WATANZANIA waishio ughaibuni wamesema tukio la Tanzania Diaspora Business Forum 2026 lililofanyika jijini London limeendeleza kwa vitendo ...
WATANZANIA waishio ughaibuni wamesema tukio la Tanzania Diaspora Business Forum 2026 lililofanyika jijini London limeendeleza kwa vitendo dhana ya kuwathamini wazalendo wanaoishi nje na kuwajumuisha kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania.
Hatua ya Serikali
ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwafuata na
kukutana ana kwa ana na Watanzania hawa ughaibuni inadhihirisha nia thabiti ya
kutambua mchango wao mkubwa kama wadau muhimu wa maendeleo ya Taifa.
Mmoja wa
watanzania aishie Uingereza Freddy Macha amesema kwamba mkutano huo uliokuwa na
lengo la kuunganisha juhudi za Watanzania walioko nyumbani na walioko nje ya
nchi, ulifana na kuonesha nia ya serikali kwa wanadiaspora ya kuwataka kuwekeza
mitaji na ujuzi wao katika miradi mbalimbali ya kimkakati nchini Tanzania.
Macha alisema
katika andiko lake kwamba, mamia ya Watanzania walisafiri kutoka majimbo na
maeneo mbalimbali ikiwemo Uingereza, Scotland, Ireland na Wales ili kukutana na
Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Lameck Nchemba katika hoteli za Marble Arch na
Millennium Gloucester Kensington.
Mkutano huo
uliwajumuisha zaidi ya wajumbe mia tatu na hamsini kutoka vikundi na taasisi
mbalimbali kama TZ UK, ATUK, Zanzibar Welfare Association in the UK na Tanzania
UK Business Group, ulifanyika katika mazingira rafiki.
Waziri Mkuu Dkt
Nchemba ambaye aliambatana na ujumbe mzito wa viongozi na watendaji wa Serikali
akiwemo Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Angella Kairuki, Balozi
wa Tanzania Uingereza Mbelwa Kairuki, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje
Balozi Said Shaib Mussa, Makatibu Wakuu wa Mipango, Uwekezaji na Uchumi wa
Bluu, pamoja na Watendaji Wakuu wa TISEZA na ZIPA,alieleza kwa kina hatua kubwa
ambazo Serikali imezichukua katika kukuza uchumi na kuboresha miundombinu ili
kuweka mazingira salama na yenye tija kwa uwekezaji wao.
Akiwahutubia
wanadiaspora hao, Dkt Mwigulu Alibainisha kuwa uchumi wa nchi umeendelea kuimarika
licha ya kukabiliwa na changamoto za kimataifa na kitaifa kama athari za UVIKO
19, mabadiliko ya sera za biashara duniani, migogoro ya kivita Mashariki ya
Kati, uhaba wa fedha za kigeni na maafa ya mafuriko Hanang.
Katika sekta ya
usafirishaji, alieleza kukamilika kwa ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR kipande
cha Dar es Salaam hadi Dodoma, maendeleo ya vipande vya Isaka hadi Mwanza,
Tabora na Manyoni ili kuunganisha na Makutupora, na matarajio ya Rais Dkt Samia
Suluhu Hassan kuzindua rasmi reli ya Dar es Salaam hadi Mwanza kabla ya
kumalizika kwa awamu yake ya pili.
Akiendelea
kufafanua fursa hizo za kiuchumi, Waziri Mkuu alieleza kuhusu maendeleo ya
upembuzi yakinifu wa reli ya kimataifa ya kutoka Uvinza na Kigoma kwenda
Musongati na Gitenga Burundi mpaka Kindu na Uvira DRC, ambayo pindi
itakapokamilika itakuwa ya kwanza kwa urefu barani Afrika na ya tano duniani.
Pia aligusia
mchakato wa kumpata mkandarasi wa reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay pamoja na
utekelezaji wa miradi ya bomba la mafuta. Katika sekta ya nishati na maji,
alieleza kuwa umeme umeunganishwa katika vijiji vyote nchini na sasa juhudi
zipo kwenye vitongoji na nishati safi ya kupikia, huku vijiji visivyo na maji
vikiwa vimepungua hadi chini ya elfu moja. Kwenye elimu, alitangaza maandalizi ya
elimu ya lazima hadi kidato cha nne kuanzia Januari 2028 itakayopokea wanafunzi
zaidi ya milioni tatu, ikihusisha ujenzi wa madarasa elfu kumi na sita na
maabara elfu hamsini.
Katika sekta ya
afya, Serikali imesogeza huduma bora karibu na wananchi kwa kuboresha
miundombinu na kuweka vifaa tiba vya kisasa kama MRI, CT Scan na Ultrasound
hadi ngazi ya hospitali za wilaya. Dkt Mwigulu alihitimisha kwa kueleza kuwa
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa
kipato cha kati cha juu, akisisitiza kuwa Serikali inaweka mazingira wezeshi na
inawahitaji Watanzania wote wa nyumbani na walioko ughaibuni kushirikiana na
kuwekeza katika sekta zenye fursa kubwa kama vile madini, kilimo, mifugo,
uvuvi, utalii na uchumi wa bluu.
Kama sehemu ya
utekelezaji wa vitendo wa kuondoa vikwazo na kuingiza wanadiaspora katika mfumo
wa kiuchumi, mikutano hiyo ilihusisha vikao vidogo vya kibiashara,
ushirikishwaji wa mabenki makubwa ya nyumbani kama CRDB, NMB na Azania, pamoja
na makampuni ya uwekezaji wa majengo kama Hamidu City Park.
Pia wanadiaspora
walipata fursa ya kukutana na mmiliki wa kampuni ya NALA Benjamin Fernandes
inayoshughulikia usafirishaji wa fedha, huku wakitatuliwa changamoto zao za
kisheria na uraia kupitia huduma za usajili wa Vitambulisho vya Taifa
zilizotolewa papo hapo na Maafisa wa NIDA waliosafirishwa kutoka Tanzania
wakiongozwa na Maryamu Issa, wakisaidiwa na Afisa Uhamiaji wa Ubalozi Ally
Mtanda.
Ili kuhakikisha
sauti na kero zao zinazungumzwa na kufanyiwa kazi kwa haraka, wanadiaspora
walikabidhiwa namba ya simu ya WhatsApp ya Waziri Mkuu kwa ajili ya mawasiliano
ya moja kwa moja.




COMMENTS