RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume amesema kuwa siri ya maendeleo ya Zanzibar tokea mwanzo wa...
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume amesema kuwa siri ya maendeleo ya Zanzibar tokea mwanzo wa awamu yake yametokana na ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato wa maendeleo.
Rais Karume aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Falsafa ya Udaktari wa Sayansi na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki katika sherehe zilizofanyika huko katika viwanja vya Karimjee mjini Dar es Salaam.
Katika sherehe hizo viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali walihudhuria akiwemo Waziri Kiongozi Mhe. Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi Mhe. Ali Juma Shamuhuna, Mama Shadya Karume pamoja na Mawaziri, Mabalozi, Wabunge, Wawakilishi Makatibu Wakuu, Wakuu wa vyuo Vikuu na viongozi wengine. Aidha, viongozi wa ngazi za juu wa vyama mbali mbali vya siasa walihudhuria.
Chama cha CUF kiliwakilishwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad na vingozi wengine wa chama hicho.
Katika hotuba yake kwenye mahafali hayo ya saba ya chuo hicho, Rais Karume alisema kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika nyanja mbali mbali za maendeleo ambapo alisisitiza kuwa serikali pekee isingeweza kuyafanya haya bila ya kuungwa mkono na wananchi.
Alisema kuwa wananchi wameweza kushirikishwa kupitia wajumbe wao katka shughuli zote za utayarishaji wa Mpango wa Kwanza wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA) ambao ulizinduliwa mwaka 2002.
Akieleza juu ya mafaniko yaliopatikana katika sekta ya elimu, Rais Karume alisema kuwa wananchi wameweza kushirikishwa kuanzia ngazi za mashina kupitia Kamati za maendeleo za shehia na Majimbo.
Alisema kuwa wananchi wenyewe wanaanzisha ujenzi wa majengo ya skuli na serikali kukamiliha majenzi, kutoa vifaa na kupeleka walimu sanjari na kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya elimu.
“ Matokeo haya ni kutuwezesha kufikia lengo la Maendeleo la Milenia la uandikishaji watoto wote waliofikia umri wa kuanza darasa la kwanza. Lengo hili limefikiwa kabla ya mwaka 2015 ambapo dhamira yetu hivi sasa ni kuhakikisha kila mtoto wa skuli za msingi anaendelezwa hadi sekondari”, alisema Rais Karume.
Aidha, Rais Karume alisema kuwa anazikubali sifa zote zilizotolewa kwa upande wa huduma za afya lakini aliendelea kusisitiza kuwa mafanikio hayo yote yametokana na ushirikiano wa wananchi wa Zanzibar
Akitolea mfano maniko katika kupunguza Malaria, hadi chini ya asilimia moja, ni matokeo ya wananchi katika kuunga mkono unyunyizahi dawa majumbani mwao na kukubali dawa za mchanganyiko katika kutibu Malaria “Pamoja na hayo tunaishukuru serikali ya Marekani kwa Mpango wake wa ‘Presidetial Malaria Initiative’ na Mfuko wa Dunia (Global Fund) kwa misaada yao mikubwa”,alisema Dk. Karume.
Pia, alieleza kuwa wananchi waliunga mkono na kushiriki katika mpango wa kuzuia matende kwa kula dawa zilizogawiwa nyumba hadi nyumba sanjari na mipango ya kudhibiti ukimwi ambayo inafanikiwa na kuungwa mkono na wananchi hadi kuzuia ukuaji wa maambukizi.
Rais Karume alisema kuwa hali nzuri ya kuwaweesha watu inatokana na kuwepo utawala bora, amani, umoja na usalama wa watu na mali zao na kueleza kuwa Zanzibar katika miaka michache iliyopita imefanya maendeleo katika maeneo hayo.
“Sina wasi wasi kusema kuwa heshima hii leo itapokewa vyema n wananchi kwa sababu ni dhihirisho la kutambuliwa juhudi zao katika kuleta mafanikio ya nchi, mimi binafsi nashajihika na tunzo hii na itaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi katika kuleta maendeleo zaidi ya taifa letu”, alieleza Dk. Karume.
Rais Karume alieleza kuwa chuo cha Habert Kairuki kimefanya maendeleo makubwa tokea kuanzishwa kwake mwaka 1997 a kutoa pongezi kwa Mkuu wa Chuo Dk. Salim Ahmed Salim, Mweyekiti wa Baraza la Wadhamini, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Makamu Mkuu wa Chuo na uongoz wote wa chuo na wanachuo kwa kukiongoza kufikia mafaniki hayo.
Mapema akitoa maelezo kuhusu kutunukiwa Shahada hiyo ya Uzamifu kwa Rais Karume, Mwenyekiti Idara ya Anatomia, Kitivo cha Tiba katika chuo Kikuu hicho, Professa Boniface Msamati alieleza kuwa Dk. Karume ni kiongozi anayejali watu wake na anaehuzunishwa na taabu na matatizo ya watu wengine hususan watoto, wananwake na wazee.
Aidha, alisema kuwa ni kiongozi anaetambua uhalisia wa mambo, ni mpenda kazi na mchakato wake mkubwa kwa Unguja na Pemba unaonekana wazi katika kuendeleza huduma za maendeleo zikiwemo afya, elimu pamoja na miundombinu ya kiuchumi.
Alieleza kuwa Dk. Karume alianza kutafuta misaada kutoka kwa wahisani na kuanzisha na kutekeleza kampeni ya kupiga vita malaria iliyoitwa KATAA MALARIA ambayo mefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Pia, alimpongeza Rais Karume kwa kuanzishwa kwa chuo cha Udaktari cha Zanzibar kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Mantissas cha Cuba.
Rais Karume alieleza kuwa kuwepo kwa viongozi wakuu wa vyama vya upinzani katika sherehe hizo kunadhihirish umoja, maelewano yaliofikiwa wiki iliyopita.
Viongozi wote wa chuo kikuu hicho walimpongeza Rais Karume kwa mafanikio aliyoyapata na kueleza kuwa chuo hicho kimeridhia Dk. Karume atunukiwe Shahada hiyo ya Heshima ya Udaktari ambapo ni mara ya kwanza kwa katika historia ya chuo Kikuu hicho kutoa Shahada ya Heshima ya aina hiyo.
Katika sherehe hizo chuo pia kilitoa zawadi kwa wanafunzi bora.
Rajab Mkasaba Ikulu Zanzibar
Pichani:Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki, Dkt. Salim Ahmed Salim, akimtunuku Shahada ya Heshima ya Uzamifu, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume wakati wa Sherehe ya Mahafali ya 7 ya Chuo hicho yaliyofanyika Dar es Salaam jana. Picha hii ni mali ya Yusuf BADI wa Daily news.
COMMENTS