KAMPUNI ya Bharti Airtel imeingia makubaliano ya kimkataba na kampuni ya American Tower Corporation (NYSE: AMT) ya kununua  minara ya mawasiliano 1,350 ya Airtel Tanzania.
Chini ya mkataba huo, kampuni ya American Tower pia itachukua minara mingine  takribani 100 ambayo iko katika hatua ya kujengwa na kuendelezwa.
Kwa mujibu wa meneja mawasiliano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando mchakato wa kukamilisha makubaliano hayo  ambayo yatafanya Airtel Tanzania  sasa kulipia gharama za kukodi minara hiyo chini ya mkataba wa awali wa miaka 10, yanaendelea.
 “Unajua sisi tunamilikiwa asilimia 40 na serikali kwa hiyo mpaka pande zopte ziwe zimeridhia ndio tutasema maafikiano ya kuanza utaratibu huo yanaanza lini” alisema mbando akifafanua kuhusu mauzo na uendeshaji wa baadae wa minara hiyo.
Akizungumza kuhusu makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Bharti Airtel Africa Christian de Faria alisema: “ Tunayofuraha kukuza ushirikiano wetu na kampuni ya American Tower barani Afrika.  Mapendekezo ya makubaliano haya ni mwendelezo wa filosofia yetu ya kuhakikisha tunaachana na utamaduni wa kumiliki rasilimali na kuhamasisha matumizi ya minara ya mawasiliano kwa pamoja ili kuboresha utoaji wa huduma za mawasiliano ambao zitasaidia huduma za mawasiliano kuwa bora zaidi.
“Airtel bado inaendelea na dhamira yake ya kuwekeza katika uendeshaji wa huduma zake Tanzania na kutoa huduma bora na za kisasa kwa wateja wake nchi nzima’’  
 Mauzo ya minara ya mawasiliano itaiwezesha Airtel kuwa makini na kuongeza ufanisi kwenye kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wake,na vile vile kupunguza madeni na gharama za uendeshaji wa minara kwa kiasi kikubwa.
 Makubaliano ya mkataba huo yanategemewa kufungwa katika kipindi cha kwanza cha mwaka 2016.
Naye rais wa American Tower, Hal Hess,  ( ukanda wa ulaya, mashariki ya kati na Afrika)   alielezea furaha yake katika kufanya biashara nchini Tanzania.
“ Tunayofuraha kubwa kutangaza kuingia katika biashara nchini Tanzania na kuendeleza ushirikiano wetu na Airtel, moja kati ya kampuni  kubwa  ya huduma za mtandao inayoongoza duniani’’ alisema
 Aidha alisema Tanzania ni moja kati ya nchi yenye matarajio ya kukua kwa idadi ya watu na kasi kiuchumi ni kubwa  na ni eneo ambalo wanaona linafaa kwa biashara zao.
Makubaliano hayo yamefikiwa mjini New delhi, India ambapo Bharti iliiwakilisha Airtel Tanzania.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO