HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 AGOSTI, 2012 U...
HOTUBA
YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 AGOSTI, 2012
Utangulizi
Ndugu
Wananchi;
Kila mwisho
wa mwezi nimekuwa nazungumza na taifa kuhusu masuala mbalimbali muhimu kwa
taifa letu na watu wake. Leo nina mambo
mawili ya kuzungumza nanyi. Lakini, kama
ilivyo mazoea yetu hatuna budi kwanza tumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wetu,
kwa kutujaalia baraka zake, za uhai na uzima na kutuwezesha kuwasiliana leo
tarehe 31 Agosti, 2012.
Ndugu
Wananchi;
Jambo la
kwanza ninalotaka kuzungumzia leo ni zoezi la Sensa ya Watu na Makazi
lililoanza tarehe 26 Agosti, 2012 ambalo linatarajiwa kumalizika tarehe 01
Septemba, 2012. Mtakumbuka kuwa tarehe
25 Agosti, 2012 nilizungumza nanyi na kuwaomba mjitokeze kwa wingi na muwape
ushirikiano unaostahili Makarani wa Sensa watakapopita majumbani mwenu
kutekekeza wajibu wao. Tumebakisha siku
moja kufikia kilele cha sehemu ya kwanza ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka
2012.
Napenda kuwashukuru
kwa dhati Watanzania wenzangu wote kwa kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa. Mpaka sasa mwelekeo ni mzuri na ugumu
ulioonekana kuwepo pale mwanzoni uliendelea kupungua siku hadi siku kadri
utekelezaji wa zoezi ulivyokuwa unaendelea.
Kwa mwenendo huu nina matumaini makubwa kuwa Sensa ya mwaka huu itakuwa
na mafanikio mazuri.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa wito kwa wale wote ambao hawajahesabiwa wafanye hivyo.
Naomba waitumie siku moja iliyosalia yaani tarehe 1 Septemba, 2012 kufanya
hivyo. Aidha, namuomba Mkurugenzi Mkuu
wa Ofisi Kuu ya Takwimu ya Serikali ya Muungano na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kuwa kasoro zo zote zilizopo mahali po pote
zinatafutiwa ufumbuzi ili mambo yakamilike bila upungufu wowote.
Ndugu
Wananchi;
Baada
ya kazi ya Makarani wa Sensa kuhesabu watu kufikia kilele chake, tarehe 2
Septemba, 2012, linaanza zoezi la kuwashughulikia wale ndugu zetu ambao
watakuwa bado hawajahesabiwa. Itakuwepo
fursa ya siku saba kwa watu hao kuhesabiwa.
Watatakiwa wao wenyewe kupeleka taarifa zao kwa Wenyeviti wao wa
Serikali za Mitaa au Vijiji. Taarifa
hizo zitafikishwa kwa Kamishna wa Sensa kwa ajili ya kujumuishwa. Baada ya muda huo kwisha, zoezi la kuhesabu
watu litakuwa limefika mwisho. Yule
ambaye atakuwa hakutumia fursa hizo mbili atakuwa amekosa kuingizwa katika
hesabu ya Watanzania ya mwaka 2012.
Napenda kuwasihi ndugu zangu, Watanzania wenzangu kutumia siku ya tarehe
1 Septemba, 2012 kuhesabiwa na kama
hapana budi basi tumia fursa ya kupeleka taarifa zako kwa Mwenyekiti wako wa
Mtaa au Kijiji katika siku saba zinazofuatia siku hiyo ili nawe ujumuishwe.
Ndugu
Wananchi;
Baada ya kazi
ya kuhesabu watu kwa namna zote mbili kufikia mwisho, itaanza kazi ya uchambuzi
na kuunganisha takwimu na taarifa zilizokusanywa. Kazi hiyo ni muhimu na ni kubwa hivyo inahitaji
umakini na uangalifu wa hali ya juu sana, kwani ikikosewa zoezi zima la Sensa
litaingia dosari. Nafarijika
kuhakikishiwa na Viongozi wa Sensa na Wakuu wa Idara za Takwimu za Serikali
zetu mbili, kwamba wanatambua ukweli huo na wajibu wao. Wameniarifu kwamba kama mambo yatakwenda kama
ilivyopangwa, matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi kuhusu idadi ya watu
na jinsia zao yatatolewa mwishoni mwa mwaka huu. Taarifa nyingine zitafuata
baadaye. Narejea kuwasihi Watanzania
wenzangu kuwapa nafasi wataalamu wetu wafanye kazi yao kwa ufanisi ili tupate
matokeo yaliyo sahihi.
Mpaka na
Malawi
Ndugu
Wananchi;
Jambo la pili
ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni kuhusu mpaka baina ya Tanzania na Malawi
katika Ziwa Nyasa. Kama mjuavyo, kwa
miaka mingi nchi zetu mbili zinatofautiana kuhusu wapi hasa mpaka uwe. Sisi, Tanzania, tunasema mpaka upo katikati
ya ziwa wakati wenzetu wa Malawi wanasema upo kwenye ufukwe wa ziwa upande wa
Tanzania. Kwa maneno mengine wanasema ziwa
lote ni mali ya nchi yao.
Utata kuhusu mpaka wetu katika Ziwa Nyasa
haujaanza leo. Ulikuwepo tangu wakati
nchi zetu mbili zikiwa bado zinatawaliwa na wakoloni na kuendelea baada ya
Uhuru wa nchi zetu mpaka sasa. Jambo kubwa
lililo tofauti na jipya ni kwamba hivi sasa, nchi zetu mbili zimeamua kukaa
mezani na tunalizungumza suala hilo.
Chimbuko
la Mzozo
Ndugu
Wananchi;
Chimbuko la mzozo wa mpaka uliopo sasa, baina
ya nchi zetu mbili jirani, rafiki na ambazo watu wake ni ndugu, ni makubaliano
baina ya Waingereza na Wajerumani kuhusu mpaka baina ya nchi zetu yaliyofanywa
tarehe 1 Julai, 1890. Makubaliano hayo
yajulikanayo kama Mkataba wa Heligoland, (The Anglo-Germany Heligoland Treaty) yalitiwa
saini kule Berlin, nchini Ujerumani baina ya Waingereza na Wajerumani. Wakoloni hao walikubaliana kuhusu mipaka
baina ya makoloni yao na baina yao na wakoloni wengine waliopakana nao. Kwetu sisi hayo ndiyo makubaliano yaliyoweka
mipaka ya Tanganyika na ile ya Zanzibar na majirani zake. Kwa upande wa Ziwa Nyasa, Waingereza na
Wajerumani walikubaliana kuwa mpaka uwe kwenye ufukwe wa nchi yetu. Kwa maana hiyo ziwa lote likapewa nchi ya
Malawi. Kwa upande wa Mto Songwe mpaka
ulikuwa ufukweni upande wa Malawi kwa maana hiyo mto wote ukawa upande wa
Tanzania.
Ndugu Wananchi;
Katika kipengele cha Sita (Article VI) cha
Mkataba huo, wakoloni hao walikubaliana kufanya marekebisho ya mpaka mahali po pote
kama itakuwa ni lazima kufanya hivyo, kulingana na mazingira na hali halisi ya
mahali hapo. Kwa mujibu wa kutekeleza
matakwa ya kipengele hicho mwaka 1898 Tume ya Mipaka iliundwa. Ilianzia kazi katika Mto Songwe kuhakiki
mpaka baina ya nchi yetu na Malawi. Tume ilikubaliana kuhamisha mpaka kutoka
ufukweni mwa Mto Songwe upande wa Malawi na kuwa katikati ya mto. Baada ya uhakiki katika eneo hilo kukamilika,
mwaka 1901 mkataba mpya ulisainiwa kuhusu mpaka huo.
Tume iliendelea
na kazi yake katika Ziwa Tanganyika na kuhamisha mpaka kutoka ufukweni hadi
katikati ya ziwa na mkataba mpya kusainiwa mwaka 1910. Tume iliendelea katika ziwa Jipe ambapo mpaka
ulihamishwa pia hadi katikati ya ziwa.
Ndugu Wananchi;
Bahati mbaya Tume hiyo haikufanikiwa kufanya
uhakiki wa mpaka katika Ziwa Nyasa kutokana na kutokea kwa Vita Kuu ya Kwanza
ya Dunia kati ya mwaka 1914 - 1918. Kama
tunavyokumbuka, Waingereza na Wajerumani waligeuka kuwa maadui na kupigana hata
hapa nchini. Baada ya vita hivyo na
Ujerumani kushindwa, Baraza la Umoja wa Mataifa (The League of Nations)
liliikabidhi Uingereza udhamini wa Tanganyika. Hivyo, Uingereza ikawa inatawala
Malawi na Tanganyika.
Ndugu Wananchi;
Wakati Tume ya Uingereza na Ujerumani
ilipokuwa imekufa, Tume ya Mipaka kati ya Uingereza na Ureno iliendelea na
kazi. Matokeo yake, mwaka 1954,
Uingereza na Ureno zilitengua mkataba wao wa mwaka 1891 ulioweka mpaka wa Ziwa
Nyasa katika ufukwe wa mashariki ya Ziwa, yaani kwenye ufukwe wa Msumbiji, na
kuuhamishia katikati ya ziwa.
Ndugu Wananchi;
Jambo la kustaajabisha ni kuwa, Waingereza
walioona umuhimu na busara ya kurekebisha mpaka kati ya Malawi na Msumbiji,
hawakuona umuhimu wa kufanya hivyo kati ya nchi yetu na Malawi. Inashangaza, kwa sababu wakati huo Uingereza
ilikuwa mtawala wa nchi zetu mbili hivyo kazi ya marekebisho ingekuwa rahisi,
lakini hawakufanya hivyo. Na, baya zaidi
ni kuwa hata pale watu wa nchi yetu walipotaka
kupatiwa ufafanuzi na kutaka ukweli uwekwe wazi kuhusu mpaka hawakusikilizwa. Watu walitaka ufafanuzi kwa sababu
inasemekana kati ya mwaka 1925 na 1938, taarifa ya Uingereza kwa Umoja wa Mataifa
ziliweka mpaka katikati ya ziwa. Lakini,
kuanzia mwaka 1948 mpaka ukawekwa tena ufukweni.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 1959, 1960 na 1962, suala la mpaka wa
Malawi lilijitokeza tena na kujadiliwa na Bunge la Tanganyika, wakati ule
lilijulikana kuwa Baraza la Kutunga Sheria, (Legislative Council – LEGCO). Hoja ya Wabunge wa Tanganyika ilikuwa kwamba mpaka
kuwekwa kwenye ufukwe wetu kunawanyima wananchi wa Tanganyika wanaoishi kando
kando ya ziwa haki yao ya msingi ya kutumia maji kwa kunywa, kuoga, kuvua samaki
na kupata manufaa mengine yatokanayo na ziwa bila ya kuomba ridhaa ya Serikali
ya Koloni la Nyasaland kama Malawi ilivyokuwa inajulikana wakati ule. Hoja iliyotolewa ilikuwa kwamba Serikali ya
Tanganyika ijadiliane na Serikali ya Nyasaland kupitia Serikali ya Malkia wa
Uingereza ili ufumbuzi upatikane. Wakoloni
hawakujali na wala hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka Tanganyika ikapata uhuru
wake tarehe 9 Desemba, 1961 na Malawi kupata uhuru wake mwaka 1964.
Juhudi
za Kubadili Mpaka wa Ziwa Nyasa Baada ya Uhuru
Ndugu
Wananchi;
Wakati
tulipopata Uhuru mwaka 1961, mjadala kuhusu mpaka wa Tanganyika na Malawi
uliendelea Bungeni, ambapo ilitolewa hoja kwamba zifanyike juhudi za makusudi
za kuanzisha na kuendeleza mazungumzo ya kurekebisha mpaka huo kwa manufaa ya
wananchi wote wanaoishi pembezoni mwa ziwa.
Iliamuliwa kwamba tusubiri mpaka wenzetu wa Malawi wapate uhuru ili yafanyike
mazungumzo baina ya nchi mbili huru.
Kulijengeka matumaini kuwa mambo yangekuwa rahisi. Bahati mbaya haikuwa hivyo na kwamba mambo
yakageuka na kuwa magumu na ya uhasama. Miaka
mitatu baada ya Malawi kupata Uhuru wake (1964), kunako tarehe 3 Januari 1967,
Serikali ya Tanzania iliandika barua kwa Serikali ya Malawi kuelezea tatizo la mpaka
wa ziwani na kupendekeza nchi zetu mbili zizungumze na kulitafutia
ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri tarehe 24 Januari, 1967,
Serikali ya Malawi ikajibu kukiri kupokea barua hiyo na kuahidi kuwa itatoa
majibu baada ya muda si mrefu. Hata
hivyo, tarehe 27 Juni, 1967, Rais Kamuzu Banda akilihutubia Bunge la Malawi, alikataa
maombi ya Tanzania. Alisema hayana
msingi na alidai kuwa kihistoria Songea, Mbeya na Njombe ni sehemu ya
Malawi. Hivyo basi, mazungumzo yakafa.
Tanzania haikukata tamaa. Alipochaguliwa Rais wa Pili wa Malawi, Mheshimiwa
Bakili Muluzi, juhudi zilifanyika lakini nazo hazikufika mbali. Bahati nzuri
tarehe 9 Juni, 2005, Rais wa Tatu wa Malawi, Mheshimiwa Bingu Wa Mutharika,
ambaye sasa ni marehemu, alimuandikia barua aliyekuwa Rais wa nchi yetu wakati
ule, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, kushauri nchi zetu zifanye mazungumzo
kuhusu mpaka wa ziwani. Alipendekeza iundwe
Tume ya Pamoja itakayojumuisha Mawaziri na Wataalamu kutoka nchi zetu
mbili. Tume hiyo itatoa mapendekezo kwa
Marais wa nchi zetu mbili ambayo yatakuwa msingi wa majadiliano baina yao. Alisisitiza umuhimu wa kulipatia ufumbuzi
suala hilo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuwa ilikuwa kipindi cha mpito kuelekea
kuchaguliwa Serikali ya Awamu ya Nne, Rais Benjamin Mkapa hakuwahi
kuishughulikia barua hiyo. Nilipoletewa barua hiyo nikaijibu kukubali ushauri
na mapendekezo yake. Aidha, nilipendekeza
Wizara na Idara zipi za Serikali zetu zishirikishwe katika Tume hiyo. Bahati nzuri Rais wa Malawi alikubali
mapendekezo yangu pamoja na lile la kwamba Malawi waitishe mkutano wa kwanza wa
Tume hiyo.
Ndugu Wananchi;
Mpaka sasa mikutano mitatu ya Tume ya Pamoja imeshafanyika,
wa kwanza ulifanyika tarehe 8 – 10 Septemba, 2010. Mkutano wa pili ukafanyika tarehe 27 – 28
Julai, 2012 hapa Dar es Salaam na wa tatu ukafanyika Mzuzu na Lilongwe tarehe
20 – 27 Agosti, 2012. Hatua kadhaa zimepigwa lakini bado muafaka haujapatikana
kwa maana ya madai yetu ya kutaka mpaka uwe katikati ya ziwa na madai yao kuwa
mpaka ubaki ufukweni kwetu kama ilivyo kwenye
Mkataba wa Heligoland wa Julai 1, 1890.
Hoja ya wenzetu ni kuwa huo ndiyo mpaka tuliorithi wakati wa uhuru. Wanataka tuthibitishe hivyo na kwamba tuzingatie
kauli ya OAU ya kuheshimu mipaka tuliyorithi kwa wakoloni. Wananukuu kauli ya
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akisisitiza hoja hiyo katika mkutano wa
OAU mwaka 1963.
Hoja
za Msingi za Kutaka Mpaka Uwe Katikati ya Ziwa
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wetu tumekuwa na hoja kadhaa za
kutaka mpaka uwe katikati ya ziwa. Ya msingi
kabisa ni ukweli kwamba Mkataba wa Heligoland umekosewa kwa kuamua kuwanyima
wananchi wa Tanzania wanaoishi ufukweni mwa ziwa haki yao ya msingi ya kutumia
maji na rasilimali zilizomo katika Ziwa Nyasa.
Zipo sababu kadhaa kwa upande wetu kudai hivyo. Mojawapo ni sheria ya kimataifa inayoelekeza kwamba
po pote kwenye maji ya asili kama vile ziwa na mito iliyopo kati ya nchi mbili
mpaka huwa katikati. Ndiyo utaratibu
unaotumika duniani kote, na mifano iko tele.
Kwa nini iwe tofauti katika ziwa Nyasa na kwa upande wa Tanzania tu
wakati kwa upande wa Msumbiji mpaka upo katikati ya ziwa?
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mto Songwe, mpaka baina ya nchi
zetu mbili upo katikati. Iweje hapa
kanuni hiyo itambulike na kuheshimiwa lakini isiwe hivyo ziwani? Kama nilivyoeleza awali, mwanzoni Mto Songwe wote
ulikuwa umewekwa upande wetu, lakini Tume ya Mipaka iliyoundwa mwaka 1898
ilifanya marekebisho na kuweka mpaka katikati ya mto. Kama nilivyokwishagusia kwenye ziwa hilo hilo
la Nyasa kwa upande wa Msumbiji mwaka 1954 mkataba wa mwaka 1891 ulioipa Malawi
ziwa lote ulirekebishwa na mpaka kuwekwa katikati. Kwa nini isifanyike hivyo hivyo kwa upande wa
Tanzania? Hivi hasa ni kipi ambacho
wenzetu wa Msumbiji walichotuzidi na kustahili kupata haki yao ya msingi ya kumiliki
na kutumia maji ya Ziwa Nyasa ambacho sisi Tanzania tumepungukiwa?
Ndugu Wananchi;
Maji ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu
wake, waitumie kwa uhai na maendeleo yao.
Iweje leo, kwa watu wanaoishi pembeni mwa ziwa hilo hilo wengine wapewe
na wengine wanyimwe haki ya kulimiliki na kulitumia? Kwa nini wanyimwe haki ya kunufaika
na zawadi hiyo? Hivi kauli ya wakoloni waliokaa Berlin ya kusema fulani apate
na fulani asipate inatosha? Hivi kweli ni
rahisi kiasi hicho?
Mpaka wa kwenye maji ni tofauti na ule wa
nchi kavu. Huu una rasilimali ambayo huwezi
kuamua kumnyima mwanadamu mwingine anayeishi pembeni yake kwa vile haina badala
yake. Unapowaambia watu wa Mbamba Bay,
Liuli, Lituhi, Manda, Ngonga, Matema, Mwaya, Itungi na wengineo waishio kando
ya ziwa kuwa maji hayo si yao bali ni mali ya Malawi hawakuelewi na
watakushangaa sana. Watadhani
umechanganyikiwa kwani tangu waumbwe wamekuwepo hapo wanamiliki na kutumia maji
ya Ziwa. Unataka wafanyeje? Waende Malawi kuomba kibali cha
kuyatumia? Wao watakuuliza swali moja
tu “hivi hao wenzao wanaoishi ng’ambo ya pili wamewazidi nini katika ubinadamu
wao hata wapewe maji yote na wao wanyimwe?”
Ndugu Wananchi;
Kwa maana halisi ya Mkataba wa Heligoland
tangu tarehe 1 Julai, 1890, wananchi wa upande wa Tanzania wamekuwa wanakunywa,
kuoga, kuvua samaki na kusafiri katika maji ya Ziwa yasiyokuwa yao bali ya nchi
nyingine. Na kwa kuwa wamekuwa wanafanya
hivyo bila ya kupata kibali cha Malawi wamekuwa wanaiba maji na samaki wa
Malawi na kusafiri isivyo halali katika nchi ya watu. Jambo hili haliingii akilini hata kidogo. Ndiyo maana tunadai haki yetu stahili.
Ndugu Wananchi;
Na
hiyo pia, ndiyo maana, busara na hekima
ya Sheria ya Kimataifa kuhusu mpaka wa kwenye
maji kuwa katikati. Sheria hii inazingatia
hali halisi ya maisha ya jamii inayozunguka ziwa ambayo imekuwa inalitegemea maisha
yao yote kwa shughuli zao za kuwapatia uhai na maendeleo yao. Haiwezekani kuwatenganisha watu waishio kando
ya Ziwa Nyasa kumiliki na kutumia maji hayo na rasilimali zake. Hawataelewa wala kukubali kuambiwa kuwa wanatumia
maji na rasilimali za ziwani kwa hisani
ya nchi ya Malawi.
Kwa watu waliokuwepo tangu Mungu anawaumba
wao na wenzao wa ng’ambo ya pili, siyo sawa na siyo haki hata kidogo kuwafanyia
hivyo. Kwe kweli ni unyanyasaji wa hali
ya juu. Ndiyo maana wazee wetu walidai
suala hili liwekwe sawa wakati wa ukoloni, kabla na baada ya Uhuru. Na ndiyo maana na sisi tunafuata nyayo zao
katika madai haya ya haki.
Ndugu Wananchi;
Kuna mambo mengine mawili ambayo yanatufanya
tudai haki ya kumiliki na kutumia Ziwa Nyasa.
La kwanza ni ule ukweli kwamba mito mingi ya Tanzania nayo inachangia
kujaza maji katika ziwa. Iweje leo maji yanayojaza
ziwa ni jambo jema, lakini yakishaingia ziwani, ziwa hilo si mali yao wenye
mito hiyo tena na wakiyatumia wanaiba mali ya watu wengine. Hivi kweli
ndivyo wanavyostahili kufanyiwa watu wanaotunza vyanzo vya mito hiyo na kuruhusu
maji yake kutiririka na kuingia ziwani?
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kwamba mpaka wa Tanzania na
Malawi kuwa ufukweni kunafanya ukubwa wa nchi zetu kuwa haujulikani kwa
uhakika. Unategemea mabadiliko kutokana
na kujaa na kupungua kwa maji
ziwani. Kunafanya mpaka wa nchi kuwa
hautabiriki na unaweza kuwa tatizo siku moja mbele ya safari. Isitoshe kuwa na nchi isiyojulikana ukubwa
wake nalo ni tatizo la aina yake. Ndiyo
maana mpaka kuwa katikati ya ziwa ni bora zaidi.
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyokwishasema, chimbuko la mzozo huu
ni mkataba wa Heligoland ambao umepanda mbegu ya fitina baina ya nchi
zetu. Bahati mbaya sana Tume ya Mipaka
haikumaliza kazi ya kuhakiki mipaka yote ya nchi yetu na majirani zake kufuatia
kuzuka kwa Vita Kuu ya Kwanza mwaka 1914.
Ujerumani ikashindwa vita na koloni lake kuwa sehemu ya himaya ya
Uingereza. Bahati mbaya kwetu Waingereza
waliotawala nchi zetu mbili tangu 1918 hawakuchukua hatua za kurekebisha mpaka
kabla ya uhuru wa nchi zetu. Ni maoni yetu
kuwa nchi zetu sasa zifanye kile ambacho hakikufanywa na Tume ya Mipaka ya wakoloni
– Waingereza na Wajerumani. Tukifanye
sisi wenyewe kama nchi mbili huru kwa njia ya mazungumzo.
Bahati mbaya majaribio ya mwaka 1967
hayakufanikiwa. Bahati nzuri kufuatia
uamuzi wa kijasiri wa marehemu Rais Bingu wa Mutharika nchi zetu sasa zinazungumza. Bado hatujafikia muafaka kuhusu kurekebisha
mpaka na huenda ikatuwia vigumu kufikia muafaka. Jambo linaloleta faraja, hata hivyo, ni kuwa
sote wawili tumekubaliana kuwa tutafute mtu wa kutusuluhisha.
Ndugu Wananchi;
Hayo ndiyo matokeo ya mazungumzo ya Tume yetu
ya pamoja tangu ngazi ya Wataalamu, Makatibu Wakuu mpaka kwa Mawaziri, katika
vikao vya Mzuzu na Lilongwe kati ya tarehe 20 – 27 Agosti, 2012. Katika mkutano wao wa tarehe 27 Agosti, 2012
Mawaziri husika wa nchi zetu chini ya uongozi wa pamoja wa Waziri wa Mambo ya
Nje wa Malawi, Mheshimiwa Ephraim Chiume na mwenzake wa Tanzania, Mheshimiwa
Bernard Membe, wameafiki mapendekezo hayo.
Aidha, wamekubaliana kuwa pande zote mbili wakutane tena Dar es Salaam
kati ya tarehe 10 – 15 Septemba, 2012 kukubaliana juu ya usuluhishi wa aina
gani unafaa.
Ndugu Wananchi;
Mtakubaliana
nami kuwa tumepiga hatua muhimu kuelekea kwenye kupata ufumbuzi wa kudumu wa
suala hili. Hata hivyo, bado safari ni
ndefu na huenda ikawa na magumu mengi.
Maombi yangu kwa viongozi na wananchi wa Tanzania na Malawi ni kuendelea
kuunga mkono jitihada hizi. Tuwaunge
mkono wataalamu na Mawaziri wetu ili wafanikishe vizuri jukumu lao. Tuzingatie na kuheshimu walichokubaliana
Lilongwe kuwa viongozi na wananchi wa nchi zetu wajiepushe na kutoa kauli au
kufanya vitendo vinavyoweza kuchafua hali ya hewa, kuleta uchochezi na kuathiri
majadiliano yanayoendelea.
Nawasihi Watanzania wenzangu kuzingatia
ushauri na rai hiyo ya Mawaziri na wataalamu wetu, ili kuwe na mazingira mazuri
ya mazungumzo na kuwezesha mzozo huu kuisha kwa amani na kirafiki.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda
kusisitiza kuwa si makusudio yangu wala ya Serikali yetu kutafuta suluhisho la
suala hili kwa nguvu ya kijeshi. Nawahakikishia
Watanzania wenzangu kuwa hatuko vitani na Malawi na wala hakuna maandalizi ya vita
dhidi ya jirani zetu hawa kwa sababu ya mzozo wetu wa mpaka katika Ziwa. Ondoeni hofu na endeleeni na shughuli zenu za
ujenzi wa taifa letu kama kawaida.
Nilimhakikishia hivyo Rais wa Malawi,
Mheshimiwa Joyce Banda nilipokutana naye Maputo, Msumbiji tarehe 18 Agosti,
2012. Tanzania haina mpango wa kuingia
vitani na Malawi. Mimi na wenzangu
Serikalini tunaona kuwa fursa tuliyoitafuta miaka mingi ya kukaa na ndugu zetu
Malawi kuzungumzia suala hili lenye maslahi kwetu sote sasa tumeipata. Hatuna budi kuitumia ipasavyo. Naamini, tukifanya hivyo, inaweza kutufikisha
pale tunapopataka. Ni muhimu, kwa ajili hiyo kwa pande zetu mbili, kuipa fursa
ya mazungumzo nafasi ya kuendelea bila ya vikwazo visivyokuwa vya lazima.
Ndugu Wananchi;
Kwa sababu hiyo
basi , napenda kutumia nafasi hii kuwasihi ndugu zetu wa vyombo vya habari na
wanasiasa wenzangu tuepuke kauli au matendo yatakayovuruga mazungumzo na
kuchochea uhasama kati ya nchi zetu mbili jirani na rafiki. Kuna manufaa makubwa ya kumaliza mzozo wetu
kwa njia ya mazungumzo kuliko kwa njia ya vita.
Kufikiria sasa kutumia njia nyinginezo hasa za nguvu za kujeshi, si
wakati wake muafaka. Aidha, tukitumia
njia ya vita, badala ya kuwa tumepata suluhisho inaweza kuwa ndiyo mwanzo wa
mgogoro mpana zaidi. Tuendelee kuwaunga
mkono wawakilishi wetu katika Tume yetu ya pamoja. Naahidi, Serikali itakuwa inawapa taarifa
kadri mazungumzo yetu na wenzetu wa Malawi yatakavyokuwa yanaendelea. Nina hakika tutamaliza salama.
Mungu
Ibariki Tanzania!
Mungu
Ibariki Afrika!
Asanteni
kwa Kunisikiliza
COMMENTS