Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameuhakikishia uongozi wa Mahakama Kuu kuwa serikali itaendelea kuimarisha maslahi ya watumishi wake pamoja na kuimarisha mazingira ya kazi kadri ya upatikanaji wa fedha unavyoimarika. 

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama Kuu lililopo Chake Chake Pemba jana, Dk. Shein amesema kukamilika kwa ukarabati mkubwa wa jengo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya serikali ya kuimarisha huduma za mahakama nchini.

Aliwaeleza mamia ya wananchi waliojumuika na viongozi wa Mahakama na taasisi nyingine za serikali katika uzinduzi huo kuwa serikali itashirikiana na uongozi wa Mahakama kuhakikisha kuwa inakuwa na majengo ya kisasa, kunakuwepo utaratibu endelevu wa ukarabati wa majengo yake na pia kuvipatia vifaa vinavyokidhi mahitaji ya sasa ya idara hiyo.        

Aidha, Dk. Shein ameuhakikishia uongozi huo wa Mahakama kuwa serikali itaendelea kufanya kazi nayo kwa karibu, bila ya kuathiri uhuru wake, katika kuweka mikakati madhubiti na mipango thabiti ya utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini katika kufanikisha malengo yake.

Katika mnasaba huo, Dk. Shein ameiagiza Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhakikisha kuwa inatenga fedha za kutosha katika mwaka wa fedha ujao ili ujenzi wa Mahakama Kuu uweze kuendelea na kukamilika ifikapo mwaka 2019.

Aliutaka uongozi wa Mahakama kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu uwepo wa mahakama hiyo kisiwani Pemba vinginevyo wananchi hawataelewa kuwa lengo la ukarabati huo mkubwa ni kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi.

Dk. Shein aliwataka watumishi wa Mahakama kuwa mstari wa mbele katika kupiga vita rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na uhujumu uchumi na kuwatahadharisha dhidi ya vitendo vinavyochafua heshima na taswira ya Mahakama katika jamii.

"itakuwa ni jambo la aibu kubwa katika jamii pale inapobainika Jaji au Hakimu wa ngazi yoyote ameshirika katika kitendo cha kutoa rushwa au kupokea rshwa ya aina yoyote na ya kiwango chochote kile" Dk. aliwaeleza viongozi na watumishi hao wa  Mahakama.

Aliwataka wananchi pia kuelewa kuwa huduma katika taasisi za serikali ikiwemo Mahakama ni haki yao hivyo wajizuie na wasipitiwe na mawazo ya kutaka huduma kwa kutoa 'chochote' na kusisitizia kuwa "katu wasinunue haki yao wapambane na rushwa".

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu alieleza kuwa kukamilika kwa ukarabati wa jengo hilo Mahakama sasa haitakuwa na sababu za kuchelewesha kesi kwa kuwa jengo hilo limeimarisha mazingira ya kazi katika mahakama hiyo.

Alieleza kuwa Uongozi wa Mahakama sasa umepanga kumleta Jaji Mkaazi kisiwani Pemba badala ya utaratibu wa sasa wa majaji kuja kisiwani Pemba kwa muda maalum.
Alibainisha kuwa  Mahakama imeanza matayarisho ya kuweka mfumo wa kisasa wa wa kuhifadhi kumbukumbu ambao unagharimiwa kwa pamoja kati ya serikali Shirika la Maendeleo la Umoja wa  Mataifa(UNDP) na Umoja wa Ulaya(EU).

Sambamba hatua hiyo alieleza pia kuwa uongozi wa Mahakama unakusudia kutumia mfumo unaotumiwa sasa na Mahkama za Tanzania Bara wa kukubaliana juu ya idadi ya kesi na aina zake zitakazoamuliwa na kila Jaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu wa ngazi za Mikoa, Wilaya na Mahkama za Mwanzo.

Mfumo huo alieleza kuwa unalenga kuleta ufanisi katika Mahkama na kupunguza msongomano wa kesi lakini zaidi utaisaidia Tume ya Mahkama kujua Hakimu gani anastahiki kupandishwa daraja au cheo kwa wakati nafasi mpya za kuajiri Mahkama zinapoteokea.

Jaji Mkuu alilishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa linalshughulikia Watoto-UNICEF kwa kutoa mafunzo kwa majaji kuendesha kesi za udhalilishaji watoto.

Awali Mrajisi wa Mahkama Kuu Jaji George Kazi alieleza kuwa ukarabati wa jengo hilo ambalo lilijengwa mwaka 1920 na kuanza kutumika mwaka 1922 umegharimu jumla ya shilingi milioni 621.

Aliffanua kuwa ukarabati huo ambao ulikuwa wa awamu mbili umeiwezesha Mahkama kuongeza vyumba vingi kwa watumishi, kuongeza vyoo, kupata ofisi za Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka pamoja na kuwepo sehemu ya Mahkama ya Watoto.

Mrajis huyo alilishukuru Shirika la Save the Children kwa kusaidia uwekaji wa mahkama hiyo ya watoto kwa kutoa vifaa muhimu na kutengeneza mazingira rafiki wa watoto.Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO