AJALI za barabarani zimeendelea kukatisha uhai wa Watanzania baada ya watu 18 kufa na wengine watatu kujeruhiwa juzi usiku katika ajali iliyohusisha magari mawili yaliyogongana uso kwa uso katika Kijiji cha Nsalala mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne, ajali hiyo ilitokea saa 1.30 usiku katika Kijiji cha Nsalala, Shinyanga Vijijini wakati gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T232 BQR lililokuwa likitokea Nzega, Tabora kwenda Tinde, Shinyanga kutaka kuyapita magari yaliyokuwa mbele na kwenda kuligonga lori aina ya Scania lenye namba za usajili T198 CDQ lililokuwa na tela lenye namba T 283 CBG.
Alisema Noah ilikuwa ikiendeshwa na Seif Muhamed (32) mkazi wa Tinde wakati lori lilikuwa likiendeshwa na Aloyce Kavishe (46) mkazi wa Dar es Salaam ambao wote wanashikiliwa na Polisi kwa hatua zaidi za kisheria kuhusu ajali hiyo.
“Waliokufa, wanaume ni saba, wanawake tisa na watoto wawili na miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga na tayari tisa imeshatambuliwa na ndugu zao; na ajali hii imesababishwa na uzembe wa dereva wa Noah kuamua kuyapita magari yaliyokuwa mbele, alieleza Kamanda Muliro.
Aliwataja waliopoteza maisha na kutambuliwa ni Daud Maja (34) mkazi wa Kishapu, Dina Masanja (20), Chausiku Kasapa (42), Specioza Dotto (23), Esther Kasapa (59), Vincent Nzamala (23), Emmanuel Jumanne, Andrew Mambosasa (33) wote wakazi wa Tinde, Maganga Lubala wa Uyui, Tabora na Debora Maingu mkazi wa Samuye Shinyanga.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Daniel Maguja alithibitisha kupokea miili hiyo na majeruhi watatu wakiwemo watoto wawili ambao ni Hamisa Matiko (5) na Salima Kiza (mwaka mmoja) ambao mama yao alifariki katika ajali hiyo na majeruhi mwingine ni Boniface Richard.
Source:habarileo


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO