Na Mwandishi wetu Katika jitihada za kukabiliana na ongezeko la habari za uongo, chuki na upotoshaji mtandaoni, Baraza la Habari Tanzania (M...
Na Mwandishi wetu
Katika jitihada za kukabiliana na ongezeko la habari za uongo, chuki na upotoshaji mtandaoni, Baraza la Habari Tanzania (MCT) limetoa mafunzo maalum ya ukaguzi wa habari (fact-checking) kwa wahariri na mabloga.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Agosti 14 na 15, yamelenga kuwaandaa wadau hao wa habari katika mazingira ya Uchaguzi Mkuu, ambapo habari za uongo huongezeka kwa kasi.
Watoa mada, akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Nukta Afrika Nuzulack Dausen na Daniel Mwingira, wamesisitiza umuhimu wa kukagua kila habari kabla ya kuchapisha kuona usahihi wake na kuzuia taharuki.
Walisema kwa nyakati tofauti katika mada zao kuwa katika zama hizi za maendeleo makubwa ya teknolojia, kuna zaidi ya zana (tools) 200 za kutambua habari za uongo, chuki zenye kuleta taharuki.
Baadhi ya zana hizo zilizotajwa ni InVID, Search,TinEye, CrowdTangle, Wayback Machine,Whois Lookup na Google Reverse Image, ambazo husaidia kutambua picha, video, na maudhui mengine yaliyotumika kwa njia potofu.
"Zana za kuhakiki husaidia wahariri na waandishi wa habari kuepuka kuchapisha au kutangaza maudhui ya kupotosha au ya uongo, hasa wakati wa tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025."
Pamoja na zana hizo Dausen aliwasilisha mada namna ya kutambua taarifa potofu, za kupotosha, na matamshi ya chuki katika mitandao ya kidijitali.
Dausen alisema kuna mambo matatu ambayo unaweza kuiyafanya haraka kujiweka salama hasa ikizingatiwa kwamba kila hatua katika uwasilishaji wa habari katika kipindi inapaswa kuwa yenye kujijenga katika weledi mkubwa na kuondoa makosa.
Alisema jambo la kwanza ni kuangalia chanzo:"Nani amechapisha habari hii? Je, ni chombo cha habari kinachojulikana na kinachoaminika au ni mtu au chanzo kisichoeleweka? Je, tovuti inaonekana ya kitaalamu?" na kuwataka wahariri kuangalia kama kuna makosa ya lugha, matangazo mengi kupita kiasi, au muundo wa tovuti usio wa kawaida.
Pia aliwataka kuchunguza maudhui kwa kuhakikisha kwamba unasoma habari nzima na sio kusoma kichwa cha habari tu. Mara nyingi vichwa vya habari huweza kupotosha. Soma habari nzima ili kupata picha kamili.
Kwenye picha na video aliwataka wahariri na mabloga kuzitazama kwa jicho la pekee kwa kujihichi picha au video zinatumiwa katika mazingira sahihi? Tumia zana kama vile Google Reverse Image Search au Invid ili kujua picha hiyo ilichapishwa wapi kwa mara ya kwanza.
Pia mhariri au bloga anapaswa kuangalia hisia zinazojitokeza: Je, maudhui yanajaribu kukuchochea kuwa na hasira au woga kupita kiasi? Hii ni ishara ya matamshi ya chuki.
Jambo la tatu ni kulinganisha habari hiyo na vyanzo Vingine:Je, vyombo vingine vya habari vimeripoti habari hii? Ikiwa hakuna chombo kingine chochote kinachoaminika kimeripoti habari hiyo, inawezekana si ya kweli.
Pamoja na kuwa mwangalifu Dausen aliwataka wahariri na mabloga kuwatafuta wachunguzi wa ukweli (fact-checkers) na hapa nchini kuna Nukta Check na Jamii Check ambao wanaweza kusaidia kuthibitisha ukweli wa habari.
Mabloga Wapewa Tahadhari Maalum
Wakati wa mafunzo hayo, tahadhari maalum ilitolewa kwa mabloga, ambao walielezwa kuwa wapo katika mazingira magumu zaidi ya kuthibitisha ukweli. Mtoa mada Nurzack alieleza kuwa, tofauti na vyombo vya habari (mainstream media) ambavyo vina mifumo mingi ya uhakiki, mabloga wanafanya kazi kama "one-man-show," jambo linalowafanya kuwa rahisi kuanguka kwenye mtego wa habari za uongo. Kwa hiyo, walisisitizwa sana kuwa makini na kuwa na nidhamu ya uandishi kwa kuchunguza kwa undani habari wanazozipata.
Wataalam Mwingira na Nurzack walisisitiza kuwa hata katika shinikizo kubwa la kuchapisha habari haraka, kitu muhimu zaidi ni uangalifu (observation). Mwingira alitoa mifano mbalimbali na kueleza kuwa uwezo wa kujua picha ilipigwa wapi kwa mara ya kwanza ni muhimu sana, na aliwataka washiriki kutumia zana maalum za kuonyesha mahali (geolocating tools).
Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka, kwani Jamii Check na Nukta Check zimetajwa kuwa miongoni mwa zana za ukaguzi wa habari zinazotumika nchini Tanzania. Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa, kuelekea Uchaguzi Mkuu, jamii inapata habari sahihi na zenye ukweli, na hivyo kuzuia machafuko yanayoweza kusababishwa na habari za uongo na chuki.
Wakati huo huo Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, amesema maazimio yote yaliyopitishwa kwenye mkutano mkuu wa kimataifa wa mabaraza ya habari Afrika na duniani, uliofanyika mkoani Arusha, ni muhimu yazingatiwe kwani yanagusa mwelekeo wa mafunzo waliyonayo.
Sungura ameyasema hayo Agosti 14,2025 wakati akizungumza katika mafunzo ya kupambana na taarifa potofu, upotoshaji na habari za chuki wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Amesema, katika mkutano huo walipitisha azimio moja la msingi sana, ambalo ni serikali za mataifa ya Afrika ziwekeze kwa kiasi kikubwa katika teknolojia na uchumi wa kidigitali. Amesisitiza kuwa azimio hilo la msingi linapaswa kufikishwa kwenye kila wizara husika na kila taifa, kwani limepitishwa na wadau walioshiriki kwenye mkutano huo na hivyo serikali za mataifa husika zitalazimika kulizingatia.
Ametaja azimio la pili kuwa ni serikali za mataifa ya Afrika kutunga sheria, kanuni na sera zinazozingatia ukuaji wa matumizi ya teknolojia na akili bandia.
“Kukua kwa matumizi ya teknolojia na kuweka mazingira wezeshi kwa taaluma ya habari kutatekeleza wajibu wake. Vyombo vya habari vina wajibu wa kutambua majukumu yao, lakini wanahitaji mazingira wezeshi yanayoundwa na sheria, sera, kanuni na taratibu. Hivyo, wamepitisha azimio la kuyataka mataifa ya Afrika kutunga sheria na kanuni zinazotengeneza mazingira hayo wezeshi,” amesema.
Ametaja azimio la tatu kuwa ni mataifa ya Afrika kulinda utamaduni wa Kiafrika na kutunza kumbukumbu ya urithi wa namna habari za Afrika zinavyopaswa kusimuliwa, kwa kuepuka kuchakachuliwa na utamaduni wa kigeni.
“Sasa hivi dunia imehamia mtandaoni, na huko mtandaoni kuna utamaduni wa kigeni unaotamalaki. Azimio hili lililenga tuzingatie utamaduni wetu na namna tunavyosimulia simulizi na urithi wa Kiafrika kwa faida ya Afrika. Na sisi lazima tuendelee kulinda namna tunavyosimulia habari za Afrika kwa faida ya Waafrika wenyewe,” amesema.
Amesema azimio la nne ni kuhusu vyuo vya uandishi wa habari na vyuo vikuu, kwani vijana wa leo walioko vyuoni wanaweza kuwa mbele zaidi kiteknolojia kuliko walimu wao. Ameeleza kuwa inapaswa kuandaliwa mitaala inayowawezesha walimu kuwa na ufahamu na upeo mkubwa wa masuala ya kiteknolojia na akili bandia, pamoja na mitaala inayokidhi mahitaji yanayoendana na teknolojia na kuzingatia matumizi ya akili bandia.
COMMENTS