STATE HOUSE ZANZIBAR OFFICE OF THE PRESS SECRETARY PRESS RELEASE Zanzibar 7.10. 2008 MADAGASCAR imeahidi kuanzisha uhusiano na ushirikiano w...
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 7.10. 2008
MADAGASCAR imeahidi kuanzisha uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar katika sekta za uchumi na kuelezea kufurahishwa na mafanikio yaliopatika Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Amani Abeid Karume.
MADAGASCAR imeahidi kuanzisha uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar katika sekta za uchumi na kuelezea kufurahishwa na mafanikio yaliopatika Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Amani Abeid Karume.
Kauli hiyo imetolewa leo na Rais wa Madagascar Mhe. Marc Ravalomanana wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake Rais Ravalomanana ambaye alifuatana na mkewe pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na ujumbe wake alimueleza Rais Karume kuwa Madagascar iko tayari kuanzisha ushiririkiano na uhusiano kati yake na Zanzibar katika sekta za uchumi ikiwemo utalii na biashara.
Ravalomanana alimueleza Dk. Karume kuwa juhudi zitaanza kufanywa kwa kukaa pamoja kati ya Mawaziri wa nchi mbili hizo kwa kuangalia taratibu za kuanzisha na kuendeleza ushirikiano huo wa kibiashara na utalii.
Alieleza kuwa kutokana na Madagascar na Zanzibar kuwa vyote ni visiwa ambavyo vinazalisha zao la karafuu itakuwa ni jambo la busara kushirikiana kwa pamoja katika kuangalia soko la pamoja hali ambayo itasaidia kuimarisha sekta ya biashara kwa pande zote mbili.
Rais huyo wa Madagacar alieleza kuwa ipo haja ya kukaa pamoja na kuzungumza pamoja kwa mustakabali wa kushirikiana katika kuendeleza na kukuza sekta hizo kwa lengo la kuleta manufaa kwa pande zote mbili.
Aidha, Rais Ravalomanana na Rais Karume walitoa nafasi ya mazungumzo kati ya viongozi wa ujumbe huo na waziri wa Biashara, Utalii na Uwekezaji Mhe. Samia Suluhu Hassan ambao walijadili hapo hapo juu ya kuanza kwa taratibu hizo haraka iwezekanavyo.
Katika majadiliano yao mafupi yaliofanyika hapo hapo Ikulu viongzi hao walifikia makubaliano ya kukutana kati ya Waziri anayeshughulikia masuala hayo wa nchini Madagascar pamoja na Waziri Suluhu kukaa pamoja na kwa lengo la kushirikiana kwa karibu.
Hasa katika suala zima la zao la karafuu. Pia, viongozi hao walieleza namna ya kuanzisha usafiri wa ndege wa moja kwa moja kutoka Madagascar kuja Zanzibar hali ambnayo itazidi kupanua soko la biashara na utalii. Sambamba na hayo, katika mjadala huo kulikubalika kuanza taratibu hizo kabla ya mkutano wa Kimataifa wa Biashara.
Nae Rais Karume alitoa pongezi zake kwa Rais Ravalomanana kwa mashirikiano mazuri anayoyaendeleza ikiwa ni pamoja na azma yake hiyo ya kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi katika sekta za maendeleo. Dk. Karume alisifu mafanikio mbali mbali yaliopatikana katika sekta za maendeleo na uchumi nchini Madagascar na kueleza kuwa kufanikiwa huko kunatokana na juhudi za wananchi na viongozi wao.
Rais Karume alisema kuwa kuna njia nyingi za kushirikiana kati ya Zanzibar na Madagascar ikiwemo biashara, utalii na hata usafiri wa anga kwani usafiri huo wa ndege kutoka Madagascar hadi Zanzibar ulikuwemo mnamo miaka ya sabini.
Alisema kuwa katika sekta ya utalii ipo haja ya kushirikiana zaidi kwa pande mbili hizo kwani tayari Madagascar imeshapiga hatua kubwa katika sekta hiyo ambapo pia Zanzibar hivi sasa nayo inasonga mbele kwa kasi katika kuimarisha na kuendeleza sekta hiyo ambayo ni muhimu.
Sambamba na hayo, Rais Karume alisifu uhusiano na ushirikiano wa nchi mbili hizo ambapo alisema unaweza kuimarika na kutoa mafanikio kwa pande zote mbili na Zanzibar itaendelea kuuthamini na kuutunza.
Rais Ravalomanana akiwa na mkewe walipokelewa na mwenyeji wao Dk. Karume akiwa na mkewe Mama Shadya Karume katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar. Viongozi mbali mbali wa Vyama vya siasa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walifika uwanja wa ndege kumpokea mgeni wao huyo, akiwemo Naibu Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Mhe. Ali Juma Shumuhuna.
Mara baada ya mapokezi hayo kiongozi huyo alifanyiwa taratibu zote za mapokezi wanayofanyiwa viongozi wa Kitaifa wanapofika nchini, Pia kiongozi huyo akiwa na ujumbe wake na pamoja na mkewe waliangalia ngoma za asili kutoka vikundi vya utamaduni vya Zanzibar. Mara baada ya mazungumzo na Dk. Karume, Ravalomanana aliendelea na ziara yake ya siku moja Zanzibar kwa kwa kwenda kuangalia sehemu za kihistoria likiwemo Kanisa la Mkunazini na kupata historia juu ya soko la utumwa na baadae kuelekea Kizimbani kuangalia shamba la viungo na baada ya hapo alirejea Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya chakula kilichotayarishwa kwa ajili yake na ujumbe aliofuatana nao, chakula kilichotayarishwa na mwenyeji wake ambae ni Rais Karume.
mwisho
Pichani Rais wa Madagascar Marc Ravalomanana akisalimiana na watoto baada ya kutembelea Kanisa la Mkunazini mjini Unguja leo ikiwa ni sehemu ya ziara yake nchini. Picha hii ni mali ya Mwanakombo Jumaa.
COMMENTS