TAMKO LA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU KUFUNGIWA KWA MWANAHALISI Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)...
TAMKO
LA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU KUFUNGIWA KWA
MWANAHALISI
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kinalaani uamuzi wa Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kulifungia kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kwa kutumia mwanya
wa sheria mbovu ya magazeti inayokwenda kinyume na haki za binadamu na utawala
bora.
CHADEMA kinaitaka Serikali
kulifungulia gazeti hilo haraka iwekanavyo na kimewasiliana na Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA kuchukua hatua za kibunge kuisimamia
Serikali kurekebisha udhaifu huo ikiwa
inaheshimu uhuru wa habari na inazingatia maslahi ya taifa.
CHADEMA kinatafsiri hatua hiyo ya
Serikali ya kufungia gazeti la MwanaHalisi kuwa ni sawa na kufungia uhuru wa
kusambaza habari, uhuru wa kupokea habari na uhuru wa kutoa maoni, hivyo
tunatoa mwito kwa wananchi na wadau wote wa habari kuungana pamoja kupinga
hatua hiyo, na CHADEMA kitaeleza hatua za ziada za kuchukuliwa iwapo Serikali
haitasikiliza kauli za wadau wa habari juu ya suala hili.
CHADEMA kinatambua kuwa uamuzi wa
Serikali kufungia gazeti hilo kwa mara nyingine tena ni kwenda kinyume na haki
za binadamu, kinyume na utawala bora na ni kikwazo kwa demokrasia na maendeleo
nchini.
CHADEMA kinapinga hatua ya Serikali
ambayo viongozi na watendaji wake wakiwa wametajwa kama watuhumiwa katika
habari zilizoandikwa na gazeti hilo imetumia mamlaka haramu ya Waziri mwenye
dhamana ya sekta ya habari kugeuka mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mfungaji
huku ikipuuza taasisi za kusimamia uwajibikaji na haki.
CHADEMA ilitarajia badala ya
kulifungia gazeti la MwanaHalisi ingewezesha kufanyika kwa uchunguzi huru
kufuatia habari za kiuchunguzi zilizoandikwa na gazeti hilo juu ya watendaji na
watumishi wa Serikali kuhusishwa na jaribio la mauji ya Dr Ulimboka Steven,
kupanga njama za mauji ya viongozi wa CHADEMA na matukio mengine ambayo yenyewe
ndiyo yenye mwelekeo wa kufanya wananchi wapoteze imani na vyombo vya dola hali
ambayo inaweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.
CHADEMA kinalinganisha uamuzi huo
wa Serikali uliotangazwa tarehe 30 Julai 2012 na Msajili wa Magazeti chini ya
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
kuwa ni sawa kujichukulia sheria
mikononi kwa kuwa Serikali yenye kuheshimu misingi ya asili ya haki
ingezingatia kwamba ikiwa chombo chochote cha habari kimedaiwa kuvunja sheria
ama kukiuka maadili dhidi ya Serikali, viongozi wake ama watu binafsi mashtaka
au malalamiko yangepelekwa kwa taasisi zinazohusika mathalani Baraza la Habari
(MCT) au mahakama.
CHADEMA kinafahamu kuwa Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa
kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi,
kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya
mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i); hata hivyo uamuzi huo ni kinyume cha misingi
ya asili ya utawala wa sheria.
CHADEMA kinaelewa kwamba
zipo sheria nyingine katika nchi yetu ambazo Serikali ingeweza kuzitumia
kushughulikia madai iliyoyatoa kuwa Gazeti la Mwanahalisi limeandika habari na
makala za uchochezi, uhasama na uzushi kupitia mahakama lakini imeamua kwa makusudi
kuendelea kutumia sheria mbaya isiyokuwa na uhalali wa kihaki (illegitimate).
CHADEMA kinakumbusha kuwa
kwamba Sheria hiyo ni kati ya Sheria zilizotajwa na Tume ya kukusanya maoni juu
ya mfumo wa vyama vingi (Tume ya Nyalali) kuwa ni sheria mbaya miaka 20
iliyopita kuwa na Sheria mbaya na Serikali imekuwa ikikwepa kutunga sheria mpya
pamoja na wadau wa habari kuandaa miswada ya sheria ya huduma za vyombo vya
habari na uhuru wa taarifa kwa nyakati mbalimbali.
CHADEMA kinatoa mwito kwa
wananchi na taasisi zote za kitaifa na kimataifa kufuatilia kwa karibu tukio
hili la kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi na matukio mengine ya hivi karibuni
kuhusu asasi za kiraia, makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo madaktari na
vyama vya siasa hususan CHADEMA yenye kuashiria kwamba Serikali inayoongozwa na
CCM imeanza mkakati wa kuficha ukweli na kudhibiti mabadiliko kwa kutumia
sheria kandamizi, vyombo vya dola na njia nyingine haramu.
Hivyo, ieleweke kwamba
hatua hii dhidi ya Gazeti la MwanaHalisi ni mwanzo tu wa hatua zingine zaidi
dhidi ya magazeti mengine na taasisi nyingine hali ambayo inahitaji wananchi na
wadau wote kuunganisha nguvu za pamoja katika kuchukua hatua za haraka
kuinusuru nchi na mwelekeo huo.
Imetolewa tarehe 30 Julai 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
COMMENTS