SERIKALI imewasilisha bungeni kwa mara ya pili Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 ukiwa na mabadiliko katika maeneo saba ikiwemo kuviondolea vyombo vya habari adhabu kwa baadhi ya makosa ya mwandishi na ukamataji wa mitambo na vifaa vya wanahabari.
Aidha, Serikali imewatoa hofu waandishi kuhusu muswada huo na kusema ikiwa waandishi wa habari watasimamia maadili yao na kutii sheria, hawana haja ya kuhofu kwani Serikali itakuwa mlinzi wao namba moja.
Muswada huo ukiwa na maboresho, uliwasilishwa jana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.
Wakati Serikali ikieleza hayo, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inayohusika na habari, imeupinga Muswada huo na kueleza kuwa unakuja kuua na kuzika kabisa haki na uhuru wa kupata habari kwa wananchi, kuwafunga wahariri na waandishi na umelenga kusambaratisha kabisa tasnia ya habari.
Msemaji wa Kambi hiyo bungeni, Joseph Mbilinyi, katika hotuba yake jana, alishauri Waziri mwenye dhamana ya habari asiachiwe mamlaka ya kuweka viwango vya elimu katika kanuni bali Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Habari likaweka viwango hivyo. Ilipendekeza kiwango kiwe diploma.
Kambi hiyo ilitaka Bodi ya Ithibati isiishie kwa waandishi wa habari bali pia iwe na mamlaka ya ithibati kwa elimu inayotolewa na vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari nchini.
Mbilinyi alipendekeza kuwepo kifungu mahsusi cha kuwalinda wanahabari  dhidi ya vitendo viouvu vinavyoweza kufanywa  dhidi yao na kuzungumza kuhusu habari za uchunguzi ambazo alidai umeziua kabisa.

Hata hivyo kambi hiyo ya upinzani iliunga mkono kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati pamoja na Baraza Huru la Habari ili kuwe na viwango na uangalizi pamoja na uratibu wa kitaaluma katika tasnia ya habari pamoja na kuwakatia bima waandishi wa habari.
Aidha, Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kuhusu muswada huo, imependekeza pamoja na uvaaji wa vitambulisho kwa waandishi wa habari, kanuni zieleze kuhusu mavazi kama ilivyo kwa wanasheria, madaktari na wauguzi. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Selukamba, ndiye aliyetoa maoni ya kamati hiyo bungeni jana.
Maboreshi saba:
Nape alisema walifanya maboresho kwa kuzingatia mawazo ya wadau ikiwemo Kamati ya Bunge, taasisi za habari kama Jukwaa la Wahariri (TEF), Baraza la habari (MCT), Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Taasisi ya Wanahabari Kusini mwa Afrika, Tanzania (MISA-TAN) na Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT)
Waziri Nape pamoja na kueleza kuwa muswada huo uliopigwa danadana kwa zaidi ya miaka 23 utaleta mapinduzi na kuweka historia katika tasnia ya habari nchini, alieleza maboresho kadhaa.
Maboresho hayo ni katika eneo la kuanisha haki na wajibu wa wanahabari; kuainisha haki ya chombo cha habari kukata rufaa; uwakilishi wa wanahabari katika Bodi ya Ithibati; Jaji Mkuu kuweka utaratibu kusikiliza haraka kesi za kashfa.
Maeneo mengine ni kuviondolea vombo vya habari adhabu kwa baadhi ya makosa ya mwandishi; vyombo vya dola kukamata mitambo na vifaa vya wanahabari na mitambo kutohusika moja kwa moja kwa kosa la gazeti.
Akifafanua kuhusu maboresho hayo, Nape alisema kuhusu haki ya wanahabari lazima kuzingatia mikataba ya kimataifa ambayo nchi imesaini na kuridhia pamoja na matakwa ya Kikatiba.
"Muswada sasa umeweka mfumo wa wazi zaidi na wa kidemokrasia ambapo uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya habari-Maelezo hautakuwa wa mwisho. Chombo husika kinaweza kukata rufaa kwa Waziri wa Habari na kisiporidhika na uamuzi kinaweza kupinga suala hilo mahakamani," alisema Nape.
Nape alisema katika uwakilishi wa Bodi ya Ithibati, kati ya wajumbe saba, wakiwemo wanne waandishi, sasa kutakuwa na uwiano katika sekta binafsi ya ya umma. Awali hakukuwa na uwiano huo.
Kuhusu kusikiliza kesi za kashfa kwa haraka, Nape alisema Jaji Mkuu kwa kuzingatia tathimini ya uwezo wa mahakama na rasilimali, na kama ilivyo kwa kesi nyingine za uchaguzi na za biashara, atatunga kanuni zitakazoweka muda wa kumalizika kwa kesi. Awali muswada haukueleza hilo.
"Moja ya mageuzi makubwa ya muswada ni kuviondolea vyombo vya habari au umiliki wake adhabu ya makosa yanayomuhusu mwandishi binafsi. Sasa mwandishi kama mwanataaluma kamili anaweza kuwajibishwa na Bodi ya Ithibati kwa makosa ya kimaadili badala ya mtindo wa sasa wa kila kosa la mwandishi kubebwa na chombo chake," alisema Nape.
Kuhusu kukamata mitambo, Nape alisema maoni ya wadau yamezingatiwa na sasa mamboresho yamemuondoa Mkurugenzi wa Idara ya Habari kuwa na mamlaka ya kukamata mitambo badala yake kazi hiyo itafanywa na Polisi kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA).
Aidha, Nape alisema kuhusu mitambo ya uchapishaji kuwa sehemu ya makosa chombo cha habari kinapoandika uchochezi au makosa mengine ya kashfa, wachapaji wameondolewa katika makosa yanayotokana na maudhui ya watu wengine.
Muswada huu unajadiliwa kwa siku mbili, jana na leo bungeni, utapitiwa kifungu kimoja baada ya kingine, kabla ya kupitishwa.
Source: HabariLeo

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO