STATE HOUSE ZANZIBAR OFFICE OF THE PRESS SECRETARY PRESS RELEASE TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Rais wa Zanzibar na Mweny...
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa
viongozi na wataalamu kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti zinazofanywa
zinawafikia walengwa kwa muda muafaka ili matokeo hayo yaweze kuleta manufaa
yaliyokusudiwa.
Wito huo ameutoa leo wakati uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya sikukuu ya wakulima (Nanenane)
Yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya maonesho ya Kilimo Ngogo nje kidogo mwa mji wa
Lindi.
Alisema kuwa matokeo ya tafiti za kilimo na mifugo yanayooneshwa katika maonesho hayo hayana
budi kufikishwa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili yaweze kutumika kuimarisha
shughuli zao.
Alisisitiza kuwa utafiti ni suala la msingi katika maendeleo ya taifa hivyo kauli mbiu ya
maadhimisho hayo Matokeo Makubwa Sasa, Kilimo ni Biashara utekelezaji wake hauna
budi uzingatie umuhimu wa utafiti katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili
kuzifanyia kazi changamoto zinazoweza kukwamisha kufikia lengo la kaulimbiu
hiyo.
Dk. Shein aliwaeleza mamia ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo kuwa maeonesho hayo
yanatoa fursa kwa wahusika katika sekta hizo kuanzia wataalamu, wakulima,
wafugaji, wavuvi pamoja na wadau wengine kubadilishana uzoefu na utaalamu
ikiwemo tekinolojia na mbinu za kisasa za katika sekta hiyo.
Kwa hivyo alisema hiyo ni fursa adhimu ya kuonesha mafanikio na kujifunza na hatimae kuongeza ufanisi katika kuimarisha ukuaji wa sekta hizo ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Dk. Shein alibainisha kuwa kwa Tanzania Bara sekta ya kilimo
inachangia asilimia 24.5 ya pato la taifa na kutoa ajira kwa asilimia 80
na asilimia 30 ya mapato ya fedha za kigeni wakati kwa upande wa Zanzibar
inachangia asilimia 30.1 ya pato la taifa na kutoa ajira kwa asilimia 70 na
mapato ya fedha za kigeni asilimia 19.6.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesifu jitihada kubwa zinazofanywa na
wakulima, wafugaji na wavuvi wa Tanzania na kueleza kuwa maonesho hayo
yanadhihirisha jitihada zao hizo katika kuzalisha chakula na malighafi
zinazotumiwa na viwanda humu nchini.
Halikadhalika ameeleza kuridhishwa kwake na kazi zinazofanywa na watafiti nchini na kutumia
fursa hiyo kuwapongeza kwa kazi nzuri waifanyayo ambayo imechangia kuongeza
tija katika kilimo, ufugaji na uvuvi.
Kwa hiyo ametoa wito kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kuendelea kutumia vyema ushauri wa
kitaalamu katika kufanya shughuli zao kwani kufanya hivyo watakuwa sio tu kuwa
wameonesha thamani ya kazi za kitafti wa wataalamu wetu bali pia kuongeza
kipato chao na kuinua uchumi wa taifa.
Katika hotuba yake hiyo alihimiza pia wakulima na wafugaji kuzingatia ubora wa mazao na mifugo yao
kwa kuwa hicho ndicho kigezo muhimu katika kufikia bei ya kuuza na kununua.
Alisisitiza kuwa mifugo ni rasilimali muhimu na kubwa kwa taifa na ambayo inaweza kuchangia kwa
kiasi kikubwa katika kupiga vita umasikini endapo wafugaji watazingatia
miongozo na kanuni bora za ufugaji.
Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa lengo la Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi Zanzibar ni kuona wakulima na wafugaji wanaishi maisha bora na wanachangia katika suala zima la kuwa na masiha bora jkwa kila mtanzania.
Alitoa mfano kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia programu mbalimbali ukiwemo Mkakati na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo ili kuleta mabadiliko katika sekta ya
kilimo nchini.
Katika mnasaba huo aliwataka viongozi na wataalamu wa kilimo na mifugo nchini kuitekeleza progamu
hiyo kwa makini na kwa ufanisi kufikia malengo ya programu hiyo.
Alikumbusha na kusisitiza pia umuhimu wa wakulima kupatiwa elimu ya kutosha ya hifadhi na
utunzaji wa mazingira hasa kwa kuzingatia matatizo yanayotokana na mabadiliko
ya tabia nchi yanayoathiri shughuli za uchumi ikiwemo kilimo na ufugaji.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa vyombo vya habari kuwahamasisha wakulima, wafugaji na wananchi kwa
ujumla kufika katika maonesho hayo ili kujionea mafanikio na kujifunza mambo
mbalimbali yatakayoweza kuwasaidia kuendeleza shughuli zao.
Kabla ya kuzindua rasmi maadhimisho hayo Dk. Shein ambaye alikuwa amefuatana na mawaziri wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar alipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali katika manesho hayo.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015,
Fax: 024 2231822
COMMENTS