Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiongozana na Waziri wa Ardhi Mhe John Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Dar e...
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 06 Septemba, 2016 amewatembelea
Wakazi wa Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam ambao nyumba walizokuwa wakiishi
katika eneo hilo zilivunjwa mwaka 2012 kwa makubaliano ya kujengwa nyumba za
kisasa na kuwaahidi kuwa Serikali itaanza kujenga nyumba hizo katika kipindi
cha Miezi miwili kuanzia sasa.
Rais Magufuli amesema ujenzi wa
nyumba hizo utakamilika katika kipindi cha mwaka mmoja na baada ya hapo Wakazi
wote 644 walioondolewa kupisha ujenzi wa nyumba za kisasa watapatiwa nyumba za
kuishi na kwamba wataishi katika nyumba hizo kwa muda wa miaka mitano bila
kulipa pango na baada ya muda huo kuisha wataandaliwa utaratibu wa kila mmoja
kuuziwa nyumba anayoishi.
"Nakwenda kutoa pesa Mwezi
huu, ili Mkandarasi atakayeteuliwa aanze kujenga nyumba za wakazi wote 644,
wakati wanapojenga hayo majengo ya wakazi 644, ujenzi utaendelea pia katika
maeneo mengine, ili kusudi kama yanajengwa maduka makubwa (Shopping Malls) au
zinajengwa nyumba zingine za wananchi wanaohangaika nao tuwalete hapa.
"Nataka katika miji yetu ya
Tanzania tuanze kupambana na makazi ya wananchi, tuwe tunajenga nyumba ili hata
hawa masikini wa Tanzania waweze kufaidi kukaa kwenye ghorofa" Amesema
Rais Magufuli.
Aidha, Dkt. Magufuli ameelezea
kusikitishwa kwake na namna tatizo la wakazi wa Magomeni Kota
lilivyoshughulikiwa na amewaahidi kuwa Serikali yake itahakikisha wananchi hao
hawasumbuliwi tena.
Pamoja na hatua alizochukua kwa
wakazi wa Magomeni Kota ambao nyaraka zimeonesha walikuwa wakiishi katika
Nyumba za Shirika la Nyumba (NHC), Rais Magufuli ameagiza maeneo yote katika
mikoa 20 hapa nchini yenye nyumba za kuishi za NHC kama lilivyo eneo hilo
yatwaliwe na Serikali na kwamba Serikali itatoa maelekezo ya namna
yatakavyotumika ama kuendelezwa.
Pamoja na kumpongeza kwa kazi
nzuri anazofanya, Rais Magufuli amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Shirika na Nyumba
la Taifa (NHC) Bw. Neemia Mchechu Kyando kuwaondoa wapangaji ambao ni wadaiwa
sugu wa pango zikiwemo Taasisi za Serikali ambazo amezipa siku saba kuwa
zimelipa madeni yao.
"Wale wapangaji wote lazima
walipe madeni yao, nimetoa maagizo leo, wapangaji wote wa Serikali, Wizara ya
Ujenzi, Wizara gani kule... ndani ya siku saba lazima wawe wameshalipa madeni
yao wasipolipa endelea kuwatoa nje.
"Endelea hivyo hivyo
usiogope kumtoa nje mtu yeyote, awe amepangishwa ni wa CCM mtoe nje, awe wa
UKAWA mtoe nje, awe Serikali mtoe nje, awe Waziri Mtoe nje, mpangaji huyo awe
ni Rais mtoe nje, ni lazima upate pesa zitakazowezesha kuendesha Shirika la
Nyumba la Taifa" Amesisistiza Rais Magufuli.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni ya
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa ahadi
aliyoitoa kwa chuo hicho alipokwenda kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa
maktaba ya kisasa ya chuo hicho tarehe 02 Juni, 2016.
Jumla ya majengo 20 yenye ghorofa
nne kila moja yanajengwa katika eneo hilo la mashariki mwa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam na yatakapokamilika tarehe 31 Desemba, 2016 yatakuwa na uwezo wa
kuchukua wanachuo 3,840 kati ya wanachuo 7,000 wanaolazimika kupanga vyumba vya
kuishi mitaani kutokana na kukosa nafasi katika mabweni ya chuo yaliyopo.
Akizungumza na wafanyakazi wa Wakala
wa Majengo Tanzania (TBA) na Vijana walioajiriwa katika kazi za ujenzi wa
majengo hayo Rais Magufuli amepongeza moyo wa uzalendo waliouonesha kwa kufanya
kazi usiku na mchana na amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga
kuendelea kuwatumia vijana hao katika miradi mingine ambayo Serikali
itaitekeleza kwa kutumia TBA.
TBA ikitumia wataalamu na Vijana
wa Kitanzania itatumia Shilingi Bilioni 10 kukamilisha ujenzi huo
ikilinganishwa na endapo ingetumia Wakandarasi ambao walitaka kulipwa kati ya
Shilingi Bilioni 50 na Bilioni 100.
Rais Magufuli ameutaka uongozi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuacha kuingia mikataba mingine na wafanyabiashara
wanaotumia maeneo ya chuo hicho kujenga majengo ya kibiashara na badala yake
amesema Serikali itaendelea kutafuta namna ya kulimaliza tatizo la mabweni kwa
wanafunzi wa chuo hicho na vyuo vingine hapa nchini.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano
ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Septemba, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akihutubia
alipotembelea na kuongea na wakaazi wa Magomeni Kota wilaya ya
Kinondoni jijini Dar es salaam leo Septemba 6, 2016
|
COMMENTS