Katika kuadhimisha miaka mitano tangu kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Watanzania wamekumbushwa kuishi na ...
Katika kuadhimisha miaka mitano tangu kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Watanzania wamekumbushwa kuishi na kuyaendeleza maono ya uongozi wake yaliyojikita katika uthubutu, uzalendo na uchapakazi usiolala.
Wito uliotolewa katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Chato, mkoani Geita, unawataka wananchi kutofanya kumbukizi hiyo kuwa ya maneno pekee, bali wachote busara zake na kuzifanyia kazi kwa vitendo ili kuliisukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa.
Hayati Dkt. Magufuli anakumbukwa kama kiongozi shupavu na mtetezi wa wanyonge ambaye aliacha alama zisizofutika kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati. Miradi kama Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP), ujenzi wa daraja la J.P. Magufuli (Kigongo-Busisi), na upanuzi wa reli ya kisasa (SGR) imetajwa kama kielelezo cha maono yake ya kujenga uchumi imara. Dhamira yake ya kuhakikisha "maskini wanapumua" ilijidhihirisha katika mapambano yake dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, na kuimarisha nidhamu ya kazi kwa watumishi wote.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria misa hiyo ya kumbukizi, akiwemo Makamu wa rais Dk Emmanuel Nchimbi,Waziri Mkuu Mstaafu Kassim Majaliwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi, na wote wamemsifu Hayati Magufuli kwa kuwa mzalendo wa kweli aliyeweka maslahi ya Taifa mbele.
Uwepo wa viongozi hao uliambatana na ujumbe wa amani, umoja, na staha miongoni mwa Watanzania, huku wakisisitiza kuwa njia bora ya kumpa heshima ya kweli ni kwa kila mmoja katika nafasi yake—iwe ni askari, mwanasiasa, au mfanyakazi—kutumika kwa uadilifu na kumlinda mwananchi wa kawaida.
Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi, ambaye amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa la kutathmini na kuenzi misingi ya uthubutu, ujasiri, na uzalendo uliotukuka ambao Hayati Magufuli aliishi katika kipindi chote cha uongozi wake.
Akitoa salamu za Serikali, Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa njia bora ya kumuenzi kiongozi huyo ni kwa kila Mtanzania kujitoa na kufanya kazi kwa bidii, akirejea falsafa yake ya “Hapa Kazi Tu” kama mwarobaini wa umaskini kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.
Makamu wa Rais amebainisha kuwa maisha ya Hayati Magufuli yalikuwa ni "darasa la uongozi," akimmulika kama kiongozi aliyekuwa na kipawa cha kipekee cha kunena na kutenda yale aliyoyaamini kuwa na manufaa kwa nchi, hususan katika kupiga vita uzembe, rushwa, na kusimamia rasilimali za taifa zibaki mikononi mwa Watanzania wenyewe.
Katika kielelezo cha dhati cha kuenzi urithi huo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha shilingi milioni 100 zilizokuwa zimebaki ili kukamilisha ujenzi wa makumbusho ya Hayati Magufuli yaliyopo Chato, hatua inayolenga kuhifadhi historia ya kiongozi huyo kwa vizazi vijavyo.
Naye Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, naye ametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani na mshikamano wa Muungano, akimuelezea JPM kama muumini mkubwa wa uwajibikaji na mtetezi wa wanyonge aliyerejesha nidhamu ya utumishi wa umma nchini.
Majaliwa amesisitiza kuwa JPM alikuwa kiongozi asiyeyumba katika kupambana na wala rushwa, wezi, na wabadhilifu wa mali za umma, na kwamba kutokana na msimamo huo wa kutetea wanyonge, kumbukumbu yake itabaki imara na haiwezi kufutika kwenye mioyo ya wananchi. Alitoa wito kwa kila mmoja, kuanzia askari hadi viongozi wa vyama, kutumika kwa uadilifu, kulinda amani, na kuacha chokochoko zinazoweza kubomoa umoja wa Taifa.
Majaliwa amesisitiza kuwa kumbukumbu ya JPM haitafutika mioyoni mwa watu kutokana na uthubutu wake wa kupambana na ubadhirifu na kuweka misingi ya uwajibikaji inayopaswa kuendelezwa na kila mtumishi wa umma.
Katika ibada hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Mhashamu Severine Niwemugizi, alitoa homilia iliyojikita katika amani, haki, na staha, akiwakumbusha waumini kuwa amani ya nchi ndiyo kila kitu na ni wajibu wa kila mmoja kuilinda.
Mhashamu Severine Niwemugizi, alisema amani, haki, na upendo ni nguzo kuu za kulinda umoja wa kitaifa.
Askofu Niwemugizi amewakumbusha waumini kuwa kumuombea na kumuenzi kiongozi huyo ni pamoja na kuishi maisha ya utakatifu na unyenyekevu, huku akitoa faraja kwa familia na kusisitiza kuwa amani ndiyo kila kitu kwa ustawi wa nchi.
Kwa upande wake, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza, amebainisha kuwa Magufuli ameacha "muujiza" wa kuishi mioyoni mwa watu kutokana na kazi zake kubwa, akisisitiza kuwa njia bora ya kumuenzi ni kufanya maridhiano ya kweli na kurekebisha changamoto za kidemokrasia ili kuliweka Taifa katika mstari ulionyooka mbele za Mungu.
Aidha, Askofu Bagonza, ametoa rai kwa taifa kutumia kumbukizi hiyo kurekebisha pale palipokuwa na changamoto ili kujenga Tanzania yenye haki na maridhiano ya kweli.
Naye kada wa ACT-Wazalendo ,Luhaga Mpina, ametoa wito kwa viongozi na wananchi kuacha kumsifia Magufuli kwa maneno pekee na badala yake waige uadilifu wake katika kulinda uchumi wa nchi. Mpina amesisitiza kuwa msiba wa Magufuli uliacha pengo kubwa si tu Tanzania bali duniani kote, hivyo njia bora ya kuziba pengo hilo ni kuhakikisha miradi ya kimkakati aliyoiacha, kama Daraja la Magufuli na ujenzi wa miundombinu, inalindwa na kukamilishwa kwa viwango vya juu.
Maadhimisho haya ya miaka mitano yameonyesha kuwa licha ya kupita kwa muda, misingi ya "Hapa Kazi Tu" na utetezi wa wanyonge bado ni dira muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Naye kada mkongwe wa CCM, Stephen Wasira, amesisitiza kuwa ni vigumu kuifuta historia ya Magufuli kwani kazi alizozifanya, hususan miradi mikubwa ya maendeleo na madaraja, ni mashahidi tosha watakaomkatalia yeyote atakayejaribu kuzihujumu.

COMMENTS