Baraza la Wawakilishi limepitisha bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ya mwaka wa fedha 2008/2009 ambayo inakusudia kutumia Sh bilioni 341.709.
Katika mchanganuo wa bajeti hiyo iliyowasilishwa wiki iliyopita na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Fedha na Uchumi) Dk. Mwinyihaji Makame, kati ya fedha hizo, Sh bilioni 149.435 ni matumizi kwa kazi za kawaida na Sh bilioni 192.274 kwa kazi za maendeleo.
Bajeti hiyo iliyopitishwa jana kwa wawakilishi wa upande wa CCM wote kuiunga mkono na wote kutoka CUF kuipinga.

Kodi maalumu kwa bia, vinywaji vikali na sigara imeanzishwa.
Ili kufanikisha kutoza kodi hizo, sheria ya biashara itapitiwa upya na kuweka tozo la Sh 400 kwa lita ya bia na vinywaji vikali huku Sh 500 itatozwa kwa kila sigara 1,000 zinazoingizwa Zanzibar.
Akihitimisha michango ya bajeti hiyo, Dk. Mwinyihaji alisema SMZ inatoa misamaha ya kodi kwa mujibu wa sheria na misamaha mingi inakwenda kwenye miradi ya maendeleo.
“Wenzetu wafadhili huwa wanatuambia tusamehe kodi katika vifaa wanavyotuletea kwa ajili ya miradi yetu ya maendeleo nasi tunakubali mfano katika ujenzi wa bandari ya Malindi tumesamehe kodi ya shilingi milioni 240, Zantel tumeisamehe milioni 143.25 ili iweze kujitanua Tanzania Bara…., hata wenzetu wa bara wanasamehe kodi labda kama hawaweki wazi kama sisi,” alisema.
Aliwataka wawakilishi kuacha kubeza mafanikio ya Serikali ya Zanzibar na kutukuza za nje ambazo hazina mafanikio na kuongeza “think globally, act locally according to your environment.”
Alisema ujenzi wa bandari ya Malindi unatarajiwa kukamilika mwaka huu ambapo makontena yaliyokwama katika bandari ya Dar es Salaam yataanza kuletwa kisiwani hapa.
Kuhusu kilimo cha karafuu, Waziri huyo alisema Wizara ya Kilimo, Mifugo na Mazingira kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya karibuni itaanza utafiti wa kuboresha kilimo cha zao hilo na kuwataka wakulima kutoharibu mashamba yao ya karafuu.
Picha ni Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Ali Mzee Ali (Kushoto) akibadilishana mawazo na Mwakilishi nwa Dole, Shawana Buheti Hassan, (katikati) na Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, nje ya Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar leo. Picha ni mali ya Martin Kabemba wa Unguja

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO