hili, lililowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Fund, Bw. Peter Sands, wakati wa mkutano wake na Rais Samia na timu yake kwa njia ya mtandano.
Ombi hilo linaashiria imani kubwa ya jumuiya ya kimataifa kwa uongozi wa Rais Samia.
Ombi hili limetokana na hali tete ya kifedha inayokabili Global Fund, kufuatia baadhi ya nchi wafadhili kujitoa katika utoaji wa fedha, jambo linaloufanya mfuko kuwa katika wakati mgumu.
Global Fund inategemea michango kutoka serikali, sekta binafsi, na taasisi mbalimbali, zikiwashwa kupitia mizunguko ya miaka mitatu ya ukusanyaji fedha (Replenishment cycles).
Mzunguko wa saba wa ukusanyaji fedha, uliofanyika Septemba 2022 nchini Marekani, ulilenga kukusanya dola bilioni 18. Hata hivyo, hadi kufikia mkutano huo, ni dola bilioni 14.25 tu zilikuwa zimepatikana.
Lengo kuu la fedha hizo ni kuokoa maisha ya watu zaidi ya milioni 20 na kupambana na magonjwa hayo matatu hatari hadi mwaka 2026. Changamoto za kiuchumi duniani, pamoja na athari za janga la COVID-19, zimechangia pakubwa katika kudhoofisha uwezo wa nchi kuchangia, na hivyo kuweka shinikizo kwa Global Fund.
Uongozi wa Rais Samia unatarajiwa kuleta nguvu mpya katika jitihada za Global Fund za kukusanya fedha na kuhakikisha inaendelea na majukumu yake muhimu ya kupunguza maambukizi na vifo vinavyosababishwa na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria duniani kote. Kujitolea kwake kunatarajiwa kuhamasisha nchi nyingine na wafadhili kuwekeza zaidi katika mapambano ya afya ya umma.
Tanzania na Global Fund awamekuwa na uhusiano imara na wa muda mrefu, ukinufaisha sana sekta ya afya nchini. Global Fund ni mmoja wa washirika muhimu na wakubwa wa sekta ya afya Tanzania, ikichangia pakubwa katika kuboresha maisha ya mamilioni ya Watanzania.
Tangu mwaka 2002, Global Fund imewekeza zaidi ya dola bilioni 3.8 nchini Tanzania kwa ajili ya kupambana na magonjwa hayo matatu, pamoja na kuimarisha mifumo ya afya.
Mwezi wa Januari 2024, Tanzania ilisaini mikataba minne ya misaada mipya yenye thamani ya dola za Marekani milioni 606.9 (zaidi ya shilingi trilioni 1.4) kutoka Global Fund. Fedha hizi zitatumika kwa miaka mitatu ijayo (2024-2026) na zinalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kukabiliana na changamoto zinazoendelea.
Nchini Tanzania, Global Fund imewekeza katika maeneo mbalimbali muhimu ya sekta ya afya yakiwemo mapambano dhidi ya UKIMWI/VVU ambapo inatoa msaada muhimu kwa upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs), ikihakikisha takriban Watanzania milioni 1.7 wanapata matibabu kila mwaka.
Pia imekuwa ikisaidia programu za kuzuia maambukizi mapya ya VVU, ikiwemo elimu ya afya, usambazaji wa kondomu, na huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT).Aidha inasaidia vituo vya upimaji VVU na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za ushauri nasaha.Msaada kwa Walioathirika: Kusaidia programu zinazotoa msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI.
KaKika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu (TB), Global Fund inasaidia upatikanaji wa vipimo vya TB, ikiwemo vipimo vya kisasa kama GeneXpert, na kutoa matibabu kamili kwa wagonjwa wa TB, ikiwemo TB sugu ya dawa.
Pia wamesaidia uwapo wa mifumo ya ufuatiliaji wa matibabu ili kuhakikisha wagonjwa wanamaliza dozi zao kikamilifu na Kusaidia jitihada za kuzuia kuenea kwa TB, hasa katika makundi hatarishi.
Katika mapambano dhidi ya Malaria, Global Fund imekuwa msaada mkubwa katika usambazaji wa vyandarua vyenye viuatilifu (LLINs) kwa kaya, jambo lililosaidia sana kupunguza maambukizi ya malaria nchini. Shughuli nyingine ni Kusaidia upatikanaji wa dawa za kutibu malaria, kuimarisha upatikanaji wa vipimo vya malaria (RDTs na microscopy).Pia Global Fund inasaidia programu za kudhibiti mazalia ya mbu na kusaidia kuimarisha Mifumo ya Afya (Health Systems Strengthening - HSS).
Pia wamesaidia ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, maabara, na maghala ya dawa, mafunzo ya Wahudumu wa Afya
Usambazaji wa Dawa na Vifaa Tiba, kusaidia kuimarisha mifumo ya kukusanya, kuchambua na kutumia taarifa za afya kwa ajili ya kupanga na kufanya maamuzi sahihi na usimamizi wa utawala.
Mafanikio yaliyopatikana nchini Tanzania, ikiwemo kupunguza maambukizi mapya ya VVU na vifo vinavyotokana na Malaria, yanashuhudia ufanisi wa ushirikiano huu, alise Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo Ikulu.
Ufanisi wa Tanzania katika matumizi ya fedha za Global Fund, ikifikia asilimia 92 ya utumiaji, umekuwa kielelezo kwa nchi nyingine na unachangia kuendelea kupokea misaada mikubwa.
Uhusiano huu wa kimkakati kati ya Tanzania na Global Fund unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha afya bora na ustawi kwa Watanzania wote, sambamba na malengo ya maendeleo endelevu ya kimataifa.




COMMENTS