TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA YA CHAMA CHA WAFANYAKAZI WA SERIKALI ZA MITAA-TALGWU KUHUSU KUUDAI MFUKO WA NHIF SH B...
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA YA CHAMA CHA WAFANYAKAZI WA SERIKALI ZA MITAA-TALGWU KUHUSU KUUDAI MFUKO WA NHIF SH BILIONI 3.6 ZA MAKATO YALIYOFANYIKA MWAKA 2001/2002:
1. UTANGULIZI;
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) katika mkutano wake na Waandishi wa Habari jana, kimedai kuwa kinaudai Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Shilingi Bilioni 3.6, ambazo ni makato yaliyokatwa kimakosa kwa wanachama wao ambao wakati huo walikuwa hawajajumuishwa katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Sisi katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hatutaki malumbano, bali tunapenda kupitia kwenu umma wa Watanzania na wanachama wetu waelewe ukweli kuhusu suala hili ambalo:-
• Kwanza siyo suala geni,
• Pili madai haya yamekuwa yakitolewa au kuibuka kunapokuwa na uchaguzi ndani ya TALGWU au uchaguzi mkuu wa Serikali,
• Tatu kwamba kitu ambacho viongozi wa TALGWU hawakisemi na kuwaambia wanachama wao ni maagizo waliyopewa na Serikali katika suala hili na nini wamefanya ili kulimaliza kabisa suala hili ambalo Mfuko tayari ulishatekeleza kwa upande wake, kulingana na maagizo na miongozi ya Serikali,
2. Historia ya madai ya TALGWU;
Sheria ya Kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
ilianza kutekelezwa tangu mwezi Julai 2001. Menejimenti ya Mfuko ilikabidhiwa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa sheria hii.
Katika kuitekeleza sheria hii, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, iliweka mwongozo wa misingi ya makato (eligibility criteria) ya Watumishi wa Serikali Kuu waliostahili kuchangia katika Mfuko wa Bima ya Afya.
Katika kipindi cha mwanzo cha utekelezaji wa Sheria hii (Julai, 2001 hadi April 2002), serikali ilitoa muongozo ambao uliweka bayana ni nani wanastahili kuchangia katika Mfuko wa Taifa a Bima ya Afya na nani hawakustahili. Serikali kupitia Idara Kuu ya Utumishi ( sasa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma) ilitoa muongozo ufuatao:
• Idara Kuu ya UTUMISHI ilitoa mwongozo wa pili wa makato wa mwezi Mei 2002, uliofafanua zaidi watumishi wanaostahili kukatwa ambao walikuwa ni wale waliolipwa na Serikali kuu ingawa walikuwa katika Serikali za Mitaa na kubainisha kuwa watumishi ambao hawahusiki na makato ni wale walioajiriwa na Serikali za mitaa na kulipwa kwa kutumia vyanzo vya mapato vya Serikali za Mitaa.
• Serikali, Mwezi Novemba, 2002 illifanyia mapitio Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kuwajumuisha Watumishi wote walioko kwenye Serikali za Mitaa.
Serikali na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya baada ya kubaini kuwa kulikuwa na Watumishi 12,894 waliokatwa kimakosa iliwarejeshea kiasi cha Shilingi 269,563,469.54 watumishi hao. Zoezi la kuwakabidhi lilifanywa kwa pamoja kati ya Mfuko na Chama cha TALGWU makao makuu na matawi yake mikoani. Pamoja na hatua hiyo ya kuwalipa watumishi hao, TALGWU ilikuja na madai mapya wakisema bado kuna watumishi 53, 000 ambao hawajalipwa na wanadai kiasi cha Shilingi bilioni 1.8 na sasa wanadai Shilingi Bilioni 3.6 kwa watumishi 58,000.
Kwa taasisi yoyote inayofuata misingi ya fedha na hata ninyi wenyewe mnaweza kuona jinsi madai na idadi ya watu inavyobadilika kila siku.
3. CHIMBUKO LA MADAI YA CHAMA CHA TALGWU NA MSIMAMO.
Chimbuko la madai ya TALGWU ni kuwa wao hawaikubali tafsiri iliyotolewa na Serikali kuhusu ni nani waliotakiwa kuchangia na vilevile haikubali miongozo ya makato iliyotolewa na Serikali, jambo ambalo liko nje ya uwezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
4. HATUA ZILIZOCHUKULIWA KULIPATIA UFUMBUZI SUALA HILI
Uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya baada ya kuwalipa Watumishi 12,894 waliokatwa kimakosa kulingana na miongozo ya Serikali, Mfuko umeendelea kupata malalamiko kutoka TALGWU, kutoka kwa watumishi waliodai kutorejeshewa michango yao (hasa wa Kasma 5004 na 5006) ambapo ulichukua hatua zifuatazo:-
a. Kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na Chama cha TALGWU ili kuwaelimisha na kuwafahamisha miongozo iliyotumiwa na Serikali katika kuwakata watumishi. Mfuko pia uliwakabidhi miongozo hiyo chama cha TALGWU ambao wanakiri kuipokea lakini inawachanganya.
b. Kwamba TALGWU waratibu zoezi hilo badala ya kila Tawi kuwasilisha majina ya watumishi hao moja kwa moja Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI- kulingana na maagizo ya Serikali. Na kwamba kamati iliyoundwa na kushirikisha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Fedha, TAMISEMI na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wangeyahakiki madai hayo na kuyawasilisha kwenye Mfuko kwa hatua zaidi. TALGWU hawajafanya hivyo ndio maana suala hili linachukua muda mrefu.
5. MAOMBI YA MFUKO KATIKA SUALA HILI:
Tunauomba uongozi wa TALGWU kama kuna madai yoyote halali basi wafuate maelekezo waliyopewa ya kuwasilisha orodha ya majina ya watumishi wanaodai kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na yakishahakikiwa na kuletwa kwetu, sisi tutawalipa mara moja.
Napenda kumalizia kwa kusema kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakati wote unafanya kazi zake kwa kuzingatia Sheria ya kuundwa kwake na kusimamia majukumu yake kwa mujibu wa Sheria. Fedha hizi ambazo tunazisimamia ni fedha za umma (Public Funds) ambazo zinasimamiwa na kikaguliwa na Mkabidhi na Mdhibi Mkuu wa Serikali (CAG). Ndiyo maana hata malipo ya awali tuliyalipa kwa kuzingatia taratibu za fedha na idhini kutoka Serikalini.
Hakuna wakati wowote ambapo Mfuko huu umekaidi kutekeleza maelezo yoyote halali, kama TALGWU wanavyodai katika taarifa yao iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari jana.
Mkurugenzi Mkuu,
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Tarehe 27/08/2010.
Pichani:Mkurugenzi mkuu wa NHIF akifafaunua jambo kwa whariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali juu ya malalamiko ya madai yaliyotolewa jijini jana na uongozi wa TALGWU Taifa na kutishia kuifikisha mahakamani NHIF. waliopo kushoto kwake viongozi waandamizi wa mfuko huo.
COMMENTS