Mzee Machano akiwa na mwandishi wa makala haya
Mimi nilikuwapo kwenye kutengeneza banda la fete pale Kisiwandui na nilikuwepo kwenye doria wakati Sheikh Karume akitangaza mapinduzi katika kituo cha radio pale Rahaleo, anasema  mzee Machano Mjomba Machano akiwa ameegemea ukuta pale nyumbani kwake Gamba Mabatini, kiasi cha kilomita 25 kutoka Malindi.
Mpango wa fete uliokuwa umebuniwa na Chama cha Afro Shiraz ulilenga sana katika kuondoa mashaka ya serikali ya Sultani na vyombo vyake na kuwawezesha vikundi vya wanamapinduzi kuingia mjini na kutekeleza kazi yao.
Fete na mkutano ulilenga kuweka sawa mambo ambayo yanahitaji usiri mkubwa.
Mzee Machano anasema alikuwa na kundi kubwa ambalo analikumbuka kutoka katika jimbo lake ambalo lilishiriki moja kwa moja kama viongozi wa vijana walioshiriki mapinduzi kutoka katika maeneo hayo.
Anamkumbuka Nasoro wa Donge , ambaye aliwaongoza wenzake kwenda kwa miguu katika fete iliyowezesha usiku watu kuanza kazi ya kuvamia na kushika maeneo muhimu. Wengine ambao aliwakumbuka wazi ni Ahmed Ameir, Kinyeshi na haji mabunduki wa Kidoti.
Ukiwa mvumilivu unaweza kupata faida kubwa katika mazungumzo na mzee huyu ambaye kama serikali ingelifanya juhudi kidogo ya kupima umri wake, ni lazima ingelikuwa, sherehe kubwa kwa taifa kuwa na mtu mwenye umri mkubwa anayeweza kuingia katika vitabu vya rekodi za dunia.
Kuwepo kwa rekodi sahihi ya Mzee Machano Mjomba Machano kwa kuwa na matokeo ya vipimo kama vya skana (MRI) tungekomesha maneno ya watu kwamba ukiwa katika nchi zinazoendelea huwezi kukatisha zaidi ya miaka 120 na kutoa fumbo kubwa kwa ushiriki wake wa kwenye mapinduzi akiwa na umri mkubwa.
Kwenye mazungumzo yangu na mzee huyu niliyofanya hivi karibuni nilifurahishwa sana jinsi anavyoelezea ushupavu, ushujaa wa kizazi chake katika kufanikisha mapinduzi ya Zanzibar yaliyompa heshima Mwafrika baada ya kudhalilika kwa kipindi kirefu.
Mwafrika katika visiwa vya Unguja alidhalilika kwa namna tofauti kuanzia kipindi cha warenjo, waarabu na usulutani wao na Waingereza waliojichukulia mamlaka ya kutawala visiwa na kasha kuwageuka waafrika kwamba hawawezi kujitawala na kula sahani moja na sultani kuwapandisha Hizbu kwenye chati.
Ni nadra sana kupata taarifa  za undani za mapinduzi hayo, kutokana na wengi walioshiriki moja kwa moja kutangulia mbele za haki na kutokuwapo kwa taarifa za kutosha kuhusiana na maandalizi na utekelezaji wa shughuli hiyo nzito, mtu mwenye masimulizi japo kidogo ni Sheikh Thabiti Kombo Jecha.
Lakini unapokutana na mzee huyu akakusimulia jinsi watu walivyotoka kwa wingi katika maeneo ya makodeni na hata katika jimbo hilo ambalo ni la Chama cha Mapinduzi likiwa pia na uasili wa Afro Shiraz unajikuta ukiuma meno kwa ushujaa wa kukataa uhuru bandia wa mwaka 1963 na kasha kutengeneza mapinduzi yaliyorejesha heshima kwa mwafrika.
Pamoja na vizuizi vingi walivyowekewa na utawala wa sultani kwa wakazi wa makodeni na shambani kutoshiriki pamoja na kwenda mjiini, akili pevu ya kamati  kuu ya ASP ambayo tangu mkutano wa pili wa kutengeneza katiba London, walkiona hawana chao kwa jinsi mambo yalivyokuwa yakisukwa, viongozi wa ASP mashambani waliendelea kunoa vijana wao kukataa udhalilishaji mpya wa mwaka 1963.
Watu wengi wameandika kinyume na mapinduzi ya mwaka 1964, na waandishi pamoja na maandishi yao ya kupinga na kulaani ni wale wenye uwezo waliopokonywa tonge mdomoni baada ya sultani  kulazimika kukimbilia baharini na baadae Dare s salaam kwenye hifadhi ya Mwalimu Nyerere akiwa njiani kwenda Uingereza.
Mzee Machano anasema japo yeye hajui kusoma na kuandika na kwamba mapinduzi yalitokea akiwa na umri wa takribani miaka 70  amesema kwamba hasira za Wazanzibari weusi za kunyimwa madaraka katika uchaguzi kwa njia ya voti, zilipoozwa na mafanikio ya mapinduzi yaliyopangwa kwa usiri wa kutosha.
Anasema kabla ya mapinduzi yeye alikuwa anaongoza branchi mbili za Kidoti na Tazari kabla ya Kidoti kukabidhiwa Haji mabunduki na kwamba mafunzo ya mapinduzi yalifanyika kwa haraka.
Nilipata nafasi ya KMumuuliza John Okello   na katika jibu lake alisema kwamba ni mtu aliyeingizwa katika mapinduzi kusaidia kufunza watu na kuwaelekeza namna nzuri ya kufanya mapinduzi bila kuwa na silaha za moto kwa kutumia marungu na mikuki.
Anasema katika mazungumzo kwamba Okello si mzanzibari bali alikuwa mganda ambaye alikuwa anajua vyema medani na alifanya kazi njema ya kufunza wazazibari namna ya kuendesha mafunzo hayo.
Wilaya ya kaskazini A katika mkoa wa Kaskazini Unguja ni sehemu ambayo waafrika wengi wenyeji wa tumbatu na Paje wanaishi na ambao mchango wao katika ufanisi wa mapinduzi ya Ungtuja si haba.
Baada ya Kamati kuu ya ASP kutambua kwamba hawana cha kufanya zaidi ya kutwaa nchi kwa nguvu wakaanza kufanya maandalizi  kwa kuwa uanzishaji wa vikundi  ambapo juu yake muongozaji alikuwa Sheikh Karume mwenyewe.
Kwa upande wake mzee Machano anakumbuka wajumbe wa baraza la apinduzi akina Hamis Haji, Wagu, Nyangemse , Mwadini Ally na  Musahaji.
Ingawa mtoto wake ambaye alikuwapo  alisema kwamba haoni kama mzee wake alifaidika  na masuala ya siasa. Machano anasema alianza kushiriki siasa kwenye mikaka ya 1930 wakati waafrika walipoanza kuwa pamoja kutafuta nafuu ya mambo yao kufuatia kubanwa na mataifa mengine kama waarabu na wahindi.
Wakati Afro Shiraz Party (ASP)  ilipoanzishwa alikuja kuwa mtu wa kutegemea katika eneo lake la  Kaskazini  ambalo kwa sasa ni jimbo la Mkwajuni.
“ Hapa katika eneo lote hili la Gamba , mzee anaheshimika sana lakini kama unavyoona alivyo na eneo analokaa, na bado anaipenda CCM yake kama alivyoipenda ASP” alisema Musa Machano Mjomba ambaye ni mtoto wake wa pili kutoka mwisho.
Anasema  Mzee wake baada ya kushiriki mapinduzi ya mwaka 1964 alirejea gamba mabatini na kuishi hapo akiendelea na nmaisha yake ya useremala na kulima muhogo na mpunga.
Hata hivyo katyika maisha yake pamoja na kusimuliwa na mzee wa ke kuhusu mapinduzi na ushiriki wake wa karibu sana, hajawahi kuona wanamapinduzi wengine wakienda kumjulia hali mzee huyo ambaye eliumu dunia ambayo ingelimwezesha kusoma kuandika na kuhesabu hakuweza kuipata.
Anawakumbuka watu wengi akiwamo Thabiti Kombo Jecha ambaye anasema wakati wakiwa viongozi vijana yeye alikuwa mzee na walikuwa wakitumia makazi yake kwa shughuli mbalimbali zinazohusu siasa za kupigania uhuru na hadi mapinduzi.
“Mimi naona kama mzee wamemtenda vibaya, ni mzalendo lakini naona anaishi maisha ya shida. Mzee aliyepigania nchi hii anaishi kwa shida.”  Anasema Mussa ambaye anasema haoni faida ya ushiriki wa baba yake katika mapinduzi kwani wengine waenziwa yeye anataabika.
Huenda ni kweli kwani makazi ya mzee huyu hayana hadhi hata kidogo hata kwa mtu wa kawaida, mtoto wake anasema anahitaji milioni moja kurekebisha eneo analokaa mzee wake, ni hela ndogo lakini mwalimu wa skuli  hana uwezo huku ikifikiriwa wazi ni lazima ahakikishe mzee wake katika umri mkubwa vile anapata chakula na nguvu za kuendelea mbele.
mwisho

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO