OFISI YA MKUU WA MKOA
RUVUMA

TAARIFA KWA UMMA
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Satano Mahenge anapenda kuutaarifu Umma kuwa kazi ya kuwatafuta watu waliozama boti iliyopata ajali kwenye kivuko cha mto Ruvuma kutoka kijiji cha Mkenda Songea kwenda kijiji cha Mitomoni Nyasa tarehe  02 Julai, 2016 majira ya saa nane mchana imekamilika.  Boti hiyo inayokadiliwa kubeba watu kati ya 30 hadi 50 ilisababisha watu tisa (9) kuzama mtoni na wengine 36 kuokolewa.
Kazi ya kutafuta miili  iliyopotea ilianza tarehe 03 Julai, 2016 hadi jana tarehe 09 Julai, 2016.  Napenda kuwajulisha wananchi wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla kuwa miili yote tisa ya watu waliozama imepatikana. Taratibu za mazishi zimefanyika kwa familia zikishirikiana na Serikali.
Orodha ya maiti zilizopatikana ni kama ifuatavyo:-
1.     Omari Jela (miaka 11) alipatikana tarehe 05 Julai 2016.
2.     Fadhili Hamis Fadhili (miaka 8) alipatikana tarehe 05 Julai, 2016.
3.     Hadija Said (miaka 41) alipatikana tarehe 06 Julai, 2016.
4.     Zulfa Ally (miaka 14) alipatikana tarehe 06 Julai, 2016.
5.     Awetu Mohamed (miaka 14) alipatikana tarehe 06 Julai, 2016.
6.     Omar Waziri (miaka 13) alipatikana tarehe 06 Julai, 2016.
7.     Stumahi Abdallah (miezi 5) alipatikana tarehe 07 Julai, 2016.
8.     Rajabu Said Machupa (miaka 17) alipatikana tarehe 08 Julai,2016.
9.     Tupishane Mustafa (miaka 5) alipatikana tarehe 09 Julai, 2016.

Serikali inawapongeza  wote walioshiriki kufanya kazi hii ya utafutaji wa miili ya ndugu zetu waliopata ajali, kipekee inawashukuru wananchi wa vijiji vya Mkenda na Mitomoni kwa ushirikiano wao walioutoa kwa kikosi kazi nilichokiunda kusimamia zoezi la utafutaji miili.   Pia  Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa kutoa boti ya kisasa iliyofanya kazi kubwa na nzuri ya kutafuta miili ndani ya mto Ruvuma.  Boti hii imesaidia sana kufanikisha kazi ya upatikanaji wa maiti ndani ya Mto Ruvuma. 
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewashukuru viongozi wa kikosi kazi Bi. Salma Mapunda –Afisa Tarafa ya Muhukuru na Bwana Siima Beebwa – Afisa Tarafa ya Mpepo kwa kusimamia kikamilifu zoezi hili.  Shukrani za pekee ziwafikie Kamati ya Ulinzi na Usalama za Wilaya ya Songea na Nyasa kwa kazi nzuri waliyofanya na Askari wa Kikosi cha Wanyapori kutoka Pori la Akiba Liparamba kwa kushiriki zoezi hili ambapo limesaidia kuwaondoa viboko waliokuwa wakisumbua ndani ya Mto Ruvuma kipindi cha Uokoaji.
Kwa kupitia ajali hii, Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo yafuatayo kwa Wakuu wa Wilaya zote za Ruvuma; kwanza wafanye kazi ya kuvitambua na kuanisha vivuko vyote vilivyopo ndani ya maeneo yao, pili wafanye sensa ya vyombo vya usafiri vinavyotumika kuvusha abiria na mizigo na kuona umakini wake, tatu wawatambue wamiliki na waendeshaji wa boti kwenye mito na Ziwa Nyasa na nne waweke utaratibu wa abiria wote kujisajili kila watumiapo vyombo vya majini.
Mwisho, amewasihi wananchi wote kuzingatia Sheria na Taratibu kila watumiapo vyombo vya moto ili kuepusha ajali zinazosababisha vifo na ulemavu.

Imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa – Ruvuma
Jumapili tarehe 10 Julai, 2016

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO