NAIBU Waziri wa Kazi na Ajira, Dr. Makongoro Mahanga ameshauri vyuo vya elimu ya juu kurekebisha mitaala yao ili kukazania zaidi mas...
NAIBU Waziri wa Kazi na Ajira, Dr. Makongoro Mahanga ameshauri vyuo vya elimu ya juu kurekebisha mitaala yao ili kukazania zaidi masomo ya hisibati na sayansi, na pia kuhakikisha kwamba kwenye kila fani au program katika vyuo hivyo, kunakuwepo na masomo ya ujasiriamali na stadi za maisha ili kuwaandaa wahitimu kujiajiri kama hawatapata kazi za kuajiriwa. Aidha ameshauri kwamba, kama ilivyofanywa kwa fani ya ualimu, kuwepo na program au shahada mahsusi ya ujasiriamali katika kila chuo cha elimu ya juu.
Dr. Mahanga ametoa ushauri huo jana mjini Mtwara alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mtwara, viongozi na wahitimu katika chuo kishiriki cha Stella Maris kilichoko Mtwara na kinachomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Alisema sababu kubwa ya baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu kukosa ajira ni pamoja na vijana hao kutotaka au kuweza kuchukua masomo ya sayansi na hisibati na pia kutotaka kuchukua fani kama ya ualimu ambazo zina fursa za uhakika za ajira. Aidha, alisema sera na mitaala ya elimu haijazingatia sawasawa mahitaji ya soko la ajira. Alisema sababu nyingine ni ukosefu wa nafasi za kujifunza elimu ya ufundi, ujasiriamali na stadi za kazi au kufanya mazoezi ya stadi za kazi ili kupata ujuzi wa aina ya ajira nzuri kwenye soko la ajira. Hivyo kuanzisha masomo au shahada ya ujasiriamali kwenye vyuo vikuu vyote ingeweza kuwa suluhisho la wahitimu wengi kukosa ajira. Alisema kwa sasa kati ya vijana zaidi ya 800,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka baada ya kumaliza elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu, vijana 240,000 hawapati ajira kabisa na baadhi yao ni wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu.
> >>
> >> Dr. Mahanga, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ya kwanza ya chuo hicho ambacho ni chuo kishiriki cha Chuo Kikuu cha St. Augustine cha Mwanza, aliwataka pia wahitimu wanaokopeshwa na Bodi ya Mikopo ya wanafunzi kurejesha mikopo hiyo wakishaanza kufanya kazi. Akitoa takwimu za mikopo ya wanafunzi, alisema kwa miaka 18 kuanzia mwaka 1994/95 ambapo mikopo hiyo ilianza kutolewa kwa wanafunzi hadi Juni 2012, Serikali imeshatoa mikopo ya shs. 1.184 trilioni kwa wanafunzi 593,712. Hata hivyo alisema kati ya mikopo ilioiva na kustahili iwe imesharudishwa na wahitimu waliokopa ni asilimia 49% tu imeshalipwa kwa Bodi.
HOTUBA CHINI
HOTUBA YA MHE. DKT. MILTON MAKONGORO MAHANGA (MB), NAIBU WAZIRI WA KAZI NA AJIRA KWENYE MAHAFALI YA KWANZA YA CHUO KIKUU CHA STELLA MARIS MTWARA (STEMMUCO), TANZANIA TAREHE 5 DESEMBA, 2012
Mhashamu Baba Askofu Mkuu, Norbet Mtega – Mkuu wa Chuo,
Mhashamu Baba Askofu Gabriel Mmole, Askofu wa Jimbo la Mtwara na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo,
Mhashamu Baba Askofu John Ndimbo, Askofu wa Jimbo la Mbinga na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo,
Mhashamu Baba Askofu Bruno Ngonyani, Askofu wa Jimbo la Lindi,
Mhashamu Baba Askofu Castor Msemwa, Askofu wa Jimbo la Tunduru Masasi,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara,
Waheshimwa Wakuu wa Vyuo na Taasisi za Elimu,
Mabibi na Mabwana.
Tumsifu Yesu Kristu!
Ni heshima kubwa kwangu binafsi na kwa Serikali kwa ujumla kunipa mwaliko wa kuwa Mgeni Rasmi katika tukio hili la kihistoria, tukio la mahafali ya kwanza ya Chuo hiki Kishiriki cha Stella Maris hapa Mtwara.
Kwa kunialika kushiriki tukio hili, ni ishara wazi inayoonyesha ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Taasisi hii katika suala zima la kutoa elimu kwa Watanzania – elimu inayowajengea wahitimu uwezo kiujuzi, kiuelewa, kiutaalam, kimitazamo na kimaamuzi ili waweze kushiriki kwa vitendo kuleta maendeleo halisi ya Taifa letu.
Waheshimiwa Maaskofu, Mabibi na Mabwana,
Umuhimu wa elimu katika maendeleo ya taifa lolote haliwezi kusisitizwa zaidi. Nchi zote ambazo zimeendelea kwa haraka duniani zimewekeza katika elimu ya watoto na vijana wake. Tanzania vile vile imekuwa ikiwekeza kiasi kikubwa cha bajeti yake katika sekta ya elimu na kuipa kipaumbele cha kwanza kila mwaka. Kwa mfano, katika mwaka 2010/11 Serikali ya Tanzania ilitenga shs. 2.195 trilioni kwa ajili ya sekta ya elimu, hii ikiwa ni asilimia 18.9% ya bajeti nzima ya Serikali. Kwa mwaka 2011/12, Serikali ilitenga shs. 2.415 trilioni kwa ajili ya sekta ya elimu (asilimia 17.86%).
Kwa kushirikiana na watu binafsi na Taasisi mbalimbali likiwemo Kanisa Katoliki, Serikali inatilia maanani umuhimu wa kutoa elimu bora kwa raia. Serikali imekuwa inafuatilia kwa makini kupitia Tume na vyombo vyake vingine, utoaji wa elimu iliyo bora, elimu yenye kumkomboa mwanadamu na kumpa uwezo wa kuyatawala na kuyaboresha mazingira yake. Kwa misingi hiyo, kwa niaba ya Serikali, natoa shukrani zangu za dhati kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa ushiriki wake wa kutoa elimu bora ya ngazi zote tangu elimu ya awali hadi elimu ya juu. Ushiriki wa Kanisa katoliki na taasisi zingine za kidini na watu binafsi katika fani ya elimu umechangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo ya Taifa letu.
Wakati ambapo kufikia mwisho wa mwaka 2010/11 vyuo vya elimu ya juu vilikuwa na jumla ya wanafunzi 139,638, vyuo vya Serikali vilikuwa na wanafunzi 104,129 huku vyuo binafsi vikiwa na wanafunzi 35,509. Hata hivyo vyuo vya elimu ya juu vya Serikali vilikuwa 11 tu kulinganisha na 21 vya binafsi. Hii ina maana kwamba vyuo binafsi vilikuwa vingi (65.6%) kulinganisha na vya Serikali (34.4%) lakini viliweza kudahili wanafunzi asilimia 25.4% tu. Kwa maana hiyo kuna haja ya vyuo binafsi kupanua miundombinu ya vyuo vyake na udahili ili viweze kuchukua wanafunzi wengi zaidi.
Maaskofu, Mabibi na Mabwana,
Ikijua na kujali umuhimu na mchango wa vyuo binafsi, Serikali, kupitia Tume yake ya Vyuo Vikuu (TCU), mnamo Desemba 2009, iliruhusu Taasisi hii ianze kutoa elimu ya juu kama kituo cha chuo kikuu cha SAUT. Miaka miwili baadaye, yaani Julai, 2011 Serikali iliipandisha hadhi Taasisi hii na kuifanya Chuo Kikuu Kishiriki.
Ikitambua uwezo mdogo wa kiuchumi wa Watanzania, Serikali kupitia Bodi yake ya mikopo imekuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wenye vigezo vinavyotakiwa. Kwa miaka 11 toka mikopo hii ianze kutolewa mwaka 1994/95 hadi 2004/2005, jumla ya wanafunzi 113,240 waliweza kukopeshwa jumla ya shilingi 51,103,687,000. Lakini kwa miaka saba ya awamu ya nne ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kutoka mwaka 2005/06 hadi 2011/12, Serikali, kupitia Bodi ya Mikopo iliyoundwa mwaka 2005, ilikopesha wanafunzi 480,472 jumla ya shs. 1,133,386,869,000.
Mabibi na Mabwana,
Kama ilivyoelezwa hapa leo, chuo hiki pia kilifaidika na mikopo hii ambapo asilimia 94% ya wahitimu wake wamewezeshwa kwa njia ya mikopo hiyo. Aidha kupitia Serikali za Mitaa hapa Mtwara-Mikindani, Serikali imetoa ardhi takribani ekari 140 kwa ajili ya maendeleo ya chuo hiki. Haya yote yanaonyesha jinsi Serikali yetu inavyojali watu wake katika masuala ya elimu. Kwa niaba ya Serikali nawaahidi kwamba ushirikiano huu utaendelea kudumishwa.
Inafurahisha na kutia moyo kuwa Chuo hiki kiliona ni vema kuanza kazi yake Mkoani Mtwara kwa kuandaa walimu wa sekondari. Tunda la kwanza la chuo ni walimu walioandaliwa kutoa elimu ya Sekondari. Elimu hii itachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo ya watanzania tukizingatia kuwa zipo shule nyingi za sekondari zenye idadi ndogo ya walimu. Tukianzia na Mikoa ya Kusini, mmejionea wenyewe uhaba wa walimu uliopo. Ninawahimiza wahitimu wa leo wawe tayari kuitumia elimu yao kuchangia kuleta maendeleo ya watanzania.
Mabibi na Mabwana,
Ukosefu wa ajira bado ni tatizo kubwa nchini, hasa kwa vijana. Kati ya vijana wapatao 800,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka baada ya kumaliza masomo ya msingi, sekondari na vyuo vya juu, ni asilimia kama 5 tu (au vijana 40,000) ndio wanapata ajira kwenye sekta rasmi isiyo ya kilimo. Waliobaki wanaingia kwenye ajira kwenye sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi (asilimia 35) na sekta isiyo rasmi (aslimia 30), huku asilimia 30 waliobaki (vijana 240,000) wakikosa kazi. Kati ya vijana wanaoingia kwenye soko la ajira na kukosa kazi, wako pia wahitimu wa vyuo vikuu.
Sababu kubwa ya baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu kukosa ajira ni pamoja na vijana hao kutotaka au kuweza kuchukua masomo ya sayansi na hisibati na pia kutotaka kuchukua fani kama ya ualimu ambazo zina fursa za uhakika za ajira. Aidha, sera na mitaala ya elimu haijazingatia sawasawa mahitaji ya soko la ajira. Na pia kuna ukosefu wa nafasi za kujifunza elimu ya ufundi, ujasiriamali na stadi za kazi au kufanya mazoezi ya stadi za kazi ili kupata ujuzi wa aina ya ajira nzuri kwenye soko la ajira.
Ningependa kutoa wito kwa vyuo vya elimu ya juu kurekebisha kasoro hizi kwa kutilia maanani masomo ya hisibati na sayansi, na pia kuhakikisha kwamba kwenye kila fani au program katika vyuo vikuu vyote, kunakuwepo na masomo ya ujasiriamali na stadi za maisha ili kuwaandaa wahitimu kujiajiri kama hawatapata kazi za kuajiriwa. Aidha ningeshauri kwamba, kama ilivyofanywa kwa fani ya ualimu, kuwepo na program au shahada mahsusi ya ujasiriamali (Bachalor of Business Administration/Management in Entreprenuership) katika kila chuo cha elimu ya juu. Nimeona kwamba ingawa leo wahitimu wa chuo hiki ni wa fani ya ualimu mlioanza nayo, lakini kwa sasa mmeshaanzisha program za shahada zingine hapa chuoni. Angalieni pia uwezekano wa kuanzisha shahada ya ujasiriamali katika mipango yenu ya baadaye.
Waheshimiwa Maaskofu, Mabibi na Mabwana,
Kabla sijamaliza hotuba yangu, nitoe wito kwa wenzetu 1,100 wanaohitimu leo katika chuo hiki cha Stella Maris kama ifuatavyo:-
• Uadilifu kazini: Wahitimu mmefundishwa sio tu kuwa walimu bali walimu-walezi. Serikali inawatazamia kuwa mifano bora kazini kwa kuyaishi maadili ya kazi yenu. Epukeni upendeleo, rushwa na unyanyasaji. Fanyeni kazi kwa haki na ueledi wa hali ya juu.
• Utayari wa kurudisha pesa ya mikopo: Mmesoma kwa pesa ya mikopo. Kumbukeni kulipa madeni ili wakopeshwe wengine. Tatizo la wahitimu wa vyuo vikuu kurudisha mikopo waliokopeshwa bado ni kubwa. Kwa mfano, kufikia Juni 2012, madeni ya wahitimu wa vyuo vya juu yaliyokuwa yameiva yalikuwa Tshs. bilioni 160.7 na kati yake, shs. 39.5 bilioni zilitakiwa ziwe zimeshakusanywa kutoka kwa waliokopa, lakini ni asilimia 49% tu kati ya hizo zilikuwa zimekusanywa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi
• Maslahi Binafsi: Katika kazi zenu za ualimu lazima mtangulize maslahi ya wengi na wala si maslahi binafasi
• Migomo na Vurugu: Ni muhimu mkaepuka migomo na vurugu kazini. Pale migogoro inapotokea, ni lazima mtafute suluhisho za migogoro kwa mazungumzo na pande zote zinazohusika.
• Utayari wa kufanya kazi popote bila kubagua maeneo: Fanyeni kazi popote nchini bila kupendelea mijini au maeneo ya nyumbani kwenu. Katika risala ya chuo mmeeleza jinsi imekuwa vigumu wahitimu kufanya kazi kwenye maeneo fulani ya nchi, kwa mfano katika mikoa hii ya kusini ikiwemo Mtwara na Lindi. Kwanza sitegemei wahitimu wa chuo hiki hapa Mtwara baada ya kuzoea mazingira ya mkoa huu na ya jirani walipokuwa wakisoma, wakashindwa kufanya kazi huku baada ya kumaliza masomo yao. Lakini pia nyie wenyewe ni mashahidi kwamba Serikali imekuwa ikichukua hatua za makusudi kuboresha hali ya maisha na miundombinu ya mikoa iliyokuwa inaonekana iko nyuma kimaendeleo kama Mtwara ili wananchi wa mikoa hii na watanzania wengine wanaopangwa kufanya kazi kwenye mikoa hii wasione tofauti kubwa na mikoa mingine.
Kwa upande wa Mtwara na mikoa mingine ya kusini, ukiacha uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya barabara, umeme na bandari, kumekuwepo vile vile uwekezaji kwenye miradi ya kiuchumi kama utafiti na uchimbaji wa gesi asilia, utafiti wa mafuta na viwanda kadhaa kama vya saruji na mbolea vinavyotarajiwa kuanza kujengwa karibuni. Yote haya yamefanya mikoa hii ianze kuwavutia hata wananchi wengine kupenda kuishi, kufanya kazi, kuwekeza na kufanya biashara katika mikoa hii.
Hapa ningependa kuwapongeza Baraza la Maaskofu Katoliki kwa kuanzisha chuo hiki hapa Mtwara na kukipa jina la Stella Maris linaloendana na maendeleo yanayoendelea kuwepo katika mkoa huu wa Mtwara. Jina hili nimeambiwa maana yake ikitafsiriwa kwa kilatini ni “Nyota ya Bahari”. Jina hili linabeba dhana nzima ya uwepo wa chuo hiki mkoani Mtwara, kwa maana ya kuwa chimbuko la mwanga na matumaini katika misukosuko ya kimaisha, kielimu, kitaaluma na kiuchumi. Jina hilo pia linaendana na maendeleo na uwekezaji unaoanza kuonekana hapa mkoani Mtwara kama nilivyoeleza hapo juu.
Waheshimiwa Maaskofu, Mabibi na Mabwana
Kwa upande wa Serikali ningependa kuahidi yafuatayo:-
Ajira kwa walimu: Kwa kuzingatia uhitaji uliopo, Serikali inawaahidi wahitimu wa chuo hiki kupewa ajira katika fani ya ualimu, kama ambavyo imekuwa ikifanya kila mwaka kwa wahitimu wa fani hii. Kwa mfano katika mwaka 2011, Serikali ilitoa ajira 11,629 kwa walimu wa shule za sekondari kote nchini na kufanya shule hizo kuwa na walimu 52,146 mwaka 2011 kulinganisha na walimu 40,516 waliokuwepo mwaka 2010 katika shule zote za sekondari za Serikali na binafsi nchini.
Sera nzuri kwa kazi ya ualimu: Serikali inaahidi kuendelea kuweka sera nzuri kwa kazi ya ualimu ili kuondoa kero za walimu zinazowapelekea kugoma na kuona kwamba taaluma yao haithaminiwi na Serikali.
Mwisho kabisa, niwaombe wananchi na wakazi wa Mtwara, mpokee taasisi zilizo Mtwara kama baraka na wadau wa kuleta maendeleo. Kwa misingi hiyo wapokeeni wanafunzi wasomao vyuoni Mtwara kama watoto wenu. Wapokeeni kama wapangaji kwenye nyumba zenu kwa gharama za kiungwana bila kuwadai pesa nyingi kupita uwezo wao. Wenye vyombo vya usafiri tozeni gharama za haki.
Nimalizie kwa kuwashukuru tena Baraza la Maaskofu Katoliki na uongozi wa chuo kwa kunialika kujumuika nanyi katika mahafali ya kwanza ya chuo hiki kikuu kishiriki cha Stella Maris, na niwatakie kila la heri kwenye kazi zao wahitimu wetu wa leo.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
COMMENTS