TIMU ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’,chini ya uongozi wa nahodha Mbwana Samatta na kiungo mchezeshaji mahiri, Faisal Salum 'Fei Toto...
TIMU ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’,chini ya uongozi wa nahodha Mbwana Samatta na kiungo mchezeshaji mahiri, Faisal Salum 'Fei Toto', leo kinaenda kuandika historia mpya katika michuano ya AFCON 2025 nchini Morocco kitakaposhuka dimbani kumenyana na miamba wa soka barani Afrika, Morocco, katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).
Mtanange huo wa kukata na shoka utapigwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat.
Rekodi zinaonesha kuwa timu hizi mbili zimekutana mara nane katika michuano mbalimbali. Katika mikutano hiyo, Morocco imeibuka kidedea mara saba, huku Taifa Stars ikifanikiwa kuifunga Morocco mara moja pekee hapo Machi 24, 2013, siku ambayo Taifa Stars iliandika historia ya kipekee jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2014, Stars iliishangaza Afrika kwa kuichapa Morocco mabao 3-1.
Katika ushindi huo wa kishindo, Thomas Ulimwengu alifungua milango ya mabao kabla ya nahodha wa sasa, Mbwana Samatta, kupigilia msumari wa mwisho kwa mabao mawili (brace) yaliyoamsha hisia za kitaifa. Morocco walipata bao la kufuta machozi kupitia kwa Youssef El Arabi, huku mchezo wa marudiano mwezi Juni mwaka huo ukiisha kwa Morocco kushinda 2-1 mjini Marrakech.
Hata hivyo, jeraha la hivi karibuni zaidi liko kwenye michuano ya CHAN 2024 (iliyochezwa Agosti 22, 2025). Katika hatua ya robo fainali, Morocco waliiondoa Taifa Stars, waliokuwa wenyeji wenza, kwa ushindi mwembamba wa 1-0. Bao la Oussama Lamlioui katika dakika ya 65 lilitosha kuwapeleka Morocco nusu fainali na hatimaye kutwaa ubingwa huo.
Mchezo wa leo wa 16 bora katika AFCON 2025 siyo tu unatafuta nafasi ya robo fainali, bali ni fursa adhimu kwa vijana wa Miguel Gamondi kulipa kisasi cha kuondolewa nyumbani mwaka jana na kurudia maajabu ya mwaka 2013.
Katika hatua ya makundi ya michuano hii, Morocco walimaliza kileleni mwa Kundi A wakiwa na alama saba. Kwa upande wao, Taifa Stars walifuzu kama mmoja wa "washindi watatu bora" (best losers) baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika Kundi C wakiwa na alama mbili.
Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, amebainisha kuwa mchezo huo utakuwa mgumu lakini wamejipanga vizuri kiufundi. Gamondi amesisitiza kuwa mbinu zitatofautiana kulingana na mahitaji ya mchezo.
"Tunajua nini cha kufanya kiufundi. Mliona namna tulivyocheza na Tunisia, itakuwa mechi ngumu ila mpira tunaenda kucheza wachezaji 11 dhidi ya 11. Haijalishi watakuwa na mashabiki wengi kiasi gani," alisema Gamondi.
Katika mchezo huu, Tanzania inatarajiwa kutumia mfumo wa 4-2-3-1 wakati Morocco wakitarajiwa kutumia 4-3-3. Morocco wanapewa nafasi kubwa kutokana na usahihi wao wa pasi, mashuti mengi langoni, na umiliki wa mpira.
Naye Kocha Mkuu wa Morocco, Walid Regragui, ametoa onyo kwa kikosi chake kutoibeza Tanzania. Regragui, ambaye anaifahamu Morocco vizuri kutokana na maisha yake hapo awali akiwa na klabu ya FUS Rabat, amesema Tanzania ina ligi nzuri na wachezaji mahiri wa kimataifa.
"Hakuna timu ndogo kwenye AFCON. Unapoteza mchezo mmoja na unatolewa; hii hatua haina chumba cha makosa kabisa," alisisitiza Regragui.
Historia Mpya kwa Stars
Hii ni mara ya nne kwa Taifa Stars kushiriki michuano ya AFCON tangu kuanzishwa kwake (ikishiriki miaka ya 1980, 2019, 2023, na sasa 2025). Hata hivyo, safari hii imeweka rekodi ya kipekee kwani ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufanikiwa kuvuka hatua ya makundi na kuingia hatua ya mtoano yaani kutinga hatua ya 16 bora—mafanikio ambayo ni makubwa zaidi ikizingatiwa kuwa Kocha Ángel Miguel Gamondi alikabidhiwa timu wiki chache tu kabla ya mashindano kuanza.
Licha ya muda mfupi, Gamondi ameweza kupandikiza mbegu ya kujiamini, nidhamu, na mfumo thabiti kikosini.
"Kufuzu huku ni somo kubwa kwa Tanzania. Taifa lazima lijivunie," alisema Gamondi. "Nilitaka kubadilisha ile dhana ya kuonekana timu dhaifu (underdogs)... hatushiriki tena kwa ajili ya kutafuta 'heshima' pekee; tunaamini katika uwezo wetu wa kufika mbali."
Ligi ya Ndani Inavyobeba Timu ya Taifa
Tanzania imeingia AFCON ikiwa na hali ya kujiamini iliyojengwa kwa miaka mingi kupitia ukuaji wa ligi ya ndani. Klabu kama Simba SC, Young Africans (Yanga SC), na Azam FC zimewajengea wachezaji uzoefu wa michuano ya kimataifa ya CAF, jambo lililowapa ujasiri wa kuhimili presha katika mechi kubwa.
Matokeo uwanjani yanajieleza: Tanzania imefunga bao katika kila mechi ya hatua ya makundi. Faisal Salum alitikisa nyavu, huku Novatus Dismas—mchezaji anayekipiga nchini Uturuki na zao la Azam FC—akitoa pasi mbili za mabao (assists), akionyesha akili kubwa ya kushambulia akitokea safu ya ulinzi.
Katika hatua ya makundi, Tanzania iliihenyesha Nigeria (bingwa mara tatu) kabla ya kufungwa 2-1, wakaibana Tunisia (bingwa wa 2004) na kutoka sare, kisha wakagawana alama na Uganda. Matokeo haya ni dhihirisho kuwa Tanzania sasa inaweza kupambana na mataifa makubwa ya soka barani Afrika.
Umoja na Nguvu ya Kisaikolojia
Taifa Stars inadhihirisha alama ya "Pamoja" ya AFCON, ikionyesha umoja mkubwa ndani na nje ya uwanja. Miaka ya Gamondi aliyoishi Morocco imemsaidia kujua namna ya kukabiliana na presha ya wenyeji:
"Niliishi hapa kwa miaka mingi na najua presha inayotengenezwa na mashabiki wao, lakini wakati mwingine presha hiyo inaweza kuwaathiri wao wenyewe (Morocco)."
Chini ya uongozi wake, timu imeunganisha nidhamu ya mbinu na ari ya kutoogopa mpinzani—hali ambayo imeibadilisha Tanzania kutoka kuwa washiriki wa kawaida hadi kuwa washindani wa kweli.
Wachezaji Nguzo Wanaoongoza Mapambano
Nahodha Ally Samatta amekuwa muhimili wa timu, akiongoza kwa mfano na utulivu katika nyakati ngumu. Faisal Salum anatoa ubunifu na uwezo wa kumalizia mashambulizi, huku Novatus Dismas akiongeza nguvu kwenye mashambulizi kutokea nyuma. Kwa ujumla, timu imeonyesha uwiano mzuri na uwezo wa kutengeneza nafasi katika kila mchezo.
Mtihani wa Kihistoria Mbele
Sasa, Tanzania inajiandaa kuvaana na wenyeji Morocco katika hatua ya 16 bora—mpinzani mgumu mwenye msaada wa mashabiki wa nyumbani. Hata hivyo, Taifa Stars wanaingia uwanjani bila hofu, wakiwa wameimarishwa na matokeo yao ya hivi karibuni na imani ya pamoja.
Kuinuka kwa soka la Tanzania ni uthibitisho kuwa uwekezaji kwenye ligi ya ndani, uongozi madhubuti, na mentality ya kutoogopa vinaweza kuifikisha timu kwenye mafanikio ya kihistoria. Hawatafuti tena kuheshimiwa—wanajipatia heshima hiyo wenyewe, kwa pamoja.

COMMENTS