Waziri Mahiga akizungumza na Jean-Marc Ayrault

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Maendeleo ya Kimataifa wa Ufaransa Bw Jean-Marc Ayrault amefanya ziara  nchini Tanzania tarehe 2  Agosti, 2016.
Waziri huyo yupo nchini kwa ziara ya mashauriano na serikali ya awamu ya tano  ya Rais John Pombe Magufuli iliyoingia madarakani baada ya uchaguzi wa Oktoba 2015.
Bw Aryault alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki  Bw. Augustine Mahiga  na kuzungumza kuhusu uhusiano kati ya Ufaransa na Tanzania uliodumu kwa muda mrefu na unaoendelea kushamiri.  Bw.Jean-Marc Ayrault aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kupigania amani na usalama katika bara la Afrika na hasa juhudi zake  za mara kwa mara za kuhakikisha kwamba kunapatikana suluhu kwa migogoro ya nchi za Maziwa Makuu.  Aidha alipongeza Tanzania kwa kukubali kupokea maelfu ya wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi na kuwahifadhi na pia mchango wake katika kukabiliana na ugaidi duniani.
Mawaziri hao pia walitambua mchango wa  Shirika la AFD (the AgenceFrançaise de Developpement) ambalo lipo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Maendeleo ya Kimataifa ya Ufaransa.  Shirika hilo limekuwa likitoa mikopo kwa Tanzania inayolenga kuendeleza sekta mkakati za nishati, maji, usafi na usafirishaji.  Waziri wa Ufaransa amesema Ufaransa hivi karibuni itaongeza maradufu  mchango wake katika kuendeleza sekta mbalimbali nchini Tanzania kutoka wastani wa euro milioni 50 kila mwaka, ambazo huzitoa kupitia shirika lake la maendeleo la AFD.
Waziri wa Ufaransa katika mazungumzo yake alisema ongezeko hilo maradufu limelenga kuboresha hali ya maisha ya Watanzania na pia kuwezesha ndoto za kuwa nchi ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda. Kutokana na hali hiyo pia aliahidi mchango wa Ufaransa katika ukarabati wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es salaam Terminal 2.
Waziri Ayrault katika ziara yake hiyo alikutana na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Bw. Benjamin Mkapa, ambaye  ni  msuluhishi wa mgogoro wa Burundi. Katika mazungumzo yake alimpongeza msuluhishi huyo kwa juhudi zake za kutaka pande zinazokinzana zinafikia muafaka  kwa mujibu wa makubaliano ya Arusha. Aidha alisema taifa lake lipo bega kwa bega naye katika kuhakikisha kwamba mgogoro wa Burundi unamalizika.
Akiwa nchini, Waziri Ayrault pia alikutana na wawakilishi wa makampuni ya Ufaransa yanayofanya shughuli mbalimbali nchini Tanzania  na kuwasisitizia kwamba uwekezaji wanaoufanya una maana kubwa kwa Tanzania hasa katika kuwezesha upatikanaji wa nafasi za kazi.

Aidha alisema kwa uwekezaji huo na kuambukiza utaalamu na teknolojia katika  sekta mkakati za maendeleo kama uhandisi, maji, fedha na mawasiliano, kutakuza zaidi ushirikiano wa Tanzania na Ufaransa katika masuala ya kiuchumi.
Waziri Ayrault  alimaliza ziara yake kwa kuzuru Bandari ya Dar es salaam  ambayo ni lango kubwa la uchumi kwa Tanzania na nchi  jirani. Makampuni ya Ufaransa yanashawishiwa kuwekeza katika usafirishaji baharini na kwenye maziwa ambayo ni sekta muhimu kwa Tanzania na nchi jirani.
Mwisho

Dar es Salaam, Agosti 2, 2016

Issued by the Communication and Information Services
Embassy of France
Dar es Salaam

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO