Monday, September 15, 2008

Moto wamtibua Waziri Mkuu aamua kufundisha


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda jana alilazimika kutoa somo la Baiolojia kuelezea athari za uchomaji moto misitu kwa wanakijiji wa Inyonga katika wilaya ya Mpanda.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo jana (Jumamosi, Septemba 13, 2008) Waziri Mkuu aliwaasa waache tabia ya kuchoma moto misitu kwa sababu madhara yake ni makubwa kwao na kwa viumbe wanaoishi humo.
“Madhara yake ni makubwa kuliko tunavyodhani, ule uoto ambao ungekua na kukomaa sie tunauua kila mwaka. Ni lini uoto huu utakomaa, na je mvua tutapata wapi?, alihoji.
Alisema wakitaka kuona ukubwa wa madhara ya mioto kichaa, ifike siku wakute hawana majani ndipo watajua madhara ya vitendo vyao kwani hakutakuwa na hewa safi ya kuvuta.
“Hewa safi tunayovuta inaitwa oksijeni na hii inatengenezwa na majani ya miti, yenyewe yanachukua hewa chafu tunayoipumua halafu yanatupa hewa safi , sasa itokee siku hakuna miti kabisa tutaanza kuanguka mmoja mmoja kwa kukosa hewa safi ,” alisema.
Alisema: “Uchomaji moto ni kama vile umegota hapa kwani kila kiangazi ni lazima mchome moto… kuna mtu ameshajiuliza madhara kwa wadudu na wanyama wanaoishi msituni, wadudu wengine ni mapambo wengine wanatengeneza hewa ardhini... ninawaomba ndugu zangu tuache tabia hii…”.
Alisema kuna haja ya kufufua kampeni ya kutunza mazingira ili mwaka kesho kusiwe na tatizo la uchomaji moto kama hali ilivyo sasa.
Wakati msafara wa Waziri Mkuu ukiwa njiani, ulishuhudia maeneo mengi yakiwa yamechomwa moto na mengine yakiendelea kuwaka. Kati ya kilometa 134 alizopita Waziri Mkuu kutoka Mpanda mjini hadi Inyonga ni kama kilometa tano tu ambazo hazijachomwa moto.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Bw. Thobias Sijabaje akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya mkutano huo, alithibitisha ukubwa wa tatizo hilo na kuongeza kuwa kutoka barabarani moto huo huweza kusambaa kilometa kati ya 20 na 30 ndani ya msitu na kufanya kazi ya kuuzima kuwa ngumu zaidi.
Alisema mara nyingi mioto hiyo huwashwa na wawindaji, warina asali na wakimbizi wa Kihutu kutoka kambi ya Katumba ambayo iko jirani. Pia alisema wengine wanaowasha mioto hiyo ni wenye kufuata imani za ushirikina kwa madai ya kutabiri urefu wa siku zao za kuishi.
“Mtu akiuguaugua huambiwa na mganga wake nenda kawashe moto… kadri utakavyowaka ndivyo utabaini siku zako za kuishi… ukienda mbali sana na ukiwaka siku nyingi maana yake una maisha marefu zaidi…” alisema huku akishangaa watu wanavyokubali kupotoshwa kirahisi.

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

Links to this post:

Create a Link

<< Home