Hotuba ya kufunga kikao cha Bunge Mkutano wa Saba

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU   WA   JAMHURI YA   MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA SAB...



HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU  WA  JAMHURI
YA  MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA SABA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA – DODOMA, TAREHE 23 APRILI 2012*


UTANGULIZI


Mheshimiwa Spika,
1.           Nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema
kwa kutuwezesha kutekeleza majukumu yote yaliyopangwa kwa ufanisi mkubwa
katika Mkutano huu wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ulioanza  tarehe  10  Aprili  2012. Tumefanikiwa  kufanya hivyo  kutokana  na
maandalizi mazuri ya Mkutano, ushirikiano  miongoni  Mwetu na Waheshimiwa
Wabunge wote kujiandaa vizuri katika kuchangia hoja mbalimbali zilizopangwa.



Mheshimiwa Spika,

2.           Katika Mkutano huu, tumepata Waheshimiwa Wabunge Wapya Wawili
wote kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Napenda kutumia
nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa *Joshua Samwel Nassari* kwa kuchaguliwa
kuwa Mbunge Mpya wa Jimbo la Arumeru Mashariki. Vilevile, nampongeza
Mheshimiwa *Cecilia Daniel Paresso* kwa kuteuliwa kuwa Mbunge kupitia Viti
Maalum (CHADEMA). Kipekee kabisa nawapongeza Wananchi wa Arumeru Mashariki
kwa kutumia haki yao ya Kidemokrasia vizuri. Lakini kwa dhati kabisa,
nakipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kukubali Matokeo ya Uchaguzi Mdogo wa
Arumeru Mashariki. Kitendo hicho kinaonesha uungwana na ukomavu wa Kisiasa
na Demokrasia katika Nchi yetu. Huu ni mfano mzuri wa kuigwa na Vyama
vingine vyote vya Siasa Nchini.

3.           Kwa Waheshimiwa Wabunge wapya tunawatakia mafanikio na
tunawaahidi  ushirikiano wetu ndani ya Bunge na katika Kujenga Taifa letu.
Vilevile, napenda kutumia nafasi hii pia kuwapongeza Waheshimiwa Madiwani
wote waliopata Ushindi katika Chaguzi zilizofanyika katika Kata za
Vijibweni (Temeke), Kiwangwa (Bagamoyo), Kirumba (Mwanza), Logangabilili
(Bariadi), Chang’ombe (Dodoma), Kiwira (Rungwe),   Lizaboni   (Songea)   na Msambweni    (Tanga). Tunawatakia wote waliochaguliwa afya njema na
maisha mazuri ili muweze kuwatumikia Wananchi waliowachagua na Taifa kwa
ujumla.


Mheshimiwa Spika,
4.           Katika Mkutano huu wa Saba wa Bunge tulifanya Uchaguzi wa
Wawakilishi wa Nchi yetu katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Napenda nitumie nafasi hii kuwapongeza  wafuatao  kwa kuchaguliwa kuwa
Wabunge wa Bunge hilo, Mheshimiwa Makongoro Nyerere; Mheshimiwa Abdullah
Hassan Mwinyi; Mheshimiwa Nderakindo Kessy; Mheshimiwa Angela Kizigha;
Mheshimiwa Adam Kimbisa; Mheshimiwa Twaha Issa Taslima; Mheshimiwa Bernard
Murunya; Mheshimiwa Shy-Rose Bhanji; na Mheshimiwa Mariam Ussi Yahya.
Tunawapongeza
Wote! Tuna imani kubwa kwamba watatuwakilisha vyema katika Bunge la
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa maslahi ya Tanzania Kiuchumi na Kijamii
na Nchi zote kwa ujumla.


Mheshimiwa Spika,
5.           Tangu kuhitimishwa kwa Mkutano wa Sita wa Bunge lako Tukufu,
kumekuwepo na matukio mbalimbali ya kusikitisha, kusononesha, kuhuzunisha
na yenye Majonzi makubwa yaliyosababishwa na Misiba na Ajali ambazo
zimesababisha Vifo na kujeruhi Watanzania wenzetu wakiwemo Waheshimiwa
Wabunge.


6.           Napenda kupitia Bunge lako Tukufu, kutoa Salaam za Rambirambi
kwa Familia, Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Watanzania wote waliopoteza
Maisha. Tuwaombee Marehemu wote ili Mwenyezi Mungu azilaze Roho zao Mahali
Pema Peponi. Amina!


7.           Vilevile, nawapa pole Majeruhi wote walionusurika na kupata
Majeraha kutokana na Ajali mbalimbali zikiwemo ajali za Magari, Pikipiki,
Baiskeli na vifaa vingine vya barabarani na ile ya Shirika la Ndege Nchini
(ATCL) iliyotokea kule Kigoma.


Mheshimiwa Spika,
8.           Wote tunafahamu kwamba katika kipindi hiki tumekuwa na
Waheshimiwa Wabunge wenzetu ambao wamekuwa wakisumbuliwa na Maradhi
mbalimbali. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kusikia Maombi yetu. Wote
tumefarijika kutokana  na  kurejea kwa Mheshimiwa Dkt. Harrison George
Mwakyembe  ndani  ya  Bunge lako Tukufu akiwa na  Afya  Njema. Tunaamini  Afya
yake itazidi kuimarika katika siku zijazo. Vilevile, ni matumaini yetu
makubwa kwamba, wenzetu wengine akiwemo Mheshimiwa Profesa Mark James
Mwandosya, Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki  na  Waziri  wa Maji;
Mheshimiwa Dkt.John Pombe  Magufuli,  Mbunge  wa  Chato  na  Waziri wa
Ujenzi; pamoja na Mheshimiwa Highness Samson Kiwia, Mbunge wa Ilemela
ambao bado wako katika Matibabu watapata nafuu haraka itakayowawezesha
kuungana na sisi tena ndani ya Bunge letu Tukufu.


Mheshimiwa Spika,
9.           Mwisho, naungana na Watanzania wote kuipongeza Timu ya Simba
kwa kufikia Mzunguko wa Tatu wa Mashindano ya Kombe la Mabingwa Barani
Afrika. Sote tunawatakia Maandalizi mema ili wazidi kufanya vizuri katika
Mechi zijazo kwa kuwa ushindi wao ni ushindi wa Nchi yetu. Kwa Wachezaji na
Viongozi, wao nawaasa msibweteke na ushindi mlioupata, ila mnatakiwa
kuelewa kuwa safari bado ni ngumu na ndefu.

SHUGHULI ZA SERIKALI

 (a)              Maswali
Mheshimiwa Spika,
10.       Katika Mkutano huu wa Saba tunaouhitimisha leo, Jumla ya Maswali *
131* ya Msingi na mengine *315* ya Nyongeza kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge
yalipata majibu ya Serikali.  Vilevile, jumla ya Maswali *16* ya Msingi na *
9* ya Nyongeza kupitia utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Mheshimiwa
Waziri Mkuu yalijibiwa.

(b)         Miswada


Mheshimiwa Spika,

11.       Katika Mkutano huu Miswada ifuatayo ilisomwa na kujadiliwa:

(i)           Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za
Biashara wa Mwaka 2011 [*The Business Laws (Miscellaneous Amendments) Bill,
2011*];

(ii)          Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania wa
Mwaka 2011 (*The Tanzania Livestock Research Institute Bill, 2011*);

(iii)        Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii wa Mwaka 2012 [*The Social Security Laws (Amendments) Act,
2012*]; na

(iv)        Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka
2011 [*The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.2) Act, 2011*].

Vilevile, Muswada wa Sheria ya Haki za Wagunduzi wa Mbegu za Mimea wa Mwaka
2012 [*The Plant Breeder’s Rights Bill, 2012*] ulisomwa kwa mara ya kwanza.

(c)        Taarifa Mbalimbali

* *

*Mheshimiwa Spika,*

12.       Bunge lako Tukufu lilipata fursa ya kupokea na kujadili Taarifa
mbalimbali kama ifuatavyo:

(i)         Taarifa za Kamati za Bunge zinazosimamia Fedha za Umma; na

(ii)        Taarifa za Kamati za Bunge za Kisekta na zisizo za Kisekta.


Mheshimiwa Spika,
13.       Napenda nitumie nafasi hii kuwashukuru kwa dhati Waheshimiwa
Wabunge wote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika siku zote za Mkutano
huu zikiwemo kujadili na kupitisha Miswada niliyotaja hapo juu. Nawashukuru
pia kwa michango yenu wakati wa kujadili Taarifa mbalimbali
zilizowasilishwa hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika,
14.        Kipekee kabisa nitumie nafasi hii kuwapongeza  Wenyeviti
na  Wajumbe
 wa  Kamati  za Bunge  zilizowasilisha Taarifa mbalimbali mbele ya Bunge
lako Tukufu. Ni  dhahiri  kuwa  utaratibu  huu unatoa fursa kwa Waheshimiwa
Wabunge kupitia kwa kina masuala mbalimbali ya Kisekta na  kutoa ushauri
kwa Serikali. Aidha, utaratibu huu unatusaidia kuwepo kwa ‘*Checks  and
Balances*’ ndani ya Nchi yetu. Niwashukuru pia Wabunge wote kwa jinsi
walivyochangia   kwenye   mjadala  wa  kujadili   Taarifa  hizo.

Waheshimiwa Wabunge wameonesha hisia zao katika kujadili masuala yote haya
muhimu na mengineyo na hasa katika Mwenendo wa Matumizi ya Fedha za
Serikali kwenye Wizara, Taasisi za Umma, Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa. Nawashukuru sana kwa kujadili Taarifa zote kwa uwazi na hatimaye
kutoa mapendekezo kwa Serikali namna ya kushughulikia matatizo
yaliyojitokeza kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika,

15.       Mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge yako katika makundi muhimu
yafuatayo:

Kwanza:   Ni uimarishaji wa Uongozi na Utendaji katika Wizara, Taasisi za
Serikali, Mashirika ya Umma, Mikoa na Serikali za Mitaa;

Pili:  Ni usimamizi wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazohusu
masuala ya Mapato na Matumizi ya Fedha;


Tatu:  Ni uimarishaji wa hatua za Kupambana na Rushwa, Ubadhirifu
na Wizi wa Mali za Umma;

Nne:           Ni uendelezaji wa hatua za kubana matumizi yasiyo ya
lazima ndani ya Serikali na Vyombo vyake; na

Tano:         Ni ulinzi wa Rasilimali za Nchi kwa maslahi ya Taifa letu.



*Mheshimiwa Spika,*

16.       Siku  zote  Serikali imekuwa tayari kupokea ushauri wa Bunge lako
Tukufu na baada ya kusikiliza mjadala na mapendekezo ya Waheshimiwa
Wabunge, Serikali inaahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Ushauri na
Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hizo. Niwahakikishie Waheshimiwa
Wabunge kwamba Serikali itachukua hatua stahiki kuimarisha usimamizi na
utendaji ndani ya Wizara na Serikali za Mitaa na Vyombo vyake na
kuhakikisha Viongozi na Watendaji wake wanafanya kazi kwa umakini na
uadilifu zaidi.

Mheshimiwa Spika
17.       Katika  Hotuba  yangu  hii  ningependa  kuzungumzia kwa kifupi
mambo machache yanayohusu: Hatua zilizofikiwa katika Mchakato wa Kutekeleza
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba; Dhana ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii;
Matokeo ya Shule  za  Msingi na Kidato cha Nne Mwaka 2011; Maendeleo ya
Viwanda; Sensa ya Watu na Makazi; na mwisho Mpango wa Kutoa Kifuta Machozi
cha Mifugo.

HATUA   ZILIZOFIKIWA  KATIKA  MCHAKATO   WA KUTEKELEZA SHERIA YA
MABADILIKO YA KATIBA


Mheshimiwa Spika,

18.       Kama Waheshimiwa Wabunge watakavyokumbuka, katika Mkutano wa Sita
mwezi Februari 2012, Bunge lako Tukufu lilijadili na kupitisha Marekebisho
ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83). Napenda kuliarifu Bunge
lako Tukufu kuwa, mara baada ya Marekebisho hayo kupitishwa, Mheshimiwa
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete  kupitia Tangazo la Serikali Namba 66
la  tarehe
24 Februari 2012; alialika Vyama  vya  Siasa  vyenye Usajili wa Kudumu,
Jumuiya za Dini, Asasi za Kiraia, Taasisi na Makundi ya Watu wenye malengo
yanayofanana kuwasilisha kwake majina ya watu wanaoweza kuteuliwa kuwa
Wajumbe wa Tume itakayoratibu na kukusanya maoni ya Wananchi kuhusu
Mabadiliko ya Katiba.

* *

19.       Kwa mujibu wa Tangazo hilo, siku ya mwisho ya kuwasilisha
mapendekezo
 ya  majina ilikuwa tarehe 16 Machi  2012.  Hata  hivyo, kutokana na  umuhimu
 wa  zoezi hilo  na  ili  kutoa  fursa  zaidi   kwa   Wananchi  na  Taasisi
 au Makundi yaliyopo  Mikoani, Mheshimiwa Rais kupitia Tangazo la Serikali
Namba 101 la tarehe 16 Machi 2012 aliongeza  muda  huo hadi  tarehe 23
Machi 2012. Mapendekezo ya majina yaliyopokelewa yalikuwa mengi na hivyo
kumpa Mheshimiwa Rais uwanja mpana zaidi wa kufanya uteuzi.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

20.       Tarehe 6 Aprili 2012, Mheshimiwa Rais baada ya kushauriana na
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliteua
Wajumbe 32 wa Tume itakayoratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu
Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na Wajumbe hao, Mheshimiwa Rais aliteua Katibu
na Naibu Katibu wa Tume hiyo. Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe,
Katibu na Naibu Katibu wa Tume waliapishwa na Mheshimiwa Rais tarehe 13
Aprili 2012. Kutokana na *umuhimu wa Tume hii katika historia ya Nchi yetu*,
naomba niwataje Wajumbe wote wa Tume walioteuliwa:

1.   Mheshimiwa  Jaji  Joseph  Sinde  WARIOBA – Mwenyekiti;

2.   Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino RAMADHANI  - Makamu Mwenyekiti;

3.   Mheshimiwa Dkt. Salim Ahmed SALIM – Mjumbe;

4.   Ndugu Abubakar Mohammed ALI – Mjumbe;

5.   Ndugu Ally Abdullah Ally SALEH – Mjumbe;

6.   Mheshimiwa Al-Shaymaa J. KWEGYIR (Mb.) – Mjumbe;

7.   Ndugu Awadh Ali SAID – Mjumbe;

8.   Dkt. Edmund Adrian Sengondo MVUNGI – Mjumbe;

9.   Ndugu Esther P. MKWIZU – Mjumbe;

10.       Ndugu Fatma Said ALI – Mjumbe;

11.       Ndugu Humphrey POLEPOLE – Mjumbe;

12.       Ndugu Jesca Sydney MKUCHU – Mjumbe;

13.       Ndugu John J. NKOLO – Mjumbe;

14.       Ndugu Joseph BUTIKU – Mjumbe;

15.       Ndugu Kibibi Mwinyi HASSAN – Mjumbe;

16.       Ndugu Maria Malingumu KASHONDA – Mjumbe;

17.       Ndugu Muhammed Yussuf MSHAMBA – Mjumbe;

18.       Ndugu Mwantumu Jasmine MALALE – Mjumbe;

19.       Prof. Mwesiga L. BAREGU – Mjumbe;

20.       Ndugu Nassor Khamis MOHAMMED – Mjumbe;

21.       Ndugu Omar Sheha MUSSA – Mjumbe;

22.       Prof. Palamagamba J. KABUDI – Mjumbe;

23.       Mheshimiwa Raya Suleiman HAMAD – Mjumbe;

24.       Ndugu Richard Shadrack LYIMO – Mjumbe;

25.       Ndugu Riziki Shahari MNGWALI – Mjumbe;

26.       Alhaj Said EL- MAAMRY – Mjumbe;

27.       Ndugu Salama Kombo AHMED – Mjumbe;

28.       Ndugu Salma MAOULIDI – Mjumbe;

29.       Ndugu Simai Mohamed SAID – Mjumbe;

30.       Ndugu Suleiman Omar ALI – Mjumbe;

31.       Ndugu Ussi Khamis HAJI – Mjumbe;

32.       Ndugu Yahya MSULWA – Mjumbe;

33.       Ndugu Assaa Ahmad RASHID – Katibu; na

34.       Ndugu Casmir Sumba KYUKI – Naibu Katibu.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

21.       Kwa namna ya pekee, nampongeza  Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde
Warioba, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu kwa kuteuliwa kuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Mheshimiwa Augustino
Ramadhani, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania kwa kuteuliwa kuwa Makamu
Mwenyekiti. Vilevile, napenda kuwapongeza Wajumbe wote, wakiwemo Katibu na
Naibu Katibu kwa kuteuliwa kuunda Tume hii. Ni matumaini yangu na ya
Watanzania wote kwa ujumla kuwa, Wajumbe wa Tume watatumia ujuzi, maarifa
na uzoefu wao katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu waliyopewa kwa
mujibu wa Sheria na kwa ufanisi mkubwa.



*Serikali  ilivyojipanga  (Maandalizi ya Tume)*

* *

*Mheshimiwa Spika,*

22.       Wakati wa hafla ya kuwaapisha Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti,
Wajumbe, Katibu na Naibu Katibu wa Tume, Mheshimiwa Rais aliihakikishia
Tume kuwa Serikali itaipa kila aina  ya  ushirikiano  ili  itekeleze
majukumu yake kwa ufanisi. Kwa niaba ya Serikali kupitia Bunge lako Tukufu,
naomba kwa mara nyingine tena nikuhakikishie kuwa Serikali imejipanga kwa
kuweka mazingira yatakayoiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kama Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83) inavyoelekeza. Hivi sasa, Serikali
inakamilisha maandalizi muhimu kuiwezesha Tume kuanza kazi tarehe 1 Mei
2012 kama ilivyopangwa.



*Mheshimiwa Spika,*

23.       Naomba  kutumia fursa hii kuwaomba Wananchi wote kuipa Tume
ushirikiano wa kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Vilevile, napenda kuwasihi Wananchi wajitokeze  kwa wingi katika Mikutano
itakayoitishwa na  Tume na watoe maoni yao kwa uhuru na utulivu bila
vikwazo vyovyote. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Watanzania wote
wanashiriki kikamilifu bila ubaguzi wowote katika mchakato huo wa kuandika
Katiba Mpya ili Nchi yetu iweze kupata Katiba itakayokidhi mahitaji ya
Karne hii na miaka mingi ijayo.



*Mheshimiwa Spika,*

24.       Napenda kusisitiza maagizo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa siku ya
kuwaapisha Wajumbe wa Tume kwamba Mchakato huu wa Mabadiliko ya Katiba siyo
mchakato wa kuwepo au kutokuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu
ni mchakato unaolenga kukubaliana namna bora ya kuendesha Nchi kwa
kuzingatia uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uwepo wa Haki za
Binadamu na Misingi ya Utawala Bora, uwepo wa Mihimili Mitatu ya Dola yaani
Bunge, Mahakama na Serikali na namna nzuri ya kuboresha utendaji kazi wa
Mihimili hiyo. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge kuwaelimisha Wananchi juu ya
kuzingatia mambo haya ya msingi wakati wa kutoa maoni yao.



*MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII*

* *

*Mheshimiwa Spika, *

25.       Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa Bunge lako Tukufu
lilipitisha Sheria Namba 8 ya Mwaka 2008 ya kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi
na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii.* *Umuhimu wa Hifadhi ya Jamii
Nchini unatambuliwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika Ibara ya *11(1)* inayosomeka, nanukuu:

* *

*“Mamlaka ya Nchi itaweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha
utekelezaji wa Haki ya Mtu Kufanya Kazi, Haki ya kujipatia Elimu na Haki ya
kupata Msaada kutoka kwa Jamii wakati wa Uzee, Maradhi au hali ya Ulemavu,
na katika hali nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi.”* Mwisho wa kunukuu.

* *

Hivyo, Hifadhi ya Jamii ni nguzo muhimu katika kutekeleza dhana ya Utawala
Bora katika Jamii na kuchochea ukuaji wa Uchumi.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

26.       Lengo Kuu la kuwa na Mipango ya Hifadhi ya Jamii ni kuondoa
Umaskini wakati wa Uzee na kutoa  kinga ya Kiuchumi na Kijamii pale
panapotokea matukio na majanga mbalimbali yanayosababisha kupungua kwa
kipato. Hivi sasa kuna Mifuko Sita ya Hifadhi ya Jamii ambayo inatoa Mafao
ya muda mfupi na muda mrefu kulingana na taratibu zilizopo katika Sheria za
Mifuko husika. Mifuko hiyo ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF);
Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma (PPF); Mfuko wa Pensheni kwa
Watumishi wa Umma (PSPF); Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali za
Mitaa (LAPF); Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa Serikali (EGPF); na Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).* *



*Mheshimiwa Spika,*

27.       Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, ni Asilimia *5.9* tu ya nguvu
kazi ya Watanzania waliopo katika Sekta rasmi ndiyo wanaopata huduma ya
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Takwimu hizi ni kielelezo tosha kuonesha
changamoto inayoikabili Sekta ya Hifadhi ya Jamii katika kuhakikisha
Watanzania wengi wanajiunga na kunufaika na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Aidha, changamoto hii si kwa Wananchi wanaojishughulisha katika Sekta isiyo
rasmi tu bali hata kwa wale waliopo katika Sekta rasmi ambao kwa namna moja
au nyingine hawajajiandikisha katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

28.       Changamoto nyingine zinazokabili Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii
ni pamoja na kupishana sana kwa Mafao kati ya Mfuko mmoja na mwingine japo
kiwango cha kuchangia kinalingana yaani Asilimia 20 ya Mshahara wa
Mtumishi. Lipo pia tatizo la Pensheni isiyoendana na gharama za maisha,
gharama kubwa za uendeshaji wa Mifuko, huduma hafifu kwa Wanachama wa
Mifuko, Kukosekana kwa Kanuni za Uwekezaji zinazolingana pamoja na Idadi
kubwa ya Wananchi kutoelewa umuhimu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

29.       Katika kukabiliana na baadhi ya changamoto zilizoko kwenye Sekta
hii ya Hifadhi ya Jamii, Serikali imechukua hatua mbalimbali. Moja ya hatua
hizo ni kuanzisha na kutekeleza Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka
2003 ambayo ni Dira ya shughuli zote za Hifadhi ya Jamii hapa Nchini.
Vilevile, mwaka 2008 Serikali ilianzisha Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii.
Jukumu kubwa la Mamlaka hii ni kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii ikiwamo
Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii Nchini. Ni matumaini yangu kuwa Mamlaka ya
Hifadhi ya Jamii itatusaidia kuzifanyia kazi Changamoto nilizozitaja hapo
juu na nyingine ili kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wanajiunga na kupata
Hifadhi ya Jamii.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

30.       Ili kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya
Hifadhi ya Jamii, Serikali ilileta katika Kikao hiki cha Bunge Muswada wa
Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Nichukue fursa hii
kulipongeza Bunge lako Tukufu kwa kupitisha Muswada huu. Muswada huo
uliopitishwa na Bunge unalenga kuwianisha Sheria za Mifuko na Sheria ya
Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii. Lengo ni kuipa Mamlaka uwezo zaidi wa
kutekeleza majukumu yake; na kuiwezesha Mifuko kutoa huduma bora kwa
Wanachama wake. Muswada huu unaiwezesha pia Mifuko kutambua uwezo wa
Mamlaka kuleta mageuzi kwenye Sekta kwa kutoa Miongozo mbalimbali.

*Mheshimiwa Spika,*

33.       Nachukua fursa hii kuwakumbusha Waajiri wanaokiuka Sheria kwa
kuwachagulia Wafanyakazi wao wapya, Mifuko ya kujiunga nayo kinyume na
matakwa ya Wafanyakazi hao waache kufanya hivyo. Kila Mwajiri anatakiwa
kuweka mazingira yatakayomwezesha Mfanyakazi kuchagua Mfuko anaoupenda.
Mazingira hayo ni pamoja na kuialika Mifuko yote kutoa maelezo kuhusu Mafao
na huduma zao na kuwapa fursa Wafanyakazi kufanya maamuzi ya kujiunga na
Mfuko waupendao. Ni matumaini yangu kuwa Mamlaka itaweka Kanuni
zitakazowezesha Mifuko kuandikisha Wanachama kwa utaratibu unaokubalika na
unaomlinda Mwanachama.



34.       Kwa upande wa Uwekezaji, Mamlaka imekamilisha tathmini ambayo
itawezesha kutengeneza Miongozo kwa Mifuko kuwekeza katika Vitega Uchumi
mbalimbali. Vilevile, *Mamlaka itaweka mkakati kabambe wa kuelimisha Umma
ili Wananchi wengi zaidi waweze kujiunga na Mifuko hii kwa kuwa sasa
wanaruhusiwa kujiunga na Mifuko hiyo bila kujali kama wako Sekta Rasmi au
isiyo Rasmi*. Napenda pia kutumia fursa hii kutoa wito kwa Waheshimiwa
Wabunge na Wananchi wote kutoa ushirikiano stahiki kwa Mamlaka ili  kwa
kushirikiana na Wadau mbalimbali tuboreshe, tuimarishe na kuwa na Sekta ya
Hifadhi ya Jamii iliyo endelevu.

* *

*MATOKEO YA MTIHANI WA KUMALIZA ELIMU YA MSINGI MWAKA 2011*

* *

*Mheshimiwa Spika,*

35.       Mwaka 2011 Wanafunzi *983,545* wa Darasa la Saba walifanya
mtihani wa Taifa. Kati yao Wanafunzi *567,567,* *sawa na Asilimia 58.28 *ya
waliofanya mtihani walifaulu. Kiwango cha Ufaulu cha mwaka 2011,
ikilinganishwa na kile cha mwaka 2010 unaonesha kupanda kwa Asilimia
*4.76*kutoka
*Asilimia 53.52 ya mwaka 2010 hadi 58.28 mwaka 2011*.

* *

*Mheshimiwa Spika, *

36.       Tathmini inaonesha Ufaulu kimasomo umeongezeka kwa *masomo ya
Hisabati, Kiingereza na Sayansi*.

i)             *Kiwango cha Ufaulu kwa Somo la Hisabati* kilikuwa *Asilimia
39.4 mwaka 2011* ikilinganishwa na Asilimia *24.7 mwaka 2010*;



ii)            *Kiwango cha Ufaulu kwa Somo la Kiingereza* kilikuwa
Asilimia *46.7 mwaka 2011* ikilinganishwa na Asilimia *36.5 mwaka 2010*; na



iii)          *Kiwango cha Ufaulu kwa Somo la Sayansi* kilikuwa Asilimia
61.3 mwaka 2011 ikilinganishwa na Asilimia 56.1 mwaka 2010.



37.       Taarifa zinaonesha kuwa kiwango cha ufaulu kwa masomo ya
Kiswahili na Maarifa ya Jamii kilishuka kwa mwaka 2011 ikilinganishwa na
mwaka 2010. Kwa mfano, Ufaulu kwa Somo la Kiswahili ulikuwa Asilimia 68.6
mwaka 2011 ikilinganishwa na Asilimia 71.0 mwaka 2010; na kiwango cha
ufaulu kwa Somo la Maarifa ya Jamii kilikuwa Asilimia 54.8 mwaka 2011
ikilingnishwa na Asilimia 68.0 mwaka 2010.

* *

*Mheshimiwa Spika, *

38.        Ni kweli kwamba, kwa muda mrefu tumekuwa na matatizo ya ufaulu
katika masomo ya Sayansi Nchini, lakini matokeo ya mwaka 2011 yanaonesha
kuwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kukuza masomo hayo zimeanza
kuzaa matunda. Napenda kuwapongeza Wanafunzi, Wazazi, Walezi, Walimu na
Watendaji wote walioshiriki katika kuleta mafanikio hayo.



*Uchaguzi wa Wanafunzi kuingia Kidato cha Kwanza mwaka 2012*

* *

*Mheshimiwa Spika,*

39.       Katika Uchaguzi wa kuingia Kidato cha Kwanza mwaka 2012, jumla ya
Wanafunzi *515,187,* sawa na Asilimia 90.1 ya Wanafunzi waliofaulu
walichaguliwa kuingia Kidato cha Kwanza katika Shule za Sekondari za
Serikali. Idadi hii iliongezeka kwa Asilimia 12.49 kutoka Wanafunzi *456,350
* mwaka 2010. *Taarifa nilizopokea kutoka Mikoa 12 ya Arusha, Dar es
Salaam, Dodoma, Iringa, Mara, Morogoro, Mwanza,  Lindi,  Kilimanjaro,  Pwani,
 Ruvuma  na  Tanga, ***

*zinaonesha kuwa Wanafunzi wote waliofaulu wamejiunga na Kidato cha Kwanza.
Nitumie nafasi hii kuipongeza Mikoa hii kwa kuhakikisha kuwa hakuna
Wanafuzi waliofaulu na kushindwa kujiunga na Sekondari. ***



40.       Hata hivyo, sehemu kubwa ya Mikoa niliyoitaja inaonesha kuwepo
kwa uhaba mkubwa wa Vyumba vya Madarasa na Madawati. Naiagiza Mikoa yote
kuhakikisha mapungufu haya yanashughulikiwa katika Bajeti ya mwaka
2012/2013. Aidha, Mikoa iwe na Mipango endelevu ya kujenga Vyumba vya
Madarasa na kutengeneza Madawati badala ya kusubiri matokeo ya Mtihani na
kuchaguliwa kwa Wanafunzi ndipo ianze kuweka mikakati.

* *

*Matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2011*

* *

*Mheshimiwa Spika,*

41.       Matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2011 yanaonesha kuwa Wanafunzi
*181,880,* sawa na Asilimia *53.6 *ya Wanafunzi *339,330* waliofanya
Mtihani walifaulu. Kiwango hicho kimeongezeka kutoka Wanafunzi
*177,011*waliofaulu mwaka 2010 ikiwa ni sawa na Asilimia
*50.4* ya Wanafunzi *351,214* waliofanya Mtihani.

* *

*Mheshimiwa Spika, *

42.       Tangu mwaka 2008, Asilimia ya Wanafunzi wanaofeli Mitihani ya
Kidato cha Nne imekuwa ikiongezeka na kufikia Asilimia *16.3,* mwaka 2009
Asilimia *27.5,* mwaka 2010 Asilimia *49.6 *na kushuka tena hadi Asilimia *
43.3,* mwaka 2011. Sababu za kushuka kwa ufaulu huo ni pamoja na upungufu
wa Walimu, Vifaa vya Kufundishia na kujifunzia na kuimarika kwa udhibiti wa
uvujaji wa mitihani ya Kidato cha Nne. Vilevile, inaelezwa na Wanataaluma
na Watafiti kwamba kuondolewa kwa Mtihani wa Kidato cha Pili kumechangia
sana matokeo mabaya ya Kidato cha Nne.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

43.       Kutokana na hali ya kuongezeka kwa idadi ya Wanafunzi
wanaofeli  Mtihani
wa Kidato cha Nne, Serikali imechukua hatua kadhaa zikiwemo za kuongeza na
kuimarisha usimamizi wa matumizi ya *‘capitation grant’* ili kupunguza
tatizo la upungufu  wa  Vifaa  vya  Kufundishia  na  Kujifunzia  Shuleni;
Kutekeleza mikakati ya kuongeza idadi na ubora wa Walimu; na kujenga uwezo
wa Wakuu wa Shule kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wa kila siku.



44.       Ni matarajio yangu kwamba tukiyafanya haya, tutaweza kufikia Azma
yetu ya kuwa na matokeo mazuri katika siku zijazo. Niwaombe Wadau wote wa
Elimu wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Viongozi, Walimu, Wazazi, Walezi na
Wanafunzi kila mmoja atimize wajibu wake katika utoaji wa Elimu kuanzia,
Nyumbani, Shuleni na Vyuoni ili tuweze kuinua Kiwango cha Ubora wa Elimu
Nchini.

* *

*MAENDELEO YA VIWANDA   *

* *

*Mheshimiwa Spika,*

45.       Tarehe 16 hadi 23 Septemba 2011 nilifanya ziara Mkoa wa Mara na
kutembelea Kiwanda cha Nguo cha Musoma Textile (MUTEX). Tarehe 2 hadi 4
Desemba 2011 nilifanya ziara nyingine fupi Mkoa wa Mwanza na kutembelea
Kiwanda cha kutengeneza Nguo cha Mwanza Textile (MWATEX). Kwa kweli
nilikuta Viwanda hivyo vinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za
kukosekana kwa umeme wa uhakika, Wataalam na teknolojia ya kisasa.
Nilielezwa kuwa changamoto hizo zinavikabili Viwanda vingi vya Nguo Nchini.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

46.       Sote hapa tunafahamu kuwa maendeleo makubwa na ya kasi kwenye
Nchi mbalimbali Ulimwenguni yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na maendeleo ya
Viwanda vya Nguo na Mavazi. Viwanda hivi hutoa Soko la uhakika kwa zao la
Pamba linalolimwa hapa Nchini; huajiri kiasi kikubwa cha Wafanyakazi na
hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza tatizo la ajira na umaskini
hasa miongoni mwa Vijana. Pia, huchangia Mapato kwa Serikali na Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii. Kutofanya vizuri kwa Viwanda hivi kunaikosesha Serikali
na Wananchi Mapato na kuongeza tatizo la ajira Nchini. Niliona kuna umuhimu
wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizo ndani ya uwezo wa Serikali.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

47.        Tarehe 23 Machi 2012, niliitisha Mkutano wa Wadau wa Sekta Ndogo
ya Viwanda vya Mavazi na Nguo ili kwa pamoja tuweze kuainisha changamoto
zinazoikabili Sekta hiyo na kupata mapendekezo ya namna ya kukabiliana na
changamoto hizo. Kufuatia Mkutano huo, iliundwa Timu ya Wataalam ili iweze
kuangalia changamoto hizo kwa kina na kutoa mapendekezo ya hatua za
kuchukuliwa na Serikali pamoja na Wadau wote ili kukabiliana na changamoto
hizo. Timu hiyo ilipewa mwezi mmoja na wakati wowote kuanzia sasa
itawasilisha taarifa yake Serikalini.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

48.       Tarehe 15 Aprili 2012, nilipata fursa ya kutembelea viwanda
vya *Sunflag
(Tanzania) Ltd, *Kiwanda cha *A to Z na Minjingu Mines and Fertilizer
Limited* vyote vya Mkoani Arusha. Katika Viwanda vya Nguo vya *Sunflag* na *A
to Z* nilifarijika kuona idadi kubwa ya Watumishi walioajiriwa na kwamba
zaidi ya Asilimia 80 walikuwa ni akina Mama. Nawapongeza Viongozi wa
Viwanda hivi kwa jitihada ambazo wanazifanya kuendeleza uzalishaji na hivyo
kuchangia Mapato kwa Serikali na Ajira kwa Wananchi.

* *

*Mheshimiwa Spika, *

49.       Kiwanda cha *Sunflag* ni Kiwanda pekee Nchini kinachozalisha  nguo
 kuanzia  hatua  ya  Pamba  kutoka kwa Mkulima  hadi  nguo  za kuvaa. *
Sunflag* wamekuwa ni Soko zuri na la uhakika  la Pamba  ya  Wakulima.
Nawapongeza
kwa uamuzi wao huo ambao una faida kubwa kwa Wakulima wa Pamba. Viongozi wa
Viwanda hivyo walinieleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Serikali itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuimarisha Viwanda
vinavyotumia pamba ya Tanzania na kuweka mazingira yatakayoendelea kuvutia
uwekezaji katika Sekta hii ya Nguo na Mavazi. Baada ya kupata taarifa ya
Timu niliyoitaja hapo awali, Serikali itachukua hatua zitakazoondoa
changamoto zinazovikabili Viwanda vya Nguo na Mavazi Nchini.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

50.       Katika Kiwanda cha *Minjingu Mines and Fertilizer
Limited*nilielezwa kuwa wamefanikiwa kuzalisha mbolea ya
*Minjingu Mazao *ambayo ni bora kuliko Mbolea aina ya DAP kwa kuwa ina
virutubisho vya Nitrogen, Phosphorous, Sulphur, Calcium na rutuba kama
Magnesium, Zinc na Boroni. Aidha, Minjingu Mazao ina bei ndogo kuliko DAP.
Kiwanda kwa sasa kina akiba (*stock*) ya Tani 5,600 ya Phosphate na Tani
7,100 ya *Minjingu Mazao*. Nilielezwa kuwa matumizi ya Mbolea ya Minjingu
Nchini yamekuwa yakipungua mwaka hadi mwaka kutokana na matatizo mbalimbali
ikiwemo hujuma inayofanywa   kwenye   Mfumo   wa   Ruzuku   za   Pembejeo.
Napenda kuhimiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ione namna ya
kukikwamua Kiwanda cha Minjingu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu –
TAMISEMI ili kuongeza matumizi ya mbolea za Minjingu.



*SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012*



*Mheshimiwa Spika, *

51.       Itakumbukwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wakati akitoa hotuba yake ya kumaliza  mwaka  2011 alitangaza  rasmi
 dhamira  ya Serikali kufanya Sensa ya Watu na Makazi ambayo imepangwa
  kufanyika
 Nchini  kote  tarehe  26  Agosti  2012. Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa
Sensa ya Watu na Makazi pamoja na Vitambulisho vya Taifa ni mojawapo ya
vipaumbele vya Taifa kwa mwaka huu wa 2012. Tarehe 12 Aprili 2012,
Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kuhudhuria Semina kuhusu Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2012. Katika Semina hiyo yalitolewa maelezo ya kina
kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi. Nina
imani kuwa baada ya Semina hiyo ya tarehe 12 Aprili 2012, hivi sasa
Waheshimiwa Wabunge wana uelewa mpana kuhusu umuhimu wa taarifa zitokanazo
na Sensa na kwamba watatumia uelewa huo kuwaelimisha Wananchi umuhimu wa
kujiandikisha.



*Mheshimiwa Spika, *

52.       Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 madhumuni yake makubwa ni
kupata takwimu kuhusiana na idadi ya Watu na kukusanya Taarifa za kina za
Kiuchumi, Kijamii na Maelezo ya Makazi. Taarifa hizi hutumiwa na Serikali
na Taasisi nyingine kwa shughuli mbalimbali za Mipango na maendeleo.
Serikali pia hutumia Takwimu zitokanazo na Sensa katika kutunga Sera,
kufanya maamuzi juu ya Utawala wa Umma kwa kuzingatia mahitaji halisi na
vigezo vingine kama vile umri, jinsia na vinginevyo.



*Mheshiwiwa Spika*,

53.       Sensa  ya  mwaka  2012  ina  umuhimu  wa  kipekee  kwa kuwa
taarifa zitakazokusanywa zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 kwa Tanzania Bara na mwaka 2020
kwa Tanzania Zanzibar. Vilevile, taarifa hizo zitatumika kutathmini Mkakati
wa Kukuza na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA) na Mkakati wa
Kupunguza Umaskini Tanzania Zanzibar (MKUZA). Takwimu hizo zitatumika pia
kutathmini utekelezaji wa Malengo ya Milenia ifikapo mwaka 2015; Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2011/2012 – 2015/2016 pamoja na kubuni
mikakati ya utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Miaka 15 wa Utekelezaji wa
Dira ya Taifa ya Maendeleo hadi mwaka 2025.



*Mheshimiwa Spika, *

54.       Pamoja na maandalizi yanayoendelea hivi sasa, mafanikio ya Sensa
yatategemea sana ushiriki wa Umma na Wadau wengine. Sisi Waheshimiwa
Wabunge ni Wajumbe wa Kamati za Sensa za Wilaya na Halmashauri zetu na moja
ya majukumu ya Kamati hizo ni kuhamasisha na kuelimisha Umma kuhusu umuhimu
wa Sensa ya Watu na Makazi ili kuhakikisha kuwa kila mtu atakayelala Nchini
*Usiku wa Kuamkia* siku ya Sensa, yaani tarehe 25 Agosti 2012 *kuamkia
tarehe 26 Agosti 2012*, anahesabiwa, na kwamba anahesabiwa mara moja tu.



*Mheshimiwa Spika, *

55.        Zoezi* *hili ni la Kitaifa hivyo linahitaji uhamasishaji na
ushirikishwaji  wa  Wananchi  wote.  Natoa wito kwa Wananchi  wote  kushiriki
 kikamilifu katika  zoezi  la  Sensa ya Watu na Makazi na kutoa ushirikiano
mkubwa kwa Makarani wa Sensa watakaofanya kazi ya Kuhesabu Watu siku ya
tarehe 26 Agosti 2012. Vilevile, naomba nitumie fursa hii kuwaomba
Waheshimiwa Wabunge washirikiane na Viongozi  wengine  kusimamia  utekelezaji
wa shughuli zote za Sensa katika Wilaya na Halmashauri kwa kuhakikisha kuwa
elimu kwa Wananchi inatolewa. Nawaomba pia Waheshimiwa Wabunge kutumia
nafasi zao kama Wawakilishi  wa Wananchi kuhamasisha na kuelimisha Umma
kuhusu umuhimu wa kushirikiana na Makarani wa Sensa wakati wa kipindi cha
kuhesabu Watu kwa kutoa Takwimu sahihi na hivyo kupata taarifa sahihi kwa
ajili ya Mipango endelevu ya maendeleo. Kaulimbiu yetu kila wakati iwe
ni *Sensa
kwa Maendeleo ya Taifa: Jiandae Kuhesabiwa. *Napenda kuwatakia mafanikio
mema katika kazi hii muhimu kwa Taifa letu.



*MPANGO WA KUTOA KIFUTA MACHOZI CHA MIFUGO *

* *

*Mheshimiwa Spika, *

56.        Mwaka 2008/2009, Mikoa ya Kaskazini hasa Mikoa ya Arusha na
Manyara ilikumbwa na ukame mkubwa ambao ulisababisha Vifo kwa Mifugo.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo,  Mheshimiwa   Rais  aliahidi   kutoa
Kifuta  Machozi  kwa



kuwapatia Mifugo ya Mbegu Wafugaji waliopoteza Mifugo yao yote katika
Wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro. Katika kutekeleza Ahadi ya Rais,
Serikali iliunda Kikosi Kazi ambacho kilibaini kuwepo kwa Vifo vya Ng’ombe *
403,839;* Mbuzi *211,201* na Kondoo *121,118 *katika Wilaya hizo. Vilevile,
Kikosi Kazi kilibaini kwamba jumla ya Kaya *6,127* katika Wilaya hizo
zilipoteza Mifugo kutokana na ukame. Wilaya ya Longido ilikuwa na jumla ya
Kaya *2,852;* Monduli Kaya *1,484* na Ngorongoro Kaya
*1,791*zilizoathirika na ukame ulioambatana na Vifo na Mifugo.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

57.       Katika mwaka 2011/2012, Serikali ilitoa Tamko Bungeni kuhusu
kutekeleza ahadi ya kutoa Kifuta Machozi kama mbegu (*seed stock*) kwa Kaya
zilizopoteza Mifugo yote ili ziweze kurudi katika hali yao ya awali kama
Wafugaji. Aidha, Mradi maalum ulianzishwa kwa ajili ya kununua Mifugo
(Ng’ombe na Mbuzi) kwa ajili ya Wilaya husika. Ununuzi wa Mifugo hiyo
utafanyika katika ngazi ya Halmashauri za Wilaya kwa kuzingatia Sheria ya
Manunuzi Na. 21 ya mwaka 2004.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

58.       Kufuatia kuundwa kwa Kamati mbalimbali (Mkoa, Halmashauri, Kata
na Vijiji za kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Kusambaza Mifugo ya Kifuta
Machozi, Halmashauri za Wilaya zilielekezwa kutangaza zabuni za kuwapata
wanunuzi wa Mifugo ndani ya maeneo ya Wilaya husika katika kipindi cha Siku
Tisini (90). Utekelezaji wa Zoezi hili utafanyika kwa Awamu kulingana na
upatikanaji wa fedha. Aidha, Awamu ya Kwanza itaanza kwa kununua Ng’ombe
500 kwa kila Wilaya. Lengo ni kukamilisha zoezi hili kabla ya Kiangazi
kuanza.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

59.       Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Uzinduzi wa Mpango wa
kutoa Kifuta Machozi ulifanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete tarehe 19 Februari 2012 katika Wilaya ya Longido ambapo Serikali
ilitumia Shilingi Milioni *213* kwa kununua na kusambaza Ng’ombe 500.



60.        Aidha, ununuzi wa Mifugo kwa ajili ya Wilaya za Monduli na
Ngorongoro utakamilika mara Serikali itakapokamilisha taratibu za kutuma
fedha kwa Halmashauri za Wilaya hizo. Kiasi cha Shilingi Milioni *206
*zimetengwa
kwa ajili ya Wilaya ya Monduli na Shilingi Milioni *218* kwa ajili ya
Wilaya ya Ngorongoro ili kuwezesha ununuzi wa Ng’ombe 500 kwa kila Wilaya.



61.        Matumaini yangu ni kuwa zoezi la kutoa Kifuta Machozi kwa
Wananchi wa Wilaya za Monduli na Ngorongoro litakamilika katika muda mfupi
ujao kwa kuwa Mifugo hiyo ipo tayari kwa Wazabuni. Kinachosubiriwa ni
malipo ya fedha. Natoa wito kwa Wafugaji na Wananchi walioathirika na ukame
ambao wanasubiri Awamu ya Pili kuwa na subira wakati Serikali inatafuta
fedha za kutekeleza Mpango huu.



*HITIMISHO*

* *

*Mheshimiwa Spika, *

62.       Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda kusisitiza maeneo
muhimu yafuatayo:



*Kwanza*:  Tumeanza  Mchakato wa Utekelezaji  wa  Sheria ya  Mabadiliko ya
Katiba. Mchakato ambao ni Msingi wa Utawala Bora. Natoa wito kwamba,
Tuwaelimishe Wananchi kuhusu Mambo ya Msingi wakati wa kuchangia Maoni, na
kwamba Mabadiliko ya Katiba siyo Mchakato wa kuwepo au kutokuwepo kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



*Pili:        *Tunayo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo tukiitumia vizuri,
ni kinga na kichocheo muhimu cha Kuondoa Umaskini na Kukuza Uchumi.
Tushirikiane na Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii kuwaelimisha Wananchi kuhusu
umuhimu wa kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa faida yao, kwani hivi
sasa haijalishi kama uko kwenye Sekta Rasmi au Isiyo Rasmi.



*Tatu:     *Bado tunazo changamoto nyingi katika Sekta ya Elimu, hasa
katika Miundombinu na Ubora wa Elimu kwa ujumla. Tushirikiane katika
kutekeleza Mikakati ya kutuwezesha kuwa na Elimu Bora kwa Watoto wetu.
Tuwajengee utamaduni wa kujiamini na kushiriki kikamilifu katika kuboresha
Miundombinu muhimu kuanzia Shule za Msingi, Sekondari hadi Vyuo.



*Nne:      *Kuwepo kwa Viwanda Nchini ni muhimu kwa maendeleo yetu na
Uchumi wa Nchi. Pamoja na changamoto zilizopo ni vizuri kuweka umuhimu wa
kutumia bidhaa zinazozalishwa na Viwanda vyetu.



*Tano:    *Tarehe 26 Agosti 2012 itakuwa ni Siku ya Sensa ya Watu na Makazi
Nchini. Tuwahamasishe Wananchi waelewe umuhimu wa kuhesabiwa siku hiyo na
utaratibu utakaotumika ikiwa ni pamoja na kila Mtu kuhakikisha anahesabiwa
na kwamba anahesabiwa mara moja tu.



*Mheshimiwa Spika,*

63.       Tunapohitimisha Mkutano huu wa Saba, pamoja na kumshukuru
Mwenyezi Mungu tunao wajibu wa kiungwana kuwashukuru pia wote walioshiriki
katika kutoa huduma muhimu katika kufanikisha Mkutano huu. Nitumie fursa
hii kutoa  shukrani  za  dhati kwako wewe Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza
vizuri na hatimaye kukamilisha Vikao vyote kama ilivyopangwa. Vilevile,
namshukuru Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri.
Niruhusu nimshukuru Dkt. Thomas Kashilillah, Katibu wa Bunge na Wasaidizi
wake kwa kutuwezesha kufanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa. Niwashukuru pia
Wataalam wote ambao mchango wao kwetu umekuwa ni muhimu sana. Niwashukuru
Askari, Madereva, Wanahabari kwa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha
Mkutano huu.* *

* *

*Mheshimiwa Spika,*

64.       Leo tunapohitimisha Mkutano huu wa Saba, tunapata fursa ya
kujiandaa kwa ajili ya Mkutano wa Nane ambao ni Mahsusi kwa ajili ya Bajeti
ya Mwaka 2012/2013. Napenda kuwatakia maandalizi  mema  kwa  ajili ya
Bajeti ya Serikali. Ni dhahiri kwamba bado tuna changamoto nyingi. Nawasihi
kila mmoja wetu kujiwekea malengo ya kutimiza wajibu wake katika kufikia
yale yote tunayoyatarajia kuyafanya kwa ajili ya Maendeleo ya Nchi yetu.
Nimalizie kwa kuwatakia nyote safari njema ya kurejea katika maeneo yenu ya
kazi.

* *

*Mheshimiwa Spika,*

65.       Baada ya kusema haya, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu
liahirishwe hadi tarehe *12 Juni 2012* Saa *3:00* *Asubuhi*, litakapokutana
kwenye Ukumbi huu hapa Mjini Dodoma kujadili Bajeti ya Serikali.



66.       *Mheshimiwa Spika, *naomba kutoa hoja.

*

COMMENTS

Name

Anga,11,Arusha,27,Burudani,341,burundani,2,come rain,1,come sun,1,Crazy in Love kama wimbo kama wao wenyewe,1,dahh sijui kweli mbona shida,1,Dar utakuja je tumejiandaa,1,daraja sahau nini,1,demokrasia ya upanga,1,Dodoma,78,Dole tupu vijana wa zamani,1,Duhh bibie endeleza libeneke,1,Duhh kaisikie Walibana,1,duhh kwa mbagala mama lazima awe supa,1,Fedha za maiti haziliwi bure,1,Fedha za watu kwa maendeleo ya watu,1,Fikira,14,filamu,252,Filamu ndio kielelezo cha ukuzi wa taifa,1,flamu,7,Gandamiza Kibara baba ake,1,haba,1,habar,1,Habari,5214,habari dodoma,29,habari. dodoma,32,habaria,1,hadithi,19,hakika tumeweka historia,1,hakuna noma jongwe,1,hapa kwetu inakuwaje vile,1,hasira hasara,1,hata maji,1,hataki masikhara na maisha yake,1,hatubonyezi kizenji,1,haya ndiyo mambo ya Ulaya,1,haya si yangu ni ya mdau mwenye hasira,1,haya wabongo na mambo kutoka nje,1,He he he wananikumbusha upishi wa shaba,1,Headline,1,Hii hurejesha uhai,1,Hii iko sawa kweli?,1,Hii imekaa vizuri,1,Hii inakaaje vile,1,Hii kweli noma,1,Hii maana yake Moro kuna uhaba wa chakula,1,Hii mexico,1,Hii mihasira mingine bwana,1,Hii ndio moro sio mpaka dar,1,hii ni hatari,1,Hii ni kiboko anayetaka kubisha ajibishie tu,1,Hii ni moja ya staili za kunyoa nywele,1,Hii si lukwangule,1,hii staili mpya,1,hili ni jengo pacha la malaysia ghorofa 88,1,Hivi ni ngoma tu,1,hivi nini siri za serikali,1,hivi sisi tunajua kama kuna vitu vya aina hii,1,hivi vitu bwana,1,Hiyo ndiyo gharama ya demokrasia,1,Hizi imani nyingine ni hatari,1,Hizi takwimu hizi mhh,1,Hongera bibie,1,Hongera dada etu kwa kutuletea kaka etu (shemeji) kwani mwenye dada hakosi shemeji,1,Hongera sana,1,huhitaji mifedha kuwa msafi,1,Huko Ulaya,1,Huu ndio ustaarabu,1,huu ujiko utakuwa mkubwa,1,imetosha,1,Inahitaji nidhamu fulani,1,inakuuma au...,1,Inakuwaje kama filamu yenyewe itahitaji busu la nguvu,1,Inaonekana watanzania hatukuwepo,1,Ipo kazi Maximo,1,Iringa,22,Isiwe mijineno tu manake mihela hubadili watu kweli,1,Itakuwa laki moja ya halali,1,jamani huu kama si ushamba kumbe nini,1,Jamani mbona Mungu anatupigania,1,Jamani watoto wanatakiwa kupendwa,1,jamani.. jamani ukiikosa Diamond usijutie,1,Je nyumbani hakuna vitu vya aina hii?Tuambie,1,je walikuwepo watu wa huduma ya kwanza,1,Je watanzania wanalipa kodi,1,jela kwa raha,1,Jolie,1,juhudi za lazima kuinua filamu,1,kama si kiwanda cha chumvi nani atawajua hawa,1,Kama kweli ndio kweli basi kila heri,1,Kama Mkristo naamini hilo hiyo si sahihi,1,kama unajua kuyarudi nenda Malta,1,kama wao wanaweza sisi je,1,Kamua baba waache wakanyagane,1,karibu nyumbani dada yote maisha tu,1,karibu Tatiii,1,KARIBUNI,1,Katavi,5,kaza buti hakuna kukata tamaa inalipa,1,kazi kwako mheshimiwa waziri wa madini,1,kazi na burudani,1,keep it up bloggers,1,kero ya usafiri sasa kwisha,1,Kila chenye roho na mwili kitaonja umauti,1,kila kitu kina vitu,1,Kila la Heri jamila,1,kila la heri kwani ni changamoto,1,Kipya,51,Kiuno bila mfupa,1,Kolelo mzimu ambao bado hai,1,KUBWA,1,Kudumisha urafiki wa dunia,1,Kuna dalili za wasomi kukubali Uafrika,1,kuna makala humu humu ndani ya blogu sijui mnasemaje,1,Kuu,113,kwa mara nyingine tena Tigo imewezesha,1,Kwa mchanganyiko huu muungano lazima udumu,1,Kwa mihasira hajambo,1,kweli,1,Kweli ina mkono mrefu tuone,1,Kweli duniani tunatofautiana,1,la maana ni kuwa na jiko au vipi,1,labda halitabadilika tena,1,lakini mwafaka lazima,1,lengo ni kutafakari,1,leteni vitu tuvione,1,lets us,1,Lucy wanakuelewa hawa...,1,Lukwangule nyumbani kwetu,2,M ungu bariki mikono ya madaktari wafanikiwe,1,MAARUFU,1,maendeleo ya soka siku zote yanahitaji fedha ili yapatikane,1,maisha ni vyema kuyaangalia,1,MAJIBU,1,makala,52,mama ni mama tu anapendeza,1,mambo mengine we angalia tu,1,mambo msimamo,1,mambo sasa mchanganyiko,1,Mara nyingine huona tunakotoka kwa kuona wenzetu,1,Mashabiki wa rhumba mpooooooooo,1,Masitaa,12,Maskani,1,MASOKO,3,Masupa staa mnaoinukia mpoo,1,Matamasha,6,mavazi ya kuogelea yanaposhindaniwa,1,Mbeya,11,Mchakamchaka anti Asmah,1,Mchanganyiko,81,MCHANYATO,1,mchezo,5,mengi wanayoyaita siri ni public information,1,mfumuko wa bei mpaka noma,1,Mhh sijui watu wa Sua ambao wako huko wanasemaje,1,Mhh ugua pole dada watu wanataka burudani,1,Michezo,534,Michezo maalum inatakiwa kupigiwa debe,1,miguu,1,miguu babu,1,Mikataba mingine ama hakika tuiangalie hata wakopeshaji nao wanatugeuza sakala,1,MIMI NI KISURA NAJITAMBUA,1,Mimi sijajua hasa kumetokea nini kwani ninavyojua hawa huwa na ungalizi wa hali ya juu,1,Mimi simo,1,mimi sisemi,1,miochezo,1,mkiwa chumvi basi mkoze,1,Mkiwa taa mulikeni,1,Mnaonaje je hii imekaa vyema,1,Mnaweza wakwetu hapa,1,Morogoro,51,mrithi wa mwanadada Whitney Houston,1,Mtwara,4,Mungu aiweke mahali pema roho yake,4,Mungu amrehemu,1,Mungu amweke pema peponi,1,Mungu awabariki sana,1,Mungu awe nao,1,Mungu ibariki Tanzania,1,Mungu tuepushe na imani hizi za kishirikina,1,mungu tufanye tuwe na upendo,1,Mungu twaomba utuhurumie,1,Muziki,353,muziki na fasheni,6,Mwanahabari,33,Mwanza,6,Mwendo mdundo dada,1,Mwenge huo utakimbizwa duniani kwa siku 130,1,Mwenge wa olimpiki ni ishara ya urafiki,1,Mzee wa Farasi nakupa saluti,1,Mzimbabwe huyu kutoka kwa mama mkali,1,N i dar mpaka Moro au bao tatu bila,1,Na sisi je,1,Naam kama haiwezekani hapa,1,Nairobi waanzisha tena utalii,1,namna bora ya kusaidia jamii,1,nani abebe hukumu na lawama,1,nani asiyejua utamu wa pipi,1,Nani kama baba,1,naona inafaa kuchangia mimi sitoi hoja,1,ndoa za mastaa huwa na mgogoro,1,nenda mwaya nenda,1,New Zanzibar Modern Taarab na wapenzi big up,1,news,5,Ni bikini kwa kwenda mbele,1,Ni Dar mpaka Moro au.. tatu bila,1,ni furaha za muungano,1,Ni kazi ngumu yenye kuhifadhi utamaduni,1,Ni kuchakarika kuonyesha urafiki na biashara pia,1,ni mfumuko wa bei au mfumuko wa nchi,1,Ni muhimu kutazama afya yako,1,ni muziki kwa kwenda mbele,1,Ni muziki mpaka China,1,Ni raha tupu,1,Ni Serengeti Premium Lager,1,Ni Tigo na mawasiliano ya kisasa,1,Ni wakati wa kuujadili utamaduni,1,Ni zaidi ya jazz,1,Nitasubiri and welcome home,1,nje je?,1,NUKUU YA LEO,1,nyie mnasemaje kuhusu hili,1,Ona Kolelo na sindikizwa na Wazee wa Gwasuma,1,ona vya dunia,1,One step ahead,1,patna mwingine mjamzito,1,Pengine anamuogopa Jada Pinkett manake kwa wivu..,1,picha,494,Pole Jamila hayo ndiyo mashindano,1,poleni sana,1,poleni sana wanyalukolo,1,Powa sana,1,Profesa jamaa wanakumaindi,1,Roho za marehemu zipate pumziko la milele,1,Ruvuma,9,sakata dansi mpaka kwenye kilele cha dunia,1,sasa kumebakia ugonjwa mmoja polisi kuendesha mashtaka,1,sasa mifedha kila mahali hongereni,1,Sasa ni mavuno,1,Sasa ni wakati wa kutafuta upenyo ndani ya IDOLS,1,SAYANSI,5,SAYANSI ANGA,3,See Uluguru Montains,1,serikali inataka kujihami kwanini,1,Show of support Big Up Madame,1,Si kitu kidogo hata kidogo,1,si unajua tena namie naimwaga hivyo hivyo,1,Siasa,346,siasa habari,2,Sijui kama City wanajua Mbagala noma,1,Sijui tunaishi karne gani yailahi,1,Sinema,13,sio advencha....kaaa ...niko kibaruani,1,Sisi ndio tunaanza vitongoji,1,Sisi yetu macho na masikio,1,Slow slow jamani,1,sto,1,tabasamu kali la mwenge wa olimpiki,1,Tabora,1,Tazama Waziri Mkuu Pinda wasije wakapindisha maamuzi yako,1,TEKNOLOJIA,1,Thats big man game,1,This is crazy Africa,1,This is Mgeta,1,Tibet wamegeuza Olimpiki jukwaa la siasa,1,Titbits collection,1,Tubadili tamaduni,1,Tuchangie mambo yaive,1,tuendeleze sanaa,1,tuienzi na sisi mbona wizara haituambii,1,Tuipeleke kaskazini,1,Tuisaidie serikali shida ya Mererani,1,tujue namna ya kupumzika,1,Tulienda kustarehe au kufanya fujo,1,Tumsaidie mtototo huyu kurejea katika hali ya kawaida,1,tunahitaji haya,1,Tunajifunza kweli kutoka kwao,1,Tunapandisha chati tu,1,Tunasubiri,1,tunazidi kuhesabu siku,1,TUNAZISUBIRI ZA VINARA ADAR,1,Tuombe nafuu kwa wagonjwa,1,Tuombe rehema kwa mungu,1,Tuone yatufae,1,Tusingoje wengine watusemee,1,tutampa tafu kubwa Prof,1,tuuenzi utamaduni au vipi,1,Tuukuze na kuulinda,1,tuvipende,1,tuwalinde maalbino,1,Tuwe kweli wakweli,1,ubunifu siku zote hulipa,1,uchumi huzunguka kwa kuwawezesha wasukaji,1,udumu muungano,1,Ugonjwa huu wa sasa ni kitendawili,1,Ukiiona kolelo utaipenda,1,Ukirejea salama kila mtu anafurahi,1,Umelenga Mkuchika utamaduni unakufa,1,unaposaka uwakilishi wa dunia,1,urafiki,1,urembo,1,Usisahau wazee wa Ngwasuma,1,UTALII,1,UTAMADUNI,3,Video,2,Vionjo vipya ndani ya Gwasuma,1,Vita dhidi ya ufisadi,1,vitongoji Miss Tanzania navyo vimeanza,1,Vitu vikali vyazidi kuingia Dar,1,Vituko,77,Vituo vya polisi Tanga vyatelekezwa,1,VIVALO,1,Wacha tujifue,2,Wadau ilitolewa kiingereza,1,wakali wa ubunifu,1,wala usibabaike mwakwetu hii noma,1,wanadamu wanapotaka kujua zaidi,1,wanasema mpaka kieleweke,1,Wanataka kujua mali za JK na wengine,1,Wanawake wenye mvuto: Monroe,1,Wapo mabinti wa matawi ya juu,1,watu wanapofanya weli kwenye sanaa,1,waweza kurejea enzi ya Moro jazz na Cuban malimba,1,Wazee tupo kusindikiza,1,waziri,1,welcome dar baby,1,Wenzetu wameona sisi tunangoja nini kuangalia,1,wewe unasemaje,1,wigo mpana wa utamaduni,1,wilaya ya 'Mbagala' mlie tu,1,Yaaani sijui itawezekana,1,Yaani wakati mwingine hata huelewi prioty over priority,1,yeye mbele sisi nyuma,1,Yote maisha dada,1,ZA MOTOMOTO,1,Zanzibar,79,zawadi zinatakiwa ziende shule,1,ZILIZOTIA FORA,1,zitachangia kupunguza makali ya bei za umeme,1,
ltr
item
Lukwangule Entertainment: Hotuba ya kufunga kikao cha Bunge Mkutano wa Saba
Hotuba ya kufunga kikao cha Bunge Mkutano wa Saba
Lukwangule Entertainment
https://lukwangule.blogspot.com/2012/04/hotuba-ya-kufunga-kikao-cha-bunge.html
https://lukwangule.blogspot.com/
http://lukwangule.blogspot.com/
http://lukwangule.blogspot.com/2012/04/hotuba-ya-kufunga-kikao-cha-bunge.html
true
934549962738256429
UTF-8
Loaded All Posts Not found any posts VIEW ALL Readmore Reply Cancel reply Delete By Home PAGES POSTS View All RECOMMENDED FOR YOU LABEL ARCHIVE SEARCH ALL POSTS Not found any post match with your request Back Home Sunday Monday Tuesday Wednesday Thursday Friday Saturday Sun Mon Tue Wed Thu Fri Sat January February March April May June July August September October November December Jan Feb Mar Apr May Jun Jul Aug Sep Oct Nov Dec just now 1 minute ago $$1$$ minutes ago 1 hour ago $$1$$ hours ago Yesterday $$1$$ days ago $$1$$ weeks ago more than 5 weeks ago Followers Follow THIS CONTENT IS PREMIUM Please share to unlock Copy All Code Select All Code All codes were copied to your clipboard Can not copy the codes / texts, please press [CTRL]+[C] (or CMD+C with Mac) to copy