Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Ramadhani Kaswa (aliyesimama) akieleza hali ya umeme katika mkoa huo kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (mbele, kulia), wakati alipofanya ziara ya siku mbili mkoani humo ili kukagua utekelezaji wa Miradi ya usambazaji umeme vijijini Awamu ya Pili. Wengine katika picha ni Watendaji  kutoka TANESCO na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Imeelezwa kuwa ujenzi wa kituo cha kupooza umeme chenye ukubwa wa 20MVA katika eneo la Mnazi Mmoja mkoani Lindi utakamilika  Novemba, 2016.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani wakati alipofanya ziara ya kikazi mkoani Lindi ili kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini Awamu ya Pili.
Dkt. Kalemani alisema kuwa mradi huo pia utahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa 132kV yenye urefu wa kilomita 80 kutoka Mtwara hadi Lindi.
Alieleza kuwa kukamilika kwa Mradi huo kutatatua changamoto mbalimbali za umeme ikiwemo kukatika umeme mara kwa mara  kunakosababishwa na uchakavu wa miundombinu ya umeme.
“ Mradi huu utakapokamilika utaboresha pia upatikanaji wa umeme katika Wilaya za Ruangwa, Liwale na Nachingwea,” alisema Dkt. Kalemani.
 Dkt. Kalemani alisema kuwa kituo kinachotumika sasa  kina zaidi ya miaka kumi na miundombinu yake imechakaa, hivyo kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya umeme kwa mikoa ya Mtwara na Lindi Serikali imeona kuna umuhimu wa kujenga kituo hicho cha kupoozea umeme kitakachokamilika mwezi Novemba.
Alisema kuwa kwa sasa kiasi cha umeme kinachopatikana katika mikoa hiyo miwili ni megawati 18 huku matumizi yakiwa ni megawati 16 na kusisitizaa kuwa kuna umuhimu wa kufungwa kwa miundimbinu mipya ya umeme itakayoweza kusambaza umeme kwa kiwango sahihi kinachoendana na upatikanaji wa umeme katika mikoa hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Ramadhani Kaswa, alisema kuwa mkoa huo una  changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara  kwa kuwa njia ya kusafirisha umeme huo ni ndefu na ina michepuko mingi hivyo hitilafu inapotokea katika eneo moja huathiri maeneo mengine.
Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha hali ya umeme mkoani humo kwa kuwa wananchi watapata umeme wa uhakika na unaotabirika. 
Source:Rhoda James 

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO