Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba avitaka vyama vya siasa, asasi za kidini na wanaharakati kuach...
Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba avitaka vyama vya
siasa, asasi za kidini na
wanaharakati kuacha kuwaelekeza wananchi aina ya
maoni wanayopaswa kutoa
kuhusu Katiba Mpya.
Jaji Warioba ameyasema
hayo leo (Alhamisi, Agosti 9, 2012) katika mkutano wake na
waandishi wa habari
kuzungumzia tathmini ya mikutano ya awamu ya kwanza ya
ukusanyaji wa maoni ya
wananchi kuhusu Katiba Mpya katika mikoa minane ya Pwani,
Dodoma, Manyara, Kagera,
Shinyanga, Tanga, Kusini Unguja na Kusini Pemba.
“Sio wanasiasa tu, watu
wote wakiwemo viongozi wa kidini, wanaharakati na taasisi
zisizo za kiserikali
ziache kuwalazimisha wananchi watoe maoni wanayotaka wao.
Wananchi wawe huru kutoa
maoni yao,” alisema na kuongeza kuwa vyama vya siasa,
asasi zisizo za
kiserikali zitapata muda wa kuwasilisha maoni yao Tume.
SOMA TALKING NOTES ZA JAJI
MAELEZO YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA
KATIBA
JAJI MSTAAFU JOSEPH S. WARIOBA KATIKA MKUTANO WA
WAANDISHI WA
HABARI TAREHE 09 AGOSTI, 2012 KATIKA UKUMBI WA
WA MIKUTANO WA TUME, DAR ES SALAAM
_____________________________
Ndugu
Wanahabari,
Nichukue fursa hii kuwashukuru sana kwa kukubali
mwaliko wetu na nawakaribisheni. Lakini pia niwashukuru sana kwa namna
mnavyotoa habari za Tume zikiwemo za mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi
iliyofanyika katika Mikoa minane ya awamu ya kwanza.
Ndugu
Wanahabari,
Kama mnavyokumbuka tarehe 19 Juni, 2012 nilifanya
mazungumzo nanyi kwenye Ukumbi wa Karimjee hapa Dar es Salaam, na siku
iliyofuata yaani tarehe 20 Juni, 2012 nilifanya mazungumzo na wenzenu wa
Zanzibar, kwenye Ukumbi wa Salama uliopo katika Hotel ya Bwawani. Lengo la
mazungumzo yale ilikuwa ni kuzindua rasmi kazi za Tume kupitia kwenu na
kuwaeleza jinsi Tume ilivyokuwa imejipanga kutekeleza majukumu yake.
Ndugu
Wanahabari,
Pamoja na mikutano hii, Tume iliendelea kutoa
elimu kwa umma kuhusu majukumu ya Tume na kuwahamasisha wananchi wajitokeza
kutoa maoni. Tume pia imechapisha na kusambaza machapisho yafuatayo:
1. Vitabu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Katiba ya Zanzibar;
2. Kitabu cha Katiba na Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kwa lugha nyepesi;
3. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83;
4. Kijitabu kinachoelekeza wajibu na Majukumu ya Tume
ya Mabadiliko ya Katiba;
5. Kipeperushi cha maswali yanayoulizwa mara kwa mara
kuhusu Tume; na
6. Kipeperushi kinachoeleza majukumu na kazi za Tume.
Nakala zote hizo zilisambazwa kwenye Mikoa, Wilaya
na Kata zote kwenye mikoa minane iliyopangwa kufikiwa kwenye awamu ya kwanza.
Ndugu Wanahabari,
Leo nimewaalika ili niwape tathmini ya kazi ya
kukusanya maoni katika mikoa minane ya awamu ya kwanza ambayo ni Pwani, Dodoma,
Manyara, Kagera, Shinyanga, Tanga, Kusini Unguja na Kusini Pemba. Mikutano
katika mikoa hii ilifanyika kuanzia tarehe 2 Julai hadi tarehe 30 Julai 2012.
Nianze kwa kusema kuwa Tume imefika na kufanya
Mikutano kwenye Wilaya zote na kwenye vituo vyote ilivyopanga. Katika mikutano
hiyo, maoni ya wananchi yalipokelewa kwa njia ya kuzungumza na wengine
waliwasilisha maoni yao kwa maandishi.
Idadi
ya Mikutano iliyofanyika
Jumla ya Mikutano iliyofanyika kwenye Mikoa yote minane
ni 386. Kati ya Mikutano hiyo, Tume ilifanya Mikutano 8 na Makundi maalum yakiwemo
Taasisi za Dini na Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Idadi
ya Wananchi waliohudhuria Mikutano ya Tume
Wastani wa wananchi 188,679 walihudhuria mikutano
ya Tume. Hii ikiwa ni wastani wa watu 489 walifika kwenye kila Mkutano. Tume
inaridhika na idadi hii na inaonesha wananchi wana mwamko wa kutoa maoni yao.
Idadi
ya Wananchi waliotoa maoni
Jumla ya wananchi 17,440 walitoa maoni yao kwa
njia ya kuzungumza kwenye Mikutano ya Tume. Aidha, jumla ya wananchi 29,180 walitoa
maoni yao kwa njia ya maandishi na kuyawasilisha kwenye Mikutano ya Tume.
Ndugu
Wanahabari,
Kimsingi, Tume imeridhika na kazi ya ukusanyaji wa
maoni katika awamu ya kwanza na imepata mafanikio yafuatayo:
i.
Mikutano yote
iliyopangwa na Tume imefanyika kwa mujibu wa Ratiba;
ii.
Mikutano yote
ilifanyika kwa amani na utulivu na wananchi walivumiliana katika kutoa maoni
yao;
iii.
Mikoa na Wilaya wameipa
Tume ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yake;
iv.
Baadhi ya Wananchi
wametoa maoni yao bila kushawishiwa na vikundi, vyama au taasisi;
v.
Katika baadhi ya
maeneo, Tume iliweka utaratibu na ilipokea maoni kutoka kwa makundi maalum kama
walemavu na wananchi wasioweza kuzungumza kwa lugha ya Kiswahili;
Ndugu Wanahabari,
Pamoja na mafanikio niliyoyataja hapo juu, Tume
imekabiliana na changamoto mbalimbali. Changamoto kubwa ambayo Tume imekutana
nayo ni ya Vyama vya Siasa kuingilia uhuru wa wananchi kutoa maoni yao. Vyama
vya siasa vimekuwa vikitoa kauli na maelekezo kwa wanachama wao kufuata
misimamo ya vyama jambo linalowanyima wananchi uhuru wa kutoa maoni yao. Tume
inapenda kuvitaka vyama vya siasa viwaache wananchi watoe maoni yao bila
kuwashinikiza. Changamoto nyingine ni pomoja na:
i.
Wanawake bado
hawajitokezi kwa wingi kutoa maoni yao mbele ya Tume ingawa wanahudhuria
mikutano hiyo;
ii.
Baadhi ya Wananchi kutegemea
njia moja tu ya kuwasilisha maoni kwa kuzungumza wakati kuna njia nyingine kama
barua pepe, posta n.k
iii.
Shughuli za Tume
kuingiliana na shughuli nyingine za Kijamii kama vile ibada, magulio n.k
iv.
Muda wa saa tatu kwa
mkutano mmoja katika maeneo ya mjini umeonekana hautoshi kwa wananchi kuchangia
maoni yao;
Ndugu
Wanahabari,
Baada ya kuwaeleza mafaniko na changamoto, naomba
sasa nitoe wito kwenu kutumia kalamu na kamera zenu kuwaelimisha kwa kuendelea
kuwapatia wananchi taarifa sahihi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume. Jiepusheni
na kuandika habari zenye lengo la kuwapotosha na kuwakatisha tamaa wananchi.
Kama huna uhakika na jambo unalotaka kuandika wasiliana na Ofisi ya Tume utapata
ufafanuzi.
i.
Taasisi na Asasi mbalimbali
zitumie uwezo wao kuwaelimisha wananchi kufika kwenye Mikutano ya Tume na kutoa
maoni yao au kuiandikia Tume;
ii.
Vyama vya Siasa,
Taasisi na Asasi mbalimbali wawaache Watanzania watoe maoni yao kwa uhuru bila
kulazimishwa;
iii.
Wananachi wanapaswa
kutambua kwamba, Katiba inayoandikwa ndiyo nguzo na mwelekeo wa maisha yao ya
kila siku, wasikubali kutumiwa kwa namna yoyote ile na kikundi, Taasisi, Asasi
au Chama chochote katika kuwasilisha maoni yao kwa Tume;
Ndugu
Wanahabari,
Naomba nimalizie kwa kuwaeleza kuwa awamu ya pili
ya kazi ya ukusanyaji maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya itafanyika katika
mikoa saba ambayo ni Mbeya, Morogoro, Lindi, Ruvuma, Kigoma, Katavi na Mwanza.
Kazi ya kukusanya maoni kwenye Mikoa hii inatarajiwa kuaanza rasmi tarehe 27
Agosti, 2012 na kukamilika tarehe 28 Septemba, 2012. Ratiba ya mikutano hiyo
itatolewa na Tume hivi karibuni.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
TOA MAONI, TUPATE KATIBA MPYA
COMMENTS