Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imezipigilia msumari taasisi na mashirika ya umma nchini kutanguliza uzalendo kwa ...
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imezipigilia msumari taasisi na mashirika ya umma nchini kutanguliza uzalendo kwa kununua bidhaa za ngozi zinazozalishwa hapa nchini ili kukuza uchumi wa ndani.
Wito huo umetolewa Machi 13, 2026, na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu, wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua mradi wa Kiwanda cha Ngozi cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KLICL) mjini Moshi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, aliifahamisha kamati hiyo kuwa Serikali kupitia mfuko wa PSSSF na Jeshi la Magereza imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 142 kwenye kiwanda hiki.
Pamoja na uwekezaji huo mkubwa, bado kuna changamoto ya soko la ndani.
"Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha hadi jozi milioni 1.2 za viatu kwa mwaka na soli za viatu jozi milioni 2.1. Pia tunazalisha bidhaa nyingine kama mikanda, mabegi na makoti ya ngozi zaidi ya 184,500 kwa mwaka, lakini soko letu la ndani bado halijachangamka ipasavyo," alisema Waziri Sangu.
Kutokana na changamoto hizo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imezitaka taasisi na mashirika ya umma nchini kuonyesha uzalendo kwa kununua bidhaa za ngozi zinazozalishwa nchini, ili kulinda uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia fedha za walipa kodi.
Mhe. Mchafu alisema ni wakati sasa kwa mashirika ya umma na taasisi za serikali kutoa kipaumbele kwa bidhaa za ndani badala ya kuagiza nje, hatua itakayosaidia kukuza viwanda vya ndani na kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania.
"Ni lazima taasisi zetu zitangulize uzalendo na maslahi ya umma kwa kutumia fedha za walipa kodi kununua bidhaa hizi zinazozalishwa hapa nchini. Hii ndiyo njia pekee ya kukuza uchumi wetu," alisema Mhe. Mchafu.
Kwa upande wao, wajumbe wa kamati hiyo, akiwemo Mhe. Lucy Kombani na Mhe. Kafiti W. Kafiti, walishauri Serikali kuweka utaratibu madhubuti utakaolazimisha taasisi za elimu na vyombo vya ulinzi na usalama kununua viatu na bidhaa nyingine za ngozi kutoka KLICL.
Wajumbe hao waliongeza kuwa kuimarisha soko la ndani kutaifanya PSSSF kupata tija ya uwekezaji huo na kuhakikisha kiwanda kinaendelea kujiendesha kwa faida.
Baada ya kukamilisha ziara mkoani Kilimanjaro, kamati hiyo inatarajiwa kuendelea na ziara yake mkoani Tanga, ambapo kesho itakagua mradi wa Kiwanda cha Chai cha Mponde kilichopo Lushoto.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imezishauri taasisi na mashirika ya umma kutanguliza uzalendo na maslahi ya umma kwa kutumia fedha za walipa kodi kununua bidhaa za ngozi zinazozalishwa ndani ya nchi.
Ushauri huo umetolewa na wajumbe wa kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Hawa Mchafu wakati wa ziara ya kikazi waliyoifanya kukagua mradi wa kiwanda cha Ngozi cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KLICL) 13 Machi 2026 mjini Moshi.
Wakiwa kwenye kiwanda hicho, Kamati ya bunge ilijulishwa kupitia taarifa iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu kuwa licha ya kiwanda kuanza uzalishaji mwaka 2017 na kuzalisha bidhaa bora za ngozi bado kuna changamoto ya soko la ndani la bidhaa hizo.
Waziri Sangu alibainisha kuwa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Jeshi la Magereza imewekeza zaidi ya shilingi Bilioni 142 hadi kukamilika kwake.
“Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha hadi jozi milioni 1.2 za viatu kwa mwaka, soli za viatu jozi milioni 2.1 kwa mwaka, bidhaa mbalimbali za ngozi (leather articles) kama vile mikanda, mabegi, pochi, makoti (leather jackets) n.k zipatazo 184,500 kwa mwaka” alisema Waziri Sangu.
Wakizungumza baada ya ukaguzi wa kiwanda hicho Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge Hawa Mchafu aliishauri Wizara pamoja na Menejimenti ya kiwanda cha KLICL kuwa na mkakati mahsusi wa kutangaza bidhaa za ngozi ili zivutie masoko.
Mwenyekiti huyo alipongeza kiwanda hicho kwa kuzalisha ajira za watanzania ambapo ametaka jitihada zaidi za kutangaza bidhaa zake kwa kutumia jina la Tanzania.
Kwa upande wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mbunge Lucy Kombani na Kafiti W. Kafiti walipongeza jitihada za Mfuko wa PSSSF kwenye uwekezaji wa kiwanda hicho na kushauri serikali ihamasishe taasisi zake kufanya manunuzi ya bidhaa za ngozi ikiwemo viatu kwenye vyombo vya ulinzi na usalama pia shule kutoka kiwanda hicho.
Kamati hiyo ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii inaendelea na ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano ambapo kesho itatembelea mradi wa kiwanda cha chai Mponde kilichopo Lushoto mkoani Tanga.
COMMENTS