Dar es Salaam, Tanzania Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko,Julai 9,2025 ametoa wito mzito kwa vyombo vya habari ...
Dar es
Salaam, Tanzania
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko,Julai 9,2025 ametoa wito mzito kwa vyombo vya habari na vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuhakikisha wanatoa nafasi ya haki na usawa kwa wagombea wote kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akisisitiza umuhimu wa kuheshimu maoni tofauti na
kulinda mshikamano wa kitaifa, Dkt. Biteko alizungumza jijini Dar es Salaam
katika mkutano uliowakutanisha wadau wa sekta ya habari.
Umuhimu wa Umoja katika Kipindi
cha Uchaguzi
Dkt. Biteko alisisitiza kuwa
uchaguzi ni kipindi nyeti kinachopaswa kuwa na umoja wa kitaifa, akieleza kuwa taarifa nyingi husambaa na kuwa
msingi wa maamuzi ya wananchi kuhusu nani wa kumchagua.
"Katika kipindi hiki cha
uchaguzi ni kawaida hata watu wa familia moja kutofautiana kimawazo. Mkutano
huu ni sehemu ya kuwaleta pamoja wadau ili pamoja na tofauti zetu, tusalie
wamoja. Sisi ni Watanzania wenye nia ya kuijenga nchi yetu na kuifanya istawi
zaidi," alisema Dkt. Biteko.
Jukumu la Vyombo vya Habari
katika Uchaguzi Huru na Haki
Naibu Waziri Mkuu alibainisha
mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, kwa kufuatilia na kuripoti
matukio mbalimbali kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Alivitaka vyombo hivyo
kuwa waaminifu kwa jamii kwa kusambaza taarifa
sahihi na za kuaminika.
"Katika zama hizi ambapo
nguvu ya mhariri imepungua na taarifa huweza kusambazwa bila kupitia mchakato
rasmi wa uhariri, ni muhimu sana kwa wanahabari kutumia weledi wao na kulinda
tasnia hii kwa wivu mkubwa. Tukikosa uangalizi, tunaweza kugawanyika kama
taifa," alionya Dkt. Biteko.
Alitaja ongezeko kubwa la vyombo
vya habari nchini, likiwemo magazeti
375, vituo vya redio 247, vyombo vya habari mtandaoni 355, blogu 72, na vituo
vya televisheni 68, akisema haya ni matokeo ya mazingira bora
yaliyowekwa na serikali. Vyombo hivi vimeajiri idadi kubwa ya vijana na vinatoa
mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Serikali na Sekta ya Habari:
Hatua na Dhamira
Dkt. Biteko alipongeza serikali
inayoongozwa na Rais Samia Suluhu
Hassan kwa kutoa kipaumbele kikubwa kwa sekta ya habari, akitaja hatua
za mwanzo alizochukua Rais ikiwemo kufungua baadhi ya vyombo vya habari
vilivyokuwa vimefungiwa na kurejesha leseni vilivyonyang’anywa.
Aliongeza kuwa serikali imeanzisha
Bodi ya Ithibati kwa Waandishi wa
Habari ili kuhakikisha huduma za habari na utangazaji zinazingatia
viwango vya weledi na maadili.
"Waandishi wa habari mnapaswa
kuwa walinzi wa kweli, wajenzi wa amani na waoneeni wivu taaluma yenu. Katika
mazingira haya ya teknolojia na taarifa potofu, mnapaswa kuwa waangalifu sana
na kuhakikisha jamii inapata habari sahihi," alisisitiza.
Aidha, aliwataka wanahabari
kutumia lugha ya staha, kuepuka
uchochezi, na kuripoti kwa usawa bila upendeleo wakati wa kampeni,
uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.
Habari kama Nyenzo ya Uwazi na
Uwajibikaji
Dkt. Biteko alisisitiza kuwa sekta
ya habari ni nyenzo muhimu sana katika kukuza uwazi, uwajibikaji na ufuatiliaji wa mwenendo wa uchaguzi.
Waandishi wa habari wana jukumu la kuhamasisha makundi yote ya jamii kushiriki
katika uchaguzi, ikiwemo wanawake, vijana na watu wanaoishi katika mazingira
magumu.
"Mnapaswa kuwa zaidi ya
waandishi wa habari. Tambueni kuwa kupitia kazi yenu, taifa la Tanzania
linaweza kubaki moja au kugawanyika. Kwa hiyo kuwa walinzi wa amani, wachunguzi
wa ukweli, na chombo safi cha jamii kisichochafuliwa na uzushi au chuki,"
alisisitiza.
Usalama wa Waandishi wa Habari na
Ushirikiano na NEC
Kwa upande wa vyombo vya ulinzi na usalama, Dkt.
Biteko alieleza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha waandishi wa habari
wanafanya kazi zao katika mazingira salama,
huru na rafiki. Alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kulinda
usalama wa wanahabari na mali zao wakati wote wa uchaguzi.
"Tutahakikisha kuwa kila
mwanahabari anarudi nyumbani kwake akiwa salama. Tutaendelea kulisimamia hili
kwa nguvu zote kupitia vyombo vyetu vya dola," alisema.
Alimaliza kwa kutoa wito kwa
waandishi wa habari kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tume Huru ya Uchaguzi (NEC) ili kupata
taarifa sahihi na kwa wakati, na kuzitaka taasisi za habari kujitathmini mara
kwa mara.
Mchango wa Tasnia ya Habari na
Uzinduzi wa Mfumo wa Kidigiti
Tasnia ya habari nchini inatajwa
kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kabla na baada ya uhuru, ambapo
uwepo wa baadhi ya vyombo vya habari vya awali kama vile gazeti la Sauti ya
TANU na redio Sauti ya Dar es Salaam vilisaidia kutoa mchango mkubwa katika
kujenga umoja, utaifa na kuhamasisha ushiriki wa harakati za kudai uhuru.
Kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi
ya REPOA (Research on Poverty Alleviation) wa mwaka 2022, vyombo vya habari
ndiyo chanzo kikuu cha taarifa za kisiasa kwa wananchi, ambapo zaidi ya
asilimia 76 hupata taarifa za kisiasa kupitia redio na televisheni. Kutokana na
hilo, Dkt. Biteko ameviasa vyombo vya habari kutoa majukwaa ya mijadala ya kisera na kisiasa ambayo
huwasaidia wapiga kura kufanya maamuzi sahihi.
Katika mkutano huo, Dkt. Biteko
alizindua rasmi Mfumo wa Kidigiti wa
TAI – Habari wa kusajili na kutoa ithibati kwa waandishi wa habari,
unaosimamiwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari. Hadi sasa, zaidi ya
waandishi 2900 wamesajiliwa kupitia mfumo huu unaotoa Vitambulisho vya Kidigiti (Digital Press Card).
Mawazo ya Wadau Wengine
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema mkutano huo unalenga kuweka
msingi madhubuti wa ushirikiano kati ya Serikali, vyombo vya habari, asasi za
kiraia, taasisi za usalama na NEC, ili kulinda amani na kuhimiza usawa wa fursa
kwa vyama vyote vya siasa.
Mkuu wa
Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando,
akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila,
aliahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari kupata taarifa sahihi.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa
Serikali, Gerson Msigwa,
alisisitiza umuhimu wa weledi katika sekta ya habari kuelekea uchaguzi mkuu.
COMMENTS