Taarifa kwa Vyombo vya Habari 22 Aprili, 2012 Inatosha: Ubadhilifu Fedha za Walipa Kodi Ukomeshwe! Sikika imesikitishwa na ...
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
22 Aprili, 2012
Inatosha:
Ubadhilifu Fedha za Walipa Kodi Ukomeshwe!
Sikika
imesikitishwa na kushtushwa na ripoti ya iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) iliyoibua matumizi mabaya ya fedha za umma na
kiwango kikubwa cha misamaha ya kodi.
Ripoti
hiyo inaonesha kuwa misamaha ya kodi iliyotolewa imeongezeka kutoka shilingi za
Tanzania
bilioni 680.7 mwaka 2009/2010, hadi kufikia trilioni 1.016 mwaka 2010/2011.
Ongezeko hili ni sawa na 18% ya mapato yote yanayotakiwa kukusanywa nchini.
Hiki ni kiwango kikubwa ukilinganisha na majirani zetu wa Kenya na Uganda.
Mbaya zaidi, misamaha hii imetolewa kwa watu wenye uwezo na makampuni makubwa
ya kimataifa yenye mitaji mikubwa jambo linalolikosesha taifa mapato.
Fedha
zilizopotea kutokana na misamaha hii ya kodi, zingeweza kugharamia rasilimali
watu katika mpango mkakati wa maendeleo ya sekta ya afya uliohitaji kiasi cha
shilingi bilioni 500. Katika bajeti ya mwaka 2011/2012, Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii ilihitaji shilingi bilioni 66.3 ili kuimarisha rasilimali watu
kwa ajili ya maendeleo ya afya. Cha kustaajabisha, Serikali
ilitenga bilioni 13.2 tu na hadi kufikia Januari mwaka huu ni 20% tu ya kiasi
hicho ndiyo iliyokuwa imetolewa. Huu ni mzaha mkubwa unaofanywa na
Serikali, ukilinganisha na upotevu wa fedha uliotokana na misamaha hiyo ya kodi
yenye utata.
Pia,
ripoti ya CAG inaeleza kwamba kiasi cha shilingi bilioni 31 zilitumika kununua
bidhaa kwa matumizi ya Serikali pasipo kutolewa ufafanuzi, huku shilingi
bilioni 8 zikitumika bila kufuata utaratibu maalumu. Aidha, ripoti inaonyesha
kuwa shilingi milioni 143 zilitumiwa na serikali kulipa mishahara kwa
wafanyakazi hewa, watoro na waliokwisha staafu.
Wakati
huo huo, ripoti inaonesha kuwa shilingi bilioni 1.5 zilitumika pasipo
maelezo yoyote na kuwepo kwa ongezeko kubwa la malipo ya posho. Upotevu wa
fedha za umma pia uliongezeka kupitia madai yasiyoeleweka ambayo yaliongezeka
kutoka shilingi bilioni 11 kwa kipindi cha mwaka 2009/2010 hadi kufikia
shilingi bilioni 13 mwaka 2010/2011.
Wakati
upotevu huu wa mabilioni ya walipa kodi ukitokea nchini, bado nchi
inakabiliwa na matatizo lukuki ya upatikanaji wa huduma bora za
jamii. Mathalan, kumekuwepo na upungufu wa rasilimali watu katika sekta ya
afya, madawa, mfumo mbovu wa usambazaji wa madawa na vifaa tiba pamoja na uduni
wa vifaa vya kutolea huduma za afya.
Ripoti
hiyo ya CAG inaonesha matumizi mabaya ya fedha kidogo zinazotengwa kwa ajili ya
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Mfano, Wizara hiyo imeripotiwa kufanya
malipo mengine ya shilingi milioni 77 bila kufuata utaratibu wa malipo ya
vocha, milioni 50 kwa wafanyakazi wanaodaiwa kustaafu na shilingi milioni 32
kwa malipo yasiyo na umuhimu.
Imeripotiwa
hivi karibuni kwamba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitumia karibu
shilingi bilioni 1 kwa maadhimisho ya Nanenane. Ni katika mwaka huo huo wa
fedha ambapo Wizara hiyo iliingia kwenye mgogoro na madaktari waliokuwa
mafunzoni kwa kushindwa kuwalipa posho ya shilingi milioni 176 tu. Hii ni
takribani moja ya kumi ya fedha zilizotumika kwa maonesho ya Nanenane.
Kushindwa kupanga matumizi ya fedha kwa kuzingatia vipaumbelea ndiko
kulikosababisha mgomo wa madaktari nchini.
Fedha
zilizotumiwa na Wizara ya Afya kwa sherehe za Nanenane, zingeweza kutatua
matatizo mbalimbali yanayoikabili sekta ya afya kama vile kununua bandeji,
mipira ya mikononi, madawa na vifaa vingine.
Ripoti
ya CAG pia inaonesha kuwa mapendekezo mengi yaliyotolewa kipindi cha nyuma
hayakufanyiwa kazi. Hii inadhihirisha ukosefu wa uwajibikaji kwa upande wa
Serikali hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa fedha kujirudia kila mwaka.
Hali hiyo inapelekea Serikali kuendelea kuwa ombaomba na kutegemea misaada ya
wafadhili.
Sikika
inatoa wito kwa mamlaka husika kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na CAG
na kuwawajibisha watendaji wa Serikali waliohusika na upotevu huo. Tunapongeza
kazi kubwa na nzuri iliyo fanywa na CAG kwa kuibua ubadhilifu mkubwa wa fedha
za umma uliofanywa na baadhi ya watumishi wa umma na taasisi za Serikali.
Sikika
imekuwa mstari wa mbele kuishinikiza Serikali kuwajibika kwa wananchi na
inaitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa makini katika matumizi ya fedha
za walipa kodi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima na kuokoa maisha ya
watanzania.
Bw.
Irenei Kiria, Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu:
+255 222 666355/57, Simu ya kiganjani: 0784 274039, Faksi:
2668015,
COMMENTS