MENEJIMENTI ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imekanusha ya madai ya kupungua kwa uwezo wake wa kuhudumia wanachama na kusema ...
MENEJIMENTI ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
imekanusha ya madai ya kupungua kwa uwezo wake wa kuhudumia wanachama na kusema
kama wangelikuwa na hali mbaya wasingeweza kulipa zaidi ya bilioni 200 kwa
mwaka uliopita wa fedha 2015/2016.
Aidha imesema kitendo walichofanya cha marekebisho ya
malipo katika huduma zake imelenga kuboresha na si kweli kwamba imetokana na
kukosekana kwa wake imetoa ufafanuzi wa
ongezeko la bei za matibabu na kusema kwamba halitaathiri michango ya wanachama
wake na kwamba imelenga kuboresha zaidi huduma wanazopatiwa wanachama
wanapotafuta msaada wa tiba katika vituo vilivyosajiliwa na mfuko huo.
Aidha, menejimenti hiyo imesema kwamba bei mpya ambazo
zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 13 zimeridhiwa baada ya majadiliano ya muda
mrefu.
Imesema mabadiliko yaliyotokea ya kuboreshwa kwa bei
yamelenga kutanua wigo huduma na uwezeshaji, ikiwamo za upasuaji na ada ya
kumwona daktari huku pia wakiongeza fao la vipimo na matibabu ikiwemo upasuaji
wa magonjwa ya moyo nchini.
Akizungumza Dar es Salaam hivi karibuni, Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bernard Konga alisema majadiliano ya kufanya
mabadiliko ya bei hizo yaliyofanyika kwa miaka miwili na kushirikisha wadau
mbalimbali, yapo maeneo ambayo gharama zimeongezeka, mengine kupungua lakini
pia kukiwa na maeneo ambayo hayajaguswa kabisa kutokana na mifumo na sera za
afya za nchi.
Mkurugenzi huyo akifafanua zaidi alisema si kweli kuwa
mabadiliko hayo yametokana na Mfuko huo kushindwa kulipa watoa huduma kama
inavyodaiwa bali ni kutokana na tafiti zilizoonesha kuwepo kwa haja ya
kufanyika mabadiliko kukidhi mahitaji ya matibabu bora kwa wanachama wake na
kuondoa utofauti katika malipo.
Alisema kama mfuko huo ungekuwa na tatizo usingeweza
kulipa zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka wa fedha 2015/16 kwa kuhudumia
wahitaji 6,505,492.
Aidha alisema kwamba wana uwezo wa kuhudumia wanachama
wake kwa miaka minne ijayo bila michango
zaidi.
Akizungumzia mabadiliko yaliyofanywa kwenye maboresho,
alisema nia ilikuwa kubadilisha mfumo wa ulipaji, ikiwemo ada ya kumuona
daktari ili kuondoa mfumo wa awali uliokuwa na viwango tofauti vya ada kwa
mgonjwa anayehudhuria hospitali kwa mara ya kwanza na anaporudi kwa mara
nyingine.
“Kwa sasa ada hii inalipwa kwa viwango sawa ambapo
Mfuko unalipia kadri ya uhitaji na pia upasuaji umeainishwa kutokana na aina
yake kama mdogo, mkubwa au wa kitaalamu,” alisema.
Konga alisema Mfuko huo unatekeleza sera, miongozo na
taratibu zilizowekwa na serkali na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu, hivyo vituo vilivyosajiliwa na Mfuko vina
ngazi tofauti na hivyo bei za huduma zinaruhusiwa kulipwa kutegemea na daraja
la kituo husika. Hadi kufikia Juni, mwaka huu, vituo vilivyosajiliwa na Mfuko
vilikuwa ni 6,439, kati yake vya serikali vikiwa 5,091, madhehebu ya dini 572
na binafsi 776.
Alisema dawa na vipimo ndivyo vinalipwa sawa katika
ngazi zote za vituo, huku mabadiliko ya tofauti yakiwa katika ukubwa wa
taaluma.
Alisema kutokana na kuwa Mfuko umeingia Mkataba na
watoa huduma kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanachama wake, endapo mwanachama
atakataliwa kupewa huduma hatua za kisheria zitachukuliwa na ikiwa madai
yanatokana na udanganyifu hayatalipwa. Aliwataka wanachama wanapopata matatizo
kuhusu madai yoyote yale katika tiba zao kupiga simu ya bure 0800 110063
Alisema katika kipindi cha mpito cha maboresho hayo
kinachoanzia Julai hadi Desemba, mwaka huu wataendelea kupokea maoni na
malalamiko hususani suala la vipimo
ambalo linalalamikiwa sana na baadhi ya watoa huduma baada ya Mfuko huo kuamua
kulipa gharama moja kwa watoa huduma wote.
Maeneo
yaliyoboreshwa zaidi
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kitaalamu za Matibabu wa
NHIF, Dk Aifena Mramba akizungumzia
faida za maboresho alisema baada ya vipimo na upasuaji wa moyo kuanza kufanyika
nchini wameongeza fao la matibabu ya magonjwa hao.
Dk Mramba alisema kwa huduma za upasuaji wameongeza
kwa asilimia 100 na kutoa mfano kwa
upasuaji wa uzazi iliokuwa unalipiwa Sh
130, 000 sasa ni Sh 350,000. Alisema pia upasuaji wa kufunga mirija ya uzazi na
kidole tumbo uliokuwa umetengewa Sh 130,000 tu sasa umeongezewa fedha hadi Sh
300,000.
Maboresho mengine ni ada ya kumuona daktari ambapo
Mramba alisema tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kwa Hospitali za Mikoa
walikuwa wakilipwa Sh 2,000 sasa watalipwa Sh 15,000 huku Hospitali za Wilaya
ambako walikuwa wakilipa Sh 1,000 kama ada ya kumuona daktari sasa watalipwa Sh
10,000.
Alisema Mfuko wa NHIF unasimamia upatikanaji wa huduma
za matibabu kwa wanufaika wake ambao ni zaidi ya milioni 3.3 wanaopata matibabu
katika vituo 6,400 nchi nzima.
Ufafanuzi huo wa NHIF umekuja baada ya kuwepo kwa
taarifa zinazoleta mkanganyiko kwa wanachama wa Mfuko huo kwamba umepunguza
malipo kwa asilimia 60, hatua iliyoonekana kutishia wanufaika kukosa huduma.
ends
COMMENTS