Rais Jakaya Kikwete, amewasili nchini Misri ambako kesho atakuwa Mwenyekiti wa Kikao cha 11 cha Wakuu wa Nchi za Afrika kinachoanza katika mji wa Sharm El Sheikh.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu leo, kikao hicho cha Wakuu wa Nchi wa AU kimetanguliwa na kikao cha siku mbili cha 16 cha kawaida cha Baraza la Utendaji la AU kilichoanza Ijumaa iliyopita chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Kikao hicho ni cha mawaziri wa Mambo ya Nje wa AU.
Taarifa ya Ikulu ilisema mada kuu ya Kikao cha Wakuu wa Nchi za AU ni Maji na Usafi Wake, chini ya mada ya jumla ya juhudi za Afrika kutekeleza Maazimio la Milenia – Meeting the Millennium Development Goals (MDGs) on Water and Sanitation”.
Aidha, kikao hicho chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, kitapokea na kujadili Ripoti ya Kamati ya Wakuu 12 wa AU kuhusu kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Afrika. Mjadala kuhusu suala hilo umekuwa unaendelea tangu Libya ilipotoa pendekezo hilo mwaka 2005.
Ripoti hiyo, itawasilishwa na Rais Kikwete mwenyewe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo iliyokutana katika kikao chake mjini Arusha kwa siku mbili kuanzia Mei 22, mwaka huu.
Mbali na Tanzania, nchi nyingine wajumbe wa Kamati hiyo ni Ghana, Nigeria, Senegal, Libya, Misri, Botswana, Afrika Kusini, Ethiopia, Uganda, Gabon na Cameroon, ambazo zote zilihudhuria mkutano wa Arusha.
Kikao cha Sharm El Sheikh pia kitajadili na kufikia uamuzi kuhusu pendekezo la kuunganishwa kwa Mahakama ya Afrika Kuhusu Haki za Binadamu na Watu wa Afrika pamoja na Mahakama ya AU. Pia kitateua majaji wanne kati ya saba wanaowania kuwamo katika mahakama hiyo.
Aidha, kitapokea na kujadili Ripoti ya Shughuli za Baraza la Amani na Usalama la AU na mjadala huo unatarajia kugusia hali ilivyo katika nchi za Comoro, Burundi, Ivory Coast, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Somalia, Darfur (Sudan) na Zimbabwe.

Pichani Waziri Mkuu wa Misri, Dk. Ahmed Nazif akimkaribisha Rais Jakaya Kikwete katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sharm El Sheikh, Misri leo . Picha na Freddy Maro wa Ikulu

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO