Sekta ya uchukuzi nchini Tanzania imeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi kwa kuchangia wastani wa asilimia 40 ya mapato yote ya kodi ya for...
Sekta ya uchukuzi nchini Tanzania imeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi kwa kuchangia wastani wa asilimia 40 ya mapato yote ya kodi ya forodha yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) huku ikizitisha rekodi mpya kwa kuingiza Dola za Marekani bilioni 2.79 za fedha za kigeni mwaka 2025 na kuzalisha ajira zaidi ya laki moja kupitia miradi ya kimkakati kama Reli ya Kisasa ya SGR.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi bungeni kwa mwaka wa fedha 2026/2027, amebainisha kuwa maboresho makubwa katika bandari, anga na miundombinu ya reli si tu yameongeza shehena kwa asilimia 28, bali pia yameifanya Kampuni ya Ndege ya ATCL kujiendesha kwa faida bila ruzuku huku ikisafirisha zaidi ya abiria milioni moja.
Mchango wa Uchukuzi katika Pato la Taifa na Fedha za Kigeni
Sekta ya uchukuzi imejipambanua kama kiungo muhimu kwa sekta nyingine za uzalishaji kama kilimo, madini na utalii ambapo kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), sekta hiyo ilikua kwa asilimia 4.2 na kuchangia asilimia 7.5 katika Pato la Taifa.
Ukuaji huu umechochewa na ongezeko la mauzo ya huduma za usafirishaji kwenda nchi jirani ambazo hazina bahari zikiwemo DRC, Zambia na Rwanda hali iliyopelekea sekta hiyo kuchangia asilimia 15.86 ya mauzo yote ya nje ya nchi kwa mwaka 2025.
Ongezeko hili la fedha za kigeni kutoka dola bilioni 2.35 mwaka 2024 hadi dola bilioni 2.79 mwaka 2025 ni kielelezo cha kuimarika kwa huduma zinazotolewa katika viwanja vya ndege na bandari zetu ambazo sasa zinahudumia mataifa mengi zaidi kikanda.
Mafanikio ya ATCL na Kupaa kwa Mapato ya Ndani
Katika sekta ya anga, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imeonyesha ufanisi mkubwa ambapo katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026 imefanikiwa kusafirisha abiria 1,072,528 ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.38 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Ongezeko hili la abiria lilienda sambamba na ukuaji wa mapato ambapo kampuni ilikusanya Shilingi bilioni 501.62 na kuwezesha kugharamia mahitaji yake ya uendeshaji ikiwemo ununuzi wa mafuta na mishahara bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
Aidha, ATCL imeimarisha usafirishaji wa mizigo kwenda masoko ya kimataifa kama China na India, huku ikiongeza ukusanyaji wa fedha za kigeni kufikia Dola za Marekani milioni 129.71 katika kipindi hicho cha miezi tisa.
SGR yakusanya bilioni 169 , abiria milioni 5
Serikali imetangaza mafanikio makubwa katika uendeshaji wa Reli ya Kisasa (SGR) nchini ambapo jumla ya Shilingi bilioni 169.37 zimekusanywa tangu kuanza kwa safari hizo mwezi Juni 2024 hadi Machi 2026.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake amesema takwimu za jumla zinaonesha kuwa tangu kuanza kwa uendeshaji, zaidi ya abiria milioni 5.5 wamesafirishwa, huku Shirika la Reli Tanzania (TRC) likiongeza safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro kufikia sita kwa siku ili kukidhi mahitaji makubwa ya usafiri. Serikali inakadiria kuwa hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2025/26, idadi ya abiria watakaosafirishwa kwa mwaka mmoja itavuka milioni tatu.
Katika upande wa usafirishaji wa mizigo, TRC imetekeleza ahadi ya serikali kwa kusafirisha tani 102,452 kupitia SGR huku kampuni kubwa kama Dangote zikianza kutumia reli hiyo kusafirisha saruji kuelekea maeneo mbalimbali.
Mapinduzi ya Bandari na Ujenzi wa Bandari Mpya ya Bagamoyo
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeshuhudia ongezeko la shehena kwa asilimia 27.96 ambapo jumla ya tani milioni 29.66 zilihudumiwa kutokana na maboresho ya miundombinu na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji.
Katika kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030, serikali inakamilisha maandalizi ya kuanza ujenzi wa Bandari Mpya ya Bagamoyo mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa za kisasa aina ya Megamax zinazobeba zaidi ya makasha 24,000 kwa wakati mmoja.
Mradi huu wa kimkakati utaunganishwa na Reli ya Kisasa ya SGR kuelekea Bandari Kavu ya Kwala ili kurahisisha usafirishaji wa shehena kwenda nchi za maziwa makuu na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango kuu la biashara.
Uzalishaji wa Ajira na Ustawi wa Jamii kupitia Miundombinu
Uwekezaji katika sekta ya uchukuzi umekuwa chimbuko la ajira kwa maelfu ya Watanzania ambapo mradi wa SGR pekee umezalisha fursa za kazi 181,056 tangu kuanza kwake zikiwemo ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Sekta nyingine kama ujenzi wa viwanja vya ndege na uendelezaji wa bandari zimechangia kutoa ajira zaidi ya elfu kumi na tano huku vyuo vya mafunzo ya kisekta kama NIT na DMI vikiendelea kuandaa wataalamu wa kuendesha mitambo na mifumo ya kisasa ya usafirishaji.
Kupitia uimarishaji wa mifumo ya TEHAMA na ushirikiano wa kikanda, serikali imehakikisha kuwa ukuaji wa sekta ya uchukuzi unagusa maisha ya wananchi wa kawaida na kuchochea biashara za ndani kwa asilimia 90 ya bidhaa zote zinazoingia nchini kupitia njia ya maji.





COMMENTS