TAARIFA KWA UMMA KWA takribani muda wa juma moja sasa kumekuwepo na taarifa katika vyombo vya habari na njia mbalimbali za upashanaj...
TAARIFA
KWA UMMA
KWA takribani muda wa juma moja
sasa kumekuwepo na taarifa katika vyombo vya habari na njia mbalimbali za
upashanaji habari, kuwa kampuni moja ya meli inayodaiwa kutoka Iran,
inayojulikana kwa jina la NITC (National Iranian Tanker Company), inatumia
bendera ya Tanzania, isivyo kihalali na kinyume kabisa na sheria za nchi na
zile za kimataifa, kwa malengo ambayo hayajulikani.
Pamoja na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kutoa taarifa kwenye Baraza la Wawakilishi tarehe 2 Julai 2012
kukanusha taarifa hizo, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaitaka
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia kwa Waziri wa Mambo ya
Nje na Waziri wa Uchukuzi kutoa taarifa kwa umma juu ya hatua ilizochukua
kuchunguza madai hayo.
Aidha, Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ieleze iwapo utaratibu huo umezingatia kwa ukamilifu
United Nations Convention law of the Sea, kifungu cha 91, Geneva Convention of Registration kifungu cha
6 na maazimio mengine ya kimataifa kuhusu usajili wa meli kubwa pamoja na
usafirishaji wa mafuta.
Maelezo yaliyotolewa na Serikali
ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inayoongozwa na CCM na CUF yanaibua maswali
kutokana na kampuni ya Philtex ya Dubai
inayoelezwa kupewa uwakala na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini- Zanzibar Maritime
Authority (ZMA) kufanya kazi na makampuni mengine hivyo taarifa hizo
hazijitoshelezi katika kuondoa uwezekano kwamba meli za NITC zilipeperusha
bendera ya Tanzania.
Ili kujisafisha juu ya tuhuma
hizo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilipaswa kushirikiana na Serikali ya
Muungano kufanya uchunguzi wa kubaini msingi wa tuhuma hizo na kuchukua hatua
iwapo meli za NITC zilipeperusha bendera ya Tanzania bila ridhaa ya serikali zote mbili.
Ikumbukwe kwamba hii si mara ya
kwanza kwa baadhi ya maofisa wa ZMA kutuhumiwa kuruhusu vitendo vilivyo kinyume
na sheria kama ilivyojitokeza wakati wa kashfa ya kuzama kwa meli ya Spice
Islender.
Kwa upande mwingine, Serikali ya
Muungano nayo haiwezi kukwepa kuwajibika kwa kuzingatia kuwa kuwa baadhi ya
taarifa hizo katika vyombo vya habari vimewanukuu mawaziri wa serikali
wakionekana kujikanyanga na kujikanganya juu ya suala hili nyeti la bendera ya
taifa, ambayo ni moja ya utambulisho wetu rasmi kama Watanzania, kutumika kwa
malengo yasiyojulikana na kampuni ya nje.
Moja ya vyombo vya habari hapa
nchini, vimewanukuu mawaziri husika, Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe na
Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, juu ya suala
hilo.
Wakati Waziri Mwakyembe
amenukuliwa akisema kuwa anazo taarifa za suala hilo, lakini asingeweza kulitolea
kauli mpaka Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa Tanzania Zanzibar azungumze,
Waziri Membe yeye mbali ya kukiri kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria, anasema
habari hizo zilikuwa za kushtushwa na ngeni kabisa, huku akisema kuwa vyombo
husika vitalichunguza kwa makini.
Ukimya wa serikali yetu ambayo
kwa hakika unatokana na udhaifu wake katika kuchukua maamuzi, sasa umesababisha
kitendo hicho kutafsiriwa kuwa Tanzania inaibeba na kuisaidia Iran kukwepa
vikwazo ambavyo nchi hiyo inatishiwa na mataifa ya Magharibi, hasa Marekani na
Umoja wa Ulaya, kutokana na malumbano ya muda mrefu ambayo yanatokana na
mataifa hayo kutumia mabavu na vitisho kuzichagulia baadhi ya nchi nyingine
duniani, nini cha kufanya na rasilimali zake mathalani mzozo unaoendelea na
Iran kuhusu urutubishaji wa madini ya urani.
Si nia ya CHADEMA kuingia katika
mgogoro wa Iran na Mataifa ya Magharibi hapa kupitia mjadala wa madai hayo
yaliyoandikwa kwenye vyombo vya habari; lakini CHADEMA kinatoa tamko kufuatia ukimya
na kigugumizi kinachoikumba Serikali ya CCM, kila inapohitajika kufanya maamuzi
ya haraka, hasa kuwalinda watu wake na hadhi ya utaifa wao na nchi yao ndani na
nje ya nchi.
Ni kutokana na udhaifu wa
serikali hii, ambayo umekuwa ukijidhihirisha pia kwa kushindwa kupanga bajeti
inayojitegemea hasa kwa kutumia utajiri mkubwa wa rasilimali ambazo nchi hii
imebarikiwa, hali inayotufanya tuonekane taifa ombaomba na kupoteza heshima
mbele ya mataifa makubwa na madogo, kuwa hatuna uwezo wa akili kuweza
kujitegemea. Utegemezi huu umefanya baadhi ya raia wa Nchi nyingine mathalani
Mbunge aitwaye Howard Berman wa Bunge la Marekani, akiwa kama Mwenyekiti wa
Kamati ya Masuala ya Nje, kupata uwezo wa kuandika barua ya dharau na kejeli
kwa Rais Jakaya Kikwete, juu ya suala hilo la Meli za NIT kutuhumiwa kupeperusha
bendera za Tanzania.
Kupitia tamko hili, CHADEMA
tunaitaka serikali kutoa kauli madhubuti juu ya suala hilo ambalo tayari
limechukua sura ya mjadala wa kimataifa usiokuwa na tija yoyote kwa mustakabali
wa Watanzania. Suala la bendera ambayo ni utambulisho wa taifa letu, haliwezi
kuwa suala la mchezo tu, ambapo mawaziri wazima hawawezi kutoa kauli za kina na
kuchukua hatua zinazostahili.
Imetolewa
tarehe 2 Julai 2012 na:
Hamad
Mussa Yussuf
Naibu
Katibu Mkuu Zanzibar
.
COMMENTS