*Ni bingwa wa hesabu, fizikia ya anga za juu FEBRUARI 6 majira ya saa 6:12 mchana, kwa saa za Afrika Mashariki, chombo cha anga za...
*Ni bingwa wa
hesabu, fizikia ya anga za juu
FEBRUARI 6 majira ya saa 6:12 mchana, kwa saa za Afrika
Mashariki, chombo cha anga za juu cha Urusi, Soyuz, kilitua katika ardhi ya
Khazkhstan, kikimleta duniani Christina Koch ambaye amekaa katika kituo cha
kimataifa cha anga za juu (ISS) kwa siku 328.
Dunia katika hamu yake ilitazama televisheni mbalimbali, ikiwamo
ya NASA ikionesha mbashara kuondoka kwake katika kituo hicho kinachoelea angani
kiasi cha kilomita mia nne kutoka uso wa dunia hadi mji wa Khazkhstan.
Christina na wenzake waliondoka katika kituo hicho saa 12:50
a.m. EST. (saa mbili na dakika 50 za Afrika Mashariki), wakiingia katika nguvu
za mvutano na kutua Kusini mashariki mwa
Dzhezkazgan, Kazakhstan 4:12 a.m. EST (saa 6 na dakika 12 mchana kwa saa za Afrika
Mashariki).
Binti huyo aliingia ISS Machi 14, 2019, kama rubani mhandisi kwa
safari namba 59,60 na 61 ( Expedition 59, 60 and 61).
Aidha katika msafara wa kurejea duniani Christina Koch aliambatana na mwanaanga wa anga za juu kutoka taasisi ya
utafiti wa anga za juu ya Ulaya (ESA), Luca Parmitano na mwanaanga wa Urusi
Alexander Skvortsov ambaye ndiye alikuwa kamanda wa chombo hicho.
Televisheni ya NASA ilionesha mbashara kitendo cha kujinasua
kutoka stesheni hiyo ya anga za juu safari yake kurejea duniani, kupita katika
ukuta mnene unaotenganisha anga la chini na dunia, eneo ambalo limejaa makeke
makubwa na moto na kutua kwake katika mji huo wa Kazakhstan. Walitua duniani na
kukutana na joto chini ya sentigredi sifuri, ilikuwa ni digrii ya celisius -3.
ISS ni nini?
Ni setelaiti ya kutengenezwa ambayo imeundwa kwa ushirikiano wa
mataifa mengi ikiwa inazunguka kwenye mzingo wa chini wa dunia. Mradi huu
unahusisha mataifa makubwa yenye ujuzi
mkubwa katika sayansi na anga za juu ni wa gharama kubwa.
Mataifa hayo ambayo yanawasilishwa na taasisi zao za utafiti wa
anga za juu ni Marekani kupitia shirika lake la NASA, Urusi kupitia shirika
lake la Roscosmos, Japan kupitia shirika lake la JAXA, mataifa ya Ulaya kupitia
shirika lao la ESA na Canada kupitia shirika
lake la CSA. Nchi zote hizo zinafanya uwapo kwa uhai wa chombo hicho cha
utafiti.
Setelaiti hii inatumika kwa ajili ya tafiti za nguvu za mvutano
mdogo zinavyoathiri binadamu na pia
kuangalia mazingira ya anga za juu tayari kwa ajili ya safari za mbali zaidi
kama kutoka duniani katika mwezi na sayari ya Mars.
Wanaanga wanaofika kufanya kambi katika setelaiti hii hufanya
tafiti katika masuala ya baolojia, baolojia ya binadamu, fizikia, unajimu, hali
ya hewa na tasnia nyingine.
Aidha setelaiti hii imeelezwa kuwa moja ya chombo muhimu cha kufanya
majaribio ya zana na mifumo inayohitajika kwa ajili ya kupeleka wanadamu na
kufanya kazi katika anga za juu.
Chombo hiki kipo kilomita 400 kutoka katika uso wa dunia
kikitumia mitambo maalumu ya kuendelea kuiwe mahali ilipo katika katika mzingo,
huku kikizunguka dunia kwa dakika 92 na kukamilisha mizingo 15.5 kila siku.
Setelaiti hii inatarajiwa kuendelea kuwepo hadi mwaka 2030.
Ni katika setelaiti hii mwanadada Christina aliishi kwa siku 238
akifanya majaribio mbalimbali na yeye mwenyewe akiwa kitu cha kuangalia katika
baolojia ya binadamu, kwani alikuwa sampuli iliyopelekwa na NASA kwa makusudi
ya kuendelea, kuangalia mabadiliko yanayotokea kwa mwanadamu akiwa katika
safari za anga za juu.
Mdada huyo kwa kukaa kwake hadi Februari 6 amekaribia muda wa
juu wa wanaanga wa NASA kukaa anga za juu ambao ni siku 340, rekodi
iliyotekelezwa na Scott Kelly. Kwa kawaida wanaanga hukaa katika kituo hicho
kwa miezi sita tu.
Umahiri wa
mdada
Mdada huyu ambaye
haijaoneshwa kama ana mtoto, ana mume ambao wanaishi naye jimbo la
Texas. Mdada huyu ukisoma wasifu wake ni ‘mchawi’ mkubwa wa
hesabu na fizikia hasa ya anga za juu.
Katika mahojiano na vyombo mbalimbali ya habari wakati akiwa
katika anga za juu, Koch alisikika kila mara akisema kwamba, binadamu
wanatakiwa kusaidiana kufanikisha ndoto mbalimbali kuwa kweli, ili hao
waliofanikisha ndoto waweze kuleta mafanikio katika maisha duniani.
Kitu kingine ambacho kimeelezwa katika mitandao mbalimbali ni
umahiri wake wa kuhimili mazingira magumu na katika ajira yake NASA amesaidia
kutengeneza vifaa mbalimbali vya kutumika katika vyombo vya anga za juu.
Katika mahojiano ya moja kwa moja kati ya waandishi wa habari
kupitia vyombo vya NASA na mwanaanga huyo akiwa kwenye setelaiti alisema kwamba
amefurahishwa sana kutimiza ndoto yake.
Alisema kwamba ni matarajio yake kwamba atarejea tena anga za
juu baada ya kukamilisha ngwe ya kukaa huko kuanzia Machi 14 hadi Februari 6.
Mdada huyo alisema amefurahi kuweka mikono yake katika elimu
hiyo ya anga za juu na kuwataka wanawake wenzake kufuata moyo wao katika kila
jambo analotaka kulifanya.
Akionesha namna unavyoweza kutawala maeneo unayofanyia kazi,
Koch anasema hakuna kitu kilichokuwa kinamtia kiwi wakati akiwa angani ni
kutimiza ndoto yake na kuiangalia dunia kutoka katika setelaiti hiyo.
Koch ambaye hadi Desemba 28 alikuwa angani kwa siku 289 akivuka
rekodi iliyowekwa na mdada mwingine Peggy Whitson, ambaye alikuwa ametumia siku
288 katika kituo hicho, ni mdada anayeonekana kuwa jasiri kutokana na kupitia
mambo mbalimbali magumu yaliyotengeneza ujasiri.
Alhamisi wakati chombo cha anga za juu cha Urusi, Soyuz,
kinamrejesha duniani mdada Christina Koch
aliyekaa katika kituo cha anga za juu ISS kwa siku 328, dunia
ilishangilia na kupata nafasi ya kumtambua mdada huyo asiyekuwa na makeke.
Aidha mdada huyo alishiriki katika kufanya tafiti 210 akiwa
katika setilaiti hiyo.
Alianzia wapi?
Mdada Christina Hammock Koch ambaye alipitishwa kuwa mmoja wa wanaanga wa Shirika
la Utafiti wa Anga za Juu la Marekani (NASA)
mwaka 2013, alikamilisha mafunzo Julai mwaka 2015 na kuwa tayari
kutumika katika kazi mbalimbali.
Koch aliyezaliwa Januari
29, 1979 na kupewa jina la Christina Hammock ni mhandisi na mwanaanga wa anga za juu wa Shirika la
Utafiti wa anga za juu la Marekani ( NASA ).
Mdada huyo ambaye ana umri wa miaka 40 amepitia chuo kikuu cha serikali cha North Carolina akatwaa digrii ya sayansi ya
uhandisi umeme na fizikia (2001) na
kuchukua digrii ya pili ya uhandisi umeme (2002). Kielimu Koch ni bingwa wa hesabu kwani
alimaliza Shule ya sayansi na hesabu ya
North Carolina iliyopo Durham, North Carolina mwaka 1997.
Koch mwenye asili ya Michigan na kukulia Jacksonville, North
Carolina na sasa anaishi Livingston,
Montana na mume wake Robert Koch. Na
wazazi wake ni Barbara Johnsen aliyetoka Frederick, Maryland na Dk Ronald
Hammock aliyetoka Jacksonville, North Carolina.
Kabla ya kuwa mwanaanga, Koch alikuwa katika uzalishaji wa vifaa
vya maendeleo ya sayansi ya anga za juu na uhandisi wa maeneo ya pembezoni.
Hata hivyo kabla hajawa mwanaanga wa anga za juu alifanya kazi
National Oceanic and Atmospheric Administration, kama mkuu wa kituo cha
American Samoa.
Kazi yake ya sasa ilianzia kwenye uhandisi umeme katika taasisi
ya NASA ya Goddard akijifua katika
nishati ya hali ya juu kwenye fizikia ya anga za juu.
Katika eneo hili alichangia kupatikana kwa vifaa kadha vya
kufanyika uchunguzi katika anga la juu katika upande wa nishati ya juu ya
fizikia katika anga za juu.
Baadaye Koch akawa mtafiti mshiriki katika programu ya United
States Antarctic kwa mwaka 2004 hadi
2007. Hii ni ikiwa ni mwaka mmoja wa
kukaa mazingira magumu ya baridi majira ya baridi katika kituo cha Palmer
kilichopo ncha ya Kusini maeneo ya
Admunsen-Scott.
Akiwa huko alikuwa mmoja katika kikosi cha zimamoto na uokoaji
katika bahari kuu iliyozingwa na mabarafu. Kuanzia mwaka 2007 hadi 2009, Koch
alirejea katika nafasi yake ya utengenezaji wa vifaa vya anga za juu kama
mhandisi umeme Chuo kikuu cha Johns Hopkins idara ya fizikia na anga za juu.
Pia alisaidia kupatikana kwa vifaa vya kupima na kuzuia nururisho hatari la
mwanga kwa vyombo vya NASA kama Juno na Van Allen .
Mdada huyu kutokana na kujituma kwake amepata tuzo nyingi
ikiwamo ya mafanikio ya NASA, Juno Mission Jupiter Energetic Particle Detector
Instrument, 2012; Mgunduzi wa mwaka
inayotolewa na Johns Hopkins University Applied Physics Laboratory, 2009;
United States Congress Antarctic Service Medal na Winter‐Over, 2005;
tuzo ya NASA Group Achievement, NASA Suzaku Mission X‐ray
Spectrometer Instrument, 2005; na
Mtaalamu mwanaanga ya Astronaut Scholarship Foundation.
Wanadada na
mafanikio
Kitu kinachofurahisha katika mahojiano ni ushauri alioutoa kwa
mabinti vijana akiwataka wafuatilie ndoto zao hadi mwisho
“Fanya kile ambacho wewe
kinakutisha. Kila mtu ni lazima afikirie kile kitu kinachompa mshawasha
kinachowafanya wawe wao. Vitu hivyo vinaweza kukuogofisha kidogo lakini maana
yake iko wazi kabisa unasisimukwa navyo, unavipenda. Kama utafanyia kazi
kitalipa kwa njia moja au nyingine,” alisema mdada
huyo ambaye ameshawahi kushiriki mashindano hatari ya kwenye makambi ya hatari
na kutoka salama.
Pamoja na kuwa na siku nyingi kitu kingine ambacho alikifanya
akiwa angani ni pamoja na mwanamke mwingine Jessica Meir kufanya ukaguzi wa nje
wa chombo hicho kwa saa saba na dakika 17.
Wanaanga hao walipigiwa simu na Rais Donald Trump kwa
kukamilisha kazi yao kwa umakini mkubwa.
Koch anaamini kuwa rekodi yake ya kukaa huko itavunjwa na
wanawake wengine kwa kuwa ina maana kwamba wanawake wataendelea kujitosha na
kujituma zaidi.
COMMENTS