Kijiji cha Makumbusho, kilichopo Kijitonyama, Dar es Salaam, ni moja ya maeneo muhimu sana nchini Tanzania kwa ajili ya kuhifadhi na kuonyes...
Kijiji cha Makumbusho, kilichopo Kijitonyama, Dar es Salaam, ni moja ya maeneo muhimu sana nchini Tanzania kwa ajili ya kuhifadhi na kuonyesha utamaduni na urithi wa taifa.
Katika siku ya pili ya Tamasha la Tatu la Fasihi washiriki tulipata nafasi ya kuzuru kijiji hicho na kuelezwa mambo mbalimbali na Mhifadhi Mwandamizi Wilhelmina Joseph kuhusu historia na mpangilio wa kijiji.
Alisema Kijiji cha Makumbusho ni makumbusho ya wazi iliyoanzishwa mwaka 1967 kwa lengo la kukusanya, kutafiti na kuhifadhi utamaduni wa jamii za watanzania na hasa mitindo ya ujenzi wa nyumba za asili na namna ambavyo jamii yetu iliishi.
Uwapo wa kijiji hiki ni zao la Mwalimu Julius K. Nyerere, baada ya kuvutiwa na jinsi kabila la Waha lilivyojenga mfano wa nyumba zao za kimila kwenye Maonyesho ya Sabasaba ya mwaka 1966.
Kabla hajatutembeza washiriki wa Tuzo na wageni wengine tuliketi katika duara huku katikati kukiwa na kuni za kukoka moto tukikumbuka wazee wa zamani walivyoketi na watu wao na kusimulia hadithi mbalimbali zenye kuburudisha kufunza na kutengeneza ujasiri.
Wilhelmina, ambaye wapenzi wake wanamuita Mina alisema kwamba katika kijiji hicho ambapo nyumba zilizopo ni za mtindo wa banda, msonge na tembe pia kuna msitu ambao unatumika na makabila mbalimbali kuendesha shughuli za mkole.
"Wenzetu wamakonde hufika kila mwaka wakati wa msimu kufanya mkole kabla ya kutoa wali wao na sisi tunafurahi kuwapa nafasi kwani ni katika juhudi za kulinda utamaduni na mila ambayo ndiyo kazi nya makumbusho hii " alisema Mina.
Kijiji hicho kina msitu unaofikia ekari tano ambao pia unaweza kutumika kufanya shughuli za upigaji picha wa sinema.
Alisema kukiwa na makabila zaidi ya 120 nchini, makumbusho hayo yasingeweza kuweka nyuimba zote lakini imejenga nyumba chache kwa kuzingatia ukanda.
Makumbusho hii inaonyesha maisha halisi ya watanzania hadi kufikia miongo michache iliyopita kupitia nyumba na vifaa walivyotumia.
Ni dhahiri baadhi ya nyumba zilizojengwa hapa hazitumiwi tena wakati nyumba zingine hutumiwa na wanajamii wengi waishio sehemu za vijijini zikiwa zimeboreshwa au kuondolewa uasili wake.
Tulipata nafasi baada ya masimulizi ya historia kutembelea makazi kadhaa ya Watanzania na kushiriki katika burudani ya ngoma.
Mina alikuwa mzoefu na tulianzia katika makazi ya Wabembe, ambapo alitupa historia akatueleza sababu ya kuwa vile na pia tuliona zana zao za uvuvi na kufua vyuma na akatueleza namna ambavyo katika mji huo kuna nyumba ambayo unaweza kusema ni nyumba ya mahakama.
Ndani ya nyumba kuna kitanda ambacho kinawafanya wanandoa kushikamana.
Kuna mengi ambayo unaweza kuyaona katika makazi haya ambapo kutoka Magharibi tulipelekwa Kusini magharibi na kukutana na makazi ya wanyakyusa na mila zao za ujenzi wa nyumba ambapo nyumba ya bi mkubwa huwa pembeni peke yake.Aidha kulionekana maendeleo ya zamani ambapo vijana wanaOkua walilazimika kujenga nyumba yao wenyewe ya kuishi.
Hakika japo hatukumaliza kijiji kizima kutokana na kubanwa na muda hakika ilikuwa ni furaha kuwapo pale na kuona nyumba na vifaa vya asili, mboga na miti ya asili.
Mina anasema wanafanyia kazi maelekezo ya kufanya maboresho ya kijiji hicho kama yalivyotolewa na waziri Mkuu,Kassim Majaliwa lakini kwa sasa wanazaidi ya nyumba 30.
Mina anasema Kijiji cha Makumbusho kina faida nyingi kwa Watanzania na wageni na akasema faida kubwa ni Kuhifadhi na Kuelimisha Urithi. Kijiji kinahifadhi mifano halisi ya nyumba za asili kutoka makabila mbalimbali ya Tanzania, pamoja na vifaa vya jadi na zana walizotumia mababu zetu. Hii inawapa fursa vizazi vya sasa na vijavyo kujifunza na kuelewa utamaduni wa asili.
Pia kijiji hiki ni kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotaka kujifunza na kushuhudia utajiri wa tamaduni za Tanzania.
Kwa kuwa mara kwa mara hupangisha matamasha ya sanaa za asili, ngoma, muziki, na maonyesho ya ufundi wa mikono kijiji hiki kinatoa fursa kwa wasanii kuonyesha vipaji vyao na kwa jamii kusherehekea urithi wao.
Uwapo wake unarahisisha utafiti wa Kisayansi na Kihistoria kupitia urithi na utamaduni wa mababu zetu,huku wakiendelea kupokea wanafunzi na vikundi mbalimbali kwa ajili ya kujifunza kuhusu mila, desturi, na tamaduni za makabila ya Tanzania.
Naam , muda mfupi lakini n ilielewa kwamba nahitaji kuleta watoto wangu hapa kujifunza kwani kiingilia ni rahisi karibu na bure. Hapa watoto wangu natumaini watajifunza kitu.Kwa ujumla, Kijiji cha Makumbusho kinaendelea kuwa kitovu muhimu cha uhifadhi na uendelezaji wa utamaduni nchini Tanzania, kikifanya kazi chini ya Makumbusho ya Taifa ya Tanzania (National Museum of Tanzania - NMT).









COMMENTS