TAMASHA la Nchi za Jahazi ambalo linahusisha nchi za Afrika, mataifa yaliyo katika bahari ya Hindi, India, pakistan na Iran ni moja ya matam...


TAMASHA la Nchi za Jahazi ambalo linahusisha nchi za Afrika, mataifa yaliyo katika bahari ya Hindi, India, pakistan na Iran ni moja ya matamasha yanayokua kwa kasi na mwaka huu, likiwa linatimiza miaka 11 linataka kuujadili utamaduni ambao upo njia ya panda.
Tamasha hili ambalo kwa sasa linaitisha kazi za fasihi na sanaa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia; ni tamasha ambalo kama watanzania watalitumia vyema, si tu watauza kazi zao bali pia watawezesha watalii kumiminika kwa wingi kwa kuwa watajua nini kinatokea hapa nchini .
Ingawa kipindi hicho huwa ni muda wa kutamalaki kazi za sanaa na kuikumbatia fasihi ni kipindi ambacho wanautamaduni wanapata nafasi ya kuangalia kazi za wengine na pia kupata nafasi ya kufanya mauzo au mazungumzo na watuw engine kuhusiana na programu mbalimbali za kisanii.
Katika matamasha karibu kumi yote yaliyopita nimekuwa nikihimiza kipindi kama hiki kwa wananchi wa Tanzania kulienzi tamasha hili kw akupeleka kazi zao kwa wingi na si kuwaachia watu wa kigeni kutumia tamasha hili kujipandia ngazi.
Wapo wasanii wengi ambao wametumia jukwaa la tamasha la nchi za jahazi(ZIFF) kutengeneza mustakabali wa kazi zao ambazo zimekuwa zikihusudika hasa baada ya kuzinduliwa rasmi katika tamasha hilo ambalo hufanyika visiwa vya Unguja.
Watanzania wanaposhindwa kutumia Tamasha hilo ambalo kazi yake kubwa ni kuwakutanisha wasanii na kujadili masuala mbalimbali kupitia makongamano yake,unaanza kuona woga na kuthubutu unaowakabilki wasanii wengi wa Tanzania, wawe wa muziki, filamu au sanaa ya kuchonga na hata fasihi. Tamasha hilo kubwa ambalo linaweza kuelezwa kuwa bomba kuliko yote Afrika Mashariki na ya Kati, manake lipo la Amakula la Uganda na hili la karibuni la kenya ni jukwaa la kuuza na kukutana na soko au hata uhakiki wenye lengo la kuboresha zaidi kazi za msanii.
Mara zote katika tamasha hili kunakuwepo na vyombo mbalimbali vya habari vya nchini Tanzania na nchi za nje, vyombo ambavyo hutumika kupeleka ujumbe mbalimbali kwa watu wengine wa ughaibuni ambao hupenda kujua utamaduni katika eneo hili la afrika unaenziwa vipi.
Mkurugenzi wa tamasha hili, Dk Martin Mhando, amesema katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya kwamba mwaka huu wamepania kufanya vitu vingi vizuri na ndio maana maandalizi ya tamasha yalianza Novemba mwaka jana na sasa wanaitisha kazi za watu mbalimbali kwa uhakiki.
Pamoja na filamu tamasha hilo pia hukutanisha wanazuoni wakijadili mada mbalimbali zenye upeo mkubwa na safari hii mabishano makubwa yatakuwa juu ya utamaduni njia ya panda.
Dk Martin mbaye kitaalamu ni mtengeneza sinema na hufundisha sinema katika chuo kikuu cha Australia,akizungumza kutoka katika ofisi za tamasha hilo zilizopo Forodhani katika Ngomekongwe mtaalamu huyo amesema ni kipindi muafaka kwa wasanii wa Tanzania wakatumia tamasha hilo ambalo mwaka jana serikali ya Zanzibar ilisema wazi kwamba italipiga jeki na kulitumia katika kufanikisha sekta ya utalii.
Katika eneo la ofisi ndipo pia lipo eneo kuu linalotumika kwa ajili ya kuonyesha filamu na pia muziki.Ukumbi huu wa zamani kabisa ambao ulikuwa unatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali ingawa kwanza ilikuwa ngome ya Wareno na baadaye kuwa kituo cha reli ingawa harufu yake kwa sasa haipo.
Harufu hiyo imesahaulika lakini ukifika pamoja na kuona sanaa pia unakutana na maelezo Ngome Kongwe hiyo ilikuwa na nini. Hapa watalii hujionea taarifa mbalimbali zilizorekodiwa za Sultan kutengeneza Reli kwenda Bububu na eneo lile lilikuwa ndilo karakarana na kituo cha reli. Mwaka jana kulikuwa na kila tarajio kwamba sinema ya Kitanzania itafungua dimba, pamoja na kwamba haikufungua dimba filamu nyingi zilioonyeshwa siku ya kwanza zilikuwa za Kitanzania na wakenya walitawala kwa nchi za Afrika mashariki.
Mwaka huu Filamu inayogusa Namibia ndiyo ityakayofungua dimba.Watanzania naambiwa wanasuasua kurekebisha mambo.
Kwa miaka 10 filamu za kitanzania zimekuwa hazitumiki kuanzisha tamasha hilo, si kwamba waandazi hawataki bali ushiriki wenye uhakika kutoka kwa watanzania ni mdogo sana.
kwa kuwa majaji wanatoka katika makundi matatu makubwa duniani na wanaozungumza Kiingereza na Kifaransa ni vyema kwa watengeneza sinema wa Tanzania ambao wanataka kuona soko la Ulaya kutumbukiza maelezo katika sinema zao kwa lugha ya Kiingereza ili wanaoamua (majaji) kuwa na nafasi ya kuangalia si ubora wa sinema pekee bali skrini yake na hadithi yenyewe.
Sinema kama ya Hammie Rajab ya Mama ambayo iliingizwa katika tamasha la tisa haikuweza kufua dafu kwa kuwa haikuwa na maelezo (subtitles): Ndio kusema kama watanzania wangelipenda waangaliwe kimataifa sinema zao zinastahili kuwa na maelezo ya Kiingereza.
Watanzania wanaotakiwa kupeleka kazi zao ni pamoja na wale wa filamu , fasihi watunzi wa vitabu na waghani mbalimbali, wachongaji na waumbaji wa mambo mbalimbali na pia wanamuziki na watu wa sanaa za jukwaani zikiwemo ngoma.
Inafaa kukumbuka kuwa Tamasha la nchi za majahazi si tu linaonyesha filamu lakini lina vitu vingi mno kiasi kama nilivyosema awali na kwamba wakati mwingine usipokuwa makini mengine yatakupita bila ya wewe kuwa na habari.
Vitu kama makongamano kwa watoto, wanawake, watengeneza sinema, wanamuziki, wahakiki wa filamu, wasanii wa jukwaa, michezo ya kuigiza, wachoraji na pia wasanifu maumbo ni vitu vinaweza kukupita kama nunavyoweza kupitwa na maonyesho ya sinema na maonyesho ya Forodhani kama huna uhakika unataka nini hasa.
Pamoja na uwingi wa masuala hayo,Mtendaji mkuu wa ZIFF Dk Martin Mhando alisema katika mazungumzo kuwa ushiriki wa Watanzania ni mdogo na hii inadumaza uwezo wa fikra kwa wasanii wa Tanzania kuweza kushiriki katika soko la kimataifa la sanaa. Wakati washiriki wa nje hupapatikia kutuma maombi na kutafuta maelekezo watanzania wenyewe pamoja na kupelekwa ushawishi bado wanaona kwamba si lazima kushiriki katika tamasha hili na mbaya zaidi hata vyombo vikuu vya habari vimekuwa havioni nafasi ya ZIFF katika kuboresha maisha ya wasanii na pia sanaa yenyewe.
Mwaka jana Vyombo vya nje kama BBC, Deutch Velle,VOA,Reuters AP, na AFP walituma watu wao kufanya kazi ya kurekodi matukio kwa shughuli mbalimbali na hata wengine wanafanya dokumentari ambazo baadaye wanaenda ama kuziuza kwao au kuwaonyesha watu kwa bei mbaya kabisa. Lakini vyombo vya habari vya tanzania vya elektroniki hata uhusiano wa kawaida hawataki au watataka kukutoza bei mbaya kwa huduma ya kuhabarisha.
"Makongamano mengi ambayo kwa kawaida huendeshwa na hata mwaka huu yapo yamelenga kuinua vipaji vya watanzania, lakini watanzania wenyewe huwa wanakosekana kwa wingi na badala yake watu kutoka Uganda, kenya, Rwanda, Zambia, Malawi wanajishughulisha hakika ni upotezaji wa nafasi ya pekee ya kuinuka kwa wasanii na sanaa yetu kujulikana kimataifa" anasema Dk Martin.
Ipo faida kuwa ya ushiriki katika tamasha hili. Kuna faida kubwa ambayo huenda haionwi vyema na serikali au watu kwa kawaida. Kimsingi mshiriki si tu anatangaza jina lake bali biashara yake na kupata mwelekeo mpya wa mafanikio ya wenzake.
Kimsingi tamasha la nchi za majahazi si tu linastahili kupangwa kuwa bora zaidi kwa ajili ya wasanii na kutangaza utamaduni wetu lakini pia lina nafasi kubwa ya kujadili utamaduni katika hali ya sasa ambapo utandawazi ni mwalimu mkorofi anayevuruga hata vinywa na matendo ya watu kwa sasa.
Ni wakati wa wasanii mbalimbali wakiwemo watengeneza sinema kupeleka kazi zao kwa Tamasha ili kupata nafasi ya kufanya mazungumzo na wenzao wa nje na hata wa ndani na kuwashawishi kushirikiana kutengeneza sinema hapa nchini kwa gharama nafuu zaidi.
Kama wasanii watajumuika kwakutuma kazi zao, tamasha hili litaendelea kubwa zaidi na kuwa na upeo mkubwa zaidi kuwaandaa watu wa kwenda kushiriki katika maonyesho ya nje ambayo ni muhimu zaidi katika kujitangaza. mwisho
COMMENTS