SERIKALI imekiri kwamba pengo la Spika mstaafu, Samuel Sitta ni kubwa na kamwe halitazibika ndani ya serikali, chama na jamii. Kauli hi...
SERIKALI imekiri kwamba pengo la Spika mstaafu, Samuel Sitta ni
kubwa na kamwe halitazibika ndani ya serikali, chama na jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati
akitoa salamu za Rais John Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan kwenye
maziko ya Spika huyo yaliyofanyika kitongoji cha Mwenge, Urambo mkoani Tabora
jana.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema kama serikali wamepata pigo kwa
kumpoteza mtu muhimu serikalini. Majaliwa alisema, kuondokewa na mzee Sitta ni
pengo kubwa na kamwe halitazibika ndani ya serikali, chama na jamii kwa ujumla
kutokana na mchango wake wakati wa uhai wake.
Pamoja na kutoa pole kwa familia, aliisihi wao pamoja na wana
Urambo kwa ujumla kuupokea msiba huo kwa mikono miwili, licha ya ukweli kuwa
kifo siku zote huwa hakizoeleki.
Akifafanua zaidi jinsi taifa lilivyonufaika Waziri mkuu huyo
alisema, Sitta akiwa mtumishi wa serikali atakumbukwa kwa mazuri yake kwani
alikuwa mtumishi aliyetukuka, mpenda amani, msikivu na aliyependa kushirikiana
na jamii.
Alisema uongozi wake ulikuwa mfano wa kuigwa na viongozi na
jamii kwa ujumla na kwamba kila kazi ambayo alipewa hakusita kuipokea na wala hakuwahi
kuishindwa.
Majaliwa alisema binafsi asiwe mchoyo wa fadhila, kwani
alimfundisha kazi kipindi ambacho yeye alikuwa mkuu wa wilaya ya Urambo na
Sitta akiwa mbunge wa jimbo la Urambo na Spika wa Bunge la Tisa.
“Mara kadhaa alikuwa akikaa nami pale juu ghorofani nyakati za
usiku saa mbili na kunifundisha kazi.....lakini alinionya kuwa nisipende
kujihusisha na migogoro ya watu na alinitaka kupenda kazi kamwe nisiwe mvivu,”
alisema.
Spika wa Bunge, Job Ndugai akimzungumzia Sitta, alisema kwamba
Bunge halitasahau mchango wake na kwamba Bunge hilo limeguswa na msiba huo.
Alisema kwa niaba ya wabunge wote anapenda kuieleza familia ya
Sitta kuwa wapo pamoja naye katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Huku akibubujikwa na machozi, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey
Mwanri alisema Sitta alikuwa mahiri katika kazi zake na kwamba WanaTabora
walifurahishwa kuwa na mtumishi wa aina hiyo katika maisha yao.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi alisema hakika CCM imempoteza mtu muhimu
na kiungo ndani ya CCM. Alisema siku zote Sitta hakuwahi kupewa kazi na chama
halafu akashindwa.
Msemaji kambi ya upinzani, Freeman Mbowe alisema wamepoteza mtu
ambaye alikuwa anaifariji kambi hiyo na kwamba msiba huo ni mkubwa kwa Taifa la
Tanzania.
Mbowe akizungumza aliwakumbusha watanzania kuwa na taifa lenye
umoja kwani ni maslahi ya taifa, ndiyo yanawaunganisha kama Sittta
walivyowaungabnisha katika msiba huo.
Alisema kipindi hiki Sitta atakumbukwa kwa kazi aliyoifanya na
hasa ile akiwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba kwani hadi ameondoka Katiba mpya
ilikuwa bado kupatikana.
Mbunge wa jimbo la Bukene wilaya ya Nzega mkoani Tabora,
Suleiman Zedi kwa niaba ya wabunge wote wa Tabora alisema wanaungana kwenye
msiba huo na kuwaomba wanafamilia kuwa watulivu kipindi hiki cha majonzi.
Serikali Zanzibar
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Mohammed Aboud kwa niaba ya rais na watu wa Zanzibar alisema
Wazanzibari wote wamepokea kwa masikitiko makubwa na wanaungana na familia hiyo
kuwafariji.
Alisema ametumwa kuja Urambo kuungana na familia na wana Urambo
wote kuomboleza msiba kwani sisi sote tutaenda huko.
Viongozi wa dini
Awali Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa ambaye aliongoza misa ya kuaga mwili na
maziko, amewataka viongozi wa nchi kumpenda Mungu na Ibada kama Spika mstaafu
Samuel Sitta alivyokuwa akipenda ibada na kumtumikia Mungu siku za maisha yake.
Alisema kiongozi mzuri wa wananchi ni yule anayempenda Mungu
kwani watu anaowaongoza wameumbwa na Mungu.
Dk Malasusa pia alitoa rai ya viongozi kuendeleza umoja na
ushirikiano bila kujali itikadi zao za kisiasa kama walivyofanya katika msiba
huo kukusanyika na kushirikiana kwa umoja.
Askofu huyo wa kanisa hilo Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP)
aliambatana na maaskofu wengine watano na baadhi ya wachungaji katika ibada
hiyo ya maziko akiwemo Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Paul
Luzoka, Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora na Askofu wa Kanisa la
Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Maziko
Shughuli za maziko ya Spika huyo mstaafu zilianza saa tatu
asubuhi katika viwanja vya shule ya msingi Urambo zikiongozwa na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa aliyeambatana na mkewe ambapo watu mbalimbali walipata nafasi
ya kutoa heshima zao za mwisho.
Wengine waliohudhuria ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni
Freeman Mbowe, Spika wa Bunge Job Ndugai,Naibu Spika wa Bunge, Tulia Ackson,
Spika wa Bunge mstaafu Anne Makinda, Mawaziri na wabunge.
Shughuli hizo za maziko zilifanyika kwa saa tisa kuanzia saa
tatu asubuhi hadi saa 11 jioni katika viwanja hivyo vya shule na baadaye katika
maeneo ya makaburi ya ukoo wa Sitta yaliyopo kilometa mbili kutoka nyumbani
kwake.
Katika maziko hayo, mwili wa Sitta uliingizwa kaburini saa 10:05
jioni na Askari wa Bunge huku ukisindikizwa na Mke wa marehemu, Mbunge wa
Urambo, Margareth sitta, mama yake mzazi marehemu Sitta pamoja na watoto wake
waliokuwa wameshikilia jeneza.
Baada ya mwili wa marehemu kutumbukizwa katika kaburi
lililojengwa na kusakafiwa kwa saruji lilifunikwa kwa mfuniko ya zege na kisha
kuwekwa mashada juu yake.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge na
Siasa, Uledi Mussa alisoma wasifu wa marehemu. Sitta aliyezaliwa mwaka 1942 na
kufunga ndoa na Margareth mwaka 1968 na mpaka kifo chake walijaliwa watoto
watano.
Pia alizungumzia jinsi Sitta alivyofanya kazi mbalimbali katika
utumishi wa umma ikiwemo ya Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) mwaka
1996 mpaka 2005 aliposhika nyadhifa ya Uspika wa bunge la tisa la kasi na
viwango.
Alisema katika kipindi hicho Sitta amewahi kuwa mkuu wa mkoa wa
Kilimanjaro na Iringa na akiwa waziri wa ujenzi ndipo lilijengwa Daraja la
Selander na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA).
Samuel Sitta alifariki dunia Novemba 7, mwaka huu katika
hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani na mwili wake
kuletwa nchini Novemba 10 mwaka huu na kuzikwa jana katika wilaya ya Urambo
mkoani Tabora.
Source:HabariLeo na nd Ofisi ya Waziri Mkuu
COMMENTS