Sekta ya urembo inashuhudia mabadiliko makubwa, huku makampuni yenye hadhi kubwa yakibadilika ili kwenda na wakati.Kuanzia kwa mastaa maar...
Sekta ya urembo inashuhudia mabadiliko makubwa, huku makampuni yenye hadhi kubwa yakibadilika ili kwenda na wakati.Kuanzia kwa mastaa maarufu hadi kwa mabilionea wanaomiliki makampuni makubwa, hawa ni watu wenye ushawishi mkubwa ambao wanabadilisha viwango vya urembo na kubadili jinsi biashara zinavyoungana na wateja
Bidhaa za urembo
zinaboresha uzoefu wa wateja, zikitoa bidhaa bunifu na kuvuka mipaka ya
ubunifu. Wanaoongoza mapinduzi haya ni mabilionea hawa mashuhuri, kama
ilivyoainishwa na Tatler Asia, ambao ushawishi wao unachagiza
mustakabali wa sekta hii.
Rihanna
– Fenty Beauty
Mwimbaji na
mwigizaji aliyezaliwa Barbados, Rihanna, amejenga utajiri wake wa Dola bilioni
1, sio kutokana na muziki, bali kutoka kwa biashara zake za urembo na mitindo.
Baada ya kufanya kazi na kampuni mbalimbali za mitindo, alifanya uamuzi mkubwa
zaidi mwaka 2017 kwa kuanzisha Fenty Beauty, kwa kushirikiana na kampuni
ya LVMH.
Tangu mwanzo, Fenty
Beauty ilijitofautisha kwa kuzingatia ujumuishi, ikitoa bidhaa kwa ajili ya
aina mbalimbali za rangi za ngozi. Kutolewa kwa bidhaa zao zenye rangi 40
kuliibua mabadiliko makubwa katika sekta nzima, na kuzifanya kampuni zingine
kuiga mfano huo. Hii iliashiria mabadiliko makubwa katika sekta ambayo kwa muda
mrefu ilikuwa imewasahau wanawake wenye ngozi nyeusi.
Ndani ya mwaka
mmoja, mapato ya kampuni hiyo yalizidi Dola milioni 550. Akipanda juu ya
mafanikio hayo, Rihanna alianzisha Savage X Fenty mwaka 2018, kampuni ya
nguo za ndani zinazokuza kujiamini, na baadaye akaingia kwenye bidhaa za
utunzaji wa ngozi na nywele kupitia Fenty Skin na Fenty Hair.
Françoise
Bettencourt Meyers – L’Oréal
Akiwa ni mrithi
wa kampuni kubwa ya vipodozi ya Ufaransa, L’Oréal, Françoise Bettencourt
Meyers anajulikana kwa kupenda maisha ya faragha, akionekana mara chache kwenye
hafla za kifahari.
Mbali na
ushawishi wake katika kukuza matumizi ya teknolojia bunifu na uendelevu,
Bettencourt Meyers amefanya athari ya kudumu kupitia kazi zake za kutoa
misaada.
Kupitia Mfuko wa Bettencourt
Schueller Foundation, anaongoza mamia ya mamilioni ya Dola kuelekezwa
kwenye utafiti wa kisayansi na uhifadhi wa urithi wa kitamaduni.
Mwishoni mwa
2023, alikuwa mwanamke wa kwanza kufikia hadhi ya 'centibillionaire' akiwa na
utajiri unaozidi Dola bilioni 100, ingawa utajiri wake ulishuka sana mwaka
uliofuata kutokana na mauzo ya vipodozi nchini China kupungua. Kwa sasa, yeye
ndiye mwanamke wa pili tajiri zaidi duniani akiwa na utajiri wa Dola bilioni
94.2.
Suh
Kyung-bae – Amorepacific
Suh Kyung-bae,
Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Amorepacific, anaaminika kuwa ndiye
aliyechagiza umaarufu wa kimataifa wa urembo wa Kikorea. Alichukua uongozi wa
kampuni hiyo mwaka 1997 na tangu wakati huo amesimamia upanuzi mkubwa, akijenga
mkusanyiko wa bidhaa maarufu kama Sulwhasoo, Laneige, na Innisfree.
Suh alifanya
mabadiliko ya kiteknolojia akichanganya utafiti wa kibiolojia na tamaduni za
urembo za Mashariki na Magharibi, na kuunda bidhaa zinazofaa kwa masoko
mbalimbali. Chini ya uongozi wake, Amorepacific imefikia ukuaji endelevu wa
kimataifa na imejijengea sifa kama moja ya kampuni zenye ubunifu zaidi duniani.
Kim
Byung Hoon – APR
Kim Byung Hoon,
ambaye utajiri wake unakadiriwa kufikia Dola bilioni 1.3, ndiye bilionea wa
bidhaa za utunzaji wa ngozi mwenye umri mdogo zaidi nchini Korea Kusini mwaka
2025 kupitia umiliki wake wa 31% katika kampuni ya APR, aliyoianzisha
mwaka 2014.
Kampuni hiyo
ilianza na vipodozi lakini ilifanya mapinduzi makubwa mwaka 2021 kwa
kutengeneza vifaa vya usoni kwa matumizi ya nyumbani ambavyo viliweza kutoa
matibabu kama yale yanayopatikana kwenye 'spa'. Badala ya kutegemea mauzo
kwenye maduka ya ushuru, APR ilijitofautisha kupitia masoko
yanayotegemea TikTok na bidhaa zenye teknolojia ya kisasa.
Hali hiyo
iliendelea hadi mwaka 2024, wakati kampuni ilianzisha kampeni kubwa
zilizowashirikisha Kylie na Kendall Jenner pamoja na Khloe
Kardashian. Hisa za APR ziliongezeka kwa kasi mwaka huu, na kuifanya
kuwa kampuni kubwa zaidi ya urembo nchini Korea Kusini kwa thamani ya soko.
Hou
Juncheng – Proya
Hou Juncheng
alianzisha Proya mwaka 2006 nchini China baada ya miaka mingi ya uzoefu
wa kusambaza bidhaa za vipodozi za ndani. Kwa kutumia biashara ya mtandaoni,
mitandao ya kijamii, na ‘livestreaming’, Proya ilijijengea umaarufu mkubwa
kwa haraka miongoni mwa vijana. Mapato yake mengi yanatokana na bidhaa kuu ya
“Proya”, ambayo ni maarufu sana kwa wanawake wa Kichina wenye umri wa miaka 18
hadi 24 wanaoishi kwenye miji midogo na ya kati.
Mwaka jana,
mapato ya kampuni yalizidi yuan bilioni 10 (Dola bilioni 1.4), ikiashiria mara
ya kwanza kwa kampuni ya urembo ya Kichina kufikia hatua hiyo. Chini ya uongozi
wa Hou, Proya imewekeza sana katika utafiti na maendeleo, na kusababisha hati
miliki 256. Kwa sasa Hou anataka kufungua kituo cha ubunifu huko Paris na
kutafuta makampuni ya kununua ili kuimarisha uwepo wa Proya kimataifa.
Utajiri wa Hou unakadiriwa kuwa Dola bilioni 1.7.
COMMENTS