HOTUBA YA PM YA LEO

HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA, (MB.), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FED...



HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA, (MB.), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE
KWA MWAKA 2008/2009


UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba na taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, iliyochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2007/2008 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2008/2009. Aidha, naliomba Bunge lako tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi zilizo chini yake na yale ya Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2008/2009.

2. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kwa mara nyingine tena kumshukuru Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa imani kubwa aliyonipa kuniteua kuwa Msaidizi wake wa karibu wa kuongoza shughuli za Serikali ya Awamu ya Nne. Nawashukuru tena Waheshimiwa Wabunge chini ya uongozi wako kwa kuthibitisha uteuzi wangu kwa kura nyingi.

Changamoto zilizo mbele yetu ni nyingi, lakini imani yenu kubwa kwangu na ushirikiano mnaoendelea kunipa, unanipa moyo kwamba kwa pamoja tutaweza kukuza uchumi, kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za jamii na hatimaye kuleta maisha bora kwa Watanzania.

3. Mheshimiwa Spika, mwezi Mei 2008, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri. Katika mabadiliko hayo, Mheshimiwa Rais alimteua Mheshimiwa Celina Kombani (Mb.), kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa Profesa Peter Msolla (Mb.), Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia; Mheshimiwa Dk. Shukuru Kawambwa (Mb.), Waziri wa Miundombinu na Mheshimiwa Stephen Wasira (Mb.), kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika. Aidha, alimteua Mheshimiwa Aggrey Mwanri (Mb.), kuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa, Hezekiah Chibulunje (Mb.), kuwa Naibu Waziri wa Miundombinu na Mheshimiwa Dk. Milton Makongoro Mahanga (Mb.), kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana. Napenda kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wote kwa kuteuliwa kwao kushika nyadhifa hizo muhimu.

4. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Bunge lako tukufu lilipata msiba wa marehemu Salome Mbatia aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na marehemu Benedict Losurutia aliyekuwa Mbunge wa Kiteto. Nichukue fursa hii kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki wa familia za marehemu hao. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.

5. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kisichopungua siku tano Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakijadili taarifa kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2007 na Bajeti na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2008/2009 na hatimaye kuipitisha. Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Mustafa Haidi Mkulo, (Mb.), Waziri wa Fedha na Uchumi kwa hotuba yake nzuri na jinsi alivyoweza kutoa maelezo ya ufasaha kuhusu hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushauri na michango yenu mizuri mliyoitoa wakati wa majadiliano ya Bajeti ya Serikali. Ninawahakikishia kwamba michango hiyo itazingatiwa wakati wa utekelezaji.

6. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kwa kupitia Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge. Ninazishukuru sana Kamati za Kudumu za Bunge lako tukufu kwa michango na ushauri waliotoa wakati wa kupitia Makadirio ya Matumizi ya kila Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na taasisi zilizo chini ya wizara zote.

7. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali mliyoipitisha ndiyo itakayotuwezesha kuendesha kazi za Serikali na kutekeleza kikamilifu Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005. Bajeti hiyo imezingatia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo 2025, Malengo ya Milenia 2015 na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA). Serikali itaendelea kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato kwa kutekeleza miradi na mipango mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuboresha maisha ya kila Mtanzania. Wizara, Mikoa, Halmashauri na Taasisi za Serikali zinazojitegemea zimetengewa fedha kulingana na majukumu waliyo nayo ambayo yanalenga kutekeleza MKUKUTA. Viongozi na watendaji wote wa Serikali wanao wajibu wa kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa kazi zilizopangwa na kutoa taarifa za utekelezaji kwa mamlaka husika. Ufuatiliaji huo, ukishirikisha wananchi, utaongeza uadilifu na uwajibikaji wa watendaji katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo. Natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuwa mstari wa mbele katika kuwaelimisha wananchi kuhusu bajeti hii na miradi itakayotekelezwa katika maeneo yao.


Mwandishi mmoja Glenn Bland aliandika: “Goals and plans take the worry out of living.” Kama tukiweka malengo, hatua tunazozichukua zitazingatia maisha tunayoyahitaji badala ya kutegemea kila tunapoamka asubuhi tunajisikiaje. Tumepanga, tumekadiria na tunategemea kutumia. Mipango yetu itafanikiwa kama tutatumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya kile kilichopangwa.


HALI YA SIASA

8. Mheshimiwa Spika, nchi nyingi duniani zimekuwa na mafanikio ya uchumi imara kutokana na kujiwekea misingi bora ya hali ya siasa, amani na utulivu. Aidha, uchumi imara ni matokeo ya juhudi wanazowekeza wananchi katika uzalishaji mali kwenye nchi inayozingatia utawala wa sheria na yenye sera nzuri za uwekezaji. Ninayo furaha kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba, nchi yetu ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zimepata sifa kubwa katika kudumisha amani na utulivu licha ya tofauti za kiitikadi zilizopo. Napenda kuwapongeza wananchi wote kwa kushiriki katika kudumisha amani na utulivu nchini. Nawahimiza kuzidi kuendelea kuwa mfano wa kuigwa katika bara letu la Afrika na duniani kote. Nawasihi tusiichezee sifa hii, kwani tukiipoteza madhara yake ni makubwa na siyo rahisi kuirejesha.

Muungano

9. Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua za kutatua masuala ya Muungano yanayoleta kero kwa wananchi wetu wa pande zote kwa kufanya vikao mbalimbali. Kikao kimojawapo cha ngazi ya juu ni kile kilichoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, kilichofanyika tarehe 15 Mei, 2008, Dar es Salaam. Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kikao hicho kilijadili Taarifa za Utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa katika vikao viwili vya awali kati ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi. Baadhi ya masuala yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na kufungua Ofisi ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora huko Unguja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuainisha miradi itakayoombewa ufadhili chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

10. Mheshimiwa Spika, mbali na kikao cha Makamu wa Rais, vilifanyika pia vikao vingine 11 vya ushirikiano baina ya wizara mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar. Wizara zilizohusika na vikao hivyo ni pamoja na Mawasiliano, Uchukuzi na Miundombinu; Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Maliasili na Utalii; Viwanda, Biashara na Masoko; Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Sheria, Katiba na Utawala Bora; Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Katika vikao hivyo, masuala mbalimbali yanayohusu sekta husika yalijadiliwa kwa maelewano na kufikiwa muafaka.

11. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia zimeridhia uteuzi wa Mshauri Mwelekezi atakayeshauri kuhusu mgawanyo wa mapato yatokanayo na rasilimali ya mafuta. Kazi hii inatarajiwa kukamilishwa mwezi Agosti, 2008 na kuwasilishwa katika Serikali zote mbili mwezi Septemba, 2008. Aidha, uandaaji wa kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi katika Ukanda wa Bahari Kuu utakamilika mwezi Septemba, 2008.

12. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea kutekeleza masuala yafuatayo:
a) Kuratibu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano katika vikao mbalimbali vikiwemo vya kimataifa;
b) Kuratibu, kuandaa na kushiriki katika vikao vya Makamu wa Rais na Mawaziri wa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
c) Kufanya utafiti wa mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa lengo la kudumisha Muungano;
d) Kutoa elimu kwa umma kuhusu mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano;
e) Kuanisha maeneo ya uchumi katika nchi yetu ambayo yakitekelezwa yataleta faida kwa pande zote mbili; na
f) Kuratibu mgawanyo wa mapato ya pande zote mbili za Muungano.

Ili kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo kwa karibu zaidi, vikao vya pamoja vitafanyika kila baada ya miezi miwili chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais.

Chaguzi Ndogo

13. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, nchi yetu ilifanya uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kiteto na chaguzi ndogo za madiwani katika Kkata 16 Nchini. Katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Kiteto, vyama vinne vya siasa vilishiriki. Mheshimiwa Benedict Ngalama Ole-Nangoro, alichaguliwa kuwa Mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi kwa kupata kura 21,506 sawa na asilimia 61 ya kura zote zilizopigwa. CHADEMA kilipata kura 12,561, SAU kura 300 na PPT Maendeleo kura 110. Kwa mara nyingine nampongeza Mheshimiwa Benedict Ngalama Ole-Nangoro aliyeshinda uchaguzi huo. Uchaguzi huo pamoja na chaguzi ndogo mbalimbali za madiwani zilifanyika katika mazingira yaliyokuwa huru, amani na yaliyozingatia misingi bora ya demokrasia.

14. Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Agosti, 2007 Mheshimiwa Dk. Christine Gabriel Ishengoma (CCM) aliteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kujaza nafasi ya marehemu Amina Chifupa Mpakanjia. Mheshimiwa Mchungaji Dk. Getrude Pangalile Rwakatare (CCM) aliteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kuanzia tarehe 26 Novemba, 2007 kujaza nafasi ya marehemu Salome Joseph Mbatia. Aidha, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua Mheshimiwa Al-Shymaa John Kwegyir kuwa Mbunge wa Viti Maalum kuanzia tarehe 8 Aprili 2008. Wote nawapongeza sana kwa kuteuliwa kuwa Wabunge.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

15. Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza awamu ya kwanza ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kuwaingiza wale waliotimiza sifa za kujiandikisha na kuwaondoa waliopoteza sifa. Hadi sasa, uboreshaji wa Daftari hilo umefanyika katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Iringa, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Mwanza na Kagera. Zoezi hili litaendelea kwa mikoa ya Mara, Shinyanga, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar. Awamu ya Pili ya Uboreshaji wa Daftari hilo itafanyika mwaka 2009/2010 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Lengo ni kuhakikisha kwamba kila mwananchi aliye na sifa za kujiandikisha kuwa mpigakura anapatiwa nafasi hiyo ili aweze kushiriki katika uchaguzi huo.

Vyama vya Siasa

16. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali ilianza kutoa ruzuku kwa vyama vya siasa vyenye madiwani. Vyama vinavyopata ruzuku hiyo ni CCM, TLP, CHADEMA, CUF, UDP na PPT-MAENDELEO. Kiasi cha shilingi bilioni 3 kilitengwa na Serikali kwa ajili ya ruzuku hiyo. Vilevile, Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa zilianza kutumika rasmi kupitia Tangazo la Serikali Na. 215 la tarehe 12 Oktoba, 2007. Wadau wote wamefahamishwa na kupatiwa nakala ya Kanuni hizo. Nachukua nafasi hii kuvishauri vyama vya siasa visome kwa makini, viheshimu na kuzifuata kanuni hizo, ili kuepuka migongano inayotokea kati ya vyama vyetu. Aidha, Serikali inafanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya mwaka 1992 kwa lengo la kuondoa migongano, migogoro na mahusiano mabaya ndani ya vyama vya siasa. Marekebisho hayo yatawasilishwa hapa Bungeni katika Mkutano wa Bunge wa Kumi na Tatu mwezi Novemba 2008.

17. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, usajili wa muda wa vyama viwili ulifutwa baada ya kupoteza sifa za usajili wa muda na kushindwa kutimiza masharti ya maombi ya usajili wa kudumu. Vyama hivyo ni Tanzania Peoples Organisation for Democracy and Development (TAPODD) ambacho kilifutwa tarehe 31 Julai, 2007 na National Progressive Democratic Party (NPDP) kilichofutwa tarehe 16 Aprili, 2008. Aidha, Serikali ilitoa elimu ya uraia kuhusu faida na majukumu ya kila taasisi na mwananchi katika mfumo wa demokrasia kwa vyama vya siasa.

Shughuli za Bunge

18. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Bunge lako tukufu limeendelea kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba ya kutunga sheria na kuishauri Serikali. Mabadiliko ya Kanuni za Bunge yalifanyika ambapo Kamati za Kudumu za Bunge zilizopo sasa zinawawezesha Waheshimiwa Wabunge kuchambua kikamilifu masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa na kusimamia shughuli za utendaji wa Serikali kwa umakini zaidi. Aidha, Bunge lako tukufu lilipitisha Miswada ya Sheria 24, liliridhia Maazimio 14 yanayohusu masuala mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa na maswali ya msingi 970 yaliulizwa na kupatiwa majibu. Vilevile, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kumuuliza Waziri Mkuu maswali ya papo kwa papo Bungeni. Katika mwaka 2008/2009, Ofisi ya Bunge itaendelea kusimamia mipango ya mafunzo kwa watendaji, kuendeleza mahusiano na mabunge ya nchi nyingine na kuboresha huduma mbalimbali za kiutawala na elimu kwa wabunge.

Ofisi za Wabunge

19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali ilitenga shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Wabunge. Jumla ya majimbo 40, yakiwemo 32 ya Tanzania Bara na 8 ya Tanzania Visiwani yaliteuliwa kupata fedha za ujenzi wa ofisi hizo katika awamu ya kwanza. Hata hivyo, kutokana na ongezeko la gharama, mchanganuo wa kitaalam unaonyesha kuwa gharama halisi za ujenzi wa ofisi moja iliongezeka kutoka shilingi milioni 25 zilizokuwa zimekadiriwa awali hadi shilingi milioni 40. Katika mwaka 2008/2009, Serikali imetenga shilingi bilioni moja ili kukamilisha ujenzi wa ofisi 40 katika awamu ya kwanza na kuanza ofisi 10 za awamu ya pili. Suala hili litasimamiwa kikamilifu na Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Kiongozi ili kuona lengo hilo linafikiwa.

HALI YA UCHUMI

20. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa hali ya uchumi wetu kwa ujumla unaridhisha. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Uchumi, katika mwaka 2007 uchumi wetu ulikua kwa asilimia 7.1, licha ya kuwepo kwa misukosuko mbalimbali ya kiuchumi. Mfumuko wa Bei, ambao ulifikia asilimia 9 mwezi Machi 2008, umeendelea kuwa juu kufuatia kupanda kwa bei ya nafaka, mafuta ya petroli pamoja na bidhaa nyingine kutoka nje. Wataalam wa uchumi duniani wanaeleza kuwa matarajio ya mwenendo wa bei za bidhaa katika Soko la Dunia hususan bei za nishati na nafaka kwa mwaka ujao zitaendelea kupanda.

21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaweka mazingira mazuri yatakayowezesha sekta zote kukua kwa kasi inayoridhisha ili kufikia lengo tulilojiwekea la ukuaji halisi wa Pato la Taifa la asilimia 7.8. Changamoto iliyo mbele yetu ni kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi ni endelevu na wa viwango vikubwa kati ya asilimia 8 hadi 10. Viwango hivyo ndivyo vitakavyoboresha na kuendeleza huduma za jamii na kiuchumi na hatimaye kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa. Hivyo, sote tuongeze matumizi bora ya rasilimali zilizopo na jitihada zaidi zielekezwe kuongeza tija katika sekta za kilimo, miundombinu, madini na huduma za kijamii. Aidha, juhudi zielekezwe katika utoaji wa mikopo midogo ili kujenga na kuendeleza ujasiriamali kwa mtu mmoja mmoja au vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali na utoaji huduma.

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

22. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2006/2007, Serikali ilianza kutekeleza Mpango wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi kwa lengo la kuwashirikisha wananchi wengi zaidi katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Serikali ilitenga shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya awamu ya kwanza ya mpango huo ambapo Benki za CRDB na NMB ziliteuliwa kushiriki katika utekelezaji na ziliafiki kutoa mkopo mara tatu ya kiwango cha dhamana kilichokubalika kwa kutumia mitaji yao wenyewe. Katika awamu ya kwanza ya mpango huo, Benki hizo ziliweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 32.7 kwa wajasiriamali 44,256. Kutokana na mafanikio hayo, awamu ya pili ya utoaji mikopo kwa wajasiriamali ilizinduliwa mwezi Desemba 2007. Jumla ya asasi za kifedha 14 zilijitokeza kushiriki kwenye mpango huo ili kukopesha shilingi bilioni 10.5 zilizotengwa katika awamu ya pili. Hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 3.7 zimetolewa katika asasi hizo za fedha. Kati ya hizo, shilingi milioni 881.3 zimekopeshwa kwenye Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) mbalimbali hapa nchini. Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilipatiwa shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi wananchi wa Tanzania Visiwani.

23. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi umeonyesha mafanikio na changamoto kadhaa. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuwepo na ongezeko kubwa la mwamko wa wananchi kutumia huduma za kibenki na ari kubwa miongoni mwao kuhusu faida za kujiunga na SACCOS. Hii imetokana na jitihada za uhamasishaji kupitia kwa Waheshimiwa Wabunge na viongozi mbalimbali wa kitaifa, mikoa, wilaya na vijiji. Aidha, mpango huo umehamasisha na kuendeleza dhana ya wananchi kujiajiri kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayobuniwa na mtu mmoja mmoja au vikundi. Kutokana na uhamasishaji huo, miradi mingi mipya ya kiuchumi imeanzishwa na ile iliyokuwa inalegalega imefufuliwa hivyo kuongeza ajira na kipato kwa wananchi.

24. Mheshimiwa Spika, changamoto zilizojitokeza ni pamoja na wananchi wengi kujitokeza kuomba mikopo ikilinganishwa na kiasi kidogo cha fedha kilichotengwa. Changamoto nyingine ni wananchi wengi kutokuwa na elimu ya ujasiriamali inayowawezesha kubuni na kuandaa miradi mizuri inayokopesheka, kuiendesha kwa ufanisi pamoja na kupanga matumizi bora ya mikopo waliyokopeshwa na urejeshaji wake. Aidha, katika awamu ya kwanza ipo mikoa ambayo ilipata mgao wa fedha za mikopo chini ya kiwango cha shilingi milioni 500. Pia, zipo wilaya 21 ambazo hazikupata kabisa mikopo katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa matawi ya Benki za CRDB na NMB. Hata hivyo, baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza zimetafutiwa ufumbuzi wakati wa utekelezaji wa awamu ya pili. Eneo muhimu lililoshughulikiwa ni lile la kuhakikisha kuwa mikoa, wilaya na maeneo ambayo hayakunufaika na mpango huu katika awamu ya kwanza yanapewa kipaumbele. Katika mwaka 2008/2009, Serikali itaboresha zaidi utekelezaji wa mpango huu ili uwe na tija kubwa. Napenda kutumia fursa hii kuwahimiza wananchi kote nchini kuendelea kujiunga na SACCOS ili waweze kunufaika na mpango huu.

Kituo cha Uwekezaji Tanzania

25. Mheshimiwa Spika, jitihada za kutangaza vivutio vyetu zimewezesha kuongezeka kwa miradi inayowekezwa na wawekezaji mbalimbali hapa nchini. Katika mwaka 2007/2008, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kilisajili jumla ya miradi 902 yenye thamani ya Shilingi bilioni 8.1 ambayo imetoa ajira zipatazo 127,588. Kati ya miradi hiyo, miradi 483 ni ya Watanzania, 196 ni ya wageni na 223 ni ya ubia. Takwimu za kimkoa zinaonyesha kwamba mkoa wa Dar es Salaam uliongoza kwa kusajili miradi 502, Arusha miradi 158, Mwanza 51, Kilimanjaro 32 na Pwani 31. Mikoa mingine ni Shinyanga miradi 17, Morogoro 16, Mbeya 15, Tanga 14, Iringa 13, Kagera 12, Dodoma 11, Mara 9, Lindi 6, Mtwara 4, Tabora 4, Singida 2, Manyara 3, Rukwa 3, Ruvuma 1 na Kigoma 1. Sekta ya utalii ndiyo iliyoongoza kupata miradi mingi kwa kusajili miradi 275 ikifuatiwa na sekta ya viwanda yenye miradi 236 na sekta za nyumba na biashara ina miradi 125.

26. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kitaendelea kuitangaza nchi yetu kwa kutumia mitandao ya kimataifa; kuwaunganisha wawekezaji wadogo na wawekezaji wenye viwanda vikubwa hapa nchini ili waweze kushirikiana kibiashara na kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kukuza biashara zao. Natoa wito kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa Tanzania kutumia huduma zinazotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania ili waweze kujiendeleza kibiashara. Kituo hiki hakipo kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wa nje tu bali ni kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza mitaji yao hapa nchini. Aidha, mikoa itangaze vivutio na fursa za uwekezaji zilizopo katika mikoa hiyo kwa kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo tovuti na mikutano ya wafanyabiashara popote pale itakapofanyika.

Uimarishaji wa Sekta Binafsi

27. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuiwezesha kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi. Ili kupunguza vikwazo ambavyo sekta binafsi inakumbana navyo kama vile ukosefu wa fedha za kutosha za uwekezaji, kutokuwa na taarifa sahihi za masoko ya bidhaa za nje na teknolojia duni, Serikali imetoa udhamini wa mkopo wa dola za Marekani milioni 16 kutoka Benki ya Dunia kwa taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania. Kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 6 zitatumika kuwakopesha wafanyabiashara wadogo na wa kati. Chini ya mpango huo, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania itatoa asilimia 50 ya mtaji wa biashara inayokusudiwa kuendeshwa na wafanyabiashara watachangia asilimia 50 iliyobakia. Sehemu nyingine ya fedha hizo, kiasi cha dola za Marekani milioni 10 kitatumika kuviongezea uwezo vyuo na taasisi zinazotoa mafunzo ya ufundi ili viweze kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuandaa mipango ya biashara inayouzika. Natoa wito kwa wafanyabiashara kuchangamkia mikopo hii ili iwasaidie kukabiliana na vikwazo vinavyowazuia kufanya shughuli zao kwa ufanisi. Vilevile, taasisi na vyuo vya ufundi vitakavyonufaika na mpango huu vihakikishe kwamba mafunzo yatakayotolewa yatawasaidia wajasiriamali kukabiliana na ushindani wa kibiashara.

Baraza la Taifa la Biashara

28. Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Biashara ni chombo kinachounganisha Sekta Binafsi na Sekta ya Umma kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa Tanzania. Katika mwaka 2007/2008, Baraza liliendelea kuimarisha majadiliano kati ya Serikali na Sekta Binafsi ili iwe mhimili mkuu wa uchumi. Majadiliano hayo yalilenga kuboresha mazingira ya kuendesha biashara na uwekezaji. Aidha, jumla ya Mabaraza ya Biashara ya Mikoa 21 yameundwa Tanzania Bara na jitihada za kuanzisha Mabaraza ya Biashara ya Wilaya zimeanza. Madhumuni ya mabaraza haya ni kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji na kuibua fursa za uwezeshaji kiuchumi katika ngazi za chini.

29. Mheshimiwa Spika, vilevile, Baraza la Taifa la Biashara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi liliandaa midahalo mbalimbali ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi nchi nzima. Madhumuni ya midahalo hiyo ilikuwa ni kuainisha maoni na uelewa wa dhana nzima ya uwekezaji toka kwa wananchi na jinsi wanavyoweza kuibua miradi ya kuwaongezea kipato na hivyo kuwa na maisha bora. Midahalo ilifanyika katika ngazi ya wilaya na mikoa na hatimaye Mdahalo wa Kitaifa utafanyika mara baada ya majadiliano ya Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Matokeo ya mdahalo huo yatafikishwa kwenye Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara kwa madhumuni ya kupanga utekelezaji.

30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Baraza la Taifa la Biashara, litafanya mkutano wake wa tano utakaohusisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana mawazo na uzoefu wa jinsi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Aidha, Baraza litasimamia na kuimarisha shughuli za Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya pamoja na shughuli za vikundi kazi vikuu vilivyoanzishwa na Baraza vya kuboresha Kilimo, Kukuza Viwanda na Mauzo ya Nje, Ardhi, Utalii, Rasilimali Watu, Huduma za Fedha, Miundombinu na Uwezeshaji wananchi kiuchumi.




Programu ya Uendelezaji wa Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo

31. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali kupitia Programu ya Uendelezaji wa Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo imewezesha kuundwa na kuimarishwa kwa vikundi vya wazalishaji, wafanyabiashara na wasindikaji wadogo vipatavyo 232 katika wilaya tisa za Chunya, Ileje, Kyela, Makete, Njombe, Korogwe, Simanjiro, Mwanga na Moshi Vijijini. Vikundi hivyo vimejengewa uwezo kwa njia ya mafunzo ya mbinu mbalimbali za kutafuta masoko na kuviunganisha na masoko ya mazao yao. Aidha, vikundi 1,076 vimepatiwa mafunzo ya ujasiriamali, uongozi, biashara, uchaguzi wa mazao ya biashara, utafiti shirikishi wa masoko, ukokotoaji wa gharama na masuala mtambuka, yakiwemo ya jinsia, UKIMWI na mazingira.

32. Mheshimiwa Spika, ili kusaidia jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa Wakulima, Programu imehamasisha matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani. Chini ya Mfumo huu, wakulima huhifadhi mazao ghalani na kupewa stakabadhi ambazo wanaweza kuzitumia kama dhamana kwa mikopo watakayoiomba benki na kurejesha mkopo huo baada ya kuuza mazao yao wakati bei ikiwa nzuri. Utekelezaji wa mfumo huo umefanyika katika maghala manane katika wilaya za Hanang (2), Mbarali (2), Songea, Mbozi, Mufindi na Sumbawanga Vijijini. Wakulima 879 wamepatiwa mikopo ya thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa kutumia mfumo huu.

33. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Programu hii imekarabati barabara za Vijijini zenye urefu wa Kilomita 670 ili kuboresha miundombinu inayohusiana na masoko ya mazao ya kilimo na kurahisisha muingiliano baina ya Wazalishaji, Wasindikaji na Wafanyabiashara Vijijini. Aidha, jumla ya masoko 14 yamejengwa na yamekamilika. Masoko hayo ni Kikatiti (Arumeru), Kwa Sadala (Hai), Inyala (Mbeya), Gallapo (Babati), Katesh (Hanang), Monduli (Monduli) na Matai (Sumbawanga Vijijini). Masoko mengine yaliyokamilika ni ya Tarakea (Rombo), Kiwira (Rungwe), Soni (Lushoto), Tunduma (Mbozi), Makita (Mbinga), Mlangali (Ludewa) na Mtindiro (Muheza). Masoko ya Hedaru (Same), Kinyanambo (Mufindi) na Dongobesh (Mbulu) yapo katika hatua za mwisho za kukamilishwa ujenzi.

34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea kuimarisha vikundi vya wazalishaji, wafanyabiashara na wasindikaji wadogo. Aidha, itaanza utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani kwenye maeneo ambayo yameonyesha kuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula ya Kirando (Nkasi), Ipinda (Kyela), Majimoto (Mpanda), Mpitimbi (Songea Vijijini), Monduli (Monduli) na Bashay (Mbulu). Vilevile, jumla ya kilomita 323.6 za barabara zitakarabatiwa na masoko 7 yatajengwa katika wilaya za Chunya, Ileje, Kyela, Makete, Njombe, Korogwe na Simanjiro.

Programu ya Huduma za Kifedha Vijijini

35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali chini ya Programu ya Huduma za Kifedha Vijijini, imefanikiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kipato kwa wananchi wanaoishi vijijini. Kwa kutumia mbinu shirikishi na mafunzo kwa wanachama wa SACCOS, kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanachama, hisa, amana na akiba. Aidha, ushiriki wa wanawake umeongezeka ikiwa ni pamoja na kushika nyadhifa mbalimbali katika Asasi hizo. Programu pia imeimarisha Benki za wananchi za Mwanga, Mufindi na Mbinga na Benki ya Ushirika Kilimanjaro kwa kuzipatia magari, kutoa mafunzo kwa watumishi na kuimarisha usimamizi wa mifumo ya fedha.

36. Mheshimiwa Spika, Programu ilitoa mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati za Mikopo na Maafisa wa Mikopo 1,100 wa SACCOS 276. Mafunzo hayo yaliwawezesha kuelewa masuala ya Dhana, Kanuni, Misingi na Taratibu za kutoa mikopo pamoja na kusimamia na kuhakikisha mikopo inarejeshwa. Aidha, Vikao vya pamoja kati ya Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya za Mikoa ya Mbeya, Iringa, Songea, Dodoma, Singida na Kilimanjaro viliitishwa kuzungumzia jinsi Wilaya zitakavyochukua hatamu za utekelezaji wa shughuli za kukuza na kuendeleza Asasi za Fedha Vijijini baada ya Programu kumaliza muda wake. Vilevile, Wahasibu 276 pamoja na Viongozi 100 walipewa mafunzo ya SACCOS.

37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Programu itaboresha usimamizi na utendaji wa Asasi Ndogo za Kifedha, kuimarisha mifumo ya kifedha Vijijini na kuwajengea uwezo wananchi wa Vijijini ili waweze kujiunga na kushiriki katika shughuli za SACCOS. Aidha, Programu itaendelea kuimarisha Benki za wananchi na kusaidia mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya wananchi Njombe.

38. Mheshimiwa Spika, Programu hizi zimekuwa zikisaidia juhudi za Serikali za kuondoa umaskini kwa kuwawezesha wananchi wa vijijini kuongeza kipato kwa kupata huduma za mikopo kupitia Asasi za Kifedha na masoko ya uhakika ya mazao yao. Kutokana na utekelezaji wa Programu hizi mbili, uzoefu uliopatikana umebaini kuwepo kwa mafanikio makubwa katika Wilaya ambazo Programu hizi zinatekelezwa. Baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la asasi za kifedha, wanachama na mitaji. Aidha, kwa kuimarisha Benki za wananchi, SACCOS nyingi zimeweza kupata mikopo kutoka katika Benki hizo ambayo imewekezwa katika miradi mbalimbali ya uzalishaji. Eneo jingine lililoonyesha mafanikio ni lile la kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani. Kupitia mfumo huu, wananchi wengi wameweza kupata mikopo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Changamoto kubwa zilizo mbele yetu ni kueneza uzoefu huo tuliopata katika wilaya zote nchini. Ninazisihi Halmashauri za Wilaya hususan zile za jirani kutembelea Halmashauri ambazo zinatekeleza programu hizo kwa lengo la kuona na kujifunza mafanikio yaliyopatikana na baadaye kuyatekeleza katika Halmashauri zao.

Huduma za Kiuchumi

Barabara Kuu na za Mikoa

39. Mheshimiwa Spika, maendeleo ya uchumi wa Nchi yoyote ile hutegemea sana mtandao mzuri wa barabara. Barabara husaidia shughuli za kiuchumi na kijamii kustawi, kushamiri na kuchangia katika ukuaji wa uchumi na mapato ya watu. Katika mwaka 2007/2008, Serikali ilikamilisha ujenzi wa barabara za Isuna - Singida (Km. 63), Singida - Shelui (Km. 110), Geita – Buzirayombo (Km. 100), Kyamiorwa - Buzirayombo (Km. 120), Nangurukuru – Mbwemkuru (Km. 95), Mbwemkuru – Mingoyo (Km. 95), Mkuranga – Kibiti (Km. 79) na Tarakea - Rongai – Kamwanga (Km. 32). Jumla ya kilomita 330.4 zilifanyiwa matengenezo ya muda maalum na kilomita 79.0 zilifanyiwa matengenezo katika sehemu korofi. Aidha, jumla ya madaraja na makalvati yapatayo 492 yamefanyiwa matengenezo ya kawaida katika barabara kuu na barabara za mikoa.

40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara kuu. Baadhi ya Barabara hizo ni Manyoni - Isuna (Km. 54), Mbeya - Lwanjilo (Km. 36), Nelson Mandela (Km. 15.6), Kurasini – Mbagala (Km. 11.6) Masasi - Mangaka (Km. 54), Usagara – Sengerema - Geita (Km. 90) na Mwandiga – Manyovu (Km. 60). Aidha, kwa kupitia msaada wa Serikali ya Marekani kupitia Millennium Challenge Corporation (MCC), Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara za Tunduma – Sumbawanga (Km. 224.5), Songea – Namtumbo (Km. 70), Peramiho – Mbinga (Km. 80), Tanga – Horohoro (Km. 65), na kukarabati uwanja wa ndege wa Mafia.

Barabara za Vijijini

41. Mheshimiwa Spika, barabara za vijijini ni muhimu katika kuwasaidia wananchi wanaoishi vijijini hasa wakulima kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi kwenye masoko. Ili kufikia azma hiyo, katika mwaka 2007/2008, Serikali za Mitaa zilitengewa jumla ya Shilingi bilioni 65 kutoka katika Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 37,229. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei, 2008 kiasi cha shilingi bilioni 48.2 kilikuwa kimepelekwa kwenye Halmashauri na kufanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 7,592 yakiwemo matengenezo ya kawaida kilomita 4,988, matengenezo madogo madogo kilomita 2,099, matengenezo ya muda maalum kilomita 505 pamoja na matengenezo ya madaraja na makalvati.

42. Mheshimiwa Spika, kupitia Programu ya Usafiri katika Serikali za Mitaa, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 8.2 kwa ajili ya ukarabati wa barabara. Hadi kufikia mwezi Aprili 2008 kiasi cha shilingi bilioni 5.8 kilikuwa kimepelekwa kwenye Halmashauri zote nchini kusaidia kuboresha kilomita 1,000 za maeneo korofi. Aidha, Serikali iliendelea kutekeleza Programu ya Usafiri na Uchukuzi Vijijini. Programu hii ilitumia jumla ya shilingi bilioni 1.9 katika Halmashauri 27 ili kufanya matengenezo ya barabara za jamii, ujenzi wa madaraja madogo na kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu matumizi bora ya teknolojia rahisi.

43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea kufanya matengenezo ya barabara katika Serikali za Mitaa. Jumla ya Shilingi bilioni 65 kutoka kwenye Mfuko wa Barabara zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Vijijini. Aidha, kupitia Programu ya Usafiri katika Serikali za Mitaa, jumla ya Shilingi bilioni 16.8 zitapelekwa katika Halmashauri kwa ajili ya matengenezo ya barabara, maeneo korofi, madaraja na uwekaji wa makalvati. Programu ya Usafiri na Uchukuzi Vijijini imetengewa shilingi bilioni 1.8 ili kuboresha usafiri vijijini katika Halmashauri 55. Fedha hizi zikisimamiwa vizuri barabara nyingi za vijijini zitaimarika na kupitika kwa wakati wote.

Usafiri Katika Jiji la Dar es Salaam

44. Mheshimiwa Spika, Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na tatizo kubwa la usafiri na usafirishaji kutokana na ongezeko la watu na magari. Katika jitihada za kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na maboresho ya barabara zinazoingia na kutoka barabara kuu na kuimarisha usimamizi wa Sheria ya Usalama Barabarani. Pamoja na hatua hizo, Serikali imekamilisha maandalizi ya Mpango Kamambe wa Usafirishaji kwa Jiji la Dar es Salaam. Mpango huu umeainisha kwa kina mikakati ya muda wa kati na mrefu wa kuondoa kero ya usafiri na msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam. Pamoja na jitihada hizi za Serikali, napenda kusisitiza kuwa, wakati mwingine msongamano wa magari unatokana na uendeshaji wa kibabe. Hivyo, natoa wito kwa madereva wote kuzingatia Sheria ya Usalama Barabarani na askari wa usalama barabarani wasimamie kikamilifu Sheria hiyo. Aidha, adhabu kali zaidi zitolewe kwa wale watakaokiuka Sheria hiyo.

45. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi Jijini Dar es Salaam (Dar es Salaam Rapid Transport-DART) unaendelea vizuri. Usanifu wa kina utakaowezesha kujengwa kwa miundombinu inayokidhi watumiaji wote wa barabara na matumizi ya mabasi yenye ujazo mkubwa wa kupakia abiria umekamilika. Jumla ya gharama za mradi huu katika awamu ya kwanza ni dola za Marekani milioni 158.2. Kati ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania itatoa dola za Marekani milioni 10, Benki ya Dunia itatoa dola za Marekani milioni 110 na Sekta Binafsi itawekeza kiasi cha dola za Marekani milioni 38.2 kwa kununua mabasi na kujenga mfumo imara wa kukusanya nauli. Awamu ya Kwanza ina urefu wa kilometa 21 na ina vituo vidogo 29, vituo vikubwa 5 na maeneo mawili ya maegesho na matengenezo. Fidia kwa wananchi ambao mali zao zinaathiriwa na ujenzi wa miundombinu ya DART zinaendelea kulipwa na zoezi hilo litakamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2008. Ujenzi wa miundombinu utaanza katika mwaka 2008/2009 na inategemewa utachukua muda wa miezi 24.

Vivuko

46. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha huduma ya Vivuko Nchini kwa kununua Vivuko vipya na kukarabati vilivyopo. Vivuko vipya vilivyonunuliwa ni vya Kigongo – Busisi chenye uwezo wa kubeba tani 250, kivuko cha Kilombero chenye uwezo wa kubeba tani 50 na Kivuko cha Kigamboni chenye uwezo wa kubeba tani 500. Aidha, Serikali imenunua kivuko cha Ruhuhu chenye uwezo wa kubeba tani 50 kwa ajili ya wananchi wa Wilaya za Mbinga na Ludewa. Katika mwaka 2008/2009, kivuko kipya chenye uwezo wa kubeba tani 40 kitakachotoa huduma kati ya Nyakalilo na kisiwa cha Kome kitanunuliwa na kivuko kipya cha Pangani chenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 50 kinaendelea kuundwa. Vilevile, vivuko vya M.V. Alina cha Dar es Salaam na Rugezi - Kisorya vimefanyiwa matengenezo.

Nishati

47. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na mipango ya usambazaji wa Umeme kwa wananchi Mijini na Vijijini. Katika mwaka 2007/2008, Serikali imeipatia TANESCO fedha za kununua mitambo mipya ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta ya dizeli yenye uwezo wa kuzalisha KVA 1,200 kwa ajili ya mji wa Mbinga. TANESCO pia imekamilisha kazi ya kuweka nyaya za kusambaza umeme katika mji wa Ludewa. Aidha, kwa kutumia fedha za Mfuko wa Nishati Vijijini, Wakala wa Nishati Vijijini ilifanya upembuzi yakinifu katika maeneo ya Kilolo, Mbinga, Mto wa mbu, Bahi, Uyui, Mkinga, Simanjiro na Kilindi. Serikali pia imekamilisha upembuzi yakinifu wa Mradi wa North- West Grid Study unaojumuisha Mikoa ya Kigoma, Kagera na Rukwa. Vilevile, shughuli za Mradi wa Uendelezaji Huduma za Nishati Vijijini unaohamasisha Soko la Umemenuru zimezinduliwa katika Mikoa ya Tanga, Morogoro, Kigoma, Pwani, Rukwa na Mtwara.

48. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Nishati pia itafaidika na msaada wa Serikali ya Marekani kupitia Millennium Challenge Corporation (MCC). Kiasi cha dola za Marekani milioni 206 kutoka MCC kitatumika kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Morogoro, Dodoma na Tanga. Vilevile, kiasi cha dola za Marekani milioni 63.1 kitatumika katika ujenzi wa njia ya umeme wa chini ya maji kwenda Zanzibar. Aidha, kiasi cha Dola za Marekani milioni 53.7 kitatumika kuzalisha umeme wa megawati 8 kutokana na nguvu za maji katika mto Malagarasi.

49. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itakamilisha ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Somanga Fungu. Mradi huu utanufaisha maeneo ya Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje, Somanga, Kibiti na maeneo mengine ya jirani. Serikali pia itakamilisha uwekaji umeme katika maeneo ya Kilolo, Mbinga, Mto wa Mbu, Bahi, Uyui, Mkinga, Simanjiro na Kilindi. Aidha, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini, Serikali itaongeza kasi ya usambazaji wa Nishati Vijijini chini ya Mradi wa Uendelezaji na Kupanua Wigo wa Upatikanaji na Usambazaji wa Nishati Nchini.

Mawasiliano

50. Mheshimiwa Spika, shughuli nyingi katika Sekta ya Mawasiliano zinaongozwa na Sekta Binafsi ambazo kwa ujumla zimeonyesha mafanikio makubwa. Kampuni za Simu za Mkononi zimepanua huduma za mitandao yao hadi Vijijini na hivyo kuwaongezea Watanzania wigo wa mawasiliano. Takwimu zinaonyesha kwamba Wateja wa simu za mkononi wameongezeka kutoka milioni 5.7 mwaka 2006 hadi milioni 8.5 mwaka 2007. Hii ni dalili njema kwani mawasiliano ni kichocheo muhimu cha biashara na hupunguza ulazima wa safari kutoka eneo moja kwenda jingine na hivyo kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi. Miundombinu ya huduma za utangazaji pia iliboreshwa na matokeo yake ni kupanuka kwa maeneo yanayofikiwa na huduma za utangazaji unaotolewa kwa njia za Redio na Luninga na hivyo kuwafikia wananchi wengi hususan waishio Vijijini.

51. Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliendelea na mchakato wa kuunda Mfuko wa Mawasiliano Vijijini. Mfuko huu utasaidia kufikisha huduma za mawasiliano Vijijini kwa kuwapatia ruzuku wawekezaji walio tayari kupeleka miundombinu na huduma za mawasiliano sehemu zote ambazo hazina mvuto wa kibiashara. Vilevile, Serikali iliendelea kuimarisha vituo vya Mawasiliano Nchini vikiwemo vya Dar es Salaam, Sengerema, Mpwapwa, Kasulu, Mtwara, Kinampanda mkoani Singida na Wino mkoani Ruvuma kwa ajili ya wakulima wa Kahawa. Vituo hivyo vitatumiwa na jamii katika kukuza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa ajili ya biashara, masomo, afya na utawala.

52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaanza utekelezaji wa awali wa ujenzi na uendelezaji wa Mkongo wa Kitaifa wa Mawasiliano na kuratibu uanzishwaji wa mfumo mpya wa anuani na namba za posta nchini ili kurahisisha na kuboresha huduma zitolewazo na sekta nyingine. Aidha, vituo zaidi vya mawasiliano vitaanzishwa katika mikoa mingine kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi hususan makundi ya wasiojiweza, wanawake na wengine waishio sehemu za vijijini. Vituo hivyo vitawawezesha wananchi kupata habari muhimu za kijamii na kiuchumi.

Ardhi

53. Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kwamba ardhi ni rasilimali ya msingi kwa maendeleo ya Taifa letu na ni tegemeo kubwa la wananchi wengi kwa kuzalisha mazao ya chakula na biashara. Ardhi ikigawanywa na kutumiwa bila utaratibu unaokubalika na jamii huwa chanzo kikubwa cha migogoro ya mipaka. Kwa upande mwingine, ardhi ikitumiwa holela husababisha uharibufu wa mazingira, mmomonyoko wa ardhi na hivyo kupunguza rutuba ya ardhi na hatimaye Nchi kuwa jangwa. Hivyo, Serikali ina wajibu wa kuhakikisha ardhi yetu, ambayo haiongezeki, inatumiwa kwa busara ili iweze kuendelea kuwa rasilimali endelevu kwa maendeleo ya sasa na ya vizazi vijavyo.

54. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumeshuhudia kuongezeka kwa migogoro ya ardhi inayosababishwa na jamii za Wakulima na Wafugaji kugombea maeneo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na maendeleo. Aidha kumekuwepo na migogoro ya mipaka kati ya Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji. Serikali imebaini kuwa sababu kuu za migogoro hiyo ni pamoja na kung’olewa au kupotea kwa alama za mipaka na ukuaji holela wa Vijiji kiasi cha kuingilia maeneo mengine ya kiutawala kama vile maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa au hifadhi ya vyanzo vya maji. Vilevile, kumekuwepo na ufahamu mdogo wa baadhi ya wananchi na watendaji juu ya mipaka ya maeneo yao ya kiutawala kutokana na ukweli kwamba, maelezo ya mipaka yaliwekwa miaka mingi iliyopita. Katika maeneo ya Mijini kumekuwa na ukiukwaji wa Sheria na Taratibu za Mipango Miji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba bila vibali vya Mamlaka ya Miji husika.


55. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na matatizo hayo ya ardhi, katika mwaka 1995, Serikali iliandaa Sera ya Ardhi ambayo utekelezaji wake ulianza kwa kutunga sheria mbalimbali. Maudhui ya Sheria hizo ni kutoa maelekezo ya Taratibu na Kanuni za umiliki na matumizi endelevu ya ardhi yetu. Maandalizi ya Sera na Sheria hizi yalishirikisha Wadau wengi na yamezingatia mabadiliko ya kiuchumi na mahitaji ya utandawazi. Sheria hizo zimeanza kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuunda Vyombo vya Usimamizi wa utekelezaji wake. Vyombo hivyo ni pamoja na Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi na Mabaraza ya Ardhi. Tume ina jukumu la kusimamia utayarishaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi na Mabaraza ya Ardhi yanashughulikia Mashauri ya migogoro ya ardhi.

56. Mheshimiwa Spika, Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ikitekeleza majukumu yake ya kupanga matumizi bora ya ardhi ipasavyo katika ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya, Miji na Vijiji, itazuia kwa kiasi kikubwa kutokea migogoro ya ardhi Nchini. Vilevile, Mabaraza ya Ardhi yakifanya kazi zake kwa ufanisi yataharakisha uamuzi wa Mashauri ya Ardhi na hivyo kuendeleza amani Nchini. Hali hii itawavutia Wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika mashamba ya biashara, viwanda na mahoteli katika maeneo ambayo yametengwa na kupimwa kwa shughuli hizo.

57. Mheshimiwa Spika, uzoefu uliopatikana katika zoezi la kuwahamisha Wafugaji na mifugo yao kutoka Bonde la Ihefu umedhihirisha umuhimu wa kuwashirikisha Wadau mbalimbali katika upangaji wa matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na Viongozi wa Mikoa, Wilaya, Serikali za Mitaa na Vijiji. Katika zoezi hilo, Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na Serikali za Vijiji iliweza kuainisha maeneo ya kutosha ya kuhamishia mifugo katika Wilaya za Kisarawe, Rufiji, Lindi, Nachingwea na Kilwa. Maeneo hayo ya malisho yaliweza kupatikana baada ya Halmashauri hizo kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ya Wilaya zao.

58. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mafanikio yaliyopatikana katika utaratibu Shirikishi wa kutayarisha Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi chini ya uratibu wa Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi; naelekeza kwamba, kila mwaka Halmashauri zitenge fedha za kutosha kwa ajili ya utayarishaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi. Zoezi hili liende sambamba na upimaji wa viwanja mijini na mashamba makubwa ya kilimo na ufugaji. Aidha, Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi itaimarishwa ili kuiwezesha kuratibu utayarishaji na usimamizi wa utekelezaji wa mipango hiyo muhimu. Lengo ni kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa kila Halmashauri na kila Kijiji na Miji yote. Zoezi hili liende sambamba na uboreshaji wa Kumbukumbu za Ardhi na ujenzi wa Masjala za Ardhi katika ngazi za Wilaya na Vijiji ili kupunguza migogoro ya miliki za Viwanja na mashamba.

59. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kutoa rai kwa wananchi na Viongozi wa ngazi zote kutoa ushirikiano katika utatuzi wa migogoro ya ardhi. Katika kusuluhisha migogoro hiyo, ni vyema tukajenga utamaduni wa kukaa kwa pamoja na kumaliza matatizo kabla hayajawa makubwa na kuleta athari kwa wananchi. Vilevile, napenda kutoa tahadhari kwa wananchi ambao wanavamia ardhi iliyokwishapimwa na kuendeleza makazi na kudai fidia pale wanapoondolewa Kisheria. Serikali haitavumilia ukiukwaji huu wa sheria na taratibu za nchi na haitasita kuwachukulia hatua za nidhamu mara moja watumishi watakaobainika kutokuwa waadilifu katika utoaji wa huduma za ardhi.

SEKTA YA UZALISHAJI MALI

Kilimo

60. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali ilipanga kutoa mbolea ya ruzuku kiasi cha Tani 89,820. Hadi kufikia mwezi Mei 2008 tani 74,503, sawa na asilimia 83 ya lengo zilikuwa zimesambazwa. Vilevile, jumla ya Tani 3,222 na Lita 133,463 za dawa ya korosho zilisambazwa kwa utaratibu wa ruzuku. Bodi ya Pamba ilinunua na kusambaza dawa za kuulia wadudu aina ya acrepacks 500,000 zenye thamani ya Shilingi bilioni 1.4. Aidha, jumla ya Makampuni 12 yalisaini Mkataba na Serikali wa kusambaza Tani 1,770 za mbegu za Mazao ya Mahindi, Mtama na Alizeti. Hadi mwezi Aprili 2008, jumla ya Tani 1,170 za mbegu sawa na asilimia 66 zilifikishwa katika vituo 21 vya usambazaji Mikoani ambapo Tani 969 zimeuzwa kwa Wakulima. Kwa upande wa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo, hadi kufikia mwezi Mei 2008, jumla ya Shilingi bilioni 3.1 kati ya Shilingi bilioni 3.5 zilizotengwa zimetolewa kwa ajili ya kutoa mikopo.

61. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza tija katika kilimo, hatua kabambe zitakazowezesha ongezeko la uzalishaji katika Sekta hiyo inabidi zichukuliwe. Hatua ya kwanza itakuwa ni kuhakikisha kwamba Wakulima wanapata mbolea nyingi kwa msimu ujao wa kilimo ili waweze kuongeza uzalishaji. Ili Wakulima wapate mbolea hiyo kwa wakati na kwa gharama nafuu, katika mwaka wa fedha 2008/2009, Serikali itatoa dhamana kwa Kampuni ya Mbolea Tanzania ili iweze kununua na kusambaza tani 150,000 za mbolea ya kupandia itakayozalishwa na Kiwanda cha Minjingu kabla ya msimu wa mvua kuanza. Aidha, itaongeza fedha za ruzuku kwa ajili ya usafirishaji wa mbolea ili kuwezesha vyombo vitakavyosafirisha mbolea yote inayozalishwa Minjingu pamoja na ile itakayoagizwa kutoka nje kusafirishwa na kuwafikia wakulima kwa bei nafuu.

62. Mheshimiwa Spika, tarehe 13 Juni, 2008 nilitembelea Kiwanda cha Mbolea Minjingu. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufanya mazungumzo na Uongozi wa Kiwanda hicho ili kubainisha mahitaji ya msingi ya muda mfupi na mrefu ambayo Serikali inaweza kuyatafutia ufumbuzi ili kukiwezesha kiwanda hicho kuzalisha mbolea nyingi zaidi. Aidha, nilitaka kujiridhisha kama kiwanda hiki kina uwezo wa kutengeneza mbolea ya kutosha ambayo kwa sasa tunaihitaji sana kutokana na unafuu wa bei ikilinganishwa na mbolea zinazoagizwa kutoka nje. Nimehakikishiwa na uongozi wa Kiwanda cha Minjingu kwamba kina uwezo wa kuzalisha mbolea ya Phosphate kati ya tani 150,000 hadi 200,000 kwa mwaka.

63. Mheshimiwa Spika, Serikali itakiwezesha Kiwanda cha Mbolea Minjingu kuagiza nje virutubisho maalum kama Sulphur, Nitrogen Potassium, Zinc na Copper ili viongezwe kwenye mbolea ya chengachenga inayozalishwa na kiwanda hicho. Hatua hii itaongeza ubora wa mbolea hiyo. Vile vile, Serikali itafanya mazungumzo na makampuni ya nje ambayo yako tayari kuwekeza nchini kwa ajili ya kuzalisha mbolea za aina mbalimbali. Lengo ni kuiwezesha nchi yetu katika kipindi kifupi kijacho kujitosheleza kwa mahitaji yake ya ndani ya mbolea na ziada kuuza nje.

Hali ya Chakula Nchini na Kupanda kwa Bei ya Nafaka

64. Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili 2008 wakati ninatoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge, nilielezea kwa undani hatari iliyopo mbele yetu kutokana na kupanda kwa bei ya vyakula duniani. Japokuwa takwimu za uzalishaji wa chakula zinaonyesha kwamba Taifa lingejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 106 kwa msimu wa 2007/2008, bado kulijitokeza uhaba wa nafaka uliosababisha bei za vyakula hivyo kupanda ghafla kuanzia mwezi Desemba 2007 hadi sasa. Sisi kama Taifa hatuna budi tujiandae katika kipindi cha muda mfupi na kujiwekea Mkakati wa Muda Mrefu wa kujitosheleza kwa chakula. Hatua za kuongeza mbolea ya ruzuku na kuhakikisha inamfikia Mkulima kwa wakati ni sehemu ya Mkakati wa kuongeza uzalishaji na kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada nje. Vilevile, katika bajeti ya mwaka 2008/2009, Kitengo cha Hifadhi ya Chakula kimeongezewa uwezo wa kifedha wa Shilingi bilioni 26.3 ili kiweze kununua Tani 100,000 za Mahindi na Tani 5,000 za Mtama na kuhifadhi kwa ajili ya siku zijazo. Nakiagiza Kitengo cha Hifadhi ya Taifa ya Chakula kinunue nafaka kutoka kwa wakulima kwa wakati ili kuzuia uwezekano wa wakulima kuuza chakula kwa walanguzi na nje ya nchi na baadaye kukinunua kwa bei kubwa zaidi.

65. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa sababu za kupanda kwa bei ya chakula duniani ni pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya chakula duniani, ukame na kupanda kwa gharama za uzalishaji kulikosababishwa na kuongezeka kwa bei ya mafuta. Aidha, bei zimepanda kutokana na uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula unaosababishwa na mashamba makubwa yenye ardhi nzuri kutumika kuzalisha mazao yanayotumika kuzalisha nishati mbadala itokanayo na mimea. Hali hii ya mahitaji makubwa ya ardhi nzuri kwa ajili ya uzalishaji wa nishati mbadala imeanza pia kujitokeza hapa nchini. Serikali inaandaa Sera na Mwongozo wa kuendeleza kilimo cha mazao ya nishati ili kisiathiri kilimo cha mazao ya chakula hapa Nchini. Vilevile, inaandaa mkakati wa kutambua maeneo yanayofaa kwa kilimo nchini ili kuwavutia Wawekezaji, katika kilimo cha mashamba makubwa. Hatua hizi zitasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya kilimo kwa ujumla pamoja na kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya ndani na ziada kuuza nje.

Umwagiliaji

66. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali imeendeleza hekta 11,352 za Umwagiliaji kwa kujenga miundombinu katika Kanda Saba za Umwagiliaji. Ili kuwezesha uendelezaji wa umwagiliaji katika kanda hizo, upembuzi yakinifu na usanifu wa skimu 88 za umwagiliaji na mabwawa saba umekamilishwa. Aidha, wakulima wadogo waliopo kandokando ya Ziwa Viktoria wamepatiwa vifaa vya umwagiliaji chini ya mradi wa kusaidia wakulima wadogo unaotekelezwa kati ya Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na FAO na Serikali ya Japan.

67. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itakarabati skimu 20 zilizochakaa pamoja na zilizoharibiwa na mafuriko ili kuendeleza eneo lipatalo hekta 15,000. Aidha, itakarabati mabwawa madogo 10 ili kuendeleza eneo la hekta 3,000 hususan katika maeneo yenye ukame na upimaji na usanifu wa skimu 68 zitakazowezesha kumwagilia hekta 200,000. Serikali pia itakamilisha Sera ya Umwagiliaji na Mkakati wa Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji Maji Nchini. Hatua hizi zitaenda sambamba na kufanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji.

Ushirika

68. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na utekelezaji wa Programu Kabambe ya Mageuzi na Maendeleo ya Ushirika. Katika mwaka 2007/2008, Vyama 960 vya aina mbalimbali vilikaguliwa na wananchi walihamasishwa kuanzisha na kujiunga katika SACCOS na kufanya idadi ya SACCOS nchini kuongezeka kutoka 3,469 mwezi Mei 2007 hadi 4,445 mwezi Desemba 2007. Vilevile, katika kipindi hicho, hisa za wanachama zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 18.2 hadi bilioni 21.7 na amana kutoka Shilingi bilioni 59.7 hadi shilingi bilioni 91.2.

69. Mheshimiwa Spika, Vyama Vikuu vya Msingi katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Dar es Salaam vimewezeshwa kufanya biashara ya ununuzi na uuzaji wa korosho kwa kukopeshwa fedha za udhamini wa Serikali kiasi cha Shilingi bilioni 28.4. Hadi mwezi Februari 2008, mikopo hiyo imewezesha ununuzi wa Tani 92,000 za korosho. Vyama vyote vimerejesha mikopo ya Benki na Halmashauri katika Mikoa hiyo zimelipwa jumla ya Shilingi bilioni 2.62 kama ushuru. Napenda niliarifu Bunge lako tukufu kwamba, katika mwaka 2007/2008, Serikali imetimiza ahadi yake ya kupunguza mzigo wa madeni wa Vyama vya Ushirika kwa kulipa jumla ya shilingi bilioni 2.5.

70. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea kuviimarisha Vyama vya Ushirika kwa kuwapa mafunzo Maafisa Ushirika na kuwapeleka Maafisa Ushirika katika Halmashauri zisizo na maafisa hao ili kutoa msukumo na kuimarisha usimamizi. Aidha, Serikali inaandaa utaratibu wa kuwa na chombo mahsusi kwa ajili kutoa mikopo kwa wakulima na wafugaji.

Madini

71. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa ukuaji wa Sekta ya Madini umeendelea kuwa mzuri kutokana na kupanuka kwa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini hasa dhahabu. Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 2.6 mwaka 2006 na kufikia asilimia 2.7 mwaka 2007. Mchango wa Sekta ya Madini utaendelea kukua zaidi kufuatia mabadiliko ambayo Serikali inaendelea kuyafanya katika kupitia Sera, Sheria na Kanuni za Madini ili itoe mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa Taifa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Rais chini ya Jaji Mark Bomani mwaka 2007 imemaliza kazi yake na kutoa mapendekezo yake mazuri ambayo yatazingatiwa katika maboresho ya Sera na Sheria ya Madini na Sekta ya Madini kwa ujumla. Wizara ya Nishati na Madini itatoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hili.

72. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali ilitenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika sehemu mbalimbali nchini kama ifuatavyo: sehemu za Kilindi, Kilosa na Morogoro Vijijini hekta 269,842; sehemu za Maganzo, Kishapu na Ibadakuli mkoani Shinyanga hekta 14,870; sehemu za Mererani mkoani Manyara hekta 10,490; sehemu za Rwamagaza na Nyarugusu wilayani Geita hekta 1,210; maeneo ya Ngasamo wilayani Magu hekta 229; sehemu za Rwabasi na Nyaserero wilayani Musoma Vijijini hekta 621; na maeneo ya Matabe Wilayani Chato hekta 880. Aidha, Serikali imewahamasisha wachimbaji wadogo katika maeneo mengi nchini kuanzisha SACCOS ili waweze kumiliki maeneo yaliyotengwa na kupimwa viwanja vya uchimbaji. SACCOS zipatazo 40 zimeanzishwa katika maeneo ya Rwamgaza na Nyarugusu wilayani Geita. Njia hii ya kuwaunganisha wachimbaji wadogo itawasaidia sana kupata mitaji mikubwa na kuzalisha kwa kiasi kikubwa zaidi.

73. Mheshimiwa Spika, kati ya mwezi Machi na Aprili, 2008, kulitokea maafa makubwa katika Migodi ya Mererani, Mkoani Manyara na Matundasi, Wilaya ya Chunya. Sababu ya msingi ya kutokea maafa haya ni usalama mdogo katika migodi hiyo. Hali hiyo ipo katika migodi mingine mingi ambayo inamilikiwa na Wachimbaji Wadogo. Suala hili la usalama mdogo katika migodi inabidi sasa lipatiwe ufumbuzi wa kudumu kwa kuhakikisha kwamba Wamiliki wa Migodi hii wanafuata Kanuni zilizopo za Usalama Migodini ili kuepuka maafa kama haya kutokea tena. Napenda ieleweke kwamba, baadhi ya Wamiliki wa Migodi wanaoitwa Wachimbaji Wadogo, si wadogo kiasi cha kushindwa kuwekeza kwenye miundombinu ya msingi ya usalama wa migodi. Maafisa wa Madini wahakikishe kwamba Wachimbaji hao wanazielewa Kanuni za Usalama na kuhakikisha zinafuatwa. Katika mwaka 2008/2009, Sera na Sheria ya Madini itafanyiwa mapitio kwa kuzingatia mapendekezo na maoni ya Kamati mbalimbali. Vilevile, Serikali itatoa mapendekezo ya kutunga Sheria ya Usonara na Uboreshaji Thamani ya Madini. Serikali pia itatenga maeneo zaidi kwa Wachimbaji Wadogo ikianzia na eneo lenye hekta 4,000 huko Winza, Wilaya ya Mpwapwa.

Viwanda

74. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuvutia Wawekezaji katika ufufuaji wa Viwanda vilivyopo na kujenga vipya katika Sekta zilizopewa kipaumbele. Utafiti uliofanyika katika Sekta hii mwaka 2007, ulibaini kuwepo kwa ongezeko la uanzishwaji wa Viwanda Vipya na ufufuaji wa Viwanda vya Umma vilivyobinafsishwa. Utafiti pia umebaini kwamba asilimia 97.6 ya Viwanda vipo mikononi mwa Sekta Binafsi; utumiaji wa uwezo katika Sekta ya Viwanda umekua kutoka wastani wa asilimia 37 mwaka 2005 hadi asilimia 43 mwaka 2008 na ongezeko la ajira la asilimia 8.7 kati ya mwaka 2006 na 2007. Ili kukuza Sekta ya Viwanda na kuvutia Wawekezaji, Serikali imeanza maandalizi ya Mkakati Unganishi na Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Viwanda. Mkakati huu unalenga kuendeleza viwanda vya msingi vitakavyoongeza kasi ya kuzalisha malighafi kwa ajili ya Viwanda vingine, jambo litakalosaidia kupunguza uagizaji wa malighafi kutoka nje ya nchi.

75. Mheshimiwa Spika, kupitia Mamlaka ya Mauzo Nje, Serikali imebainisha maeneo yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 2,000 katika mikoa saba ya Pwani, Kilimanjaro, Arusha, Mara, Kigoma, Mtwara, na Morogoro. Maeneo hayo ni kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya kuuza nje. Zoezi la kubainisha maeneo katika mikoa mingine linaendelea. Tangu mamlaka hiyo ianze kazi mwezi Oktoba 2006 hadi sasa viwanda 16 vimeanzishwa. Uzoefu wa nchi za China, Indonesia, Malaysia na Thailand ambazo uchumi wake umeendelea kukua kwa kasi kubwa zimewekeza sana kwenye maeneo ya aina hii. Katika Kongamano kati ya Wafanyabiashara wa China na Afrika lililofanyika mjini Arusha mwezi Aprili 2008, Wafanyabiashara kutoka China walionyesha nia ya kuwekeza katika Maeneo Maalum ya Biashara. Tutumie fursa hii kujifunza kutoka kwao ili tusaidiane nao katika kuanzisha na kuendesha maeneo haya. Aidha, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania washirikiane na Wafanyabiashara kuchangamkia fursa hii.

76. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itakamilisha Mkakati Unganishi na Mpango Kabambe wa kuendeleza Sekta ya Viwanda Nchini. Vilevile, Serikali itaanza kutekeleza Mpango Mkakati wa Kuongeza Uzalishaji na Kukuza Mauzo Nje kwa kubainisha maeneo yatakayoleta matokeo ya haraka. Serikali pia itaendelea kuhamasisha uanzishwaji na uendelezaji wa programu mbalimbali ili kuongeza mchango wa shughuli za Viwanda vidogo katika ukuaji wa uchumi.

Utalii

77. Mheshimiwa Spika, ukuaji wa Sekta ya Utalii ni muhimu sana katika jitihada zetu za kuongeza mauzo ya nje. Kwa kipindi cha mwaka 2007, mchango wa Sekta hiyo kwenye mauzo ya nje yalifikia dola za Marekani bilioni 1.04 sawa na asilimia 27.8 ya mauzo yote ya nje. Sekta hii ndiyo iliyotoa mchango mkubwa katika mauzo ya nje ikilinganishwa na Sekta nyingine zote. Mafanikio hayo yametokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali za kuitangaza nje biashara ya utalii pamoja na kushirikisha kikamilifu balozi zetu katika nchi mbalimbali duniani. Hata hivyo, Sekta hii inayo nafasi kubwa ya kuongeza zaidi mchango wake katika uchumi. Idadi ya Watalii watakaotembelea Bara la Afrika inakadiriwa kufikia milioni 77.3 itakapofika mwaka 2020. Hivyo, tuhakikishe kwamba ongezeko hili la watalii barani Afrika linafaidisha uchumi wetu. Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na balozi zetu ziandae mkakati maalum wa kutangaza vivutio vyetu hasa katika zile nchi ambazo watalii wengi hutokea.

78. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kwamba, zaidi ya asilimia 80 ya watalii duniani wanatokea katika nchi tajiri 20 tu, 17 kati ya hizo zikiwa ni za Ulaya, Marekani, Canada na Japan. Karibu nusu ya matumizi yote ya utalii hufanywa na watalii kutoka Marekani, Japan, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. Hii ni changamoto kwetu itakayotusaidia kutilia mkazo vipaumbele katika kutangaza Utalii wetu. Ni vyema hatua za makusudi kabisa zichukuliwe kuifanya Tanzania na Vivutio vyake vijulikane katika nchi hizi. Vilevile, ni muhimu kujitangaza katika nchi zile ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa kama vile India, Urusi na China na nyinginezo pasipo kusahau kutangaza vivutio vyetu kwa nchi za ukanda wetu na utalii wa ndani. Pamoja na hili, ni lazima miundombinu mingine inayowezesha Sekta ya Utalii kama vile usafiri, huduma za hoteli, fedha na nyinginezo ziimarishwe ili kusaidia watalii wawapo hapa nchini. Aidha, mafunzo katika fani ya utalii yaimarishwe ili kuweza kuwahudumia watalii vizuri. Tunaweza kupata watalii wengi sana lakini tusiweze kuendeleza ujio wao kutokana na huduma mbovu wanazopata wawapo hapa nchini. Ni vyema sasa tubadilike na tufahamu kwamba ongezeko la watalii hapa nchini litatokana na sisi wenyewe kujitangaza na huduma bora watakazopatiwa wawapo nchini.

Mifugo

79. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuipa msukumo Sekta ya Mifugo ili itoe mchango mkubwa zaidi katika uchumi. Katika mwaka 2007/2008, uzalishaji wa maziwa uliongezeka na kufikia lita bilioni 1.5 ikilinganishwa na lita bilioni 1.4 mwaka 2006/2007. Uzalishaji wa nyama pia uliongezeka kutoka Tani 370,566 hadi Tani 410,706. Ongezeko hili linatokana na kupanuka kwa wigo wa masoko mapya yanayonunua maziwa na nyama bora inayozalishwa Nchini. Vilevile, jumla ya ng’ombe 2,472 na mbuzi 733 wenye thamani ya Shilingi bilioni 1.3 wameuzwa Nchi za Comoro, Malawi na Burundi. Aidha, nyama ya kondoo, mbuzi na ng’ombe yenye thamani ya Shilingi milioni 376.6 imeuzwa Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Oman na Kuwait.

80. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, jumla ya hekta 930,276 zimepimwa na kutengwa na Halmashauri kwa ajili ya Wafugaji katika Wilaya 24 za Mikoa ya Dodoma, Iringa, Kagera, Kigoma, Lindi, Mbeya, Morogoro, Pwani, Singida na Tabora. Kuhusu chanjo za mifugo, jumla ya dozi milioni 8.1 zimezalishwa na kusambazwa sehemu mbalimbali Nchini. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza mikakati ya kudhibiti milipuko ya magonjwa Nchini. Mkakati wa kudhibiti ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa umetekelezwa na hadi mwezi Desemba 2007 jumla ya mifugo milioni 4.3 ilichanjwa. Aidha, jumla ya Wanafunzi 1,007 waliendelea na mafunzo ya Stashahada na Astashahada katika Vyuo sita vya Mifugo na kati ya hao, 393 wamehitimu na wataajiriwa katika Halmashauri. Pia jumla ya Wafugaji 21,106 walipatiwa mafunzo kuhusu ufugaji bora kwa njia za Mafunzo Vituoni na kupitia Semina mbalimbali.

Uvuvi

81. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uvuvi nayo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wetu na uwezo wa kuajiri Watanzania wengi. Katika kipindi cha mwaka 2007, mapato yatokanayo na mauzo ya mazao ya Uvuvi nje ya nchi yalikuwa shilingi bilioni 7.6 ikilinganishwa na shilingi bilioni 6.2 sawa na ongezeko la asilimia 21.7. Kwa kutambua umuhimu wa Sekta hiyo, Serikali imeandaa Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Uvuvi Usiozingatia Sheria. Mpango huo umeandaliwa ili kudhibiti uvuvi haramu na kuhakikisha usalama na viwango vya mazao ya uvuvi. Serikali pia imeanzisha mfumo wa kuratibu mwenendo wa meli baharini ikiwa ni hatua ya kudhibiti meli za nje zinazovua kiholela katika maji mengi kwenye Ukanda wa Bahari Kuu.

82. Mheshimiwa Spika, Serikali imejenga mialo 19 ya kupokelea samaki kwenye Ukanda wa Ziwa Viktoria. Vilevile, uchambuzi wa kujenga mialo sita katika Ukanda wa Bahari ya Hindi unafanywa ili kuwezesha wavuvi wadogo kushiriki katika uuzaji samaki katika soko la nje. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, nchi yetu imetimiza vigezo vyote vinavyohitajika katika Soko la Jumuiya ya Ulaya na kuruhusiwa kuuza samaki na mazao ya uvuvi katika soko hilo na mengineyo. Aidha, Maabara ya Taifa ya Uvuvi Nyegezi imethibitishwa na South African National Accreditation Services kuweza kuchunguza vimelea kwenye mazao yote ya chakula ikiwa ni pamoja na samaki. Ithibati hii imeifanya Maabara ya Nyegezi kutambulika kimataifa. Hii ni nafasi nzuri kwa nchi yetu kutumia ipasavyo mikataba ya biashara iliyopo kati ya nchi za Ulaya na Afrika kufanya biashara.

83. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itapitia na kuandaa Mikakati na Sheria zitakazoimarisha Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Lengo ni kuongeza uzalishaji, kuimarisha udhibiti, ubora na usalama, kuwa na masoko ya uhakika na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi. Aidha, Serikali itaboresha na kuongeza huduma za tafiti na ugani.

HUDuma za Jamii

Elimu ya Msingi

84. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali imeendelea kutekeleza Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM II). Idadi ya shule za msingi za Serikali imeongezeka kutoka Shule 14,400 mwaka 2006 hadi 15,300 mwaka 2007. Aidha, idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 7,959,884 mwaka 2006 hadi 8,316,925 mwaka 2007 sawa na ongezeko la asilimia 4.5. Vilevile, Serikali iliendelea kujenga na kupanua miundombinu katika shule za msingi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu 1,339, vyumba vya madarasa 2,313, matundu ya vyoo 847 na madawati 18,221. Sambamba na ujenzi wa miundombinu, Serikali iliendelea kununua vifaa vya kujifunzia na kufundishia vikiwemo vitabu vya ziada na kiada, matufe na vivunge vya sayansi na hisabati.

Elimu ya Sekondari

85. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali iliendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) na kuufanyia maboresho ili kwenda sambamba na ongezeko la idadi ya Wanafunzi wanaofaulu kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi. Usajili wa Shule za Sekondari umeongezeka kutoka Shule 2,289 mwaka 2006 hadi 3,485 mwaka 2007.
Idadi ya Wanafunzi wa kidato cha I - VI, katika Shule za Sekondari iliongezeka kutoka Wanafunzi 675,672 mwaka 2006 hadi 1,020,510 mwaka 2007. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine, iliendelea na ujenzi wa vyumba vya madarasa 777, nyumba za Walimu 1,470, maabara 84, maktaba 19, majengo ya utawala 9, ujenzi wa hosteli 12 kwa ajili ya wasichana kutoka katika mikoa ya wafugaji na iliyo nyuma kielimu na ukarabati wa miundombinu katika Shule 8 zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum. Sambamba na ujenzi huo, Serikali iliendelea kununua vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa lengo la kuboresha elimu ya sekondari.

Elimu ya Juu

86. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi pamoja na wadau wengine kugharamia Elimu ya Juu kupitia Mfuko wa Elimu. Katika mwaka 2007/2008, Mfuko wa Elimu ulipokea na kufadhili mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.8 kwa taasisi 205 katika ngazi zote za elimu. Vilevile, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imetoa mikopo kwa Wanafunzi 55,584 na imeendelea kukusanya madeni kwa Wanafunzi waliopewa mikopo kuanzia mwaka wa masomo 1994/1995. Hadi sasa kiasi cha Shilingi milioni 665.2 kimekusanywa na hivyo kufanya Bodi ya Mikopo iwe endelevu. Ili kuhakikisha kwamba idadi kubwa ya Wanafunzi waliomaliza Kidato cha Sita wanapata Elimu ya Juu, Serikali ilifungua rasmi Chuo Kikuu cha Dodoma. Katika mwaka 2007/2008, jumla ya Wanafunzi 1,116 walidahiliwa na katika mwaka 2008/2009, Chuo hicho kinatarajia kudahili wanafunzi 5,000.

87. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaongeza upatikanaji wa vifaa vya kutosha vya kujifunzia na kufundishia katika shule za msingi na sekondari. Aidha, itainua uwezo wa Vyuo vya Ufundi vya Halmashauri za Wilaya za Korogwe, Karagwe na Mwanga. Vilevile, Serikali itaendelea kutekeleza Mpango Kabambe wa Kuinua na Kuendeleza Mpango wa Elimu ya Juu na Ufundi (MMEJU). Serikali pia itaongeza udahili hadi kufikia asilimia 12.5 ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita ili wapate nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu.

Maji

88. Mheshimiwa Spika, maji ni miongoni mwa huduma muhimu kwa wananchi wote. Ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi mijini na vijijini kupata huduma ya maji safi na salama, Serikali iliendelea kukarabati miradi ya maji vijijini, kujenga mabwawa hususan katika maeneo yenye ukame na kuendeleza teknolojia ya uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua. Kufuatia jitihada hizo, upatikanaji wa huduma ya maji safi kwa Wwakazi wa vijijini umeongezeka kutoka asilimia 53.7 mwaka 2006 hadi asilimia 55.7 mwaka 2007 ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.0. Uzalishaji maji mijini uliongezeka kutoka mita za ujazo milioni 99.99 mwaka 2006 hadi milioni 100.2 mwaka 2007. Ongezeko hilo liliwezesha upatikanaji wa maji mijini kufikia asilimia 73.

89. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itakamilisha ujenzi wa matoleo ya maji na mifumo ya kusambaza maji kwa vijiji 54 na kuwaunganisha Wateja kwenye mfumo wa usambazaji maji. Aidha, itatekeleza mradi wa upanuzi wa milango ya maji na kulaza bomba kuu la majisafi lenye urefu wa kilometa 55 kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam. Serikali pia itaendelea na maandalizi ya ujenzi wa bwawa la Kidunda na kutambua wingi na ubora wa maji yaliyo chini ya ardhi katika maeneo ya Kimbiji na Mpera kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji Jijini Dar es Salaam.

Afya

90. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Afya na kuimarisha kiwango cha utoaji wa huduma za afya. Katika mwaka 2007/2008, Serikali ilianza kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano unaolenga kupunguza vifo vya Watoto Wachanga na Wanawake vinavyotokana na uzazi. Vilevile, Serikali ilikamilisha mipango ya utoaji wa huduma za upasuaji wa moyo humu Nchini na kazi ya upasuaji ilianza tarehe 21 Mei, 2008 katika Taasisi ya Mifupa ya MOI iliyoko Jijini Dar es Salaam. Hadi kufikia tarehe 13 Juni, 2008 wagonjwa 11 walifanyiwa upasuaji na wanaendelea vizuri. Serikali pia imeendelea kuzipatia dawa, vitendea kazi na vifaa vya kisasa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati za Umma hapa Nchini.

91. Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imekamilisha maandalizi ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Sera ya Afya. Lengo kuu la mpango huo ni kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kuhakikisha kuwa kila kijiji kinakuwa na zahanati, kila kata inakuwa na kituo cha afya na kila wilaya inakuwa na hospitali na kuhakikisha kwamba wataalamu wenye ujuzi wanaandaliwa kwa kila kituo cha kutolea huduma za afya. Hadi sasa, Serikali imefanikiwa kufungua zahanati 253 kati ya 652 zilizojengwa na TASAF na zahanati 399 zilizobaki majengo yake yako katika hatua za kukamilishwa. Vilevile, Serikali imekarabati hospitali 11 za mikoa ya Tabora, Lindi, Dodoma, Kigoma, Shinyanga, Singida, Rukwa, Mara, Iringa, Ruvuma na Tanga. Ukarabati wa Hospitali hizi uko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.

92. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano unaolenga kupunguza vifo vya Watoto na Wanawake na kuhakikisha kuwa huduma bora za Afya ya Uzazi na Mtoto zinatolewa bila malipo. Aidha, Serikali itaendelea kuhakikisha chanjo zinatolewa katika Vituo vya Mama na Mtoto na kwa sehemu zisizo na Vituo vya Mama na Mtoto, Huduma ya Mkoba itaendelea kutumika. Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 23 kwa ajili ya MMAM ili kuanza ujenzi wa Zahanati na ukarabati wa Hospitali za Wilaya. Halmashauri zitakazoanza kunufaika na Mpango huo zitajulikana baada ya mahitaji kuainishwa.

UTAWALA

Ulinzi na Usalama

93. Mheshimiwa Spika, hali ya mipaka ya nchi yetu kwa ujumla ni shwari. Vyombo vyetu vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi vimefanikiwa kudhibiti matukio ya uhalifu na ulinzi wa mipaka yetu. Vilevile, jeshi letu la wananchi limeweza kushirikiana na wenzao wa kimataifa katika ulinzi wa amani kwenye nchi zenye migogoro kama vile Lebanon, Sudan na Comoro. Nichukue fursa hii tena kulipongeza kwa dhati Jeshi la wananchi wa Tanzania kwa kazi nzuri waliyofanya ya kumng’oa madarakani kiongozi muasi wa kisiwa cha Anjuani, Kanali Mohamed Bakari.

94. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi liliendelea kufanya operesheni mbalimbali zenye lengo la kukomesha uhalifu. wananchi wameanza kufahamu umuhimu wa Mpango wa Ulinzi Shirikishi na ninapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa kushiriki katika Mpango huo ambao umepunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya uhalifu Nchini. Aidha, nalipongeza Jeshi la Polisi kwa juhudi wanazofanya za kulinda usalama wa raia na mali zao.

95. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Ulinzi na Usalama wa ndani ya Nchi na katika mipaka yetu na Nchi jirani utaimarishwa. Serikali itakamilisha mchakato wa kuandaa Sera za Usalama wa Raia, Polisi Jamii, Usalama Barabarani na Ulinzi wa Kampuni Binafsi. Aidha, Kitengo cha Intelijensia cha Jeshi la Polisi kitaimarishwa ili kiwe na uwezo mkubwa zaidi wa kubaini mipango ya matukio ya uhalifu. Vilevile, Serikali itavijengea uwezo Vyombo vya Ulinzi ili viwe imara na vyenye utaalam wa kisasa.

Mapambano Dhidi ya Rushwa

96. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali imeendelea na juhudi za Mapambano Dhidi ya Rushwa ndani na nje ya Taasisi zake. Hadi mwezi Machi 2008, jumla ya tuhuma 754 zilipokelewa. Aidha, tuhuma za Mikataba mikubwa na matumizi mabaya ya fedha za Serikali zilifanyiwa kazi. Kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kutoa mafunzo na Semina kwa Watumishi wa Umma na wananchi kuhusu Mapambano Dhidi ya Rushwa.

97. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, wananchi wataendelea kuelimishwa kuhusu Sheria mpya ya Kuzuia Rushwa. Ofisi saba ndogo za TAKUKURU zitafunguliwa katika maeneo ya Makambako, Ilula, Isaka, Holili, Mtukula, Kyaka na Tunduma. Uchunguzi wa tuhuma mbalimbali utafanyika na mkazo zaidi utawekwa kwa tuhuma za Mikataba Mikubwa ambayo inaiingizia Serikali hasara. Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwachukulia hatua za kisheria, kiutawala na kinidhamu wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo vya rushwa. Aidha, itajenga mazingira mazuri zaidi yatakayowapa wananchi uwezo, ari na ujasiri wa kutoa taarifa na kupambana na rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Programu ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa

98. Mheshimiwa Spika, Programu ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa Awamu ya Kwanza ilitekelezwa kuanzia mwaka 1999 hadi Juni, 2008. Lengo kuu la Programu hii lilikuwa ni kupeleka Madaraka kwa wananchi. Katika kufikia lengo hilo, Programu ililenga kuweka mgawanyo bora wa majukumu kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na kuimarisha usimamizi wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Vilevile, ililenga kuwajengea uwezo wa kitaalam Watumishi wa Serikali za Mitaa, kuboresha miundo ya Serikali za Mitaa na kuwawezesha wananchi kupanga, kufuatilia na kutekeleza mipango yao kulingana na vipaumbele vyao. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuimarika kwa nidhamu katika matumizi ya rasilimali za Umma na kuongezeka kwa kiwango cha ruzuku kutoka Shilingi bilioni 179.6 mwaka 2000/2001 hadi Shilingi bilioni 719.5 mwaka 2007/2008. Aidha, kumekuwepo na ufanisi katika Sekta za Elimu, Maji na Afya ambapo wananchi wameshirikishwa na hivyo, utoaji wa Huduma za Jamii umeanza kuimarika.

99. Mheshimiwa Spika, ili kulinda mafanikio yaliyopatikiana katika Awamu ya Kwanza, Serikali imeandaa Programu ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa, Awamu ya Pili ambayo itatekelezwa katika kipindi cha Julai, 2008 hadi Juni, 2013. Dira ya Programu hii ni kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kuongoza na kuwajibika katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kutoa huduma bora kwa lengo la kupunguza umaskini katika maeneo yao ya kiutawala. Lengo la Programu hii ni kupeleka Madaraka kwa wananchi ili waweze kushiriki na kuwajibika katika maamuzi yanayohusu maendeleo yao wenyewe.

Mfuko wa Pamoja wa Serikali za Mitaa

100. Mheshimiwa Spika, Serikali za Mitaa zimeendelea kufaidika na Mfuko wa pamoja ambao umesaidia kuharakisha mchakato wa maendeleo katika Serikali hizo. Mfuko huu umekuwa ukichangiwa na wahisani tangu mwaka 2004/2005 na hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 111.4 zimechangwa. Kwa kuwa mfuko huu utakoma mwaka 2013, Serikali imeanza kutafakari utaratibu endelevu wa kuugharamia kwa kufanya uchambuzi wa kitaalamu kwa nia ya kuangalia uwezekano wa kuanzisha mfuko kama huo ili kulinda mafanikio yaliyopatikana. Mfuko huo utasaidia kuhamasisha wananchi vijijini kushiriki kwa hali na mali katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika sekta za elimu, afya na barabara ambazo kwa sehemu kubwa zinachangia moja kwa moja katika kupunguza umaskini.

Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa

101. Mheshimiwa Spika, Halmashauri zenye sifa ya kupata ruzuku chini ya Mpango wa Kuzipatia Serikali za Mitaa Ruzuku ya Maendeleo na Ruzuku ya Kuzijengea Uwezo zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na kuongezeka kwa ufanisi na nidhamu katika matumuzi ya fedha. Katika mwaka 2004/2005, Halmashauri zilizopimwa zilikuwa 47 na zilizofaulu kupata ruzuku zilikuwa 25. Mwaka 2005/2006, Halmashauri zilizopimwa zilikuwa 113 na zilizofaulu kupata ruzuku zilikuwa 66. Mwaka 2006/2007, Halmashauri zilizopimwa zilikuwa 121 na zilizofanikiwa kupata ruzuku zilikuwa 84. Mwaka 2007/2008, Halmashauri zilizopimwa zilikuwa 121 na Halmashauri 109 zilifanikiwa kupata ruzuku. Katika mwaka 2008/2009, jumla ya Halmashauri 127 kati ya 132 zitapata ruzuku baada ya kupimwa na kufaulu kukidhi vigezo vya kupata ruzuku ya maendeleo na kujenga uwezo. Fedha hizi zitawezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo, kuwajengea uwezo wa kitaalamu na kitaaluma Watumishi wa Halmashauri.

Maslahi ya Madiwani

102. Mheshimiwa Spika, Serikali kimsingi imekubali kuboresha maslahi ya Madiwani kuhusu posho, matibabu, mazishi na unafuu wa kodi katika vyombo vya usafiri. Katika mwaka wa fedha 2008/2009, jumla ya shilingi bilioni 4.8 zimetengwa kwa ajili ya posho za Madiwani. Aidha, Serikali itaandaa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Bima ya Afya utakaowawezesha madiwani kupata matibabu kupitia Bima ya Afya. Vilevile, marekebisho ya Sheria ya Fedha yatafanyika ili madiwani wafaidike na msamaha wa kodi kwa vyombo vya usafiri.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

103. Mheshimiwa Spika, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika mwezi Oktoba 2009 katika Vijiji 10,368, Mitaa 1,785 na Vitongoji 50,832. Ili kufanikisha maandalizi ya uchaguzi huo, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4. Shughuli kubwa zitakazofanyika katika maandalizi hayo ni pamoja na kuhakiki mipaka ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa; kufanya mapitio ya Kanuni za Uchaguzi, na kufanya Mikutano ya Mashauriano na Vyama Vya Siasa. Aidha, shughuli nyingine zitakazofanyika ni kukusanya maoni ya Wadau mbalimbali kuhusu mapendekezo ya kutumia Daftari la Kudumu la Wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuchapisha vitabu vya Kanuni na Fomu za Uchaguzi. Nafurahi kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba tayari mchakato wa ushirikishwaji wa wadau umeanza na maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yanaendelea vizuri.

Muundo wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam

104. Mheshimiwa Spika, muundo wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam ni tofauti na Majiji mengine ya Afrika Mashariki. Ndani ya Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam kuna Halmashauri za Manispaa tatu zenye Mamlaka kamili ya kutekeleza majukumu ya Mamlaka za Miji kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa Namba 8 ya mwaka 1982. Uzoefu uliopatikana kwa miaka nane ya utekelezaji wa muundo mpya wa Jiji la Dar es Salaam, unaonyesha kuwa kuna matatizo ya kiuendeshaji na hivyo kutokukidhi matarajio yaliyokusudiwa ya kutoa huduma bora kwa wananchi. Aidha, matatizo mengine yanayolikabili Jiji la Dar es Salaam ni pamoja na miundombinu ya barabara isiyokidhi mahitaji yanayopanuka kila siku, miundombinu isiyotosheleza ya maji safi na taka, na ukuaji wa jiji usioenda sambamba na utoaji huduma kwa wananchi. Hali hii inalifanya Jiji la Dar es Salaam lisionekane kama kioo cha nchi yetu. Hivyo, kuna haja ya kuliangalia kwa namna ya pekee.

105. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia hali hiyo, Serikali imeunda Kamati Maalumu ya kuangalia, kuchambua na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha muundo wa Halmashauri za Dar es Salaam na uendeshaji wake ili wananchi wafaidike na huduma bora zinazopaswa kutolewa na mamlaka hizo za Serikali za Mitaa. Mapendekezo ya kamati hiyo yataisaidia pia Serikali kufanya maamuzi yenye manufaa na tija kwa maombi ya Halmashauri za Majiji mengine kama vile Jiji la Mwanza ya kutaka kuwa na muundo kama wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam. Nazisihi Halmashauri hizo ziwe na subira.

Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo

106. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuimarisha Mamlaka za Serikali za Mitaa hapa nchini, Serikali imefanya uamuzi wa kupanua na kuimarisha miundombinu ya Chuo cha Serikali za Mitaa - Hombolo ili kuongeza idadi ya wanachuo kutoka 104 hadi 2,000 ifikapo mwaka 2011. Aidha, Serikali itejenga miundombinu kwa ajili ya kuhudumia mikutano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa inayohusiana na Serikali za Mitaa pamoja na sekta nyingine. Nia ni kukifanya chuo hiki kiwe cha kisasa na kitovu cha mafunzo, utafiti na ushauri katika masuala yote yanayohusu Serikali za Mitaa ndani na nje ya Bara la Afrika. Upanuzi wa chuo hiki utatekelezwa na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa kwa udhamini wa Serikali. Hivi sasa, mshauri mwelekezi amepatikana na kazi ya usanifu inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2008. Ujenzi utafanywa katika awamu mbili kuanzia mwaka 2008/2009 hadi 2010/2011. Napenda kuchukua fursa hii kuzitaka Halmashauri zote kukitumia chuo hiki ipasavyo ili kujenga uwezo wa rasilimali watu katika Serikali za Mitaa.

Shirika la Elimu Kibaha

107. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Shirika la Elimu Kibaha limeimarisha utoaji huduma bora kwa jamii ikiwemo huduma za tiba na elimu ya kinga. Shirika pia liliendesha Kozi ya Uganga ya miaka mitatu kwa Maofisa Tabibu 100 na kutoa Elimu ya Malezi Bora kwa Wanafunzi 2,482. Katika mwaka 2008/2009, Shirika litaendelea kutoa huduma zake kwa ufanisi zaidi na kufanya ukarabati wa miundombinu na majengo. Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali Maalum ya Tumbi katika mkoa wa Pwani.

Mpigachapa Mkuu wa Serikali

108. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali inalo jukumu la kuchapisha na kudhibiti nyaraka muhimu za Serikali Kuu na Mitaa. Idara hiyo imekuwepo katika majengo yake ya sasa tangu mwaka 1952 huku baadhi ya mitambo yake ikiwa ni ya zamani. Kutokana na umuhimu wake, majengo ya Idara hiyo yanahitaji kukarabatiwa na baadhi ya mitambo yake kubadilishwa kuwa ya kisasa zaidi. Katika mwaka 2008/2009, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kuiboresha Idara kwa kuipatia mitambo ya kisasa na kuyafanyia ukarabati majengo yake. Uboreshaji huo utahusu pia Kitengo cha Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali kilichopo Dodoma. Uboreshaji wa Idara hiyo utaiwezesha kumudu majukumu yake ya kawaida pamoja na ya uchapishaji wa Nyaraka za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2009 na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2010.

Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu

109. Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi yetu, inapaswa kuangaliwa kwa namna ya pekee na kuchukua tahadhari ili kuepuka matatizo ya ukuaji wa mji usioendana na utoaji wa huduma muhimu. Serikali kupitia Programu ya Ustawishaji Makao Makuu imeendelea kuiongezea Mamlaka uwezo wa kifedha ili kuboresha miundombinu ya mji wa Dodoma. Hata hivyo, Progmamu hiyo imekuwa ikitekelezwa kwa takriban kipindi cha miaka 35 sasa. Hali hii inatanabahisha umuhimu wa kupitia upya programu hii na kufanya marekebisho ya kimfumo yatakayozingatia mabadiliko katika mazingira ya nchi yetu kwa hivi sasa.

110. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendesha Mjadala wa Kitaifa utakaoshirikisha wadau mbalimbali kuhusu suala la uhamishaji wa Makao Makuu kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma. Baada ya mjadala huo, Serikali itaandaa mapendekezo ya kutunga Sheria mpya ya kutambua rasmi Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali. Aidha, Mamlaka itaendelea kutekeleza Programu ya Ustawishaji Makao Makuu kwa kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa mji kwa kuweka miundombinu muhimu.

MASUALA MTAMBUKA

Sekta ya Habari na Mawasiliano ya Kisasa

111. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali imeendelea kuweka mazingira yanayoruhusu ukuaji wa Sekta ya Habari na Mawasiliano ya kisasa. Katika kutekeleza jukumu hili, mapendekezo ya uanzishwaji wa tovuti za mikoa yalikamilika na tovuti 21 za Sekretariati za Mikoa zilisajiliwa. Kukamilika kwa tovuti hizo kutasaidia kuboresha mawasiliano kati ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mikoa na Serikali Kuu. Aidha, itarahisisha utoaji huduma kwa wananchi na kuitangaza mikoa yetu kiuchumi Duniani. Katika mwaka 2008/2009, Serikali itakamilisha maandalizi ya maelezo ya Mikoa na Halmashauri na kuyaweka kwenye tovuti za mikoa.

Maendeleo ya Lugha ya Kiswahili

112. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na juhudi za kuingiza lugha ya Kiswahili katika medani ya Kimataifa. Kiswahili kimeendelea kutumika kuwa mojawapo ya lugha ya kazi katika Umoja wa Afrika. Aidha, mchakato wa kukiwezesha kitumike katika shughuli rasmi za Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki unaendelea vizuri. Mathalan, Jumuiya ya Afrika Mashariki iko katika hatua za mwisho za kuanzisha Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ambapo makao makuu ya Kamisheni hiyo yamependekezwa yawe Tanzania. Hivyo, ni vyema sasa tuanze kutumia lugha ya Kiswahili kama mkakati wa kuwawezesha Watanzania kupata ajira. Tunavyozidi kuhamasisha matumizi ya Kiswahili kimataifa tujue pia kwamba wanahitajika wataalamu wengi wa kufundisha na kutafsiri katika mikutano na makongamano mbalimbali ya Kimataifa. Hii ni changamoto kwetu kuhakikisha kwamba tunafundisha Kiswahili kwa ufasaha na kutumia mwanya wa kukua kwa lugha hii kama fursa ya kiuchumi. Aidha, natoa wito kwa waandishi wa vitabu vya Kiswahili kuandika vitabu vingi zaidi ili waweze kuuza vitabu na kujipatia kipato. Mama wa Kiswahili ni Tanzania, sitegemei nchi yoyote ituzidi katika kuzalisha wataalam na vitabu vya Kiswahili.

Hifadhi ya Mazingira

113. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali imeendelea na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Mazingira kwa kuandaa Kanuni, Miongozo na viwango vya usimamizi wa Mazingira Nchini. Aidha, imeendelea kutekeleza Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji katika Mikoa mbalimbali Nchini. Serikali pia imefanya tathmini ya Athari za Mazingira kwa miradi zaidi ya 50 na kupatiwa vyeti ili iendelee kutekelezwa.

114. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu Mikataba ya Kimataifa kuhusu Hifadhi ya Mazingira ambayo nchi yetu imeridhia. Uratibu wa Mikataba hiyo umewezesha Taifa letu kupata misaada ya kiufundi na fedha ili kukuza uwezo katika Hifadhi ya Mazingira. Katika mwaka 2008/2009, mkazo utawekwa katika utekelezaji wa Sera na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji na Programu mbalimbali zinazolenga Hifadhi ya Mazingira. Aidha, uratibu wa utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa inayohusu Hifadhi ya Mazingira utaimarishwa.

Uratibu wa Maafa Nchini

115. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga uwezo wa Taifa katika kudhibiti maafa kwa kutoa mafunzo na kuelimisha umma kupitia vyombo vya habari na vikundi vya jamii. Katika mwaka 2007/2008, Kamati za Maafa za mikoa mitano ya Tabora, Iringa, Ruvuma, Kilimanjaro na Rukwa, pamoja na wilaya zake zimepewa mafunzo ya kukabiliana na maafa. Hatua hii inafanya jumla ya mikoa iliyopewa mafunzo hayo hadi sasa kufikia 14. Mikoa mingine ambayo tayari kamati zake zimepewa mafunzo hayo ni Dodoma, Dar-es-Salaam, Singida, Mwanza, Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, na Tanga.

116. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Kitaifa wa Kuimarisha Uwezo wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa kwa kutoa mafunzo kwa Kamati za Maafa za Mikoa na Wilaya zilizobaki na kuzijengea uwezo wa kupunguza athari za Maafa. Aidha, kazi nyingine zitakazotekelezwa chini ya Mradi huo ni kufanya tathmini ya uwezo wa Taifa kukabiliana na maafa na kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa katika Kanda tano za Ziwa, Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini, Kati na Mashariki. Kazi hii ya kuzijengea uwezo Kamati za Maafa itatekelezwa kwa ushirikiano na Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa na Asasi zisizo za Kiserikali.

Udhibiti wa Dawa za Kulevya

117. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali iliteketeza ekari 649 za bangi katika mikoa mbalimbali nchini. Mikoa hiyo ni Morogoro (ekari 625), Mara (ekari 7), Tabora (7), Lindi (5.5), Mwanza (2.6), Iringa (0.75), Pwani (0.75) na Shinyanga (0.25). Serikali kupitia Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ilitoa elimu juu ya madhara ya Dawa za Kulevya kwa Umma na kwa makundi maalum katika jamii wakiwemo viongozi wa dini 40 na vijana walio shuleni na walioko nje ya shule. Vilevile, Tume imeandaa rasimu ya Mpango wa Uelimishaji Jamii juu ya mahusiano ya matumizi ya Dawa za Kulevya na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa Watumiaji wa Dawa za Kulevya. Aidha, Mfumo wa Ukusanyaji, Uchambuzi, na Utunzaji wa Taarifa za Dawa za Kulevya umeanzishwa ili kupata taarifa za uhakika za Dawa za Kulevya. Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya kwa mwaka 2006 iliandaliwa na kuwasilishwa Bungeni na kusambazwa kwa wadau wengine.

118. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itakamilisha Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya na kutoa elimu kuhusu athari zitokanazo na matumizi pamoja na biashara haramu ya Dawa za Kulevya. Uteketezaji wa mashamba ya kilimo cha zao haramu la bangi utaendelezwa. Aidha, Serikali itaimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa ndani na nje katika Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya.

Udhibiti wa UKIMWI

119. Mheshimiwa Spika, kampeni za kupambana na UKIMWI zinazoendelea kote nchini zinaonyesha matokeo mazuri. Uelewa wa jamii kuhusu janga hili umekuwa ukiongezeka kama inavyoshuhudiwa na kupungua kwa kiwango cha maambukizo. Matokeo ya utafiti wa pili wa hali ya UKIMWI Nchini yaliyotolewa hivi karibuni yanaonyesha kwamba kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kimepungua kutoka wastani wa asilimia 7 mwaka 2003/2004 hadi 5.8 mwaka 2007/2008. Pamoja na mafanikio hayo, Serikali imeendelea kufanya kampeni mbalimbali za Mapambano dhidi ya UKIMWI. Mwezi Julai 2007, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alizindua Kampeni ya Kitaifa ya Kupima VVU kwa hiari kwa yeye mwenyewe kupima VVU hadharani. Kampeni hii imekuwa ya mafanikio makubwa kwani hadi kufikia tarehe 31 Machi 2008, watu wapatao 4,042,055 walijitokeza kupimwa VVU ukilinganisha na watu 2,000,000 waliowahi kupimwa katika kipindi cha miaka 13 kuanzia mwaka 1995 wakati huduma hii ilipoanza kutolewa hapa Nchini. Kati ya watu 4,042,055 waliopimwa, wanawake walikuwa 2,257,052 na wanaume walikuwa 1,785,003. Jumla ya watu 194,149 waligunduliwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI wakiwepo wanaume 76,895 na wanawake 117,254. Idadi hii inaonyesha kuwa asilimia 4.8 ya watu wote waliopima, walikuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Napenda kuwakumbusha Watanzania kwamba kupima afya ni jambo muhimu na hivyo wajitokeze zaidi ili kufahamu hali ya afya zao. Aidha, kampeni hii iendelezwe ili iwe ni zoezi la kudumu.

120. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, fedha zilizotolewa na Serikali na Wahisani kwa ajili ya kudhibiti UKIMWI ziliongezeka na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 596.4 ikilinganishwa na shilingi bilioni 310.6 zilizotolewa mwaka 2006/2007. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 92. Ongezeko hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na rasilimali kutoka Global Fund na Serikali ya Marekani. Vilevile, uboreshaji wa shughuli za UKIMWI kwa kushirikiana na nchi jirani kama nchi za Maziwa Makuu, nNchi za SADC na nchi za Afrika ya Mashariki ni moja ya mambo ambayo yameleta mafanikio kwa nchi yetu kupata uzoefu wa mbinu mbalimbali za kuboresha Programu zetu. Mpango wa Uboreshaji na Ubadilishaji wa Tabia ambao uliandaliwa mwaka huu umekuwa ni nyenzo kubwa ambayo hutumiwa na watekelezaji mbalimbali nNchini. Vilevile, Serikali imewezesha sekta mbalimbali kufanya UKIMWI uwe ni sehemu ya shughuli za kila siku kupitia miongozo mbalimbali inayotolewa kwa shughuli za UKIMWI. Tumeweza pia kuboresha Elimu ya UKIMWI kwa Umma kwa kupitia maonyesho ya Sinema Mijini na Vijijini.

121. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itafanya mapitio ya Sera na muundo wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI. Serikali pia itahamasisha Wadau katika ngazi zote Nchini kuielewa Sheria ya Kudhibiti UKIMWI ya mwaka 2007. Aidha, itaongeza juhudi za udhibiti wa UKIMWI katika kinga kwa kuwa asilimia 95 ya wananchi bado hawajaambukizwa. Vilevile, magari zaidi ya sinema yatanunuliwa kwa ajili ya maeneo ya vijijini. Mfuko maalum wa fedha wa kuhudumia shughuli za udhibiti wa UKIMWI utaanzishwa kisheria. Aidha, Serikali itaboresha shughuli za udhibiti wa UKIMWI kwa kutumia mfumo shirikishi ili kuifikia jamii kwa urahisi.

Ushirikiano wa Kimataifa

122. Mheshimiwa Spika, Serikali yetu ilishiriki katika Kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kilichofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia kuanzia tarehe 31 Januari hadi tarehe 2 Februari, 2008. Katika kikao hicho, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alichaguliwa kwa kauli moja kuwa Mwenyekiti wa Umoja huo kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hili ni tukio la heshima kubwa na kielelezo cha imani na upendo ambao nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wanao kwa uongozi wa nchi yetu. Heshima hiyo imeongeza wajibu wetu katika kushughulikia changamoto zinazolikabili Bara la Afrika katika nyanja za ushirikiano, kuimarisha uchumi na kuondoa umasikini pamoja na kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro inayoendelea katika Bara la Afrika.

123. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Sera ya Diplomasia ya Kiuchumi inayolenga kutoa changamoto za kiutendaji katika Balozi zetu kuhamasisha Utalii, Uwekezaji, Kuvutia Mitaji na Kukuza Mauzo Nje. Ushirikiano wa Kimataifa umeimarishwa kwa Viongozi wa Serikali na Wafanyabiashara wa ndani kufanya ziara na kushiriki katika Makongamano ya Kimataifa kwa lengo la kuitangaza Tanzania na kuwahamasisha Wawekezaji kuwekeza Nchini. Tarehe 2-6 Juni 2008, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa nane wa Leon Sullivan ulioshirikisha zaidi ya watu 4,000 kutoka nchi mbalimbali duniani. Mkutano huo uliwapa nafasi wageni hao kufahamu fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini na vivutio mbalimbali vya utalii. Aidha, waliweza kubadilishana mawazo na wafanyabiashara wa Tanzania. Nitumie fursa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kufanikisha kufanyika kwa mkutano huu wa kihistoria. Pia nawapongeza Washiriki wote walioweza kuhudhuria mkutano huu muhimu.

124. Mheshimiwa Spika, vilevile, Viongozi wa Kitaifa wametumia ziara za nje kuimarisha mahusiano kati ya Nchi yetu na Nchi marafiki. Ziara hizo zimekuwa na mafanikio makubwa ambapo Nchi hizo zimetoa misaada mbalimbali itakayosaidia katika juhudi zetu za kukuza uchumi. Kwa mfano, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China iliahidi kufuta madeni yote ambayo Nchi hiyo inaidai Tanzania. Aidha, iliahidi kufufua miradi yote iliyoanzishwa miaka ya sitini na sabini, hususan Reli ya Tanzania na Zambia; Kiwanda cha Urafiki kati ya Tanzania na China na Kiwanda cha Zana za Kilimo cha Ubungo. Pia, imeahidi kusaidia Tanzania katika ujenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

HITIMISHO

125. Mheshimiwa Spika, katika Hotuba hii nimezungumzia mambo mengi ambayo Serikali imefanya kwa kipindi cha mwaka 2007/2008 na mwelekeo wa kazi zitakazofanyika katika mwaka 2008/2009. Napenda kuhitimisha hotuba hii kwa kusisitiza mambo muhimu yafuatayo:

a) Tunalo jukumu kubwa mbele yetu la kusimamia utekelezaji wa MKUKUTA. Fedha zinazoombwa katika Bajeti hii ni kwa ajili ya kutekeleza malengo ya MKUKUTA. Tusimamie vizuri matumizi ya fedha hizi ili kutimiza malengo tuliyojiwekea. Naelewa kwamba fedha zilizotengwa haziwezi kutosheleza mahitahi yetu yote, ila tukitumia fedha za Serikali, kwa umakini na kuhakikisha zinazalisha zaidi, miaka ijayo tutakuwa na vianzio vingi zaidi vya mapato. Hiki kidogo tulicho nacho tusikitumie kama yule mtumwa aliyepewa talanta moja na tajiri yake na kuifukia. Tuwe watumwa werevu na tuwekeze ili izae zaidi.

b) Tunayo changamoto ya kulinda ukuaji wa uchumi wetu licha ya athari za kupanda kwa bei ya nafaka, mafuta ya petroli pamoja na bidhaa nyingine kutoka nje. Sote kwa pamoja tunao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, tuongeze uzalishaji ili uchumi wetu usitetereke. Kupanda kwa bei ya nafaka iwe ni changamoto kwetu ya kuzalisha zaidi na kuuza ziada nje.

c) Tumejiwekea utaratibu mzuri wa kuwawezesha wananchi kujikomboa kiuchumi. Tutumie nafasi hii kuwahimiza wananchi kubuni shughuli za uzalishaji na miradi midogo midogo inayokopesheka katika vikundi. Fursa za wananchi kupata mikopo ni nyingi, tuwahimize kukopa na kurejesha mikopo kwa wakati.

d) Kilimo bado ni msingi wa uchumi wa Taifa letu. Tuhimize wananchi hususan vijana kupenda kilimo. Aidha, tuwahimize kutumia pembejeo zikiwemo mbolea na mbegu bora ili kuongeza tija katika uzalishaji. Mbolea itakayonunuliwa kwa njia ya ruzuku isimamiwe vyema iwafikie wakulima kwa wakati na bei nafuu. Lengo la kutoa ruzuku si kufaidisha Wafanyabiashara bali Wakulima. Nisingependa kusikia malalamiko kwamba mbolea ya ruzuku haikuwafikia Wakulima au inafika kwa bei ya juu. Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayezembea katika usimamizi wa mbolea. Narudia tena, mbolea iwafikie wahusika na kwa bei inayolengwa.

e) Wakati umefika wa kutumia hazina ya ardhi tuliyonayo kwa kuwaelimisha wananchi kuhusu Matumizi Bora ya Ardhi. Aidha, tuwakumbushe kuepukana na migogoro ya ardhi kwa kufuata Kanuni na Taratibu za Sheria za Ardhi zilizopo. Tujiepushe na dhana ya uvamizi wa maeneo ambayo tayari yametengwa kwa ajili ya maendeleo ya shughuli nyingine kwa manufaa ya Taifa.

f) Suala la elimu halina mjadala. Tuendelee kuhimiza wananchi kuthamini elimu kwa ajili ya Watoto wetu. Tuongeze juhudi kujenga miundombinu ya kutosha kwa ajili ya elimu kwa wote kuanzia ngazi ya Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Juu.

126. Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha utekelezaji wa Bajeti hii ni vyema watumishi wote wa Serikali wawajibike ipasavyo na wahakikishe kwamba fedha zilizotengwa kwenye Bajeti ya Serikali zinatumika kwa shughuli zilizopangwa. Kila mtumishi anapaswa kupima kazi yake kwa kujiuliza ametoa mchango gani wa majukumu yake kwa kuchangia kwenye Bajeti hii. Tusikubali watu wachache watumie fedha hizi kiujanja. Tuwabaini na kuwadhibiti. Naagiza Wizara, Idara za Serikali, Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kwamba watumishi wote wanafanya kazi kwa malengo, tija na ufanisi. Tukifanya kazi kwa bidii na uadilifu, tutasonga mbele haraka na kuleta maendeleo endelevu nchini.

SHUKRANI

127. Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza, napenda kuwashukuru Mawaziri wote na Naibu Mawaziri wote kwa ushauri wao ambao umewawezesha Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yao ya kitaifa kwa ufanisi. Aidha, nawashukuru wafanyakazi wote wa Serikali na taasisi zake chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Bwana Phillemon Luhanjo pamoja na vyombo vyote vya dola kwa kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuiwezesha kukamilisha maandalizi yote ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2008/2009, pamoja na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya kila Wizara, Mikoa na taasisi zinazojitegemea.

128. Mheshimiwa Spika, napenda vilevile kuwashukuru Mheshimiwa Phillip Sanka Marmo, Mbunge wa Mbulu, Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge), Mheshimiwa Celina Ompeshi Kombani, Mbunge wa Ulanga Mashariki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Aggrey Joshua Mwanri, Mbunge wa Siha, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa msaada mkubwa na ushirikiano walionipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru vilevile wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya uongozi wa Makatibu Wakuu, Bwana Vincent Mrisho na Bibi Maimuna Tarishi na Naibu Makatibu Wakuu, Bwana Andrew Nyumayo na Bwana Fanuel Mbonde kwa ushauri wao wa kitaalam ambao wamenipa katika kipindi hiki cha mwanzo katika uongozi wangu. Nawashukuru kwa kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2008/2009.

129. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, nchi yetu imepata misaada na mikopo kutoka kwa wahisani wetu mbalimbali. Misaada na mikopo hiyo imetoka kwa nchi rafiki, nchi fadhili, taasisi za fedha duniani, mashirika ya Umoja wa Mataifa, mifuko mbalimbali duniani, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya serikali. Misaada na mikopo hiyo imechangia sana katika kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Napenda kuwashukuru wote kwa dhati na kuwahakikishia kuwa Watanzania tunathamini misaada na mikopo yao na tutaendelea kushirikiana nao katika harakati za maendeleo ya Taifa letu.

MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA NA MFUKO WA BUNGE YA MWAKA 2008/2009

130. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2008/2009, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Hamsini na Sita, Milioni Themanini na Nane, Mia Nane na Sita Elfu na Mia Nane (56,088,806,800) kwa ajili ya Mishahara na Matumizi Mengineyo. Aidha, jumla ya Shilingi Bilioni Hamsini na Mbili, Milioni Mia Tisa Kumi na Moja, Mia Tatu Hamsini na Moja Elfu, Mia Moja (52,911,351,100) zinaombwa kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Kumi, Milioni Mia Tisa Thelathini na Tisa, Mia Tatu Hamsini na Saba Elfu (10,939,357,000) ni fedha za Ndani na Shilingi Bilioni Arobaini na Moja, Milioni Mia Tisa Sabini na Moja, Mia Tisa Tisini na Nne Elfu na Mia Moja (41,971,994,100) ni fedha za Nje.

131. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2008/2009, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Asasi zake inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Tisini na Tatu, Mia Saba Ishirini na Nane Milioni, Mia Moja Sitini na Nane Elfu (93,728,168,000) kwa ajili ya Mishahara na Matumizi Mengineyo. Aidha, jumla ya Shilingi Bilioni Sabini na Tatu, Milioni Hamsini na Nane, Mia Saba na Tano Elfu na Mia Moja (73,058,705,100) ni kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Thelathini na Mbili, Milioni Mia Moja Ishirini na Nne, Mia Nne Sitini na Tano Elfu (32,124,465,000 ni fedha za Ndani na Shilingi Bilioni Arobaini, Milioni Mia Tisa Thelathini na Nne, Mia Mbili Arobaini Elfu na Mia Moja (40,934,240,100) ni fedha za Nje.

132. Mheshimiwa Spika, Ofisi za Wakuu wa Mikoa zinaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Tisini, Milioni Mia Tatu Sitini, Mia Saba Themanini Elfu (90,360,780,000) kwa ajili ya Mishahara na Matumizi Mengineyo na Shilingi Bilioni Thelethini na Mbili, Milioni Mia Tisa Kumi na Saba, Mia Saba Sitini na Mbili Elfu (32,917,762,000) kwa ajili ya Mpango ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Ishirini na Tisa, Milioni Mia Tisa Arobaini na Saba, Mia Saba Sitini na Mbili Elfu (29,947,762,000) ni fedha za Ndani na Shilingi Bilioni Mbili, Milioni Mia Tisa Sabini (2,970,000,000) ni fedha za Nje.

133. Mheshimiwa Spika, Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji zinaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Tisa na Nane, Milioni Mia Tisa Tisini na Nane na Sabini na Nne Elfu (908,998,074,000) kwa ajili ya Mishahara na Matumizi Mengineyo na Shilingi Bilioni Mia Tatu Hamsini na Sita, Milioni Mia Saba Sabini na Tano, Mia Sita Arobaini na Saba Elfu (356,775,647,000) kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Thelathini na Mbili, Milioni Mia Moja na Themanini (32,180,000,000) ni fedha za Ndani na Shilingi Bilioni Mia Tatu Ishirini na Nnne, Milioni Mia Tano Tisini na Tano, Mia Sita Arobaini na Saba Elfu (324,595,647,000) ni fedha za Nje.

134. Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Bunge unaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Arobaini na Nane, Milioni Mia Nne na Nne, Mia Tisa Themanini na Tano Elfu (48,404,985,000) kwa ajili Mishahara na Matumizi Mengineyo na Shilingi Bilioni Tisa, Milioni Thelathini na Saba, Mia Tano na Tano na Mia Tisa (9,037,505,900) kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Nane, Milioni Mia Sita Sabini, Mia Mbili Sabini na Tatu Elfu (8,670,273,000) ni fedha za Ndani na Shilingi Milioni Mia Tatu Sitini na Saba, Mia Mbili Thelathini na Mbili Elfu na Mia Tisa (367,232,900) ni fedha za Nje.

135. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya kwa muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2008/2009 ya jumla ya Shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Sita Sitini na Nne, Milioni Mia Nane Thelathini na Tisa, Mia Mbili Tisini na Nne Elfu (1,664,839,294,000) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na jumla ya Shilingi Bilioni Hamsini na Saba, Milioni Mia Nne Arobaini na Mbili, Mia Nne Tisini Elfu na Mia Tisa (57,442,490,900) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge.

136. Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii yapo Majedwali mbalimbali ambayo yanafafanua kwa kina zaidi Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake ikiwemo, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge.

Bwana mmoja alipoulizwa: What’s a Budget? Alijibu: It’s an orderly system for living beyond your means”. Akimaanisha kwamba, Bajeti, ni mpangilio wa kuishi nje ya uwezo wako. Sisi tunasema “Its an orderly system for living within our means” kwamba ni mpangilio mzuri wa kuishi ndani ya uwezo tulionao. Tunaomba tuidhinishiwe fedha hizo ili tuweze kuendeleza yote ambayo tumepanga ndani ya uwezo wetu wa Serikali.

137. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

COMMENTS

Name

Anga,11,Arusha,27,Burudani,302,burundani,1,come rain,1,come sun,1,Crazy in Love kama wimbo kama wao wenyewe,1,dahh sijui kweli mbona shida,1,Dar utakuja je tumejiandaa,1,daraja sahau nini,1,demokrasia ya upanga,1,Dodoma,77,Dole tupu vijana wa zamani,1,Duhh bibie endeleza libeneke,1,Duhh kaisikie Walibana,1,duhh kwa mbagala mama lazima awe supa,1,Fedha za maiti haziliwi bure,1,Fedha za watu kwa maendeleo ya watu,1,Fikira,14,filamu,238,Filamu ndio kielelezo cha ukuzi wa taifa,1,flamu,7,Gandamiza Kibara baba ake,1,Habari,4816,habari. dodoma,24,hadithi,19,hakika tumeweka historia,1,hakuna noma jongwe,1,hapa kwetu inakuwaje vile,1,hasira hasara,1,hata maji,1,hataki masikhara na maisha yake,1,hatubonyezi kizenji,1,haya ndiyo mambo ya Ulaya,1,haya si yangu ni ya mdau mwenye hasira,1,haya wabongo na mambo kutoka nje,1,He he he wananikumbusha upishi wa shaba,1,Headline,1,Hii hurejesha uhai,1,Hii iko sawa kweli?,1,Hii imekaa vizuri,1,Hii inakaaje vile,1,Hii kweli noma,1,Hii maana yake Moro kuna uhaba wa chakula,1,Hii mexico,1,Hii mihasira mingine bwana,1,Hii ndio moro sio mpaka dar,1,hii ni hatari,1,Hii ni kiboko anayetaka kubisha ajibishie tu,1,Hii ni moja ya staili za kunyoa nywele,1,Hii si lukwangule,1,hii staili mpya,1,hili ni jengo pacha la malaysia ghorofa 88,1,Hivi ni ngoma tu,1,hivi nini siri za serikali,1,hivi sisi tunajua kama kuna vitu vya aina hii,1,hivi vitu bwana,1,Hiyo ndiyo gharama ya demokrasia,1,Hizi imani nyingine ni hatari,1,Hizi takwimu hizi mhh,1,Hongera bibie,1,Hongera dada etu kwa kutuletea kaka etu (shemeji) kwani mwenye dada hakosi shemeji,1,Hongera sana,1,huhitaji mifedha kuwa msafi,1,Huko Ulaya,1,Huu ndio ustaarabu,1,huu ujiko utakuwa mkubwa,1,imetosha,1,Inahitaji nidhamu fulani,1,inakuuma au...,1,Inakuwaje kama filamu yenyewe itahitaji busu la nguvu,1,Inaonekana watanzania hatukuwepo,1,Ipo kazi Maximo,1,Iringa,22,Isiwe mijineno tu manake mihela hubadili watu kweli,1,Itakuwa laki moja ya halali,1,jamani huu kama si ushamba kumbe nini,1,Jamani mbona Mungu anatupigania,1,Jamani watoto wanatakiwa kupendwa,1,jamani.. jamani ukiikosa Diamond usijutie,1,Je nyumbani hakuna vitu vya aina hii?Tuambie,1,je walikuwepo watu wa huduma ya kwanza,1,Je watanzania wanalipa kodi,1,jela kwa raha,1,Jolie,1,juhudi za lazima kuinua filamu,1,kama si kiwanda cha chumvi nani atawajua hawa,1,Kama kweli ndio kweli basi kila heri,1,Kama Mkristo naamini hilo hiyo si sahihi,1,kama unajua kuyarudi nenda Malta,1,kama wao wanaweza sisi je,1,Kamua baba waache wakanyagane,1,karibu nyumbani dada yote maisha tu,1,karibu Tatiii,1,KARIBUNI,1,Katavi,5,kaza buti hakuna kukata tamaa inalipa,1,kazi kwako mheshimiwa waziri wa madini,1,kazi na burudani,1,keep it up bloggers,1,kero ya usafiri sasa kwisha,1,Kila chenye roho na mwili kitaonja umauti,1,kila kitu kina vitu,1,Kila la Heri jamila,1,kila la heri kwani ni changamoto,1,Kipya,51,Kiuno bila mfupa,1,Kolelo mzimu ambao bado hai,1,KUBWA,1,Kudumisha urafiki wa dunia,1,Kuna dalili za wasomi kukubali Uafrika,1,kuna makala humu humu ndani ya blogu sijui mnasemaje,1,Kuu,113,kwa mara nyingine tena Tigo imewezesha,1,Kwa mchanganyiko huu muungano lazima udumu,1,Kwa mihasira hajambo,1,kweli,1,Kweli ina mkono mrefu tuone,1,Kweli duniani tunatofautiana,1,la maana ni kuwa na jiko au vipi,1,labda halitabadilika tena,1,lakini mwafaka lazima,1,lengo ni kutafakari,1,leteni vitu tuvione,1,lets us,1,Lucy wanakuelewa hawa...,1,Lukwangule nyumbani kwetu,2,M ungu bariki mikono ya madaktari wafanikiwe,1,MAARUFU,1,maendeleo ya soka siku zote yanahitaji fedha ili yapatikane,1,maisha ni vyema kuyaangalia,1,MAJIBU,1,makala,51,mama ni mama tu anapendeza,1,mambo mengine we angalia tu,1,mambo msimamo,1,mambo sasa mchanganyiko,1,Mara nyingine huona tunakotoka kwa kuona wenzetu,1,Mashabiki wa rhumba mpooooooooo,1,Masitaa,12,Maskani,1,MASOKO,3,Masupa staa mnaoinukia mpoo,1,Matamasha,6,mavazi ya kuogelea yanaposhindaniwa,1,Mbeya,11,Mchakamchaka anti Asmah,1,Mchanganyiko,81,MCHANYATO,1,mchezo,5,mengi wanayoyaita siri ni public information,1,mfumuko wa bei mpaka noma,1,Mhh sijui watu wa Sua ambao wako huko wanasemaje,1,Mhh ugua pole dada watu wanataka burudani,1,Michezo,501,Michezo maalum inatakiwa kupigiwa debe,1,miguu,1,miguu babu,1,Mikataba mingine ama hakika tuiangalie hata wakopeshaji nao wanatugeuza sakala,1,MIMI NI KISURA NAJITAMBUA,1,Mimi sijajua hasa kumetokea nini kwani ninavyojua hawa huwa na ungalizi wa hali ya juu,1,Mimi simo,1,mimi sisemi,1,mkiwa chumvi basi mkoze,1,Mkiwa taa mulikeni,1,Mnaonaje je hii imekaa vyema,1,Mnaweza wakwetu hapa,1,Morogoro,51,mrithi wa mwanadada Whitney Houston,1,Mtwara,4,Mungu aiweke mahali pema roho yake,4,Mungu amrehemu,1,Mungu amweke pema peponi,1,Mungu awabariki sana,1,Mungu awe nao,1,Mungu ibariki Tanzania,1,Mungu tuepushe na imani hizi za kishirikina,1,mungu tufanye tuwe na upendo,1,Mungu twaomba utuhurumie,1,Muziki,350,muziki na fasheni,5,Mwanahabari,33,Mwanza,6,Mwendo mdundo dada,1,Mwenge huo utakimbizwa duniani kwa siku 130,1,Mwenge wa olimpiki ni ishara ya urafiki,1,Mzee wa Farasi nakupa saluti,1,Mzimbabwe huyu kutoka kwa mama mkali,1,N i dar mpaka Moro au bao tatu bila,1,Na sisi je,1,Naam kama haiwezekani hapa,1,Nairobi waanzisha tena utalii,1,namna bora ya kusaidia jamii,1,nani abebe hukumu na lawama,1,nani asiyejua utamu wa pipi,1,Nani kama baba,1,naona inafaa kuchangia mimi sitoi hoja,1,ndoa za mastaa huwa na mgogoro,1,nenda mwaya nenda,1,New Zanzibar Modern Taarab na wapenzi big up,1,news,5,Ni bikini kwa kwenda mbele,1,Ni Dar mpaka Moro au.. tatu bila,1,ni furaha za muungano,1,Ni kazi ngumu yenye kuhifadhi utamaduni,1,Ni kuchakarika kuonyesha urafiki na biashara pia,1,ni mfumuko wa bei au mfumuko wa nchi,1,Ni muhimu kutazama afya yako,1,ni muziki kwa kwenda mbele,1,Ni muziki mpaka China,1,Ni raha tupu,1,Ni Serengeti Premium Lager,1,Ni Tigo na mawasiliano ya kisasa,1,Ni wakati wa kuujadili utamaduni,1,Ni zaidi ya jazz,1,Nitasubiri and welcome home,1,nje je?,1,NUKUU YA LEO,1,nyie mnasemaje kuhusu hili,1,Ona Kolelo na sindikizwa na Wazee wa Gwasuma,1,ona vya dunia,1,One step ahead,1,patna mwingine mjamzito,1,Pengine anamuogopa Jada Pinkett manake kwa wivu..,1,picha,494,Pole Jamila hayo ndiyo mashindano,1,poleni sana,1,poleni sana wanyalukolo,1,Powa sana,1,Profesa jamaa wanakumaindi,1,Roho za marehemu zipate pumziko la milele,1,Ruvuma,9,sakata dansi mpaka kwenye kilele cha dunia,1,sasa kumebakia ugonjwa mmoja polisi kuendesha mashtaka,1,sasa mifedha kila mahali hongereni,1,Sasa ni mavuno,1,Sasa ni wakati wa kutafuta upenyo ndani ya IDOLS,1,SAYANSI,1,SAYANSI ANGA,1,See Uluguru Montains,1,serikali inataka kujihami kwanini,1,Show of support Big Up Madame,1,Si kitu kidogo hata kidogo,1,si unajua tena namie naimwaga hivyo hivyo,1,Siasa,346,siasa habari,2,Sijui kama City wanajua Mbagala noma,1,Sijui tunaishi karne gani yailahi,1,Sinema,9,sio advencha....kaaa ...niko kibaruani,1,Sisi ndio tunaanza vitongoji,1,Sisi yetu macho na masikio,1,Slow slow jamani,1,sto,1,tabasamu kali la mwenge wa olimpiki,1,Tabora,1,Tazama Waziri Mkuu Pinda wasije wakapindisha maamuzi yako,1,TEKNOLOJIA,1,Thats big man game,1,This is crazy Africa,1,This is Mgeta,1,Tibet wamegeuza Olimpiki jukwaa la siasa,1,Titbits collection,1,Tubadili tamaduni,1,Tuchangie mambo yaive,1,tuendeleze sanaa,1,tuienzi na sisi mbona wizara haituambii,1,Tuipeleke kaskazini,1,Tuisaidie serikali shida ya Mererani,1,tujue namna ya kupumzika,1,Tulienda kustarehe au kufanya fujo,1,Tumsaidie mtototo huyu kurejea katika hali ya kawaida,1,tunahitaji haya,1,Tunajifunza kweli kutoka kwao,1,Tunapandisha chati tu,1,Tunasubiri,1,tunazidi kuhesabu siku,1,TUNAZISUBIRI ZA VINARA ADAR,1,Tuombe nafuu kwa wagonjwa,1,Tuombe rehema kwa mungu,1,Tuone yatufae,1,Tusingoje wengine watusemee,1,tutampa tafu kubwa Prof,1,tuuenzi utamaduni au vipi,1,Tuukuze na kuulinda,1,tuvipende,1,tuwalinde maalbino,1,Tuwe kweli wakweli,1,ubunifu siku zote hulipa,1,uchumi huzunguka kwa kuwawezesha wasukaji,1,udumu muungano,1,Ugonjwa huu wa sasa ni kitendawili,1,Ukiiona kolelo utaipenda,1,Ukirejea salama kila mtu anafurahi,1,Umelenga Mkuchika utamaduni unakufa,1,unaposaka uwakilishi wa dunia,1,urafiki,1,Usisahau wazee wa Ngwasuma,1,UTAMADUNI,1,Video,2,Vionjo vipya ndani ya Gwasuma,1,Vita dhidi ya ufisadi,1,vitongoji Miss Tanzania navyo vimeanza,1,Vitu vikali vyazidi kuingia Dar,1,Vituko,77,Vituo vya polisi Tanga vyatelekezwa,1,VIVALO,1,Wacha tujifue,2,Wadau ilitolewa kiingereza,1,wakali wa ubunifu,1,wala usibabaike mwakwetu hii noma,1,wanadamu wanapotaka kujua zaidi,1,wanasema mpaka kieleweke,1,Wanataka kujua mali za JK na wengine,1,Wanawake wenye mvuto: Monroe,1,Wapo mabinti wa matawi ya juu,1,watu wanapofanya weli kwenye sanaa,1,waweza kurejea enzi ya Moro jazz na Cuban malimba,1,Wazee tupo kusindikiza,1,waziri,1,welcome dar baby,1,Wenzetu wameona sisi tunangoja nini kuangalia,1,wewe unasemaje,1,wigo mpana wa utamaduni,1,wilaya ya 'Mbagala' mlie tu,1,Yaaani sijui itawezekana,1,Yaani wakati mwingine hata huelewi prioty over priority,1,yeye mbele sisi nyuma,1,Yote maisha dada,1,ZA MOTOMOTO,1,Zanzibar,79,zawadi zinatakiwa ziende shule,1,ZILIZOTIA FORA,1,zitachangia kupunguza makali ya bei za umeme,1,
ltr
item
Lukwangule Entertainment: HOTUBA YA PM YA LEO
HOTUBA YA PM YA LEO
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgId34yQSurm4oIKxeA_9T99UKpxjtS3gvik27FHURri7YVFUSa5HRPR-ujIH9-arLP8ZQY5ta7MFCJCH-hq6u9KwcU0Jey9xkKzO8oFuZhyphenhyphenauR5WzKIv-Wb9oOHb_CUmnSlAYRORf8VZz3/s320/WAZIRI+MKUU+MIZENGO+K.P.PINDA.jpg
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgId34yQSurm4oIKxeA_9T99UKpxjtS3gvik27FHURri7YVFUSa5HRPR-ujIH9-arLP8ZQY5ta7MFCJCH-hq6u9KwcU0Jey9xkKzO8oFuZhyphenhyphenauR5WzKIv-Wb9oOHb_CUmnSlAYRORf8VZz3/s72-c/WAZIRI+MKUU+MIZENGO+K.P.PINDA.jpg
Lukwangule Entertainment
http://lukwangule.blogspot.com/2008/06/hotuba-ya-pm-ya-leo.html
http://lukwangule.blogspot.com/
http://lukwangule.blogspot.com/
http://lukwangule.blogspot.com/2008/06/hotuba-ya-pm-ya-leo.html
true
934549962738256429
UTF-8
Loaded All Posts Not found any posts VIEW ALL Readmore Reply Cancel reply Delete By Home PAGES POSTS View All RECOMMENDED FOR YOU LABEL ARCHIVE SEARCH ALL POSTS Not found any post match with your request Back Home Sunday Monday Tuesday Wednesday Thursday Friday Saturday Sun Mon Tue Wed Thu Fri Sat January February March April May June July August September October November December Jan Feb Mar Apr May Jun Jul Aug Sep Oct Nov Dec just now 1 minute ago $$1$$ minutes ago 1 hour ago $$1$$ hours ago Yesterday $$1$$ days ago $$1$$ weeks ago more than 5 weeks ago Followers Follow THIS CONTENT IS PREMIUM Please share to unlock Copy All Code Select All Code All codes were copied to your clipboard Can not copy the codes / texts, please press [CTRL]+[C] (or CMD+C with Mac) to copy