MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan kesho atawasha  Mwenge wa Uhuru na kuzindua rasmi mbio zake katika halmashauri za wilaya na  Manispaa 179 za mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani .
Uzinduzi huo utakaofanyika katika uwanja wa Jamhuri wa mjini Morogoro ambao utatanguliwa na shamrashamra za halaiki kutoka kwa  vijana zaidi ya 1,000 na vikundi vya utamaduni kutoka wilaya za mkoa wa Morogoro na nje ya mkoa .
Katika uzinduzi huo  viongozi mbalimbali wa Serikali , dini na vyama vya siasa wamealikwa kushiriki wakiwemo pia Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  pamoja na Waziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Miongoni mwa Mawaziri ambao tayari hadi leo walikuwa wamewasili mkoani hapa ni Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia  Bunge, Sera , Uratibu , Ajira na Walemavu , Jenista Mhagama pamoja na  Waziri wa Kazi , Uwezeshaji Wazee , Wanawake na Watoto, Moudin Castico .
 Mawaziri hao waliungana na Makamu wa Rais katika ziara ya kutembelea miradi ya vijana wajasiliamali wa mafundi Seremala eneo la  mtaa wa Betero , Kata ya Sabasaba , Manispaa ya Morogoro.
Kauli mbiu za Mwenge wa Uhuru  kwa mwaka huu (2016): “ Vijana ni Nguvu kazi ya Taifa , Washirikishwe na Kuwezeshwa “.
 Hivyo itakuwa ni  kwa mara ya tatu   Mwenge wa Uhuru kuwashwa mkoani Morogoro ambapo   mara ya kwanza uliwashwa mwaka  1985 eneo la Wami Sokoine , kabla ya  wilaya ya Morogoro kugawanywa na kuzaliwa wilaya ya  Mvomero ikiwa ni   kumwezi  Waziri mkuu hayati Edward Moringe Sokoine aliyekufa kwa ajali ya gari eneo hilo mwaka 1984.
Serikali iliupatia heshima mkoa wa Morogoro kuwa mwenyeji  wa kuzindua mbio za  Mwenge wa Uhuru   mnamo  mwaka 2006  uliowashiwa katika  uwanja wa Jamhuri .

Mbali na kuwasha mwenge mara ya tatu , pia  mkoa ulipata heshima nyingine ya kuzima Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 1994  eneo la Mazimbu, Manispaa ya Morogoro  ilikuwa ni  heshima ya Ukumbozi wa Afrika Kusini , eneo  hilo la  Mazimbu, lilitumiwa na Chama cha African National Congress (ANC) ambapo palikuwa  ni Makao Makuu ya ANC katika kuendesha mapambano dhidi ya makaburu wa Afrika Kusini
Mwenge  wa Uhuru uliwashwa kwa mara ya kwanza Desemba 9, 1961 kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro kutimiza ahadi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO