Baadhi ya Wahandisi wahitimu kutoka katika vyuo na taasisi mbalimbali wakila kiapo cha utii kwa Taaluma yao mbele ya Kamishna wa Viapo w...
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuwatumia wahandisi wazalendo waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Wahandisi kwa mwaka 2015 leo jijini Dar es
salaam, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kuwa Wahandisi
wanao mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kwa kuifanya mipango iliyo
kwenye karatasi kuwa katika uhalisia unaoonekana kwa macho.
Amesema fani ya
uhandisi inagusa maisha ya watu moja kwa moja hasa sekta ya ujenzi wa
miundombinu ya maji, umeme, majengo,miundombinu ya migodi, hospitali, barabara,
viwanda na shughuli nyingine za kihandisi.
"Ni jambo
lililowazi kuwa tuna kila sababu ya kujivunia maendeleo na mafanikio
tuliyofikia, tuna kila sababu ya kuwatumia na kutoa kipaumbele kwa wahandisi
wazalendo ,wahandisi wetu wanaweza" Amesisitiza Balozi Sefue.
Amewataka wahandisi
hao kuendelea kuzingatia weledi pindi wanaposimamia utekelezaji wa miradi
ya Serikali ili miradi hiyo iendane na thamani halisi ya fedha za wananchi kwa
kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kugharamia miradi hiyo.
"Nawataka
muendelee kuzingatia weledi,muwe waadirifu na mfanye kazi kwa bidii ili tufikie
malengo ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025,mkumbuke kuwa kazi mnazofanya
zinaonekana na watu wote, zikiwa mbaya au kuwa chini ya viwango watasema
tu na mtaonekana hamzingatii taaluma wala viapo vyenu" Amesisitiza.
Amesema toka mwaka
2005 hadi 2015 Sekta ya Uhandisi nchini Tanzania imeweza kuwanufaisha
watanzania kwa kuzalisha ajira 256,480 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea
kuweka mazingira mzauri kwa kuboresha shule , vyuo na taasisi mbalimbali ili
ziweze kuzalisha wahitimu bora wenye kuhimili ushindani soko.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akikabidhi vyeti na miongozo mbalimbali ya utendaji wa kazi kwa Wahandisi baada ya kuapishwa nchini leo jijini Dar es salaam. |
Aidha, ameziagiza
Halmashauri kote nchini kuhakikisha kuwa zinakuwa na wahandisi waliosajiliwa na
Bodi ya Usajili wa Wahandisi kabla ya Juni 30, 2016 na kuongeza kuwa Serikali
itaendelea kuweka msisitizo katika ubora wa wahandisi wa ndani na nje ya nchi
pamoja na kuimarisha ushirikiano uliopo katika sekta ya ujenzi baina Tanzania
na nchi za jirani.
Awali akiongea kabla
ya kumkaribisha mgeni rasmi kuongea na washiriki wa maadhimisho hayo Naibu
Katibu Mkuu,Wizara ya Ujenzi, Muhandisi Joseph Nyamhanga, amesema kuwa siku
hiyo inatoa fursa kwa wahandisi kote nchini kukutana na kubadilishana uzoefu wa
kitaalam katika kuleta maendeleo nchini.
Amesema Bodi ya
Usajili wa Wahandisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imewezesha kufanyika
kwa maadhimisho hayo nchini Tanzania lengo kubwa likiwa ni kuweka msukumo na
msisitizo wa kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2015, kuangalia changamoto
na mikakati ya kukabiliana nzao.
Ameongeza kuwa
mkutano huo wa mwaka unafanyika nchini Tanzania kwa mara ya 13
ukizishirikisha baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Nigeria,Afrika
kusini,Malawi, Kenya na wawakilishi kutoka Norway.
Amefafanua kuwa
kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) sekta ya ujenzi imetoa
mchango mkubwa kupitia wahandisi waliopo nchini kwenye shughuri za ujenzi wa
miundombinu, ushauri na usimamizi wa miradi mbalimbali.
Amebainisha kuwa kasi
ya Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati inaendelea kutekelezwa kwa kasi
kupitia sekta ya ujenzi, viwanda,kilimo, umwagiliaji na shughuli za
migodini.
Ameeeleza kuwa
Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa wahandisi wazalendo na kuweka mkazo
katika kushughulikia changamoto walizonazo ili taifa liendelee kunufaika
kutokana na gharama kubwa inayotumika kuwasomesha.
"Serikali
inatumia gharama kubwa kuwasomesha wahandisi wetu, ni jambo jema tukiendelea
kuweka mkazo ili kuwalinda wahandisi wa ndani na mabadiliko yaliyopo yanayoweza
kusababisha wengi wao kutafuta ajira nje ya nchi" Amesema.
Kwa upande wake
Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB) Muhandisi Steven Mlote ameeleza kuwa
maadhimisho ya Siku ya Wahandisi nchini yanaambatana na majadiliano ya kina
kuhusu shughuli za kihandisi nchini na miaka 15 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2025.
Aidha, amesema kuwa
ERB imewatambua na kuwapa Tuzo na zawadi mbalimbali wahandisi na wahitimu wa
Taasisi waliofanya vizuri zaidi katika mitihani yao mwaka 2014/2015 huku baadhi
ya wahandisi wahitimu wakiapa kiapo cha utii kwa taaluma yao.
Ameongeza kuwa
katiaka kipindi cha siku 2 za maadhimisho hayo kutakuwa na
maonesho ya kiufundi ya jumuiya za wahandisi wa Tanzania na taasisi
mbalimbali za elimu ya Uhandisi zikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Taasisi
ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Uhandisi na Teknolojia
St.Joseph , Chuo cha Ardhi (ARU), Makandarasi ,Kampuni za Ushauri wa
kihandisi,Mashirika na makampuni ya kibiashara na taasisi za utafiti.
Source: Aron Msigwa-
MAELEZO
COMMENTS