Na Mwandishi Wetu Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa (U...
Na Mwandishi Wetu
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, wamekutana na kufanya mazungumzo mazito jijini Seoul nchini Korea Kusini, wakilenga kusukuma mbele agenda ya kukuza elimu ya awali na msingi kwa watoto takribani milioni 750 kote duniani.
Mazungumzo hayo ya kimkakati yamefanyika leo wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Kikwete nchini humo, anayoifanya kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE).
Viongozi hao wawili wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano ili kuwaokoa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, huku Ban Ki-moon akitolea mfano wa maisha yake jinsi alivyolazimika kusomea chini ya mti baada ya kijiji chao kuteketezwa kwa moto wakati wa Vita ya Korea (1950 - 1953), hadi alipookolewa na kuandaliwa kuwa kiongozi mkubwa duniani kupitia ufadhili wa elimu na chakula kutoka UN.
Ban Ki-moon, kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taasisi za The Ban Ki-moon Foundation yenye makao yake makuu Vienna nchini Austria, na Ban Ki-moon Foundation for a Better Future yenye makao yake makuu Seoul, Korea Kusini.
Katika mazungumzo yao Rais Mstaafu Dkt. Kikwete amempongeza Katibu Mkuu huyo Mstaafu wa UN kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kupitia Taasisi zake ya kuhamasisha ufikiwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan Lengo Namba 4 linalohusu Elimu Bora kwa Wote, Lengo Namba 13 linalohusu Kuchukua Hatua dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi, na Lengo Namba 17 linalohusu Ushirikiano wa Kimataifa kati ya Serikali, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia katika kutimiza malengo ya SDG.
Pia Dkt. Kikwete alitumia fursa hiyo pia kumshukuru Bw. Ban Ki-moon kwa msaada wake anaoutoa kwa Taasisi ya GPE uliowezesha kuimarika kwa mahusiano kati ya Taasisi hiyo ya GPE na Serikali ya Korea Kusini. Kwa mujibu wa taarifa inayopatikana kwenye tovuti ya GPE, Korea Kusini ni moja ya nchi na mashirika wafadhili 33 (donor countries organisation) wa GPE ambayo tangu mwaka 2015 imeshachangia jumla ya Dola za Kimarekeni milioni 20 kwa Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Bw. Ban Ki-moon amemhakikishia Dkt. Kikwete kuwa ataendelea Taasisi zake zitaendelea kufanya kazi kwa karibu na Taasisi ya GPE, Serikali ya Korea na mashirika mengine ya kimataifa katika kukuza elimu duniani, hususan kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Katika muendelezo wa ziara hiyo yenye tija, Dkt. Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa Serikali ya Korea Kusini na Wabunge wanaoshughulikia masuala ya elimu na maendeleo ya kimataifa, akiwemo Makamu wa Pili wa Waziri wa Mambo ya Nje, Kim Jina, Naibu Waziri Chang Wook-jin, pamoja na Wabunge Jae Jung Lee, Kyung-sook Kang, na Geong Kim, huku Balozi mpya wa Tanzania nchini Korea Kusini, Noel Kaganda, akishiriki katika baadhi ya mikutano hiyo.
Katika vikao hivyo, viongozi hao wa Korea Kusini, nchi ambayo imeshatoa jumla ya dola milioni 20 kwa GPE tangu mwaka 2015, walimueleza Dkt. Kikwete nia ya serikali yao kuongeza kiwango cha fedha za ufadhili, ahadi inayotarajiwa kutangazwa rasmi katika Mkutano wa Ahadi (Replenishment Summit) utakaofanyika tarehe 23 Septemba, 2026, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York, Marekani.
Aidha Taasisi ya GPE imelenga kutumia Mkutano huo wa New York, Marekani kuzindua Kampeni ijulikanayo kama GPE 2030 ambapo jumla Dola za Marekani bilioni 15 zinatarajiwa kukusanywa kati ya mwaka 2026 - 2030 ili kugharamia elimu ya awali na msingi kwa watoto takribani milioni 750 katika nchi zaidi ya 90 kote duniani ikiwemo Tanzania.
Mbali na diplomasia hiyo kubwa ya kimataifa, ziara hii ina tija kubwa ya moja kwa moja kwa sekta ya elimu nchini kwani Tanzania ni miongoni mwa nchi wanufaika wakuu ambapo hadi sasa imeshapokea zaidi ya Dola za Marekani milioni 207.3 kutoka Taasisi ya GPE kwa ajili ya kuboresha miundombinu na mifumo ya elimu.
Inatarajiwa kuwa kiasi hiki cha fedha kinachotolewa kwa Tanzania kitaongezeka kwa kasi kubwa kupitia mpango maalumu wa GPE wa kuziongezea fedha nchi zinazofanya vizuri katika kusimamia sekta ya elimu na kutekeleza miradi kwa ubia madhubuti kati ya Serikali na taasisi hiyo.
Hatua hizi zinaenda sambamba na heshima kubwa aliyopewa Rais Mstaafu Dkt. Kikwete na Chuo Kikuu cha Seoul National University, ambacho kilimwalika kutoa mhadhara wa wazi chuoni hapo kama sehemu ya kutambua mchango wake wa kipekee katika kukuza elimu duniani na nafasi yake kama Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

COMMENTS