HUENDA wanasayansi wanaochunguza jua wamefanikiwa kwa mara ya kwanza kunasa ishara za uwapo wa mlipuko katika jua saa chache kabla ya kutoke...
HUENDA wanasayansi wanaochunguza jua wamefanikiwa kwa mara ya kwanza kunasa ishara za uwapo wa mlipuko katika jua saa chache kabla ya kutokea kwa mlipuko wenyewe.
Pamoja na kupata ishara hizo bado wanasayansi wamepagawa sababu ya kuwapo kwa milipuko katika jua na inavyojitengeneza.
Kupitia uchambuzi wa data adimu zilizokusanywa kabla ya kutokea kwa mlipuko huo mkubwa, watafiti wamegundua mabadiliko mbalimbali katika tabaka la hewa linalozunguka jua, hatua inayotoa mwanga mpya wa namna milipuko hiyo mikubwa inavyoanza na jinsi gani matokeo haya yanavyoweza kusaidia kuboresha utabiri wa hali ya hewa katika anga za juu hapo baadaye.
Louis Seyfritz, mtafiti mkuu wa masomo ya anga za juu kutoka Taasisi ya Teknolojia ya New Jersey nchini Marekani aliyeongoza utafiti huo, amekiri kuwa hakuwa anatarajia kabisa kupata kile alichokigundua wakati akifanya uchunguzi huo.
Milipuko ya jua ni mipasuko mikubwa ya kishindo inayotoa miale yenye nguvu ya mionzi inayosukumwa na kuachiliwa kwa ghafula kwa nishati ya kisumaku kutoka kwenye jua.
Milipuko hii mikubwa ina uwezo wa kuvuruga mifumo ya mawasiliano ya redio duniani, kuharibu satelaiti zilizoko angani, na kuchochea dhoruba za kijiografia zinazoathiri miundombinu mbalimbali duniani, ingawa kwa miongo kadhaa wanasayansi wamekuwa wakihangaika bila kupata jibu la kina la nini hasa kinachosababisha milipuko hii.
Changamoto kubwa imekuwa ni ya kiutendaji kwani pamoja na kwamba vyombo vya anga za juu vinalitazama jua kila wakati, ni vigumu sana kupata picha na vipimo vya kina vya hali ya jua kabla ya mlipuko kutokea, kwa sababu vifaa vingi vyenye uwezo mkubwa wa kunasa picha huelekezwa tu kwenye maeneo ambayo tayari yanaonyesha dalili za mtikisiko au baada ya mlipuko kuwa tayari umeshatokea.
Katika utafiti huu mpya, Seyfritz na wenzake walibahatika kupata data za kipekee zilizorikodi harakati zilizokuwa zikiendelea kabla ya kutokea kwa mlipuko mkubwa wa jua wa daraja la X9. Eneo hilo la jua lililozalisha mlipuko huo lilikuwa tayari limeshatoa milipuko mingine kadhaa yenye nguvu siku chache nyuma, hatua iliyowafanya wanasayansi kuelekeza darubini na vyombo vya anga kuangazia eneo hilo, ikiwemo satelaiti ya NASA iitwayo IRIS, ambayo imeundwa maalum kuchunguza sehemu ndogo ya tabaka la hewa la jua kwa ukaribu wa hali ya juu.
Kutokana na satelaiti hiyo kuwa imeelekezwa hapo, watafiti walifanikiwa kupata data za uchunguzi wa mfululizo kwa takriban saa tano kabla ya mlipuko wenyewe kutokea, fursa ambayo ni adimu sana katika tasnia ya sayansi ya anga.
Akitumia data hizo kutoka satelaiti ya IRIS, Seyfritz alifuatilia tabia tatu kuu za plasma, ambayo ni gesi yenye joto kali sana iliyoko kwenye tabaka la jua, akipima mwanga wake, mjongeo wake kuelekea au kuondoka kwa watazamaji, na kasi ya msukosuko usio wa joto unaoonyesha kiwango cha vurugu ndani ya gesi hiyo.
Matokeo ya vipimo hivyo yalionyesha kuwa tabia hizo zote tatu zilianza kuongezeka takriban saa tatu kabla ya mlipuko wenyewe kutokea, ishara inayodhihirisha kuwa uga wa sumaku wa jua ulikuwa ukipoteza utulivu wake hatua kwa hatua.
Seyfritz amebainisha kuwa mkusanyiko wa ishara za namna hiyo kwa muda mrefu kabla ya mlipuko ni jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa mara kwa mara.
Pia, timu hiyo iligundua kuwa mwanga, mjongeo, na msukosuko wa plasma hiyo ulikuwa ukipanda na kushuka katika mzunguko maalum wa nyakati kabla ya mlipuko kutokea, ambapo mzunguko mmoja ulikuwa ukijirudia kila baada ya dakika saba hadi kumi, huku mwingine ukijirudia kila baada ya dakika 18 hadi 21.
Miendo hiyo ya mawimbi ilijikita zaidi karibu na mpaka ambapo kuta za uga wa sumaku zinazokabili pande tofauti zinakutana, eneo ambalo wanasayansi wanalihisi kuwa ndiko nishati ya kisumaku inajikusanya kabla ya kulipuka. Ingawa sababu binafsi ya mtikisiko huo bado haijajulikana, Seyfritz anasisitiza kuwa ikiwa miendo hiyo ya mawimbi itajirudia kabla ya milipuko mingine, basi itakuwa kiashiria kikubwa sana cha kutokea kwa mlipuko wa jua.
Zikiwa zimebaki dakika 15 hadi 20 kabla ya mlipuko mkubwa wa daraja la X9 kwa mujibu wa chati za astronomi kutokea, tabaka la hewa la jua lilionekana kuingia katika hali ya hatari zaidi, huku msukosuko ukiongezeka kwa kasi na plasma ikisukumwa nje kwa nguvu kubwa, mabadiliko yanayoashiria kuachiliwa kwa ghafula kwa nishati hiyo ya kisumaku inayosababisha milipuko.
Seyfritz amefafanua kuwa hakuna kipimo kimoja kilichojitegemea kutoa ishara ya wazi ya onyo, bali mchanganyiko wa kuongezeka kwa mwanga, kasi ya msukosuko, na miendo ya mawimbi kwa pamoja ndivyo vilivyosimama kama ishara ya mwanzo wa dhoruba hiyo ya anga.
Hata hivyo, matokeo haya hayamaanishi kuwa sasa wanasayansi wanaweza kutabiri milipuko ya jua kwa masaa kadhaa kabla haijatokea, kwani utafiti huu umeangazia mlipuko mmoja tu na watafiti bado hawajajua kama ishara hizi zinatokea kwa namna hiyo hiyo kabla ya matukio mengine ya milipuko.
Ili kupata majibu ya uhakika, itakuwa lazima kuchambua milipuko meninge mingi zaidi, jambo ambalo ni changamoto kutokana na uhaba wa data za namna hiyo zilizowahi kunaswa huko nyuma. Hatua inayofuata sasa ni kubaini kama mifumo hii inajitokeza katika sampuli kubwa zaidi ya milipuko ili hatimaye ishara hizi ziweze kuwa sehemu ya mifumo ya baadaye ya utabiri wa hali ya hewa ya anga za juu.
Source:Jarida la kisayansi la Solar Physics

COMMENTS