RAIS John Magufuli kesho anaanza ziara ya kiserikali ya siku mbili nchini Kenya kwa mwaliko wa Rais Uhuru Kenyatta wa Jamhuri ya Kenya, ikiwa ni ziara yake ya kwanza huko.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu leo usiku, Rais Magufuli anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi saa nne asubuhi na baadaye kupokewa rasmi na mwenyeji wake Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi ambako viongozi hao watafanya mazungumzo rasmi.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa pamoja na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Magufuli atakwenda kutoa heshima katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta na pia anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na mwenyeji wake, Rais Kenyatta Ikulu jijini Nairobi.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen jijini Nairobi, na pia anatarajiwa kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo jijini Nairobi.

Barabara hiyo mchepuko ya Southern By-pass ni moja kati ya miradi mikubwa ya barabara nchini Kenya, inayounganisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi kwa barabara za juu na chini na imejengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo.

Kwa mujibu wa Ikulu, Dk Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anatarajiwa kumaliza ziara yake kesho kutwa na kurejea jijini Dar es Salaam.

Hii itakuwa ziara ya pili kwa Rais Magufuli tangu aingie madarakani mwaka mmoja sasa, akiwa amekwenda Rwanda katika ziara ya kiserikali mapema Aprili mwaka huu.

Moja ya ahadi zake alipoingia madarakani Novemba 5, mwaka jana, Rais Magufuli ilikuwa ni kutangaza kubana matumizi ya serikali ikiwamo kufuta safari zisizo za umuhimu za nje ya nchi kwa maofisa wa serikali.Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO