JUA lilikuwa linakuchwa taratibu katika maeneo haya ya milima ya Uluguru pande za Mgeta. Maeneo ya Lukwangule tayari yalishapoteza nuru yake ya mchana na kiza kilikuwa kimejivuta kama bibi kizee.
Wakati maeneo hayo kiza kinajivuta maeneo ya kijiji cha lusungi yalikuwa bado yanachechemea na mwanga kidogo uliokuwa unavuka.
kuku wote walishaingia katika mabanda yao, wakiwa wametulia tayari kupitisha usiku mwingine tulivu. wanyama wa usiku taratibu walianza kutoka katika maficho yao, bundi mmoja akaanza kulia.
Katika nyumba moja mama kuku alikuwa anahesabu watoto wake huku analia,mbuzi katika mabanda walikuwa wanacheua na kondoo nao pia, walikuwa wameshafunguliwa makopo midomoni mwao na wametulia huku beberu mmoja mgomvi akiwa ametiwa kamba sawia.
Msichana mmoja mweusi wa wastani, mrefu na ambaye alikuwa na umbile la nane, akiwa na mfuko wake mgongoni alikuwa anatembea taratibu katika barabara inayoelekea Bumu. Njiani alikuwa peke yake, lakini alikuwa anashika kasi ya mtu ambaye hakuwa na mazoea ya milima au ambaye ni mgonjwa.
Mwenda binti pekee kwa baba na mama Mwenda alikuwa ameondoka nchini miaka saba iliyopita kwenda kusomea udaktari nchini Russia. Baada ya kupata vyeti vyake alikuwa na kila sababu ya kurejea nyumbani na kuungana na watu wake. Alikuwa amewamisi wazazi wake ambao alikuwa na mazoea ya kuwaandikia barua lakini wenyewe walikuwa na mazoea ya kutomjibu.
Alijua kwanini hawataki kumjibu. Walimweleza mapema kwamba wanaomba awatumie salamu kila mara lakini wao hawataweza kujibu kwa sababu za kiusalama.Walimwambia kwamba baba yake mdogo alikufa kwa namna ya ajabu nchini Canada baada ya kusoma barua iliyotoka nyumbani akidhani inatoka kwa ndugu zake.
Mzee mmoja mchawi alimuua ndugu yao na akatamba kijiji kizima kwamba amewapatia na hilo hawatakaa walisahau maisha yao yote.
Aliingia Dar es salaam saa nne akitokea Nairobi, Kenya ambako aliunga ndege yake. Aliunga mara nyingi sana usafiri wake kwani alipotoka Moscow, alifika Addis Ababa, Ethiopia ambako alikaa kwa siku nzima kabla ya kusafirishwa na Ethiopia Airline na kushushwa Nairobi kenya ambako alichukua Kenya Airways na kutua uwanja wa ndege wa Dar es salaam saa nne asubuhi.
Mpaka saa saba alikuwa amefika kwa ndugu yake Magomeni Mikumi katika nyumba ya Uyeka. Aliketi kwa muda kabla ya kuondoka kwenda kutafuta usafiri wa Morogoro . Pale kwa shangazi yake Magomeni nusura asiondoke baada ya kukutana na wadogo zake ambao walishakua wakubwa wakimshangaashangaa.Lakini alipiga moyo konde hasa baada ya kuelezwa kuwa wazazi wake hawakuwa katika hali nzuri sana inafaa kwenda kuwaona.
Saba nusu, pale Magomeni mapipa alikuwa abiria wa mwisho katika Double Coaster moja ambayo haikubeba abiria tena mpaka inaingia morogoro saa kumi na nusu. Alifikiria sana kwenda gesti kulala lakini aliamua kufanya kitu kimoja cha maana cha kwenda katika soko la Morogoro kuona kama hakuna lori linalopandisha kwenda kwao Mgeta.
Binti huyu bahati ilikuwa kwake, kwani anatia mguu tu akaliona lori ambalo lilikwishapakia pumba na mabati likiwa tayari kuondoka.
"Vipi mnapanda mlimani?"
"Ndio bibiye unataka usafiri?"
"Ndio kama inawezekana"
"Utakuwa mwanamke peke yako huko nyuma manake mbele kumejaa."
"Wala usijali, mpaka Lolo bei gani?"
"Mpaka Lolo? Lolo ndio wapi Hading'oka"
"Ndio Madukani kwani wewe hupajui?"
"Nimechemsha kila mara inakuwa taabu kukumbuka.mama wewe ingia tu tutaelewana sisi binadamu."
"Ninaweza kuwa sina hela hiyo?"
"Huonekani kama huna hiyo hela nitakayoihitaji. nataka shilingi 1,500 tu"alisema dereva na kisha akamhimiza apande kwani anataka kuingia bado kweupe.
Alifika Lolo lakini hakushuka, kwa kuwa lori lilikuwa alinaelekea Tchenzema, akashukia visomoro ndipo alipoanza taratibu hatua za kurejea kwao, huku fikira zikimuumiza.
Atawakuta namna gani watu wake na watakuwa vipi. Alikumbuka wadogo zake kutoka kwa mama mdogo wake hakujua atawakuta vipi.
Lakini kule nyumbani Baba yake alikuwa amelala akiwa mgonjwa na mama yake alikuwa anahangaika kufanya hiki na kile ili kusawazisha mambo kabla ya kuanza kumhudumia mgonjwa wake.
kama vile mtu aliyekwisha choka mawazo ya mtoto wake wa pekee yalikuwa yakimjia. Alifikiria mtoto wake kwa miaka saba hajawahi kumtia machoni, watu walikuwa wanamdhihaki na ndugu wa mume walikuwa wameacha kumsaidia ndugu yao zamani kabisa na juhudi kubwa ilibaki kwake yeye ambaye ndiye mke.
Kazi za shamba, kazi za kilimo, kazi za kutunza mifugo hazikuwa na msaidizi kwani hata wale walio wadogo wanaonekana kama wameambiwa wasifike pale, alikuwa anaonekana mchawi anamloga mume wake.
Mama Mwenda hakuwa na muda wa kumsaida mume wake kwa kipindi kile cha jioni ilikuwa lazima akimbizane na kutwanga kwanza kabla hajampatia chakula mgonjwa wake ambaye hakuonyesha hata dalili za kupona katika ugonjwa wake.

Siku ile alimaliza kutwanga mapema akampikia mumewe na baada ya kumkanda kwa maji ya uvuguvugu alimnyanyua na kumsaidia kumlisha. Alipoona mgonjwa wake yupo safi naye akala na kisha kuanza kujiandaa kwa usiku.
Wakati anafunga mlango kwa kuweka michi na kinu alisikia hodi ambayo alidhani kwamba ni kichaa chake.
Hodi ilirejewa tena na tena na mwisho wake akaamua kuchungulia hakuamini aliyemuona pale ndani na badala ya kumfungulia mlango akakimbilia kwa mume wake.
"Baba Mwenda, mwenda amerudi" alisema huku akiwa anashangilia.
"Yupo wapi?" aliuliza mzee kwa sauti ya taabu.
"Yupo nje"
"Sasa si kiza kimeingia unawezaje kumwacha nje"
"Ohh Mungu ashukuriwe" alikimbilia nje na kuanza kutoa vifaa alivyoweka mlangoni, akafungua mlango na kumkumbatia mwanawe kwa muda mrefu sana kabla ya kumsalimia na kumtazmaa kila mahali katika mwili wake.
"Mhh mama hujaacha tu kunikagua kote huko?"
"Mwanangu sijakuona muda gani?"
"Si hivi nipo mama." alisema akitabasamu alikuwa anamjua mama yake huwa anamkagua hata akitoka shule.Alikuwa na kawaida hiyo kiasi ya kwamba alikuwa wakati mwingine anamuona mama yake kuwa kero.
" Wooh umekuwa na rangi gani sasa manake bluu si bluu , weusi si weusi rangi gani hii" alisema huku akimpokea begi kubwa mgongoni na kwenda kuiweka katika chanja ambayo ilitengenezwa vyema kwa ajili ya kuwekea
mizigo.
Aliitazama nyumba yao, nyumba iliyomlea. Alitaka kuibadili kama watu wengine walivyobadili nyumba za wazazi wao. Alikuwa ameona nyumba nyingi zikiwa zimejengwa pau na wala si misonge kama ya kwao ingawa ilijengwa vyema.
Ilikuwa nyumba ambayo ina chumba tatu, chumba cha ndani ambacho ni jiko ambako kila mara alikuwa akihimizwa kulala humo kutokana na joto lake, chumba cha wazazi wake ambacho kilikuwa karibu na zizi la kuku na mbuzi na kondooo na kingine ambacho kilikuwa na mwanga na safi kwa ajili ya wageni.

Alikumbuka kitanda chake cha teremka tukaze ambacho baba yake alikuwa amemnunulia godoro la sufu baada ya kupata nafasi ya kwenda shule ya sekondari ya Kilakala kutoka Bumu.Ilikuwa taabu kidogo kukumbuka kama mto wake ulikuwa upo au la.
"Mhh nambie hali ya baba mama" alisema huku akiwa amekaa katika kiti cha fito kilichokuwa katika sebule ya nyumba yao hiyo ya msonge.Alikuwa ni miongoni mwa watoto ambao hawakuwa wanadeka, alikuwa amechangamka na mama yake lakini kitendo cha kutomuona baba yake pale akitoka kumuona kilimpa shida kidogo, alitarajia habari mbaya manake miaka saba si sawasawa.
"Baba yako yupo ndani hali yetu si sawasawa mwanangu" alisema kwa huzuni kisha akaanza kumweleza taabu ilianza kukohoa na ilipofika kukohoa damu wote waliwakimbia.
"Unaponiona hapa sina la kufanya, hatuna hela, hatuna dawa nimekuwa nikihangaika na mibaazi mpaka sasa tupo tu. baba zako wamenikimbia mimi sasa ndiye muuguzaji." alisema huku anadondosha machozi.
Mwenda aliamka na kwenda kumkumbatia mama yake na kisha akaongoza mahali ambapo alijua lazima baba yake yupo, chumba cha kati ambacho huwashwa moto.Kweli alimkuta baba yake.
Hali ya baba yake ilimtisha.
Alimsalimia na kumuitikia kwa taabu kubwa.
Haikuwa rahisi kuelewa kama anamsikia vyema baba yake au la. Akakimbilia kumbariki kisha akatulia sana.
"Mama ilianza lini?"
"Tunamwaka mmoja" alitulia.
Alimwangalia akatazama mapigo yake kisha akatoka na kukimbilia begi lake.
Ilikuwa taabu kubwa katika moyo wake, alijua baba yake ana kifua kikuu na huenda naye mama yake ana kifua kikuu pia.
Alienda kuchukua vidonge vya kutuliza maumivu na saplimenti za vitamini.
"Mama baba anakula?" alimuuliza mama yake wakati anaingia tena katika chumba kile.
"Bado anaweza kula japo kwa taabu."
"Basi mpe dawa hizi na kikopo hiki akikohoa tia mate yake." alisema.
"Yanini mama?" aliisikia sauti yake dhaifu.
"Kesho asubuhi asubuhi nataka kwenda kituo cha Afya Mgeta nijue nini."
"Mtaalamu amesema wamemroga kwa sababu wewe upo Ulaya" alisema mama mtu
"Inawezekana mama lakini pia inawezekana baba ana kifua kikuu ndio maana ukimpa mibaazi inatulia"
"Haya mama" alisema mama yake na kisha akachukua vidonge vile na kuhangaika kumpa mgonjwa na baada ya kumaliza kumpa alikohoa lakini hakutoa damu badaaye alipokohoa alitwaa makohozi na kuona yanadamu na kohosi la kawaida.
Bila hata kujiuliza swali mwenda alitambua kwamba nafasi ya baba yake kupona ni hamsini hamsini, kifua kikuu kilikuwa kimetafuna sana....

Kwa leo kwaheri tutaonana Jumatatu ijayo kwa mwendelezo

Post a Comment

Anonymous said... November 14, 2013 at 11:05 PM

Mzee wa Lukwangule...hii hadithi mbona haiendelei? Samahani sana, Mimi ni mpenzi wa blog hii na nimefuatilia hii hadithi lakini ni kipindi kirefu sana bado tupo mwanzoni tu. Naomba uendelee kutusimulia anayoendelea.

Anonymous said... February 12, 2014 at 12:33 PM

Muendélezo ln mbona j3 zimepita nyingi2

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO