KAMA vituo 66 vya treni havitoshi katika safari nzima ya utalii, Teresa Williamson wa Australia na Annemarie Schuller wa Uhol...
KAMA vituo 66 vya treni havitoshi katika safari nzima
ya utalii, Teresa Williamson wa Australia na Annemarie Schuller wa Uholanzi
wamesema Watanzania wanaishi katika mazingira magumu na wanastahili kubadilika.
Kauli hiyo
wameitoa wakati wakizungumza na Mwandishi wa makala haya muda mfupi kabla ya
kuondoka kurejea makwao baada ya ziara ya wiki mbili katika maeneo mbalimbali
nchini.
Katika ziara yao ya kitalii walitumia treni, barabara
na maji tena kwa kutumia jahazi wakitokea Pangani Tanga hadi Zanzibar.
Nilitaka kujua baada ya utalii wao wameona nini nchini
Tanzania walisema pamoja na kufanikiwa kuwaona wanyama wakubwa watano kama
walivyofikiria wakati wakiwa makwao wameshuhudia maisha masikini zaidi kuliko
matarajio.
“Sijui inatokeaje watu wengi wana simu za mkono lakini
ukiangalia maisha yao unayaona kuwa magumu sana,” alisema Teresa ambaye
alifafanua kwamba ugumu wa maisha unaonekana katika miundombinu na
usafirishaji, ulaji na utunzaji wa mazingira.
Wakiwa wamezaliwa mjini hawakuwa wanajua vijijini
kukoje mpaka walipofika nchini Tanzania na kukumbana na hali ambayo
hawakuitarajia hata kidogo.
Pamoja na kushuhudia matukio yasiyokuwa ya kawaida
katika safari na mbugani ugumu wa maisha ambao wao wataendelea kuangalia ni
mawasiliano, usafirishaji, na usalama.
Wamesema katika safari yao wamekumbana na tatizo kubwa la chakula, usahihi wa taarifa na
tatizo la mawasiliano.
“Pamoja na wananchi kuwa marafiki tumeona tatizo kubwa
la usafiri na aina ya chakula kinacholiwa na usafi,” alisema Schuller ambaye
kitaalamu ni mganga wa meno.
Kwa mtazamo wa watalii hao taifa hili linahitaji
kubadili wananchi wake kwa kuwapa elimu ya kutosha kuhusu mazingira
yanayowazunguka hasa kwa kujali aina ya mlo wanaokula, usafi wa mazingira na
kujali gharama kwa huduma wanazotoa kwa wageni.
Teresa alisema kwa kuwa na aina moja ya chakula Ugali
na wali muda wote bila maziwa mboga za majini kunatengeneza aina ya udumavu
ambao unachochea watu kukosa lishe bora.
“Tumekuwa tukikumbana na chakula cha aina ile ile kila
mahali tunapoenda, chakula cha nafaka ambacho ni wanga lakini hukutani na
matunda, mboga za kijani na maziwa,” alisema Teresa.
Pamoja na kuzungumzia mlo, wageni hao
walizungumzia tatizo la rushwa na kusema
walipokuwa Zanzibar pamoja na kuhisi kwamba ulinzi ni mkali kutokana na
kusimamishwa kila mara katika gari, lakini waliona kuna kitu si sahihi wakati
wa mazungumzo kati ya dereva na askari.
“Pale tuliona shida kidogo kwanini wanapenyeza mkono
tena unaona kwa uangalifu mkubwa?” Alisema
Annemarie ambaye alisema matendo waliyokumbana nayo yanatia wasiwasi
hasa unaposimamishwa mara saba katika kipindi cha dakika 40 wakati wakiwa
kisiwa cha Zanzibar.
Kwao wanaamini kwamba lipo tatizo la rushwa na pia
tatizo la lugha kwani wengi wameshindwa kuwasiliana nao kutokana na shida ya
lugha kiasi ya kwamba wapo watu walikuwa wanawakwepa kwa sababu hawaelewani na
wakati mwingine walifanya maamuzi ambayo hayakuwa sahihi kutokana na lugha
gongana.
Anasema walipofika Tanga waliambiwa wanaweza kufika
Zanzibar kupitia Pangani.Walisema usafiri uliwachosha na hata walipofika
Pangani wakagundua kwamba mawasiliano si sahihi lakini wakaingia katika boti na
kuelekea Zanzibar.
Boti hiyo ambayo ilikuwa kila mara inatolewa maji,
iliwaogopesha sana lakini hata walipokuwa wakitaka kujua wanajiokoaje
walijikuta wakiambulia kuambiwa kwamba njia za kujiokolea ni palepale walipo.
Hata hivyo walifarijika baada ya kugundua maboya ya
kujiokolea ndio waliyoyakalia.
Pamoja na kufurahishwa na matembezi yao hasa kwa kuona
kwamba wameweza kuwaona wanyama wakubwa kama tembo, chui, simba, faru,twiga na
nyati walisema ipo haja ya kupunguzwa kwa kiingilio kwani kwa sasa wanakiona
kama ghali.
Nilipomuuliza kuhusu Serengeti kama itakufa, alisema
kwamba hadhani kwani anaona kwamba bado haijavurugwa sana na kama Watanzania
watakubali kwamba ile ni mali yao haitakufa.
“Ni suala la kuelimika na kuhakikisha kwamba utamaduni
unajali mazingira, unajali afya na wajibu,” alisema Teresa ambaye katika miaka
yake 55 alisema Afrika bado ni bara la kutembelea.
Alisema walifika Sumve kuwaona jamaa zao na marafiki,
lakini walishangazwa na wingi wa vituo ambapo treni inasimama japo waliona
kwamba hali ile inaweza kuwa inasaidia mzunguko sahihi wa uchumi wa eneo hilo.
“Njiani tuliona mengi lakini nadhani baya kabisa ni
watu kutokujali mazingira yao. Uchafu unatupwa kila mahali na hata maeneo
mengine hayakuwa na vyoo na yale yaliyokuwa na vyoo hata karatasi laini za
chooni zilikosekana,” alisema Teresa.
Kwa maneno yao watu wanatakiwa kubadilika kupitia
elimu ili kutambua kwamba kuna haja ya kuwa na mazingira safi kwa manufaa yao
na kizazi kijacho.
“Unakosaje mahali pa kujisaidia? Umelipa fedha ili
ufurahi inakuaje unapokosa huduma,” aliuliza Teresa.
Kwa maneno yao wenyewe ugumu wa kupata huduma
inayoridhisha kwa fedha halisi si tu
katika maeneo waliyofikia bali hata katika usafiri.
“Ukiwa peke yako huwezi kufanikiwa,” alisema Teresa na
kuungwa mkono na Annemarie ambaye yeye kuja Afrika ilikuwa mara yake ya kwanza.
Moja ya tatizo ni kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa watu wanaoandaa usafiri
ambao wamekuwa wakiwatoza ada kubwa kuliko wanayokuja kujua baadaye.
Yalikuwa ni maoni ya mwandishi wa makala haya kwamba
tatizo hilo linatokana na kutumia wakala katika masuala ya utalii na badala
yake watu ambao wamejitangaza kujua
Tanzania na kwamba watawapokea.
Watu hao ambao unaweza kulinganisha na vishoka
wanachojali wao ni kuongeza cha juu na kuwafikisha watalii wao katika maeneo
ambayo ni rahisi na wakati mwingine bila kuwa na muunganisho mwema.
Pamoja na udhaifu katika masuala ya utalii hasa
mawasiliano na upashanaji wa taarifa elimu inayotakiwa miongoni mwa wananchi ni
kubadili masuala yao yanayowafanya wawe na maisha magumu.
Kwa watalii hao wamesema hawajawahi kuona ardhi yenye
rutuba kubwa kama Tanzania na kinachotakiwa kufanywa ni watu wake kutumia fursa
zilizopo kujikwamua katika dhiki ya umasikini na kuboresha maisha yao.
Walielezea kufurahishwa na ukarimu uliofanywa na
Wapare walipoenda kutembelea eneo la Mbagha ambako walilala Tona Lodge na
kupata maelezo kuhusu kijiji na kutembelea vivutio mbalimbali likiwemo jiwe
lililotumika kuua watoto waliokuwa wanafikiriwa wana mikosi.
Naam, mpaka mwisho wa mazungumzo wageni hao
walilalamikia usafi, utunzaji wa mazingira, mfumo wa lishe na mawasiliano
hafifu pamoja na lugha gongana unaleta utata wa uaminifu.
COMMENTS