TANZANIA SOCIAL SUPPORT FOUNDATION OFISI YA MKURUGENZI MKUU TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI YAH: KUFUNGULIWA RASMI KWA KITUO CHA...
TANZANIA SOCIAL SUPPORT FOUNDATION
OFISI YA MKURUGENZI MKUU
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
YAH: KUFUNGULIWA RASMI
KWA KITUO CHA MAENDELEO CHA KANDA YA KUSINI MASHARIKI MWA TANZANIA.
1.0 UTANGULIZI.
Ndugu Wanahabari, kwa niaba ya bodi ya Utawala wa
Shirika la Kusaidia Jamii Tanzania ambalo kwa kiingereza linaitwa “Tanzania
Social Support Foundation” ninayo heshima kubwa mbele yenu kwanza kumshukuru
Mwenyenzi Mungu aliyetujaalia uzima na nguvu za kuweza kufika hapa tulipo, pamoja
na afya njema, vitu ambavyo vimetufanya leo hii tuweze kutekeleza majukumu yetu
kwa ufanisi, kila mmoja kwa nafasi yake katika jamii. Pia Shirika linawashukuru
sana kwa kuwa mmekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa mnaihabarisha
jamii na hivyo kuutekeleza wajibu wenu vyema na kwa ufanisi Mkubwa.
2.0
KITUO CHA MAENDELEO CHA KANDA YA KUSINI MASHARIKI
MWA TANZANIA.
Kituo Cha Maendeleo Cha Kanda ya Kusini Mashariki
Mwa Tanzania (Centre for Development in South – Eastern Tanzania [CDSET]) ni
Taasisi ya Shirika la Kusaidia Jamii Tanzania ambayo imeanzishwa kwa ajili ya
kuwaandaa wananchi wa Mkoa wa Mtwara, Lindi, na Ruvuma ili waweze kuzitumia
vyema fursa za kiuchumi ambazo zinapatikana katika mikoa ya Lindi, Mtwara, na
Ruvuma.
Mtakumbuka
kwamba mnamo Desemba 2012 mpaka sasa kumekuwepo na sintofahamu mbalimbali kati
ya Wananchi wa Kanda ya Kusini Mashariki mwa Tanzania (hasa mikoa ya Lindi na Mtwara) na Serikali kuhusiana na namna
ambavyo wananchi watanufaika na rasilimali za gesi na mafuta ambazo
zilivumbuliwa hivi karibuni. Serikali kwa upande wake imekuwa ikitoa nyaraka mbalimbali za kuonyesha kuwa
ni kwa namna gani wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara watavyonufaika na
rasilimali zilizovumbuliwa hivi karibuni lakini kwa bahati mbaya sana hakuna
hatua muhimu na za haraka ambazo zimechukuliwa ili kuwawezesha wananchi katika
kujiandaa vyema ili hatimaye waweze kunufaika na hizo rasilimali.
Ni
kwa sababu hiyo sasa Shirika la Kusaidia Jamii Tanzania (Tanzania Social Support Foundation) limefungua Kituo Cha Maendeleo
Cha Kanda ya Kusini Mashariki mwa Tanzania ambacho makao yake makuu yapo katika
Ofisi za makao makuu ya Shirika la Kusaidia Jamii Tanzania (Tanzania Social Support Foundation)
ambapo ofisi za Shirika zipo katika Ploti Na. 164 Block “H”, Barabara ya TANU,
Karibu na Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mtaa wa Rahaleo Chini,
Kata ya Rahaleo, Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mkoani Mtwara.
Kituo
Cha Maendeleo Cha Kanda ya Kusini Mashariki Mwa Tanzania kitahudumia mikoa ya
Lindi, Mtwara, na Ruvuma na kitakuwa na Majukumu yafuatayo;-
(i)
Kuwawezesha
wananchi kwa kuwapa elimu itakayowajengea uwezo wa kutambua, kubaini, kuanzisha
na kuendeleza fursa za uzalishaji ili kuweza kujipatia kipato na hivyo
kujikwamua kiuchumi. Katika hilo ni vyema wananchi wakafahamu kwamba,
ujasiriamali siyo kufungua biashara ndogondogo tu bali ujasirimali ni zaidi ya
kufanya biashara. Katika jambo hili, Kituo kitawafundisha wananchi katika vikundi vidogo vidogo kuhusiana na
namna ya kupanga mipango pamoja na kuendesha shughuli mbalimbali za uzalishaji.
(ii)
Kituo
Kitatoa elimu kwa wananchi kuhusiana na namna ya kuanzisha vikundi vidogo
vidogo vya ujasiriamali, kuboresha vikundi vilivyopo kama vile VICOBA, SACCOS,
na asasi za kiraia sanjari na kutoa elimu ya kutatua migogoro katika vikundi na
asasi za kiraia ili ziweze kuwa endelevu. Mtakuwa mshahidi wa TSSF kwamba,
vikundi vingi vya uzalishaji mali na kukuza kipato ni vya akina mama na kwamba,
vikundi hivi vimekuwa vikisambaratika kwa sababu ya migogoro na kutokuelewa
hatua stahiki za kuchukuliwa pindi sintofahamu zinapokuwa zimejitokeza katika
vikundi husika. Hii ndiyo sababu kubwa inayofanya Kituo hiki kijishughulishe na
utoaji wa mafunzo kama ilivyoelezwa hapo juu.
(iii)
Kituo
kimeandaa mpango maalum wa kurasimisha asasi za kiraia, mtu mmoja mmoja ambaye
yupo katika sekta isiyo rasmi, na vikundi vidogo vidogo vya uzalishaji mali au
ujasiriamali ambavyo vipo katika sekta isiyo rasmi, ili kwamba makundi yaliyotajwa
hapo juu yaweze kutambulika kisheria na kupata fursa ambazo zitawawezesha
kujikwamua kiuchumi. Fursa hizi ni kama vile mikopo, na huduma nyingine za
kifedha ambazo zitachangia kuongezeka kwa kiwango cha uwekezaji katika shughuli
za kiuchumi na hivyo kuongeza kipato cha mwanachi mmoja mmoja na jamii nzima
kwa ujumla.
(iv)
Katika
hoja nzima ya kupambana na changamoto ya upatikanaji wa ajira kwa vijana, Kituo
kimejipanga kutoa elimu kwa vijana kuhusiana na stadi za maisha, na pia kituo
kimeanzisha kanzi data (Database) maalum ambayo inarekodi taarifa za msingi za
waombaji wa ajira na hivyo kuwaunganisha na waajiri ambao wanakuwa wametangaza
nafasi za kazi pale inapotokea. Zaidi ya hayo, Kituo kinatoa mafunzo rasmi ya
elimu ya kujitegemea jambo litakalosababisha vijana kubuni na kuanzisha
shughuli mbalimbali ambazo zitawafanya wajiajiri wenyewe na hivyo kutengeneza
ajira kwa wao wenyewe na vijana wenzao kuliko kukaa na kuendelea kusubiri
kuajiriwa kama ilivyozoeleka hivi sasa.
(v)
Kituo
kinatoa huduma za ushauri katika ufanyaji na uandishi wa tafiti mbalimbali,
ushauri katika uandishi wa miradi ya maendeleo ya kijamii inayoleta tija kwa
wananchi, ushauri katika uandishi wa wazo la kuanzisha biashara, ushauri katika
kuanzisha taasisi mbalimbali kama vile, Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali,
Vyama vya Kijamii, SACCOS, VICOBA, Makampuni na vikundi vidogo vidogo vya
kijasiriamali, kwa mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu wanaotaka kuanzisha moja
ya taasisi tajwa hapo juu.
(vi)
Elimu
ya Uraia na kujitambua ni sehemu ya mafunzo yanayotolewa na Kituo Cha Maendeleo
Cha Kanda ya Kusini Mashariki Mwa Tanzania kwa Wananchi.
(vii)
Katika
kuandaa kizazi cha sasa na vijavyo, Kituo kimeanza kutekeleza mkakati wa
kuboresha elimu katika shule za msingi na sekondari zilizopo katika kanda ya
kusini mashariki mwa Tanzania ili kuhakikisha kwamba, elimu inayotolewa inakuwa
na tija kwa wanafunzi pindi wanapohitimu masomo. Mtakumbuka kwamba, elimu siyo
kuongeza ufaulu kwamba, mwanafunzi huyu alikuwa na alama “F” katika matokeo ya
mitihani yake ya wakati uliopita sasa ana alama “A”. Bali ni kumfanya
mwanafunzi aweze kuyatawala mazingira yake baada ya kuhitimu masomo yake na
siyo kutawaliwa na mazingira. Hilo ndilo jambo kubwa linaloshughulisha kituo
chetu katika muktadha wa elimu.
(viii)
Hakuna
maendeleo yanayopatikana bila ya kufanya tafiti zenye tija, zinazoandaliwa
katika mrengo wa kati, na zenye manufaa kwa walengwa. Kwa kulitambua hilo,
Shirika la TSSF linajishughulisha katika kufanya tafiti ambapo tunda la kwanza
la kufanya tafiti ambalo limekuwa ni faida kwa wananchi ni kuanzishwa kwa kituo
hiki baada ya kubaini changamoto za kijami zinazoikabili mikoa ya kanda ya
kusini mashariki mwa Tanzania kwa sasa.
3.0
Wito wa Shirika la TSSF na Kituo Cha CDSET Kwa
Wananchi.
Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi ili
wanufaike na huduma hizi ambazo zimeletwa karibu na wao na ikumbukwe kwamba, si
busara kulalamika na kukumbatia matatizo wakati njia ya kuweza kupata suluhu ya
matatizo ipo. Pia haiwezekani kufanikiwa katika maisha bila ya kujishughulisha.
Hivyo basi naomba kwa umoja wetu kama jamii tuwajibike na baada ya kutimiza
wajibu wetu, tutaweza kutembea kifua mbele katika kuidai haki yetu.
Nawatakia
siku njema na utendaji mwema na asanteni kwa kunisikiliza.
Wenu
Ndg.
Donati Salla
Mkurugenzi
Mkuu wa TSSF.
COMMENTS